NATIONAL CONVENTION FOR CONSTRUCTION AND REFORM -MAGEUZI
(NCCR- MAGEUZI)
SERA ZA CHAMA
© Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR Mageuzi – Taifa
Utangulizi
Kitabu hiki kinaweka bayana itikadi, sera na malengo ya chama cha National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi). Kimsingi sera hizi zilibuniwa na chama tangu kilipoundwa mwaka 1992 na ndizo zilizotumika kuandikisha chama chini ya sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992. Kwa kiasi fulani kumekuwa na uboreshaji wa sera hizi mwaka hata mwaka, hadi kitabu hiki kilipochapishwa. Katika kitabu hiki sera nyingi zimeainishwa kwa muhtasari tu kwa kuwa machapisho yanayofafanua kila sera kwa kina yatatolewa na chama kila itakapobidi.
Mpango Mkakati endelevu wa chama chetu unaainisha wazi katika malengo yake kuwa ni lazima kujenga uelewa wa kina katika maono, majukumu na sera za chama miongoni mwa viongozi, wanachama na watanzania kwa ujumla. Lengo hili lilitekelezwa tangu mwaka 2002 kwa kupitishwa marekebisho muhimu ya chama. Sera za chama zimekuwa zikifanyiwa mapitio na kuandaliwa upya na Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama na hatimaye muhtasari wake umeiva kuweza kuchapishwa rasmi baada ya kupitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama, mnamo mwaka 2005.
Kuchapishwa kwa muhtasari huu kunaondoa umuhimu wa kuzirudia kwa kirefu sera hizi katika ilani ya chama ya uchaguzi kila mara unapofanyika uchaguzi mkuu nchini. Kwa maana hii, kuanzia sasa ilani ya uchaguzi ya NCCR-Mageuzi itakuwa inatangaza masuala ya msingi tu ambayo yanabeba hoja za chama katika uchaguzi husika.
Ninawashukuru wanataaluma wote, wanachama na wapenzi wetu walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha maandalizi ya kitabu hiki. Jambo la msingi ni kwamba ainisho hili la sera halisitishi mjadala kuhusu sera zilizoainishwa katika chapisho hili. Kwa hakika uchapishaji wake ni kichocheo cha mjadala makini wenye lengo la kuziboresha sera hizi ili zikidhi matumaini na mahitaji wa Watanzania.
James Fransis Mbatia
Mwenyekiti wa Taifa
August, 2005
1.1 Dokezo
Uhifadhi wa historia ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya taifa letu la Tanzania hauna budi kuzingatia kina cha harakati za umma, hususan harakati zilizoanza katika karne ya kumi na tisa na kuendelea hata sasa. Taifa lililostaarabika hutunza kumbukumbu ya pamoja, na litajitambua pale lilopo kwa kutazama lilipotoka na huko linapokwenda. Chama cha NCCR-Mageuzi kinatambua umuhimu wa kuhifadhi kwa usahihi kumbukumbu ya pamoja ya utaifa wa watu wetu kwa heshima ya wahenga wetu na kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo vya watanzania. Kwa mantiki hiyo, katika sura hii ya kwanza ya kitabu cha sera zetu, tunaeleza japo kwa ufupi historia ya nchi yetu na jinsi historia hiyo inavyohusiana na harakati za wanamageuzi ambao hatimaye ndilo chimbuko la chama chetu.
1.2 Historia ya Nchi
Katika historia ya binadamu, sisi waafrika wa Tanzania na kwingineko barani Afrika, tumepata kukumbwa na majanga matatu makuu, ambayo ni Utumwa, Ukoloni na sasa Ukoloni mamboleo. Katika janga ya kwanza ambalo lilishamiri sana kati ya karne ya 14 na 18, waafrika walitekwa na kuuzwa utumwani kuwa vyombo vya uzalishaji mali vya mataifa ya ng’ambo kwa kisingizio kuwa sisi ni sawa na nyani au sokwe mtu. Watu wa kutoka nje ya bara letu walimtazama Mwafrika kama mnyama yoyote yule na hawakumtambua kuwa ni binadamu wenye utashi na roho.
Wengi kati ya watu weusi walioko Amerika ya Kaskazini na Kusini, Uarabuni, bara la Ulaya na Asia leo, ni vizazi vya watu waliochukuliwa utumwani kutoka barani kwetu. Zaidi ya waafrika milioni 12 waliuzwa katika Bara la Amerika na Visiwa vya Karebea katika biashara hiyo dhalimu ya utumwa. Maendeleo ya sasa ya nguvu za kiuchumi za mataifa hayo ni matokeo ya nguvukazi ya watumwa wenye asili ya kiafrika.
Janga la pili, yaani Ukoloni; lilifuatia lile la Utumwa. Mabadiliko kutoka kulidhulumu bara la Afrika kwa njia ya Utumwa hadi njia ya Ukoloni kulitokana na mabadiliko ya uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyopunguza mahitaji ya nguvukazi ya watumwa. Ilibidi watumwa waachiwe huru ili kujenga uchumi wa soko la dunia. Ilionekana kuwa kuna faida kubwa kumtawala mwafrika katika bara lake la asili na kumtumia kuzalisha mali ghafi za kilimo, madini na nyinginezo kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vya Ulaya Magharibi. Hivyo pilikapilika za mataifa ya kigeni za kujitwalia makoloni barani Afrika zilibuniwa na kutekelezwa haraka kiasi kwamba ilipofika mwaka 1884 mataifa ya kibeberu yalikutana Berlin , Ujerumani kugawana bara letu. Katika kilele cha mkutano huo wa Berlin nchi zilizojipatia makoloni barani Afrika ni pamoja na Ujerumani (mwenyeji wa mkutano), Uingereza, Ufaransa, Ubeligiji, Ureno, Hispania na Italia. Katika mgawanyo huo, Tanganyika iliangukia mikononi mwa utawala wa kijerumani.
1.2.1 Tanganyika chini ya utawala wa Ujerumani
Ukoloni uliingia Tanzania kuanzia nchi yetu ilipotawaliwa na Ujerumani kati ya mwaka 1884 na 1918, na ikapewa jina la Deutsch Ostafrika. Koloni la Deutsch Ostafrika lilijumuisha eneo lote lililo kati ya maziwa makuu ya Tanganyika na Nyasa. Eneo hilo sasa ndipo zilipo nchi za Rwanda , Burundi na Tanzania (bara). Wakati wa uvamizi huo wa kikoloni mnamo mwaka 1884, sehemu ya ukanda wa pwani ya Tanganyika ilikuwa chini ya Sultani wa Zanzibar hivyo ilibidi Wajerumani wainunue kutoka kwa Sultani wa Zanzibar . Hatimaye, mwaka 1890 visiwa vya Zanzibar viliwekwa chini ya himaya ya Uingereza.
Tokea enzi hizo, waafrika wenyeji wa Deutsch Ostafrika walipigana kuzuia uvamizi wa Wajerumani lakini kwa namna moja au nyingine baadhi ya viongozi wenyeji walijikuta wakigawanywa na kuanza kusaidiana na maadui kuisaliti nchi yao . Mashujaa thabiti wa nchi yetu waliopambana na ukoloni ni pamoja na viongozi wa Wachaga, Mkwawa wa Wahehe na wanaharakati wa vita ya Majimaji. Bahati mbaya juhudi zao hazikufanikiwa kuzuia uvamizi wa wajerumani. Tunazidi kuuenzi na kuuheshimu moyo huo wa mashujaa wetu wa kipindi hicho.
1.2.2 Tanganyika chini ya Utawala wa Uingrereza
Mwaka 1919 baada ya Ujerumani kushindwa vita ya kwanza ya dunia, Deutsch Ostafrika ilitwaliwa na taifa la Uingereza chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa awali (League of Nations) na ikapewa jina jipya la Tanganyika . Mnamo mwaka 1945, Umoja wa Mataifa wa awali ulivunjwa na kuundwa upya kuwa Umoja wa Mataifa wa sasa (United Nations Organisation). Nchi zote zilizokuwa zimeshikiliwa chini ya Umoja wa Mataifa wa awali ziliwekwa chini ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa wa sasa, Tanganyika ikiwa mojawapo. Hivyo, Uingereza iliendelea na mkataba wa kuitawala Tanganyika kwa niaba ya Umoja wa Mataifa hadi itakapokuwa na uwezo wa kujitawala.
Wakati wa utawala huu wa mkoloni mwingereza, wanamageuzi wazalendo walianza harakati za kudai uhuru wa taifa letu. Harakati zao zilikuwa kwa njia ya kujikusanya pamoja katika vyama ama vya burudani au vya wafanyakazi. Hatimaye vikaanza kuibuka vyama vya siasa ambavyo lengo lake kuu lilikuwa ni kudai uhuru wa Tanganyika. Kwa mfano, mnano mwaka 1929 chama cha watanganyika kijulikanacho kwa jina la African Association (AA) kiliundwa jijini Dar es Salaam. Jitihada za vyama hivyo zilifanikiwa kumshinikiza mwingereza aone haja ya kukomesha utawala wake kwa Tanganyika.
Mnamo mwaka 1961, Uingereza ilifuta mkataba wa udhamini wa Umoja wa Mataifa na kuiweka chini ya himaya yake ili kuliwezesha Bunge lake kuwa na mamlaka ya kutoa uhuru kwa Tanganyika. Kwa hiyo, katika kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe 9 Desemba mwaka 1961 hadi Tanganyika ilipokuwa Jamhuri mwaka 1962, Tanganyika ilikuwa sehemu ya himaya ya Uingereza.
1.2.3 Uhuru Kamili wa Tanganyika
Tarehe 9 Desemba 1962, Tanganyika ilijipatia uhuru kamili kwa kuwa Jamhuri. Bunge la Tanganyika lilifuta sheria ya Bunge la Uingereza iliyokuwa imeiweka Tanganyika chini ya himaya ya Uingereza na kutunga katiba mpya ya Jamhuri. Kwa jinsi hii, tarehe Tanganyika ilipokuwa jamhuri ndiyo tarehe halisi ya uhuru kamili wa Tanzania bara.
