TAMKO LA NCCR
MAGEUZI KUHUSU UFISADI WA IPTL KUPITIA AKAUNTI YA TEGETA ESCROW
UTANGULIZI
Itakumbukwa
na watanzania kuwa kwa takribani miezi miwili sasa watanzania wamekuwa
wakishuhudia bunge la bajeti ambalo pamoja na mambo mengine, hoja ya ufisadi wa
fedha za Umma zilizochotwa kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ilichukua
sehemu kubwa ya mjadala wan chi hii. Kama chama tunachukua nafasi hii
kumpongeza Mbunge wetu Mhe David Kafulila kwa ujasiri wake wa kutimiza wajibu
wake wa kibunge kwa kiwango cha juu kabisa katika kuhakikisha Bunge linakuwa na udhibiti wa fedha za serikali
ambazo ni mali ya Umma.
Aidha,
Chama kinachukua nafasi hii kuwapongeza wabunge wote wanaounda Kambi rasmi ya
upinzani hususani wa CHADEMA na CUF pamoja na NCCR MAGEUZI kwa ushirikiano wao
mkubwa katika kuhakikisha wanaisimamia
serikali katika mambo yote ya msingi likiwemo hili la ufisadi wa fedha za akaunti ya Escrow. Wameonesha mfano mzuri
ndani ya bunge na tunaomba wadau wote wa maendeleo tuungane katika vita hii
kwani ni kwa maslahi ya Taifa letu masikini kabisa. Kwa nukta hii tunaomba
viongozi wa dini, Asasi za kiraia(NGO), Wanazuoni watanzania kwa ujumla tuungane pamoja kutaka
uwajibikaji ili kudhibiti mzimu huu wa ufisadi wa IPTL/ESCROW ulioanza tangu
awamu ya pili ya uongozi wan chi hii na sasa huenda ukaendelea kulitafuna taifa
hadi awamu wa tano.
KWANINI
ESCROW AKAUNTI ILIFUNGULIWA
Pamekuwa
na upotoshaji wa maksudi kabisa kuhusu sababu za kufunguliwa akaunti hii.
Upotoshaji huu umefanywa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni na watuhumiwa
wenzake kwa maana ya Maswi na Muhongo kwa maana ya watuhumiwa ambao tayari
wamesikika wakizungumzia suala hili. Watuhumiwa hawa wamesikika wakidai kuwa
escrow ilifunguliwa kufuatia mgogoro baina ya wabia wa IPTL kwa maana ya
Mechmar mwenye 70% na VIP mwenye 30%. Haya wanayapotosha ili kuhalalisha hoja yao kuwa fedha hizo sio
za serikali
NCCR
MAGEUZI inapenda Umma wa Watanzania ufahamu kuwa akaunti hii ilifunguliwa na
pande mbili; Tanesco na Serikali kwa upande mmoja na IPTL kwa upande wa pili.
Na kwamba Akaunti hii ilifunguliwa kufuatia mgogoro wa malipo ya gharama za umeme
ambapo Tanesco ililalamika kuwa inatozwa zaidi. Msingi wa Tanesco kulalamika
kutozwa zaidi kulitokana na IPTL kudanganya kuhusu mtaji wa asilimia 30%
(equity) ambapo ilidai iliwekeza dola 38millioni kumbe iliwekeza dola 50, sawa
na Tsh 50,000/= wakati huo mwaka 1995-1998 ambapo exchange rate ya dola kwa Tsh
ilikuwa 1; 1000.
Nikatika
msingi huo, Mwaka Februari2014 Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro ya kibiashara
ICSID ilielekeza gharama ziangaliwe upya tangu TANESCO ilipoanza kununua umeme
wa IPTL maka 2002 mpaka 2014 ili kuona ni kwa kiasi gani IPTL ilipata fedha
isiyostahiki na kiasi gani ilikuwa stahiki ili kuweka msingi wa mgawo wa fedha
za escrow.
