Monday, 22 July 2013

NCCR-Mageuzi yaibomoa CCM Kasulu


Mhe. Moses Machali (Mb)
CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimekibomoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuvuna wanachama wake zaidi ya 200. Tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Nyamidaho, Kata ya Nyamidaho, Jimbo la Kasulu Vijijini, wakati Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo.

Kabla wanachama hao hawajajiunga na chama hicho cha upinzani, Machali aliwaambia kuwa, shida wanazozipata katika maeneo yao, zinasababishwa na CCM ambayo licha ya kuongoza nchi kwa miaka mingi, imeshindwa kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Kutokana na hilo, aliwataka wananchi hao wasiendelee kuiunga mkono CCM kwa kuwa kama wataendelea kushirikiana na chama hicho tawala, uwezekano wa maisha yao kuboreka ni mdogo kwa kuwa viongozi wa CCM hawaguswi na matatizo ya wananchi.

“Leo hapa naona kila mmoja anaonekana kuwa na maisha magumu, naona hapa maisha yenu hayatofautiani na maeneo mengine nchini na muelewe kwamba, shida zote hizi zinasababishwa na CCM ambao hawaguswi na shida zenu.

“Kwa maana hiyo, ili muonyeshe kwamba mnaguswa na hampendelei kuwa na maisha magumu, hameni CCM na mjiunge NCCR-Mageuzi kwa sababu hiki ndicho chama kinachoonyesha mwelekeo wa kuwakomboa Watanzania tofauti na vyama vingine vya siasa,” alisema Machali.

Baada ya maneno hayo na mengine, baadhi ya mamia ya wananchi waliokuwa wamehudhuria mkutano huo, walijitokeza kupokea kadi za NCCR-Mageuzi, wakiongozwa na Diwani wa zamani wa Kata ya Nyamidaho kupitia CCM, Mageleyanya Baliyanga.

Wakati huo huo, Machali alisema atawasiliana na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaitun Buyogela ambaye hakuwa eneo la mkutano, achangie fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya kilichoko katika Kijiji cha Nyamidaho.

Kwa mujibu wa Machali, ujenzi wa kituo hicho ni muhimu kwa afya za wananchi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani na kwamba ili umuhimu huo uonekane, kuna kila sababu Buyogela kuchangia ujenzi wa kituo hicho.

Pamoja na hayo, aliwataka wananchi wa Nyamidaho, wasikate tamaa pindi maendeleo yanapochelewa katika maeneo yao, kwa kuwa yanakwamishwa na CCM ambao ni wengi katika vyombo vya maamuzi kama mabaraza ya madiwani na bungeni.

No comments:

Post a Comment