1.2.4 Utawala wa kigeni Zanzibar
Visiwa vya Unguja na pemba ambavyo ni sehemu inayounda taifa letu la Tanzania, vilipata kuwa chini ya utawala wa kigeni wa Sultani toka Uarabuni na baadaye mkoloni mwingereza alitwaa utawala toka kwa Sultani kati ya mwaka 1890 hadi 1963. Katika kipindi hicho cha utawala wa kigeni, wazanzibar wenye moyo wa uanamageuzi walipinga kutawaliwa na wageni, hata wakaanzisha harakati za vyama vya siasa kwa ajili ya kutetea maslahi ya wazanzibari na kudai uhuru wa Zanzibar.
1.2.4 Uhuru wa Zanzibar
Mnamo Oktoba, 1963 Uingereza ilifuta mkataba ulioipa jukumu la kuilinda himaya ya Sultani wa Zanzibar . Tangu hapo Zanzibar ikawa imerejeshwa chini ya sultani wa Zanzibar ambaye alikuwa ndiye mkoloni wa kwanza wa visiwa hivyo. Ilibidi wenyeji wa Zanzibar kuendeleza harakati za kupigania uhuru ili kuung’oa ukoloni wa kiarabu visiwani. Harakati hizo zilifaulu tarehe 12 January, 1964 pale wazalendo wakiongozwa na chama cha Afro Shirazi walipompindua Sultani Jamshid; ambaye alifanikiwa kutoroka na kukimbilia Uingereza. Kwa jinsi hii, tarehe ya uhuru kamili wa Zanzibar ni 12 January, 1964.
1.2.5 Kuzaliwa kwa Taifa la Tanzania
Taifa la Watanzania lilizaliwa tarehe 26 April, 1964, siku Zanzibar na Tanganyika zilipoungana na kuwa nchi moja yenye dola moja la Jamhuri. Ikumbukwe kuwa japokuwa zilikuwepo sababu nyingi za nchi hizi mbili kuungana na kuwa moja, ukweli ni kuwa muungano wa nchi hizi mbili ni mfano hai na uthibitisho kuwa lengo la umoja wa Afrika linaweza kufanikiwa.
1.2.6 Mfumo wa Siasa Chama Kimoja
Baada ya kuzaliwa kwa Tanzania, yaliibuka matatizo kadhaa yaliyo kinyume na haki, hususan tatizo la udikteta na ukiritimba ya chama kimoja uliojitokeza katika nchi yetu tangu ilipojipatia uhuru wake kamili wa kisiasa mwaka 1962 (kwa upande wa Tanganyika) na mapinduzi mwaka 1964 (kwa upande wa Zanzibar). Tatizo hili ni moja tu ya sura zilizojitokea za utawala wa kibeberu ambao sasa ulikuwa katika enzi ya ukoloni mamboleo.
Kama ilivyoelezwa awali, vilikuwepo vyama mbalimbali vya siasa vilivyoshiriki harakati za kudai uhuru wa taifa letu. Hata hivyo, vyama vya siasa vilivyofanikisha hasa harakati hizo za uhuru ni Tanganyika African National Union (TANU) kwa upande wa Tanganyika, na Afro Shirazi Party (ASP) kwa upande wa Zanzibar . Baada ya hatua hii ya harakati za ukombozi, vyama hivi viwili viliingia katika njia potofu ya utawala wa kiimla na ukiritimba. Vilianza ukandamizaji wa umma, na mnamo mwaka 1965 vikapiga marufuku vyama vingine vya siasa na kujenga dola ya chama kimoja kimoja kila upande wa muungano. Utawala wa nchi tangu nyakati hizo ulikuwa mbaya kwa kuwa haukufuata sawasawa katiba ya nchi wala kulinda haki za binadamu ipasavyo.
Wakati huo huo, wakoloni wetu wa zamani waliibuka na njia mpya za kulinyonya bara la Afrika, yaani Ukoloni mamboleo (janga kuu la tatu kwa Afrika). Utawala wa chama kimoja ulishindwa kabisa kubaini mikakati na mbinu dhidi ya ukoloni mamboleo. Badala yake taifa likaingizwaa katika sera za utaifishaji wa mali binafsi na kujenga sekta kubwa ya dola (sio umma, kama ilivyodaiwa) katika uchumi na huduma za jamii badala ya kuwawezesha wenyeji wa nchi hii (umma wenyewe) kuingia katika shughuli kuu za kiuchumi na kuongoza uchumi wa nchi yao wenyewe.
Matokeo ya upotofu huo wa kisera na kiutawala yalidhihirika miongo miwili baadaye pale mashirika yaliyohodhiwa na dola yaliposhindwa kutimiza malengo yake na kuanza kufilisika. Hali ya maisha ya wananchi ilizidi kuwa duni kiuchumi vijijini na mijini. Hali hii iliandamana na kuporomoka kwa huduma za jamii kama vile elimu, afya na miundombinu ya usafirishaji, nishati na mawasiliano.
Kadhalika taifa liliingizwa katika shimo la ubadhirifu wa mali iliyopaswa kuwa ya umma, ukiritimba, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na udikiteta. Tarehe 5 February, 1977 vyama vya TANU na ASP viliungana na kuwa chama kimoja kiitwacho “Chama cha Mapinduzi” kwa kifupi CCM. Sambamba na matukio haya katiba ya nchi ilitungwa upya kuhitimisha matakwa ya muundo wa dola ya chama kimoja cha siasa. Hii ndiyo katiba inayotumika hadi leo ambayo imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara badala ya kuandikwa upya ili iwe katiba ya kudumu kama zilivyo katiba zinazoheshimika duniani.
1.2.7 Harakati za Kurejeshwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa
Kwa kuwa utawala wa chama kimoja ulijidhihirisha kuwa mbaya kiasi cha kuwa karibu kufanana na ule wa kikoloni wanamageuzi wazalendo walibuni mbinu mpya za ukombozi. Hatua ya awali ilikuwa ni kuleta ukombozi wa kisiasa utakaoliwezesha taifa kuondokana na mfumo wa siasa na utawala wa chama kimoja. Hii ilipelekea kuundwa kwa Kamati ya kupigania Mageuzi ya kikatiba nchini iliyoitwa National Committee for Constitutional Reforms (NCCR). Kamati hii iliundwa mnamo tarehe 11 na 12 Juni 1991 na wanamageuzi waliotoka kwenye sekta mbalimbali za jamii nchini.
Harakati dhidi ya mfumo wa chama kimoja nchini ziliungana na vuguvugu dhidi ya udikiteta na ukiritimba wa kisiasa kwingineko duniani. Mnamo 1992 serikali ya Tanzania ililazimika kuridhia kubomolewa kwa mfumo wa chama kimoja na kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vyingi nchini. Katiba ya nchi ilirekebishwa na kufuta mfumo wa Chama kimoja na kufungua milango kwa mfumo wa vyama vingi.
Baada ya mafanikio hayo, baadhi ya wanamageuzi waliokuwa katika kamati ya NCCR walitumia fursa ya uwepo wao katika kamati hiyo, wakuunda vyama mbalimbali vya siasa. Hatua hiyo wapo waliodhani kuwa ni mbaya kwa kuwa kwao iliashiria kuzaliwa kwa ‘utitiri’ wa vyama. Mtazamo huo hauzingatii ukweli kuwa vyama vya siasa ni vyombo vya uainishaji wa fikra mbalimbali za kisiasa zenye misingi katika falsafa mbalimbali za jinsi gani binadamu anaiona jamii, uchumi na siasa. Ni vyombo vinavyowapa wananchi uhuru wa kufuata mitazamo ya kisiasa wanayoitaka. Kila chama ni chombo cha kiitikadi na hivyo ni jambo lililokuwa la kutegemewa kuwa mara itakapokuwa halali kuunda vyama, basi vitaibuka vyama vingi kulingana na itikadi zinazoshindania fursa ya kuongoza dola.
1.3 Kuzaliwa kwa Chama cha NCCR- Mageuzi
Wanamageuzi ambao hawakuondoka ndani ya kamati ya NCCR kwa ajili ya kwenda kuunda vyama vingine, waliamua kuibadilisha kamati hiyo na kuunda chama cha Mageuzi kwa jina la NCCR-Mageuzi, mnamo tarehe 15 Februari 1992. Neno NCCR lilipewa maana mpya, yaani; National Convention for Construction and Reform. Tafsiri rasmi ya jina hili ni Chama cha Mageuzi na Ujenzi wa Taifa.
Hivyo, NCCR-Mageuzi ni chama cha siasa kilichosajiliwa mnamo tarehe 29 Julai, 1992 kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992. Kwa ujumla Chama hiki ni matokeo ya juhudi za wananchi wa Tanzania kujikomboa kutokana na ubeberu ambao umejikita katika nchi yetu tangu mwaka 1884.
2.1 Dokezo
Kwa mantiki ya jina lake Chama cha NCCR-Mageuzi kina mtazamo kwamba; Taifa letu la Tanzania linahitaji mageuzi katika mifumo mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi inayotumika nchini; na kwamba taifa letu linahitaji kujengwa upya ili lifikie maendeleo makubwa katika nyanja zote; na kwamba, falsafa na itikadi sahihi, na sera madhubuti zinazosimamiwa na chama chenye nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi, ndizo zinazoweza kujenga nchi yenye uchumi imara, jamii iliyostawi vyema na taifa lenye amani ya kweli. Ni katika mtazamo huo, chama cha NCCR-Mageuzi kinafuata falsafa na itikadi ya kipekee inayowajali watu wote yaani; UTU.
2.2 Itikadi ya UTU
Katika siku za mwanzo za kuanzishwa kwake, chama chetu kiliamua kufuata itikadi ya Demokrasia ya Kijamii, ambayo misingi yake mikuu ni, Uhuru, Usawa, Udugu, Haki na Ustawi wa jamii. Hatimaye chama kiliifanyia uboreshaji itikadi hiyo na kuanza kutumia itikadi ya UTU.