Hivyo Akaunti ya Escrow ilifungulimwa mwaka 2006 ikiwa
ni miaka miwili tangu 2004 ambapo TANESCO ilibaini kasoro hiyo ya udanganyifu
uliofanywa na IPTL kwenye equity ya dola 38milioni wakaweka dola 50.
KWANINI
FEDHA ZA ESCROW NI MALI YA UMMA
Fedha
ya Escrow ni mali ya Umma kwa sababu zifuatazo;
1.Ziliwekwa
kusubiri kumalizika mgogoro wa gharama ambazo IPTL ilikuwa anatoza TANESCO
kifisadi. Mgogoro huo ambao msingi wake ulitokana na IPTL kudanganya kuhusu
mtaji wa dola 38milioni kumbe ilikuwa dola50.Mpaka sasa hakuna mahala mgogoro
huo umeamuliwa.
2.Ndio
sababu Hukumu ya awali ya ICSID ilielekeza pande mbili zifanye hesababu upya
ili kubaini ni kiasi gani IPTL ilizidisha na ni kiasi gani ilikuwa halali kwa
kuangalia tangu mwaka 2002.
3.Ndio
sababu fedha hizo zilionekana kwenye vitabu vya shirika la Umma Tanesco
4.Ndio
sababu Kamati ya PAC, Spika na Waziri Mkuu wote wamelekeza CAG achunguze
akaunti hiyo kwani kisheria CAG hana mamlaka ya kuchunguza fedha za
wafanyabiashara bali fedha za Umma. Na CAG anachunguza fedha za Umma kwenye
makampuni ambayo umiliki wake sio chini ya asilimia 50
MASWI,
MUHONGO, MRAMBA, WEREMA NA IPTL NDIO WALISHINIKIZA UFISADI HUU
May
30, 2014 Waziri wa Nishati na Madini Mhe Muhongo alidanganya Bunge kuwa uamuzi
wa Serikali kumlipa IPTL/PAP ulikuwa uamuzi wa hukumu ya Mahakama ya Setemba
2013. Ukweli ni kwamba hukumu hiyo hakuna mahala ilielekeza PAP alipwe fedha
hizo. Ukweli ni Kwamba uamuzi wa kifisadi wa kutoa fedha hizo ulifanywa na
Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco kwa upande mmoja na IPTL kwa upande wa
pili na ukapewa Baraka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hivyo Tunaomba Umma
uelewe hivyo.
NYARAKA ZA PAP
KUMILIKI ASILIMIA 70 ZA IPTL NI ZA KUGUSHI
Nyaraka
za TRA zinaonesha kwamba SingaSinga ambaye ndiye mliki wa PAP alinunua hisa asilimia
za 70 za IPTL kutoka kwa PIPERLINK kwa 480millioni, na kwamba PIPERLINK
ilinunua Asilimia hiyo 70 kutoka kwa Merchmar kwa Tsh6millioni wakati kampuni
hiyohiyo ilinunua asilimia 30 kutoka kwa VIP alinunua kwa 120billioni. Pia
inaonesha kwamba kodi ililipwa disemba 6, 2013 wakati alipewa hela za escrow
tangu Novemba 2013. Kwa tafsiri nyingine alilipwa fedha za Escrow kabla ya kuwa
mmiliki halali wa IPTL.
Na
zaidi Umma unapaswa kuelewa kuwa Kwa mujibu wa sheria ya kodi(Finance Act
2012), hisa zinapouzwa kutoka kampuni moja kwenda nyingine uhamishaji huo
unathibitishwa na waziri wa wizara husika baada ya kodi kulipwa. Sasa muulizeni
waziri wa Nishati na Madini ni lini uhamishaji huo wa hisa aliupitisha kama
waziri? Na zaidi taarifa za TRA zinaonesha kuwa kodi ya mauzo ya hisa hizo
asilimia 70 kutoka Mechmar kwenda PIPERLINK na Kutoka PIPERLINK kwenda PAP
ilipwa tarehe moja yaani Disemba6, 2013.
