Thursday, 8 August 2013

Mtihani wa Darasa la Saba nao Majanga!

Kutoka Gazeti la nipashe

8th August 2013

*        Ni wa majaribio katika wilaya 40

*        Maswali mengine yakosa majibu

*        12 yamtoa jasho Profesa UDSM

 

Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani), mtihani ya kujipima kwa wanafunzi wa darasa la saba uliofanyika Julai 8 na 9, mwaka huu katika wilaya 40 za Tanzania bara.

Madudu zaidi yamebainika katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, baada ya mtihani wa kujipima wa darasa la saba uliofanyika Julai, mwaka huu katika wilaya 40 za Tanzania Bara kuwa na mapungufu makubwa na ya wazi.

Aidha, maswali 12 kati ya 50 katika mtihani wa Hisabati hayana majibu, 14 ni magumu ambayo mtoto wa darasa la saba hawezi kuyajibu na mengine matano yamekosewa na hata yafanywe kwa kiasi gani hayawezi kuwa na majibu.

Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alibainisha madudu hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kuwataka Watanzania kushiriki kupinga anguko la elimu linalotia aibu Taifa.

Mbatia alibainisha kuwa katika mtihani huo uliofanywa Julai 8 na 9, mwaka huu, kwa masomo ya Hisabati, Kiswahili na Kiingereza, jina la Wizara limeandikwa ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi huku usahihi hakuna neno Stadi.

Alisema matokeo hayo yamekuja katika kipindi ambacho serikali iko katika dhana ya matokeo makubwa sasa (big result now), katika sekta ya elimu na mtihani huo umetungwa kwa dhana hiyo.

Alisema baada ya kupata mtihani huo, alikusanya baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika moja ya shule jijini Dar es Salaam na kuufanya na zaidi ya nusu walishindwa kupata daraja la tatu yaani C.

“Sikuishia hapo, nilimtafuata msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yaani Profesa na kumpa mtihani wa hesabu aliufanya kwa muda wa saa 2:03, lakini na hakupata daraja la kwanza, alishindwa kujibu baadhi ya maswali na mengine kukosa majibu kabisa,” alisema.

Kwa mujibu wa Mbatia, Profesa huyo alisema swali namba 33 ni gumu ambalo linafanywa na mwanafunzi wa fani ya uhandisi na linahitaji muda mrefu kupata jibu.

“Sikutaka kuridhika na majibu yao, nilijifungia ofisini majira ya asubuhi kwa saa 2:30 na kuufanya mtihani wote nikalinganisha na majibu ya wengine, lakini sikupata alama A…ninachojiuliza hii ndiyo Big Result Now?” alibainisha na kuhoji.

Alisema kwa muundo wa mtihani huo, ni kuwakatisha tamaa wanafunzi na kuwafanya wazidi kulichukia somo la hisabati na kiwango cha taaluma nchini kuendelea kuporomoka.

Katika somo la Kiingereza, kulikuwa na mapungufu makubwa ya kisarufi na majina ikiwamo historia ya Tanzania kwa viongozi wa Taifa kama Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

Mbatia alisema jina la Mwalimu Nyerere limekosewa na kuandikwa Julias na Rais wa awamu ya Pili likiandikwa Ally Mwinyi badala ya Ali Hassan Mwinyi, huku wakishindwa kueleza kifo cha Karume na kueleza kama kifo cha kufanana na Mwalimu Nyerere. Itakumbukwa kwamba, Mwalimu Nyerere alifariki dunia baada ya kuugua wakati Karume aliuawa.

Aidha, alisema katika mtihani wa Kiswahili, kuna mapungufu mengi hususani ya usahihi wa lugha na kuwafanya Watanzania kujiuliza kama mitihani hiyo ilitungwa na wanataaluma walibobea au ni ubabaishaji.

Alisema suala hilo linakwenda sambamba na makosa yaliyopo kwenye vitabu vinavyotumiwa na wanafunzi wa shule za msingi hadi sekondari ambavyo vimepitishwa na kupewa cheti cha ithibati.

“Tumefika mahali pagumu kielimu yaani ni janga la kitaifa,” alisema Mbatia.

Alisema kitabu cha uraia cha darasa la nne, kuna mahali kimeandikwa ‘Serikali za mitaa zinaongozwa na viongozi wa vitongoji’ huku cha hesabu kikieleza namba nzima ni moja hadi 99 badala ya moja hadi tisa.

“Haya yote wanalishwa watoto wa maskini wa nchi hii, hakuna mtoto wa kigogo anayesoma kwenye shule hizi na hawajafanya mitihani hii,” alisema.

MAPENDEKEZO YA MBATIA

Kuundwa kwa tume ya kudumu ya elimu nchini, itakayoshughulika pamoja na mambo mengine, kuhakikisha ubora wa elimu nchini na kudhibiti mambo yote yanayosababisha kutetereka kwa ubora huo (Education quality assurance and control).

Aliongeza kuwa tume hiyo iwe na mamlaka ya kuhakiki utendaji wa taasisi mbalimbali za elimu ambazo hadi sasa zimeonekana kutotimiza vyema majukumu yake.

“Tume itakapoundwa inaweza vile vile kusaidia kubainisha wazi ni nini falsafa na malengo hasa ya utoaji wa elimu nchini kulingana na wakati tulionao,” alisema.

Januari 31, mwaka huu, Mbunge huyo aliwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini.

Alianisha sura hizo ni kuporomoka kwa uwajibikaji, kutokuthamini rasilimali za Taifa, kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, kumomonyoka kwa uadilifu miongoni mwa watumishi wa umma na kupungua kwa uzalendo.

Hata hivyo, hoja hiyo haikutiliwa maanani ingawa siku chache baada ya hoja hiyo, Wizara ilifuta Kamati ya Uthibitishaji ya Vifaa vya Elimu (Emac).

Aidha, Februari 18, mwaka huu, Wizara hiyo ilitangaza matokeo ya kidato cha nne yaliyonyesha zaidi ya watahiniwa 240,000 walipata daraja sifuri ikiwa ni asilimia 66 na baadaye matokeo hayo yalipangwa upya na watahiniwa 210,000 wakapata daraja la sifuri.

Kwa mujibu wa matokeo ya ualimu ngazi ya Astashahada na Shahada yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Julai, mwaka huu, watahiniwa 2,606 wa Stashahada wanarudia mtihani na 533 wamefeli.

Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu, alipotafutwa na NIPASHE, alithibitisha mitihani hiyo kufanyika katika halmashauri 40 nchini na kusema kwamba asingeeleza undani wa makosa yaliyobainika hadi atakapopata ufafanuzi wa kitaalam.

No comments:

Post a Comment