Itikadi ya UTU ina misingi mikuu ifuatayo; Udugu (Fratenity), Maadili (Ethics), Usawa (Equality and Equity), Haki (Justice), Imani (Trust), Mabadiliko/Mageuzi (Reform), Uhuru (Freedom/liberty), Wajibu (Responsibility), Asili (Human essence), Kazi (Work), na Endelezo (Sustainability). Katika kifupisho cha misingi hii tunasema; Misingi ya UTU ni UMUHIMU WAKE.
2.2.1 Msingi wa Udugu
Katika msingi huu wa kiitikadi, wanamageuzi tunaamini kuwa jamii yote ya wanadamu ni ndugu. Kwa sababu hiyo hatuna budi kuheshimu udugu huo na kuishi tukithaminiana. Hivyo mifumo yetu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi sharti itambue na kuzingatia ukweli huu. Vile vile, kwa kuzingatia msingi wa udugu, kila mwanachama wa NCCR-Mageuzi anamchukulia mwanachama mwenzie kuwa ndugu yake, na anatambua udugu alionao na watanzania wote popote walipo.
2.2.2 Msingi wa Maadili
Kwa msingi huu wa kiitikadi chama cha NCCR-Mageuzi kinaamimi kuwa, katika jamii yenye utu zipo amana za jamii za kiutu; yapo maadili ya kiutu ambayo yanaheshimika, yanazingatiwa na kuenziwa miongoni mwa watu na taasisi zao. Vile vile katika jamii yenye utu, heshima ya kila mmoja anayopewa na jamii inathamini utu wake; wema unashamiri miongoni mwa watu; kujali na kutunza ni sifa ya kila mmoja; upo ukarimu na upendo tele; kutakiana heri hakuko katika maneno tu bali hata katika vitendo; na matendo ya udanganyifu, rushwa, dhuluma, utapeli, uonevu, udhalilishaji na maovu mengine ya aina hii huwekewa alama ya ukengeufu wa utu na hutungiwa sheria na kanuni za kuyadhibiti.
Kwa msingi huu, chama cha NCCR-Mageuzi kinayo nia ya dhati ya kuakikisha maadili yanashamili nchini Tanzania iwe katika siasa, uchumi na nyanja nyinginezo. Aidha, kwa msingi huu chama kinatambua na kusisitiza uzingativu wa maadili ya kijamii na ya taaluma mbalimbali, kama vile taaluma za uganga, ualimu, uanasheria, utafiti, uandishi wa habari, na taaluma nyinginezo. Kadhalika, chama kinasisitiza uzingativu wa maadili ya viongozi na watumishi wote katika kada mbalimbali.
Chama kinatambua kuwa, katika siasa za jamii yenye utu, uongozi unachukuliwa kuwa ni alama ya mfano wa uadilifu na utu uliotukuka; Uongozi unakuwepo ili kuzidi kuiekeza jamii katika kiwango kikubwa zaidi cha utu na kuwezesha kurithishwa kwa utu huo toka kizazi hata kizazi; Wanasiasa na wote wanaopewa dhamana ya kuongoza, wanatarajiwa katika kauli zao mbele ya watu, katika utekelezaji wa majukumu yao, na katika maisha yao binafsi wawe vinara wa utu; na hawatarajiwi viongozi hawa kuwa upande wa dhuluma za kiwango chochote kile na/au aina yoyote ile, bali ni wazingativu wa sheria na kanuni za utu.
Chama kina maoni kuwa, hakika kukosa uadilifu ni kukosa utu. Leo hii mataifa yanapoendelea kushuhudia ongezeko la ufisadi, rushwa nene, ubadhilifu, uchafu wa viongozi na watumishi wa umma, ushirikina, na udhalilishaji wa akina mama na watoto, tatizo ni kuwa, wanaoshiriki vitendo hivyo wamepoteza utu. Kwa maana fisadi au mtu yoyote asiye mwadilifu hana utu, vinginevyo asingeyafungamanisha maisha yake na kuiridhisha nafsi yake kwa gharama ya kuwadhulumu wengine; asingeweza kujilimbikizia fedha na mali asizozihitaji kana kwamba yeye ni hayawani wa porini.
2.2.3 Msingi wa Usawa
Chama cha NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa watu wote ni sawa, na ni lazima mifumo ya nchi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi izingatie usawa wa binadamu. Chama kinaamini katika usawa wa jinsia, yaani wanawake na wanaume ni watu sawa. Vile vile kwa msingi huu chama kinasisitiza kuwa watu wa makabila mbalimbali, watu wa rangi tofauti, nasaba tofauti, asili tofauti za wanakotokea wote ni sawa. Hivyo, chama kinapinga kwa nguvu zote ubaguzi wa watu kwa wa namna yoyote ile, na kinalenga kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi anayekosa fursa fulani au anayetendewa tofauti na wengine kwa sababu ya rangi yake, dini, kabila, au jinsia yake.
Ni katika mantiki hii ya msingi wa usawa, kwamba chama kinapinga kwa nguvu zote mifumo yoyote inayozalisha matabaka katika jamii; matabaka au madaraja ya wenyenacho na wasionacho, walalahai na walalahoi, walaraha na walakaraha, mabwana na watwana, waheshimiwa na wadharauliwa. Lengo la kiitikadi la NCCR-Mageuzi ni kuhakikisha madaraja ya namna hiyo yanafutika katika jamii yenye UTU.
2.2.4 Msingi wa Haki
Chama cha NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa, shughuli zote za mwanadamu na mahusiano ya watu hapa duniani yanapaswa kuwa ni kwa ajili ya kuboresha hali MTU kimwili, kiakili, kiroho na kuongeza ubora wa mahusiano yake na viumbe wengine. Hivyo, mchakato wa kila shughuli afanyayo unapaswa kuwa katika namna ambayo haina dhuluma, uonevu, madhalilisho, taabu, ubaguzi, wala vikwazo kwa awaye yeyote na kwa kiumbe hai kingine chochote.
Hali hiyo ya mchakato ulio mwema wa shughuli za watu inawezekana pale tu mifumo iliyopo ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii imeelekezwa katika kiwango cha juu kabisa cha kuzingatia haki ya kila mtu. Dunia itakuwa mahali bora pa kuishi endapo tu kutakuwa na haki kila wakati, haki kila mahali, haki kwa kila mmoja.
Haki katika Uchumi: Mfumo wa uchumi unaoheshimu haki unatambua uwepo wa haki ya raslimali asili, haki ya mwenye mtaji na haki ya mwenye nguvukazi. Mfumo huu unasisitiza kwamba sharti kuwepo maridhiasawa (amicability) kati ya pande tatu; raslimali asili, mtaji na nguvukazi au kati ya pande mbili; mtaji na nguvukazi/ raslimali asili na nguvukazi; kuhusu gawio (dividend) la uzalishaji. Kwa imani hii, NCCR-Mageuzi kinakusudia kujenga uchumi wa aina hiyo.
Haki katika Siasa: Mfumo wa siasa unaoheshimu haki unazingatia utashi na uamuzi wa kila mtu, unatambua haki ya mtu kuwa mfuasi wa chama cha siasa na hiyo unaruhusu uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa na demokrasia huru katika dola moja (Multi party system and free/pure democracy) chini ya mfumo huu, maamuzi ni ya wote. Aidha, itikadi ya mtu kisiasa au kutokuwa mfuasi wa itikadi yoyote haiwi sababu ya yeye kubughudhiwa katika nchi yake, kunyimwa ajira ya utumishi wa umma au kupewa dhamana ya uongozi wa umma uwe wa kuchaguliwa au kuteuliwa. Kwa imani hii, NCCR-Mageuzi kinakusudia kujenga siasa za demokrasia huru nchini Tanzania.
Haki katika Jamii: Mfumo wa jamii unaoheshimu haki unazingatia unamthamini kila mwanajamii; awe mwenye uwezo na nguvu mwilini, au mzee, mgonjwa na ama mtoto, au mtu wa jamii fulani kati ya jamii kadhaa kulingana na tamaduni za watu. Mahali ambapo mfumo haki umesitawi hakuwezi kujitokeza tena hali ya kukandamizwa kwa baadhi ya jamii za watu kama ilivyowahi kutokea na inavyoendelea kujitokeza katika historia ya dunia yetu. Mfumo wa jamii wenye haki huwapa hifadhi wenye udhaifu utokanao na magonjwa, udhaifu wa viungo (ulemavu) au umri. Ni kwa msingi huu, NCCR-Mageuzi inalo kusudio la kuwapa hifadhi ya uhakika wanajamii wote nchini Tanzania.
Haki katika sheria: palipo na haki, sheria zote katika nchi sharti zizingatie haki za binadamu na viumbe hai wengine, kwa mfano, haki ya uhai. Sheria zote sharti zipimwe kwa viwango vya haki kama zinavyozingatiwa na katiba ya nchi na katika miafaka/matamko ya kimataifa. Haki hii inazingatia usawa tulionao; kwamba watu wote wana haki sawa, na wako sawa mbele ya sheria.
2.2.5 Msingi wa Imani
NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa, katika jamii yenye UTU kuna kiwango kikubwa cha kuaminiana kati ya wanajamii. Ni kwa msingi huu, mtu awapo safarini ugenini anaweza kuamini kupata hifadhi mahali alipofikia na mwenyeji wake anaweza kuaminika kwamba atatenda utu kwa wale waliofika kwake. Kadhalika imani ndio utuongoza katika kupokea na kutoa huduma mbalimbali zitolewazo katika taasisi za huduma. Hapa waweza kuchukuliwa mfano wa imani ambayo mgonjwa anampa dakitari wakati wa huduma ya utabibu. Ni sharti kwa pande zote mbili katika jamii yenye UTU kutunza imani hiyo.
Katika siasa, viongozi hupewa dhamana ya uongozi kwa Imani, wanao wajibu wa kuitunza imani hiyo (wasiwe wasaliti wa umma). Katika uchumi, imani kati ya walaji/wahitaji na wagavi isipotunzwa, uchumi huingizwa katika vitendo vya kitapeli, uhujumu, utakatishaji fedha, bidhaa bandia na maovu mengineyo. NCCR-Mageuzi kinapigania kujengeka kwa imani katika jamii.