Huu
ni uthibitisho kuwa documents hizi zote ni za kughushi, na watanzania hawawezi
kuchezewa akili kiasi hiki.
MKATABA WA
WIZARA YA NISHATI NA IPTL KWENDA BOT NI UFISADI
Mkataba
huu ulikuwa kifisadi kwasababu hauna msingi wowote wa kisheria wala kimkataba.
Mkataba wa kuzitoa fedha hizi ni wa kifisadi mgogoro uliosababisha fedha hiyo
iwekwe hapo haukuwa na haujamalizika. Ndio msingi wa hukumu ya mahakama ya
ICSID uliotaka mahesabu kufanywa upya. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa mkataba wa
IPTL, pande mbili zilikubaliana kuwa maamuzi kuhusu mgogoro baina yao utamuliwa
na mahakama ya ISCID na sio vinginevyo.
MMILIKI
WA PAP ANA REKODI YA UFISADI AFRIKA SIO MWEKEZAJI
Kwa
mujibu wa report ya wikleaks, Singasinga anaetajwa kuwa mmiliki wa kampuni ya
PAP ametajwa katika orodha ya mafisadi waliohusika katika skendo ya ufisadi wa
Goldenberg nchini Kenya jina lake likiwa no8 akishirikiana na mtoto wa Rais
mstaafu wa Kenya, Gideon Moi. Huu ndio ufisadi mkubwa kupata kufanyika nchini
Kenya, uliohusisha Majaji, Viongozi wakubwa kisiasa, familia ya rais na
watendaji wakubwa serikalini. Kama CCM haitachukua hatua kali kuhusu ufisadi
huu wa escrow ijiandae kufuata nyayo za chama cha KANU kwani kuna kufanana sana
kwa skendo hii na ile ya Goldenberg.
KIFO
CHA MGIMWA KICHUNGUZWE
Mhe
Mbunge David Kafulila, alisisitiza ndani ya Bunge kuwa kama tungekuwa na Bunge
makini hata kifo cha aliyekuwa waziri wa Fedha, Mhe Mgimwa kilipaswa
kuchunguzwa. Chama kinapenda kusisitiza kauli hiyo kwakuwa Mzee Mgimwa aliugua
na kufariki katika kipindi ambacho kulikuwa na shinikizo kubwa la kutoa fedha
za escrow bank kuu. Hivyo Kama Chama tunapenda Umma uelewe kuwa huo ndio msingi
wetu wa kutaka uchunguzi wa kifo hicho. Na familia ya Mhe Mgimwa tunaipa pole
kutonesha madonda lakini tunafanya haya kwasababu ndugu yao alikuwa public
figure, alikuwa kiongozi ndani ya nchi hivyo umma una maslahi na chochote
kinachomuhusu mtu huyu.
HATMA
YA USALAMA WA MBUNGE KAFULILA
Mhe
Spika amegoma kuchukua hatua kuhusu mwongozo uliombwa na mbunge Mhe David
Kafulila kuhusu kutishiwa maisha ndani na nje ya Bunge. Kama Chama Tunapenda
kurejea na kusisitiza kuwa tuna hofu na uhai wa Mbunge wetu hasa kutokana na
mazingira yanayozunguka ajenda hii anayoisimamia ikiwa inagusa vigogo na
mafisadi wakubwa. Tunao uzoefu wa mazingira kama haya pale kijana Amina Chifupa
alipozungumzia madawa ya kulevya, tunao uzoefu na kilichotokea kwa Dr Mvungi
alipokuwa mhimili imara wa serikali tatu ndani ya Tume ya warioba, wote
tunafahamu kilichowakuta. Kama chama kwakuwa Bunge la vyombo vya dola havioni
umuhimu huo, tunamwachia Mungu, lakini
chochote kikitokea tunafahamu ushiriki wa serikali na vyombo vyake.