2.2.6 Msingi wa Mbadiliko
NCCR-Mageuzi kinaamini kwamba, ili kujenga jamii yenye utu, mifumo (iliyopo) ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii inahitaji mabadiliko (mageuzi)chanya. Ni kwa sababu hii pia, kwamba chama kilipewa jina hili; NCCR-Mageuzi. (Rejea maelezo ya awali katika sura hii ya pili). Katika kuleta mabadiliko, tathmini ya njia zinazotumika huitajika ili kubaini udhaifu na uimara na hivyo kutambua wapi parekebishwe.
Upo usemi maarufu kuwa; ‘Kitu pekee duniani ambacho hakibadiliki, ni mabadiliko.’
2.2.7 Msingi wa Uhuru
NCCR-Mageuzi kinaamini kwamba, kila mmoja wetu amezaliwa huru. Hivyo katika jamii inayotambua hilo, ni mwiko kumfanya mtu yeyote mtumwa wa mtu mwingine, ni mwiko kutoa adhabu za kudhalilisha (degrade) utu wa mtu. Kukamatwa, kutiwa kizuizini (detention), kupelekwa uhamishoni (exile) ni kinyume na msingi wa utu wa uhuru. Wanamageuzi tunathamini na kuheshimu Uhuru binafsi , na haki yake ya kuwa na faragha na usalama, kwenda utakako, kutoa maoni, kuwa na imani utakayo, kushirikiana, na kushiriki katika mambo halali amabayo mtu anayataka.
2.2.8 Msingi wa Wajibu
NCCR-Mageuzi kinaamini kwamba, kila mtu mwenye utu pamoja na kuwa na stahili ya haki zake anao wajibu wa kutimiza katika haki hizo. Msingi huu pia unaimiza uwajibikaji na utimizaji wa majukumu ambayo kila mmoja wetu anapewa katika nafasi yake.
2.2.9 Msingi wa Asili yetu
NCCR-Mageuzi kinaamini kwamba, asili yetu wanadamu (essence) ndio inayopaswa kuongoza jamii, siasa na uchumi wetu. Yatupasa kujitambua sisi ni kina nani na tuko katika sayari ya dunia kwa sababu gani, na je, tuna tofauti gani na viumbe vingine. Japo sisi ni viumbehai kama walivyo viumbehai wengine, kwa asili yetu tunajua jema na baya. Hivyo kuishi kwetu na jinsi tunavyohusiana na viumbe wengine hakuwezi kuwa katika namna ambayo ni sawa na matendo ya hayawani wa mwituni.
Tunapaswa Kutosheka badala ya kutawaliwa na Tamaa; kusimamia Ukweli dhidi ya Uongo; Uaminifu dhidi ya Wizi; Upendo dhidi ya Uuaji; Usafi dhidi Uchafu; Heshima dhidi ya Dharau; na Usahihi dhidi ya Upotofu.
2.2.10 Msingi wa Kazi
NCCR-Mageuzi kinaamini kwamba, kila mtu anapaswa kufanya kazi (isipokuwa katika hali ya ugonjwa au kutoweza kwa sababu ya umri wa utoto/uzee). Kama alivyopata kutamka, mwasisi wa Taifa la letu la Tanzania; Kazi ni Kipimo cha Utu.
Kwa msingi huu, chama kinawaimiza watu wote kufanya shughuli za halali ili kujipatia riziki, kinapinga uzururaji na unyonyaji. Vile vile chama kinalo lengo la kuhakikisha kwamba, nguvukazi ya taifa inatumika ipasavyo, na kunakuwepo na upatikanaji wa ajira za kutosha.
2.2.11 Msingi wa Endelezo
NCCR-Mageuzi kinaamini kwamba, shughuli za kiutu za mtu zinapaswa kuwa katika namna ambayo si ya madhara kwa uhai wa watu, viumbe wengine na chochote kilichomo katika mazingira/raslimali.
Mtu mwenye utu, hachukulii udhuru wa mahitaji yake yatokanayo na mazingira kumfanya awe mharibifu wa kila kilichomo katika mazingira yake, bali mahitaji ya kiutu hutoshelezwa kwa namna ya kistaaarabu .
Hayawani wasio na utu, hawashangazi wanapokuwa wakatili katika harakati zao za kujitafutia mahitaji na wala hawatambui kama wanafanya ukatili. (Chukulia mfano wa chui katika mbuga za Serengeti na kwingine, jinsi maisha yake yanavyoongozwa na sirika ya kuua takribani kila mnyama mnyonge anayekatiza mbele yake hata kama tayari amekwisha kupata kimtoshacho kwa ajili ya siku. Ataendelea kuua tu hata asivyovihitaji, na huo ndio uhayawani halisi)
Tunahitaji kuwa na maendeleo endelevu.
Mtu mwenye utu hawezi kufanya vitendo vya kimaendeleo bila kuzingatia manufaa yake kiutu. Hivyo, maendeleo ya viwanda na technolojia, kama ni ya madhara kwa watu, basi hayo si maendeleo ya kiutu bali matumizi ya kiayawani ya karama ya maarifa. Vile vile, ugunduzi wa technolojia sio ukamilifu wa mambo bali ukamilifu wake ni uboreshaji wa utu wa mtu.
Dunia ya leo inalia juu ya ongezeko la joto duniani, uharibifu wa mazingira na matatizo mengine, kama vile machafuko, vita na mauaji ya mtu mmoja mmoja na ya kimbali, ugaidi, uvamizi na ukaliaji wa kimabavu wa nchi moja dhidi ya nyingine, na Utengenezaji wa silaha za maangamizi (WMD), nyukilia, za kibaiolojia na nyinginezo. Tatizo kuu linalosababisha haya ni kwamba, mtu kaacha au kapunguza uhusiano wake wa kiutu na mazingira yake.
Mtu mwenye utu si mtumiaji wa rasilimali kana kwamba hakuna kesho, ufujaji wa aina yoyote ile si utu. Mtu mwenye utu hawezi kuthubutu kuanzisha moto wa pori ili uteketeze mbuga, misitu, viumbe-anuai, na vyanzo vya maji.
Mtu mwenye utu hawezi kudiriki kuachia taka zenye sumu ziiharibu ardhi, ziyachafue maji na hewa chafu iendelee kuzalishwa kwa wingi toka viwandani.
Kukosekana kwa utu kunamfanya mtu asione mbele na wala asitambue uhusianao wa uhai wake na uhai wa viumbe wengine. (balance of the eco system, and biodiversity)
2.3 Nguzo za Itikadi ya Utu
Nguzo kuu (mojawapo) ya ikitikadi yetu ni Demokrasia. Nguzo hii ya ina maana kuwa katika taifa lenye utu, dola huundwa na hutawala kwa ridhaa na kwa ushirikishwaji wa wananchi. Wanamageuzi hawawajibiki kuitambua wala kushirikiana na serikali inayoingia madarakani kinyume na taratibu za kidemokrasia.
Kisiasa, ridhaa ya wananchi huanishwa kwa uchaguzi wa viongozi kila baada kipindi cha miaka kadhaa, kilichowekwa kikatiba. Uchaguzi lazima uwe huru na wa haki na utoe nafasi kwa wote kushiriki kuchaguliwa na kuchagua. Kushiriki katika uongozi wa nchi kupitia vyama vya siasa ni moja kati ya njia nyingi za kuwawezesha wananchi kujenga hoja kisiasa, kuchagua viongozi na kuongoza nchi. Hata hivyo si halali kuzuia ushiriki wa mtu katika uongozi wa nchi ati kwa kuwa ushiriki wake haukupitia katika vyama vya siasa.
Dola linalozingatia demokrasia ni dola shirikishi ambalo linatambua na kushirikisha wadau wengine kama vile mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta ya habari na jumuiya za kidini katika shughuli na maendeleo ya nchi.
Demokrasia katika Uchumi
Nguzo ya demokrasia huakikisha utoaji wa fursa sawa za kiuchumi kwa kila raia. Wanamageuzi tunaamini kuwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii yatapatikana kwa haraka na ufanisi kama wananchi wenyewe badala ya dola watamiliki na kuendesha shughuli za kiuchumi. Vile vile, kulingana na nguzo hii, chama cha NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa jukumu kuu la dola ni kuwawezesha wananchi kumiliki na kuendesha njia kuu za uchumi wa taifa.
Historia ya uchumi wa dunia inaonesha kwamba njia kuu na halali ya kukusanya mtaji wa taifa ni kupitia kodi inayokusanywa na serikali. Hivyo maendeleo ya kiuchumi ya taifa hutegemea sana jinsi kodi inavyotumika. Taifa linalokusanya kodi kwa ufanisi na kutumia sehemu kubwa ya kodi hiyo kama mtaji kwa kuwawezesha kimtaji raia wake kujasiriamali ndilo litakalofaulu kumudu changamoto za utandawazi.
Pamoja na kodi, kila nchi imejaliwa rasilimali za asili. Maendeleo ya kiuchumi ya taifa hutegemea sana jinsi taifa linavyomiliki na kudhibiti uvunaji wa rasilimali za asili kama vile madini, wanyama, mazao ya misitu na ardhi. Ili kuliweka jambo hili wazi, mnamo mwaka 1966 Umoja wa Mataifa ulipitisha Mkataba wa kimataifa kuhusu haki ya wananchi katika kila nchi kumiliki rasilmali za asili zinazopatikana katika nchi zao. Haki hii ni pamoja na kumiliki na kuendesha uchumi wa nchi zao. Mkataba huu wa kimataifa ulizitaka serikali katika kila nchi kudhibiti uwekezaji wa mitaji ya makampuni ya kibeberu ili kuzuia tabia ya makampuni haya kunyonya utajiri wa nchi changa na kuharibu mazingira.
Kwa kuzingatia nguzo hii, NCCR-Mageuzi kinalo kusudio la kujenga uchumi wa nchi kutoka uchumi hoi wa kijima kwa kutumia angalau asilimia kumi ya pato la taifa kuwawezesha wazalendo wa nchi kujasiria mali. Chama kitahakikisha kuwa serikali yake inaunda mfuko maalumu wa kuwawezesha wananchi kujasiria mali . Mfuko huu utakuwa wa programu kadhaa zinazolenga makundi mbalimbali ya jamii ikiwa ni pamoja na programu ya kuwawezesha wananchi kujasiria mali.
Kuna umuhimu wa kipekee wa kuwepo demokrasia katika uchumi. Katika mazingira ya kitanzania na kutokana na historia yetu, idadi kubwa ya raia wenyeji waishio majini na vijijini walinyimwa fursa ya kushiriki katika uchumi wa taifa kupitia soko.
Katika historia ya nchi yetu, kwa makusudi ya kisera na sheria, wakoloni walibagua rangi na hata makabila ili kuwagawa wananchi na kuwatawala. Wazungu walipewa daraja la kwanza, waasia, wasomali na wakomoro walipewa daraja la pili na waafrika walipewa daraja la tatu. Waliokuwa daraja la kwanza na la pili waliruhusiwa kupitia sera na sheria kumiliki mali isiyohamishika (ardhi) kwa hati iliyosajiliwa na serikali na hivyo waliruhusiwa kukopa benki. Hii iliwawezesha kuwa na mtaji wa kushiriki kwenye uchumi wa soko. Hawa walitajirika na kuwa wamiliki wa makampuni na viwanda. Waliokuwa daraja la tatu hawakuruhusiwa kumiliki mali isiyohamishika, hivyo hawakuwa wanaweza kukopeshwa na mtu au benki yoyote. Sheria na sera za nchi ziliwataja waafrika kuwa hawana sifa ya kukopeshwa, na ardhi waliyokuwa wanakalia ilikuwa chini ya sheria milki ya mila ambayo haina sifa ya kusajiliwa na kutumika kama rehani ya kuchukulia mikopo. Aidha ilikuwepo sheria ya kikoloni iliyopiga marufuku waafrika wasikopeshwe mtaji na mabenki. Sheria nyingine ya kikoloni ilipiga marufuku mauzo ya ardhi kati ya wageni na wenyeji wa asili ya kiafrika. Kwa jinsi hii waafrika walikuwa hawana njia halali ya kupata mtaji wa kushiriki katika uchumi wa soko. Wengi wao walibakia vibarua katika makampuni, mashamba na viwanda vilivyokuwa vikimilikiwa na wazungu na waasia. Hiki ndicho kiini cha umaskini wa waafrika na utajiri wa wazungu na waasia katika nchi yetu.
Baada ya uhuru, baadhi ya sheria hizo zilizomkandamiza mwafrika zilifutwa au kupuuzwa na watu weusi wakaanza kuinukia kiuchumi. Hata hivyo kwa kiasi kikubwa hali ilibakia kama vile ilivyokuwa wakati wa ukoloni. Sera za “sisi kwa sisi” (Africanisation) zilikomea kwenye kubadili sura za wazungu na waasia katika nafasi za kisiasa na utawala wa dola. Sera hizo hazikutekelezwa kwenye sekta ya uchumi. Hakuna hatua zozote za makusudi zilizochukuliwa kuwawezesha waafrika ili nao waingie katika uchumi wa soko. Chama cha NCCR-Mageuzi kimebuni sera zenye mwelekeo wa demokrasia katika uchumi kwa makusudi ya kuwapa usawa wa kiuchumi raia wote halali, waafrika walio wengi hali kadhalika wazungu na waasia walio pia wenyeji wa nchi hii. Sera zenye mtazamo demokrasia katika uchumi zinatambua kuwa ukoloni uliwajeruhi waafrika kwa kigezo cha rangi yao na hivyo kuwafanya vilema katika uchumi wa soko. Hivyo sera hizi zinakusudia kuwatibu waafrika ili waweze nao kuingia kwenye uchumi wa soko bila kuwabagua wenyeji wengine katika kuendelea kiuchumi.
Kukosekana kwa usawa na demokrasia katika uchumi, ni kisababishi kimojawapo cha umaskini wa wananchi walio wengi. Wanamageuzi wa NCCR-Mageuzi tunaamini kuwa umaskini wa wananchi walio wengi unahatarisha amani na mshikamano wa wananchi. Tutake tusitake taifa haliwezi kuendelea kuwa na umoja na amani ikiwa sehemu kubwa ya raia wake ni maskini hohehahe wakati huo huo watu wachache katika nchi hii ni matajiri kupindukia. Hatari hii ipo bila kujali kuwa umma wa maskini ni wa rangi au kabila moja wakati wachache matajiri wana rangi tofauti.
Hivyo ili kulinda amani na umoja wa taifa ni wajibu wa dola kuchukua hatua za makusudi za kusaidia waafrika ili waweze kwenda sambamba na makundi mengine katika kunufaika na raslimali na mali asili za nchi yetu. Demokrasia ya kiuchumi ni vita dhidi ya ubaguzi wa raia katika kumiliki, kuendesha na kufaidika na uchumi.
Demokrasia katika Jamii
Pamoja na kuamini katika serikali yenye mamlaka, haki za kisiasa na kijamii za wananchi lazima ziheshimiwe. Katika uongozi utakaoundwa na wanamageuzi, raia atakuwa na haki za kutoa mawazo yake mahali popote bila vitisho vya dola mradi asivunje sheria. Raia awe na uhuru wa kuabudu na kufuata dini yeyote apendayo. Raia atakuwa na haki za kushirikiana na raia wengine katika vikundi mbalimbali, vyama vya siasa, bila vitisho vya dola.
Uongozi wa wanamageuzi utavipatia Vyombo vya habari uhuru wa kutafuta, kuandika na kupasha habari. Kadhalika uongozi utatunga sheria ya nchi inayowajibisha taasisi za umma kutoa habari.
Nguzo nyinginezo za itikadi yetu ya UTU ni Maendeleo, Maelewano, Umoja na Amani. Ni kwa kuamini katika nguzo hizo, chama kimekuwa kikitumia kauli mbiu kama vile;
- Demokrasia na Maendeleo (kaulimbiu iliyoko katika nembo ya chama),
- MMUA (kaulimbui inayomaanisha; Maendeleo, Maelewano, Umoja na Amani)
- Pamoja Tutashinda (kaulimbiu inayosisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwetu wapigania haki za wengi na maslahi ya Taifa) na
- Ishara yetu ya salamu kwa Kupunga Mkono, ni alama kwamba chama chetu ni cha Amani.
2.4 Hitimisho
Kwa kuzingatia misingi na nguzo za UTU tunaamini tutaijenga nchi na jamii iliyo bora kabisa kwa munufaa ya wananchi wote. Hakika UTU ndio njia ya pekee ya kulifikisha taifa letu katika mema hayo; yaani ustaarabu wa hali ya juu katika Taifa, Maendeleo makubwa ya kiuchumi, Demokrasia halisi, na Utengemano katika jamii.
Wajibu wa dola katika nchi inayoendeshwa kwa misingi ya utu ni kulinda uhuru na maslahi ya wananchi dhidi ya maadui wa nje na ndani, kulinda usalama wa maisha na mali za watu, kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa jamii, na kutoa fursa sawa kwa watu wote kujipatia riziki zao kwa njia halali.
Katika nyakati hizi za utandawazi, nchi inayoongozwa kwa misingi ya utu huwa na katiba, sheria na sera zinazolenga kuwawezesha wananchi kisayansi, kitekinolojia na kimtaji ili kumudu changamoto za ujasiriamali katika soko la taifa na soko la dunia.
Ikitadi hii ya UTU ndio mwongozo wa sera za chama, zinazoelezwa katika sura zinazofuata.
3.1 Dokezo
Katika sura hii, kuna maelezo ya mtazamo na sera za NCCR-Mageuzi kuhusu masuala ya kiutawala, hususan kuhusu uwepo wa katiba bora ya nchi, sheria zinazosimamia haki na muundo bora wa dola.
3.2 Katiba ya Nchi
Katiba ndiyo sheria kuu ya nchi inayoainisha uamuzi wa wananchi wanavyotaka kuishi na kuongozwa. Katiba huunda dola na vyombo vyake kisha kuvikabidhi vyombo hivyo mamlaka ya utawala. Katiba huweka mipaka ya vyombo vya dola na misingi ya utawala.
Kutokana na umuhimu wake katika maisha ya jamii, utungaji wa katiba ni lazima uhusishe na kushirikisha wananchi wote. Mtazamo kwamba Bunge linatosha kutunga na kurekebisha katiba siyo mtazamo sahihi kwa kuwa Bunge lenyewe ni muhimili wa dola unaoundwa na katiba.
Hivyo, chombo halisi cha kutunga katiba katika jamii yoyote ile ni wananchi wenyewe. Jinsi ya wananchi kujipanga ili kutekeleza tendo la kutunga katiba yao hutofautiana nchi hadi nchi mradi kwamba ushirikishwaji mpana kadri inavyowezekana uzingatiwe. Katika nchi nyingi mtindo unaokubalika ni kuwashirikisha wananchi kupitia baraza la kutunga katiba (constituent assembly).
Baraza la kutunga katiba huundwa na wajumbe wanaowakilisha sekta zote za jamii pamoja na wabunge walio kwenye Bunge la taifa. Mara kitendo cha kutunga katiba kinapotimia, baraza la kutunga katiba hujivunja hadi itakapolazimu tena kutunga katiba nyingine au kufanya marekebisho ya katiba iliyopo.
Aidha, chama cha NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa njia njema ya kutatua migogoro ya kikatiba ni kwa kuunda mahakama ya katiba yenye mamlaka ya kuamua migogoro hiyo bila kuingiliwa na wanasiasa. Hivyo taifa linapaswa kuwa na mahakama ya kudumu ya katiba yenye uwezo wa kusikiliza mashauri ya kikatiba yanayoletwa na raia binafsi, taasisi za dola na taasisi zisizo za kiserikali.