SPIKA
MAKINDA ANADHALILISHA BUNGE
Kazi
ya Bunge ni kusimamia Serikali. Ufisadi wa IPTL ulianza tangu awamu ya pili
1994. Ni aibu kwa Spika kukataa Bunge lisichukue jukumu lake la kuichunguza
serikali. Wote mnafahamu CAG alivomsafisha Jailo au PCCB ilivosafisha Richmond.
Ni katika Msingi huo, Kama chama tunashauri suala hili linalogusa vigogo
wakubwa nchini, lichunguzwe na Bunge lenyewe kupitia Kamati teule au uchunguzwe
ufanywe na Kampuni za Kimataifa za ukaguzi kama ilivofanyika kwenye fedha za
EPA.
Mhe
Mbunge alitoa ushahidi wa hukumu ya Septemba 2013 ikionesha dhahili kuwa hakuna
mahala hukumu ile ilielekeza IPTL/PAP wapewe fedha hizo za Escrow. Na
kuthibitisha kuwa waziri huyu alizungumza uongo bungeni kwa jambo nyeti kama
hili, lakini Spika badala ya kutumia kanuni ya kusema uongo anaelekeza mbunge
aende PCCB, Kambiwa na nani PCCB wanachunguza uvunjifu wa kanuni za bunge?
Aidha,
Ni udhaifu wa Spika huyu ndio sababu haoni aibu kwa Bunge lake kuwa na
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa bodi
ya Tanesco. Hii Kamati inawezaje kukosoa uchafu wa TANESCO katika mazingira
hayo? Au ndio sababu taarifa ya Kamati hiyo haikuzungumza chochote kuhusu
ufisadi wa escrow unaohusu TANESCO na wizara yake?
JAJI
WEREMA AJIPIME KAMA ANASTAHILI KUENDELEA KUWA JAJI NA MWANASHERIA MKUU
Uamuzi
wa Jaji Werema kutaka kupigana bungeni hata kuzuiwa na Mhe Sitta na Wasira na
baadae nje ya Bunge kumtishia uhai Mhe Mbunge ni kielelezo kuwa amepungukiwa
sifa za msingi kuweza kuendelea kuwa mwanasheria mkuu wa serikali. Ni aibu
serikali ya Kikwete kuwa na Mwanasheria mkuu ambaye kazi yake kubwa ni
kuelekeza na kushauri utawala wa sheria nchini harafu anageuka na kuwa mfano wa
raia mwenye mapenzi ya kujichukulia sheria mkononi ndani ya bunge na kuahidi
kukata kichwa mbunge anaemkosoa. Hii haijapata kutokea katika historia ya
Tanzania.
MWISHO
Tunapenda
kuhitimisha kwamba tunaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhusu ufisadi
huu, na kwamba haturidhishwi na hatua zinazochukuliwa, na kwamba tutafanya
utaratibu wa kuwasiliana na vyama ndani ya UKAWA kuona namna bora zaidi ya
kulisukuma suala hili ili watanzania waelewe namna nchi yao inavotafunwa.
Tunaomba vyama vyote ndani na nje ya UKAWA vitambue ukweli huu kama ambavyo
wameanza kutambua ili tusaidiane kuelimisha Umma kuhusu ufisadi huu na
watanzania wafanye maamuzi ya nchi yao kwani wanayo haki ya kuhoji na kufaidi
utajiri wa taifa lao kwani hawapo kwenye ardhi hii kama wakimbizi au tumbili
kama inavyotambuliwa na Serikali ya CCM sasa. Wiki ijayo tutaanza ziara ziara
Mkoani Kigoma wakati taratibu zingine zinaendelea kushughulikiwa. Wiki ijayo
tutaanza ziara ziara Mkoani Kigoma wakati taratibu zingine zinaendelea
kushughulikiwa.
Imesainiwa
na;
…………………………….
NYAMBABE
KATIBU
MKUU
Julai
03.2014