NCCR-Mageuzi ikipewa ridhaa ya kuongoza nchi itahakikisha Tanzania inajipatia Katiba Mpya (tofauti na ile ya mwaka 1977) kwa njia ya mkutano wa kitaifa utakojadili katiba hiyo, kisha katiba mpya kukubaliwa kwa kura ya maoni na kupitishwa na baraza la katiba ambalo litajumuisha wabunge na wawakilishi wa sekta muhimu katika jamii ya watanzania na kuondoa vikwazo katika utekelezaji wa mageuzi. Katiba Mpya (Stahiki) inapaswa kuwa na mambo yafuatayo: Kuanisha maadili ya utaifa; Kupanua uwakilishi wa wananchi katika vyombo vya maamuzi ili kuleta usawa kati ya wanaume na wanawake; Kumtambua kila raia na kumpa haki ya kupewa kitambulisho; Kuanzisha mahakama ya kudumu ya kushughulikia mashauri ya kikatiba; Kulipatia Bunge nguvu ya kuwa chombo cha kutetea maslahi ya wananchi kuwa na uamuzi wa mwisho kulidhia mikataba kupitisha au kukataa uteuzi wa viongozi; Kuunda serikali shirikishi; Kutoa hakikisho la madaraka ya uhuru wa mahakama; Kulinda na kuendeleza maliasili za Taifa; Kuruhusu ushiriki huru katika siasa kwa kila mtu bila kulazimika kuwa ndani ya chama cha kisiasa; na Kutambua sekta ya habari kama mhimili wa nne wa dola.
3.3 Sheria Zinazosimamia Haki
Chama cha NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa ili kuwa na utawala bora lazima nchi iendeshwe kwa misingi ya sheria na haki. Mfumo wa sheria na misingi ya haki inayotumika hivi sasa nchini Tanzania iliwekwa na utawala wa kikoloni. Kwa kuwa sheria ni tamko rasmi la kidola kuhusu masilahi ya kiuchumi na kijamii ya tabaka tawala, ni nadra kwa sheria ya kikoloni kulinda masilahi ya kiuchumi na kijamii ya watawaliwa. Ni kutokana na ukweli huo sheria nyingi za nchi yetu bado zinalinda masilahi ya ubeberu na kuwakandamiza wananchi.
Wajibu wa wanamageuzi ni kubadili mfumo wa sheria na misingi ya haki inayofifilisha na kupora haki za wananchi. Katiba ya nchi italikataza Bunge kutunga sheria inayoonea, kupora au kufifilisha haki za binadamu za raia.
Aidha, chama cha NCCR-Mageuzi kikishika madaraka ya dola yafuatayo yatafanyika kuhusiana na sheria;
- Kufuta sheria zote kandamizi zinazotumika nchini,
- Kutafsiri sheria zote zilizopo katika lugha ya Kiswahili,
- Kuandika upya sheria ya ardhi ili ardhi ya mila isilipiwe kodi
- Kurekebisha sheria ya serikali za mitaa ili kuziimarisha serikali hizo, na
- Kuunda upya mfumo wa mahakama kwa lengo la kulinda haki za raia waishio vijijini hadi mijini.
3.4 Mamlaka na Muundo wa Dola
Kwa kuzingatia umuhimu wa kutoa huduma muhimu kwa jamii, wanamageuzi tunaamini kuwa serikali yenye nguvu ni muhimu katika kuwaongoza wananchi kujipatia maendeleo. Hata hivyo imedhihirika mara nyingi kuwa mtu mmoja au kikundi kidogo kikipewa madaraka yote kuna hatari ya kuminywa kwa uhuru wa wananchi.
Chama cha NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa madaraka bila mipaka yana tabia ya kulewesha. Ili kuepusha hilo, wanamageuzi tunaamini kuwa, ni lazima kuwepo mgawanyo wa madaraka kati ya vyombo rasmi na visivyo rasmi vya dola. Kwa jinsi hii;
Bunge liwe na mamlaka kamili ya kutunga sheria, kuainisha sera za nchi na kuwa chombo cha maamuzi ya nchi kwa ujumla.
Serikali iongoze na kutekeleza sheria, sera na maamuzi ya taifa
Mahakama iwe huru na ipewe mamlaka kamili ya kuamua migogoro katika jamii.
Vyombo vya habari: viwe na uhuru kamili wa kupata habari na kuzitangaza na kukosoa utendaji wa vyombo rasmi na visivyo rasmi vya dola.
Taasisi zisizo za kiserikali: Hivi sasa kuna ongezeko kubwa wa taasisi zisizo za kiserikali nchini (NGOs). Taasisi hizi zimekuwa tegemezi kwa misaada kutoka nje. Pia haya ni matokeo ya serikali kuwapiga vita na kuwapuuza wasomi nchini hasa kutowalipa mishahara inayolingana na gharama za maisha. Serikali ya sasa haina sera ya kuzisaidia taasisi zisizo za kiserikali, wala wananchi. NCCR-Mageuzi katika kukuza na kuendeleza demokrasia nchini itahakikisha kwamba taasisi zisizo za kiserikali, vyama huru vya kijamii, taasisi za kidini na vyama huru vya wafanyakazi na wakulima vitapewa nafasi na uhuru wa kuendesha shughuli zake na kuchangia maendeleo ya taifa kwa mujibu wa sheria. Serikali ya NCCR-Mageuzi itazikuza na kuzipa misaada taasisi zisizo za kiserikali ili ziweze kutoa mchango wake katika maendeleo ya jamii. NGOs ziwezeshwe kisera, kisheria na kimtaji kutekeleza majukumu muhimu ya jamii ambayo serikali imejiondoa kuyafanya.
Jumuiya za kidini: ziwe na uhuru wa kuendeleza imani mbalimbali za wanajamii kwa amani na ziwajibike pamoja na taasisi nyingine za malezi ya taifa kulinda na kuendeleza maadili ya taifa.
Mgawanyo wa mamlaka ya dola utapiwa upya na Bunge ili kuainisha uwiano wa uhuru na mamlaka ya serikali za majimbo (Tanganyika na Zanzibar) kwa upande mmoja na serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa upande mwingine. Kwa jinsi hii mgawanyo wa mamlaka ya dola ufafanuliwe kikatiba katika ibara zinazoainisha mamlaka na uhuru wa serikali za mitaa kwa upande mmoja na yale ya serikali kuu na serikali za majimbo kwa upande mwingine.
3.5 Muundo wa Muungano
Kutokana na ukweli kuwa Tanzania ni taifa linalotokana na muungano wa watu wa Zanzibar na watu wa Tanganyika, ni vyema muundo wa dola uchukue umbile la shirikisho badala ya serikali kuu moja au mbili. Sera ya NCCR-Mageuzi ni kuunda Serikali tatu, adilifu, zenye ufanisi na zinazowajibika kwa wananchi. Serikali ya Muungano itakuwa na mamlaka juu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Serikali mbili (moja kila upande wa muungano) yaani serikali za Tanganyika na Zanzibar zitaitwa serikali za majimbo zenye mamlaka juu ya mambo yasiyogusa muungano. Kama ilivyotajwa awali hili litazingatiwa katika katiba ya nchi.
4.1 Dokezo
Katika sura hii, kuna maelezo kuhusu sera za NCCR-Mageuzi za Uchumi na masuala ya Fedha. Sura hii inaanza kwa mapitio mafupi ya hali ya ya Uchumi wa Taifa letu, kisha inaeleza sera mbalimbali za chama.
Uchumi wa Tanzania unaenda harijojo. Takwimu mbalimbali za miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kwamba idadi ya watu nchini inakua kwa asilimia takribani 3 kila mwaka wakati ukuaji wa uchumi haujazidi asilimia 7 kwa mwaka. Ongezeko la watu mijini sasa linazidi uwezo wa serikali kupanga maendeleo ya miji. Jiji la Dar es Salaam kwa mfano, limekuwa na ongezeko la kutisha la wakazi. Mwaka 1967 jiji la Dar es Salaam lilikuwa na wakazi 272,821. Hawa waliongeza hadi kufikia 1,300,000 mwaka 1988 na mwaka 1999 walifikia watu 2,500,000. Miaka ya karibuni wanakadiriwa kufika milioni 4.
Jiji la Dar es Salaam linakua kwa kasi ya asilimia 8 kwa mwaka wakati miji mingine inakuwa kwa kasi ya asilimia 4 kwa mwaka. Ongezeko hili linaashiria kuporomoka kwa maendeleo katika maeneo mengine ya nchi, hususan vijijini. Vijana wengi sasa hukimbilia mijini kujitafutia ajira. Vijijini hakuna uchumi wa kuwasetiri tena. Mijini nako hakuna ajira. Sekta ya umma imefilisika. Viwanda vimefungwa na au kuuzwa kwa wageni. Kwa hiyo matumaini yamekwisha vijijini na hata mijini. Hiki ndicho chanzo cha fujo na ghasia, uvutaji bangi, ubwiaji wa madawa ya kulevya, uhuni na umalaya. Kama tutakavyoona baadaye huduma za jamii zimeporomoka.
Serikali za awamu ya pili na ya tatu zilikubali masharti ya shirika la Fedha duniani (IMF) kunadi rasilimali zetu ili tusamehewe madeni. Awali ya yote wananchi walipaswa kufahamishwa madeni hayo nani kakopa na fedha zilitumikaje? Kwa nini serikali ya awamu ya tatu na sasa ya nne hazikudai haki ya kuthibitisha kama mikopo inayodaiwa kweli ilitufikia watanzania? Kwa nini tubambikiziwe madeni na tukubali kulipa kama mabwege? Kwa kuwa serikali iliyopo haijaweza kutafuta majibu ya maswali haya, hii ni sababu nyingine ya haja ya kuundwa kwa serikali inayotokana na chama cha NCCR-Mageuzi, chenye nia ya kutafuta majawabu na suluhu ya tatizo la madeni.
Iwe iwavyo, ukweli ni kwamba kuingizwa kwa Tanzania katika mpango wa kusamehewa madeni siyo sifa wala ufumbuzi wa matatizo yetu ya kiuchumi. Dawa ya matatizo yetu ni kuondoa utawala mbovu na kusimamia vizuri uchumi wetu.
Chama cha NCCR-Mageuzi kinatambua fika athari za kutegemea mikopo na misaada kutoka nje. Msimamo wa NCCR-Mageuzi ni kwamba chama kitakapopewa ridhaa na wananchi kuunda serikali hakitakubali kulazimishwa kufuata masharti yanayoliangamiza taifa. Kamwe Serikali inayoundwa na NCCR-Mageuzi kwa niaba ya taifa haitakubali kuuza utu na heshima ya watu wa taifa hili, eti ili kupata mikopo na misaada kutoka nje. Juhudi za NCCR-Mageuzi na serikali yake zitakuwa kujenga uchumi unaojitegemea na kuliondolea taifa aibu ya kuwa ombaomba wa kimataifa.
Msimamo wa NCCR-Mageuzi ni kwamba kitaendelea kuheshimu na kulinda mikataba ya kimataifa ambayo ina manufaa kwa taifa letu. Chama kitadumisha ushirikiano mzuri na nchi marafiki kwa nia ya kujenga upya uchumi unaojitegemea kwa kuzingatia maslahi ya taifa.
Aidha, pato la Taifa chini ya serikali ya sasa limeendelea kudidimia. Hii ni kwa sababu ya serikali kukosa taratibu imara za kusimamia shughuli za uchumi. Vile vile ufisadi uliokithiri umeliweka pato la taifa mifukoni mwa wachache. Pato la taifa ni muhimu sana katika maendeleo ya jamii. Serikali itakayoundwa na NCCR-Mageuzi itasimamia kikamilifu suala hili muhimu kwa kukusanya kodi zinazostahili na kupunguza matumizi ya serikali. Aidha serikali ya NCCR-Mageuzi kupitia vyombo kama vile Benki Kuu na Wizara ya Fedha itahakikisha kwamba thamani ya fedha yetu inalindwa na mfumuko wa bei unadhibitiwa.
Kuhusu kodi, NCCR-Mageuzi inatambua umuhimu wa kodi katika kuiwezesha serikali hujiendesha na kusukuma mbele maendeleo. Hata hivyo tunaona kama kodi tunayolipa aidha inaisha IMF kulipia madeni au inafujwa na serikali. Hatuoni kodi yetu ikijenga shule mpya bora, hospitali mpya bora, barabara mpya zilizo imara au hata ikikidhi haja ya mishahara ya watumishi wa umma. Nyingi ya shule mpya, hospitali au barabara zinatokana na mkopo kutoka nje. Sasa kodi yetu inakwenda wapi? Serikali itakayoundwa na NCCR-Mageuzi itahakikisha inamnufaisha mlipakodi kwa kodi anayolipa. Kodi itakuwa ni kwa ajili ya ubora wa huduma za jamii na miundombinu.
4.2 Sera ya Fursa sawa katika Uchumi
Tathmini ya hali: NCCR-Mageuzi kinatambua ukweli kwamba raia wa nchi yetu kwa asili zao wanatokana na makundi mawili. Kundi la kwanza ni la raia wenyeji ambao asili yao ni weusi. Kundi la pili ni raia wenye asili ya kigeni, wengi wao wakiwa na asili ya kiasia. Makundi haya ni raia halali wa nchi yetu wenye haki sawa kikatiba.
Katika Mageuzi ya siasa yaliyotokea nchini mwetu, ajenda mpya zinazolenga kwenye usawa baina ya makundi mbalimbali zimekuwa changamoto kubwa na hatua mbalimbali zimechukuliwa kujibu ajenga hizo. Kwa mfano, ajenda ya usawa kijinsia na haki za watoto imepelekea kuanzishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto. Kwa sasa nchi yetu leo imekabiliwa na hoja ya usawa na haki za kiuchumi miongoni mwa raia wa Tanzania .
Kama ilivyoelezwa awali, uchumi wa kikoloni haukuwa na usawa. Uchumi huo ulifuatiwa na uchumi hodhi baada ya kutangazwa ka Azimio la Arusha hapa nchini, kulikoleta mwelekeo mpya katika umilikaji wa uchumi wetu. Biashara zilizokuwepo za kigeni na zile za Watanzania wenye asili ya Kiasia zilitaifishwa. Lakini hazikuwekwa katika mikono ya wananchi walio wengi bali katika miliki ya serikali. Ndio maana NCCR-Mageuzi inatamka wazi kuwa uchumi haujawahi kuwekwa mikononi mwa Wananchi. Kufuati azimio la Arusha Wafanyabiashara wenye asili ya kiasia walibadili mbinu za kibiashara kwa kuanza kufanya biashara na mameneja wa mashirika yaliyodaiwa kuwa ya umma. Wao waliendelea kutajirika wakati wananchi wengi wa asili ya kiafrika walibaki pale pale. Hata mameneja wetu kimsingi walibakia pale pale, sana sana waliambulia fedha taslimu mifukoni na kushiriki maisha ya anasa bila kumiliki mali au biashara. Ilipofika mwishoni mwa miaka ya themanini, (enzi ya mfumo ruksa), ndipo baadhi yao walitumia zile fedha taslim kujenga mahekalu ya makazi, lakini bado hawakuingia katika kumiliki uchumi wa nchi hii. Miaka ya hivi imeingia enzi ya ubinafsishaji, watanzania tumeshuhudia makampuni yaliyomilikiwa na serikali yanauzwa ama kwa raia wenye asili ya kiasia au kwa wageni kutoka nje tu, wazawa wa nchi hii wanabaki pale pale wakiwa watazamaji. Kinachochukiza zaidi ni kuona mashirika yaliyodaiwa kuwa ya umma ambayo ni jasho la wakulima na wafanyakazi yakiuzwa kwa bei ya kutupa kwa makaburu wale wale waliokuwa washirika wakubwa wa wakoloni waliotutawala, kututesa na kutunyanyasa. Wananchi tunaona sasa ubeberu wa dunia katika sura mpya ya uwekezaji na utandawazi.
Watanzania wenye asili ya Kiasia kihistoria wamemiliki sekta za biashara, viwanda na sasa wanaingia katika kilimo cha biashara na siasa. Ili kuongeza uwezo wao wa kumiliki na kudhibiti fedha wanaanzisha mabenki, makampuni ya bima, maduka ya fedha na taasisi zingine za fedha. Wameunganishwa zaidi na masoko ya ndani na nje ya nchi. Pamoja na tofauti ndogondogo walizonazo, kikundi hiki kina mshikamano mkubwa. Wanasaidiana wenyewe kwa wenyewe na kuhifadhi utamaduni, dini, mila na lugha zao. Kwa misingi hii wamekuwa kama kikundi cha wageni kilichojibagua na kisichochanganyika na wananchi wengine. Umaskini uliokithiri na kuzagaa nchi nzima hauligusi kundi hili.
Lengo la sera: Sera ya Usawa katika Uchumi inakusudia kumilikisha uchumi wa nchi hii kwa raia wote kwa usawa na kuondoa hali iliyojengeka kwa ssasa ambapo watu wengi wenye asili ya kiafrika wamefanywa kama vibarua tu katika nchi yetu wenyewe. Lengo kuu jingine katika sera hii ni kutoa nafasi kwa wote kushiriki na kuchangia katika maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi nchini yatakayotuhakikishia uhai wa uchumi wa taifa.
Mikakati wa kutekeleza sera ya Usawa katika Uchumi: Serikali itakayoundwa na chama cha NCCR-Mageuzi itafanya yafuatayo;
- Kuanzisha elimu ya ujasiriamali, biashara na utawala wa uchumi kwa wananchi walio wengi.
- Kutoa kipaumbele kwa wazalendo katika uwekezaji na zabuni za serikali
- Kusimamia kuanzishwa kwa taasisi za utafiti wa viwanda na kilimo ili kukuza ajira, tija, ubora wa mazao na ubunifu wa bidhaa mpya katika sekta ya kilimo.
- Kusimamia uanzishaji wa viwanda vya tekinolojia ya juu kwa vile viwanda vya bidhaa za umeme na elektroniki; mfano kompyuta na vyombo vya mawasiliano, ili kupanua wigo wa ajira na kukuza uchumi.
4.3 Sera ya Biashara
Tathmini ya Hali: Biashara ya ndani na ya nje nchini mwetu imedumaa. Hali hii inatokana na mambo matatu makuu. Kwanza ni ukosefu wa elimu ya biashara kwa idadi kubwa ya wananchi. Pili ni uduni wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu. Bidhaa zinazozalishwa hazikidhi viwango vya kimataifa kwa ubora na uzalishaji wenyewe ni mdogo kiasi kwamba bidhaa huwa chache mno kuweza kupata bei ya ushindani. Tatu, ni udhaifu wa miundombinu.
Aidha, Serikali iliyoko madarakani imekuwa ikitekeleza sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma yapata miaka 10 sasa. Sera hii imekuwa ikitekelezwa kinyemela bila wananchi kupewa fursa ya kuifahamu na kuijadili. Watanzania tumeporwa amana zetu bila ridhaa yetu wageni wameuziwa mashirika yetu kwa bei ya kutupa na kilichopatikana hatukioni.
Serikali imekula au kutawanya hovyo fedha itokanayo na kuuzwa kwa mashirika hayo. Ule mfuko wa mitaji ambao serikali iliyoko madarakani ilituahidi kuwa itaanzisha kutokana na fedha ya mauzo ya mashirika ya umma bado haujaanzishwa. Hivyo raia wametelekezwa bila mitaji ya kuwawezesha kushiriki katika ununuzi wa mashirika ya umma yanayotangazwa kuuzwa.
Wawekezaji wageni wanaopewa bure mashirika haya hawaheshimu sheria za nchi wala mikataba inayolinda masilahi ya wafanyakazi.
Baadhi ya mashirika yaliyouzwa kama Benki ya Taifa ya Biashara, mashamba ya sukari ya Kilombero, na ukodishwaji wa viwanja vya ndege vya Kilimanjaro na Dar es Salaam na mengine mengi, uuzaji wake haukuzingatia masilahi ya taifa na unaashiria mazingira ya rushwa.
Lengo la Sera: Sera ya NCCR-Mageuzi katika biashara ni Ukuzaji wa mauzo ya nje na Uangalifu wa Manunuzi. Lengo la Sera ni kuweka uwiano bora wa mauzo ya nje na manunuzi kutoka nje, ili kukuza uchumi wa nchi na kuimarisha fedha yetu.
Mikakati ya kutekeleza sera: Mkakati mkuu ni kuondoa vikwazo vya biashara ya taifa letu kama ifuatavyo.
Ili kuondoa tatizo la uduni wa bidhaa zizalishwazo nchini; Serikali ya NCCR-Mageuzi itaendelea kubuni mikakati ya kukuza uzalishaji wa bidhaa kwa wingi na kwa ubora kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
Ili kutatua tatizo la miundombinu hafifu; Serikali ya NCCR-Mageuzi itabuni mfumo mpya wa barabara, reli na usafirishaji wa anga na majini na kuboresha iliyopo ili kuhakikisha kwamba soko la ndani linaunganishwa, kwa wilaya zote nchini. Kipaumbele kitawekwa katika kuendeleza uchukuzi wa reli na nishati ya umeme badala ya mafuta ya petroli. Raia watahamasishwa kununua na kuendesha vyombo vya uchukuzi wa majini na anga ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hatua hizo, serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba maofisa biashara katika balozi zetu wanatimiza wajibu wao wa kuimarisha na kupanua soko la nje la bidhaa zetu, kwa kutangaza sana biashara ya Tanzania na kuwawezesha wafanyabiashara kupata masoko nje kwa kusaidia ushiriki wao katika maonesho ya kibiashara, mikutano, semina, warsha na makongamano ya kibiashara na pia kufanya juhudi za makusudi za kuwatafutia au kuwaunganisha watanzania na wabia wa nchi za nje.
Vilevile, Ili kuimarisha biashara ndani na nje ya nchi, NCCR-Mageuzi ina mikakati ifuatayo:-
Kuhamasisha matumizi ya mipaka kama vituo maalum vya masoko baina ya nchi yetu na kila nchi jirani (hususan Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro, Shelisheli na nyinginezo); kila nchi jirani, angalau kituo maalum kimoja.
Kuimarisha moyo wa ufanyabiashara kutoka kwenye ngazi ya familia hadi taifa. Kwa maana hii raia tusiwaachie wageni kuja nchini kuuza hata mkaa na mchicha. NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba wageni hawaruhusiwi kuwekeza katika biashara ndogo ndogo na hasa sekta ya huduma kwa mfano uendeshaji wa uchukuzi wa abiria, migahawa, baa na kadhalika.
Kuhakikisha kwamba raia wanapewa leseni zenye nafuu kulingana na aina ya biashara. Wenye biashara ndogo watozwe ada kidogo na wenye biashara kubwa watozwe ada kubwa kulingana na ukubwa wa biashara zao.
Kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wetu wanapewa elimu ya kodi ili kodi isiwe kero. Watozakodi wasiwe tishio kwa raia kiasi kwamba ukwepaji kodi unajengeka na kuwa mila. Raia wataelimishwa kuhusu faida za kulipa na hasara za kutolipa kodi ili walipe kodi kwa hiari.
Kuhusu ubinafsishaji; NCCR-Mageuzi kinarejea tamko lake kama ifuatavyo:-
NCCR-Mageuzi kinapigania kuundwa kwa sekta binafsi inayoongozwa na kutawaliwa na raia na inapinga kwa nguvu zake zote kubinafsishwa holela kwa mashirika yaliyokuwa yakiitwa ya umma kusikotoa kipaumbele kwa raia kuinua mashirika hayo wenyewe au kwa ubia na wageni.
NCCR-Mageuzi kitahakikisha taifa linaondokana na ubinafsishaji usiozingatia taratibu za uwazi, haki maslahi ya taifa, kulinda ajira, na kutoweka mikononi mwa wageni sekta nyeti zenye athari za kiusalama kwa taifa.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kuwa, mashirika yaliyokuwa yakiitwa ya umma ambayo yaliuzwa kiholela yataangaliwa upya na mikataba yake itapitiwa ili kuondoa dosari na patakapobainika ubadhilifu, wahusika watawajibishwa na serikali kwa mujibu wa sheria za nchi.
4.4 Sera ya Ardhi
Tathmini ya hali: Ardhi ni moja ya rasilimali muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na ya jamii. Hata hivyo kwa Watanzania ardhi haijawahi kutambuliwa rasmi kuwa ni mali kisera na kisheria. Wakati wa utawala wa kikoloni, Serikali ya wakoloni ilitunga uongo kwamba kwa mwafrika ardhi siyo mali, wala mwafrika hajui dhana ya kumiliki ardhi kama mali binafsi. Hivyo sheria ya wakati ule ilitambua haki ya wageni kumiliki ardhi kwa vipindi vya miaka 33, 66 na 99, lakini mwafrika akapigwa kiinimacho kwamba milki yake ni ya kimila na ni ya jamii nzima kwa kuwa hajui kumiliki ardhi kama mali binafsi. Hii ndiyo sababu mpaka leo ardhi ya mwafrika humilikiwa kimila na haipimwi na kutolewa kwa hati. Hali hii ilichangia katika kumwondoa mwafrika katika mfumo wa uchumi wa kibepari. Kama ardhi inayomilikiwa kimila si mali binafsi, basi mwananchi hana jinsi ya kuitumia kama rehani kuombea mikopo/mitaji.
Pia hali hii ya kutotambua umiliki wa ardhi kimila, imeipa serikali tangu wakati wa mkoloni hadi leo, mwanya wa kupokonya ardhi kutoka kwa wananchi kila inapotaka bila faida. Matokeo ya mtindo huu yamekuwa wananchi kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi katika nchi yao . Leo wanahamishwa hapa, kesho pale, kama wakimbizi katika nchi yao . Mifano hai ya waafrika kuporwa ardhi wakati wa mkoloni ni ule mgogoro uliovuma wa kunyang’anywa ardhi wananchi wa Meru mkoani Arusha. Mifano hai ya wananchi kuporwa ardhi na serikali ya sasa ni mgogoro wa ardhi ya wafugaji kwenye mbuga ya asili Hannang mkoani Arusha, mgogoro wa wafugaji katika hifadhi ya Mkomazi mkoani Kilimanjaro, mgogoro wa ardhi ya wakulima wa Kazimzumbwi mkoa wa Pwani na migogoro mingine ya hivi karibuni.
Sera na malengo yake: Sera ya NCCR-Mageuzi katika ardhi ni kuwa; Ardhi ni Mali Rasmi na ni Miliki ya Wananchi. Katika sera hii NCCR-Mageuzi inasema kwamba ardhi ni mali ya wananchi (sio ya serikali). Raia ndio wenye haki ya asili ya kumiliki ardhi ya nchi hii. Serikali ni chombo tu cha utawala ambacho hakina haki ya asili ya ardhi ila pale inaposimamia ardhi hiyo kwa makubaliano halali na ya hiari kutoka kwa wananchi. Mtizamo wa NCCR-Mageuzi kuhusu ardhi iliyoko mikononi mwa serikali ni kwamba ardhi hiyo pia ni mali ya Taifa.
Mikakati ya Kisera: Kutokana na ukweli kwamba ardhi ni mali ya wananchi, serikali ya NCCR-Mageuzi itaimarisha kikatiba na kisheria haki ya raia kumiliki ardhi kimila kama mali yao binafsi. Milki ya kimila itakuwa ni ya milele (freehold) na itapimwa na kutolewa kwa hati.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itarejesha kwa wananchi ardhi iliyoporwa bila kutumia sheria.
4.5 Sera ya Kilimo
Tathmini ya Hali: Hadi leo takribani asilimia 80 ya watanzania ni wakulima. Mchango wa sekta hii katika kuliingizia taifa fedha za kigeni ni mkubwa kuliko sekta nyinginezo. Hata hivyo hali ya maisha ya mkulima mwenyewe na watanzania wengine imeendelea kuwa duni.
Yapo mambo mengi yanayosababisha sekta hii kushindwa kutosheleza uhitaji wa watanzania kikamilifu. Mojawapo ya mambo hayo ni kwamba, Serikali ya sasa imemtekeleza mkulima. Serikali ya sasa haimpi tena mkulima wa taifa hili mafunzo mbalimbali yanayohusu kilimo. Utafiti wa kilimo katika mazao mbalimbali hauendelezwi ipasavyo. Mkulima hapati mbolea kwa bei nafuu na wala mikopo ya aina yeyote ile. Vyama vya ushirika havina mitaji na vimeshindwa kujiendesha kibiashara kutokana na usimamizi mbovu na kuingiliwa na serikali. Mkulima wa Tanzania hana hakika na soko la bidhaa zake na bidhaa nyingi za kilimo huuzwa bila kusindikwa, jambo ambalo hufanya bei za bidhaa hizo kuwa duni.
Sera na Malengo yake: Sera ya NCCR-Mageuzi katika sekata hii ni; kilimo cha kisayansi na chenye tija. Lengo la sera hii ni kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inakuwa bora zaidi, kunakuwepo ongezeko la mazao bora ya kilimo, nchi ina utoshelevu wa chakula na kuna mauzo makubwa ya mazao ya kilimo katika nchi za nje.
Mikakati ya kisera: Serikali ya NCCR-Mageuzi itachukua hatua madhubuti zifuatazo ili kukinusuru na kukiboresha kilimo chetu.
Kuondoa kodi zote za pembejeo za kilimo na pale inapowezekana kutoa ruzuku kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa faida.
Kuimarisha huduma za Ugani vijijini pamoja na miundombinu ya kilimo.
Taasisi za kifedha zinazotoa mikopo zitakazoanzishwa zitaipa kipaumbele sekta ya kilimo na hasa wakulimu wadogo.
Kuviimarisha vyama vya ushirika kwa kuviacha viendeshe shughuli zao kwa manufaa ya wanachaama bila kuingiliwa na dola.
Kutoa nafuu ya kodi kwa wawekezaji wanaoanzisha viwanda vya kusindika bidhaa za kilimo.
Kuimarisha kilimo cha umagiliaji
Kuibua viwanda vya teknolojia za kisasa za kilimo nchini.
4.6 Sera ya Ushirika
Tathmini ya hali: Historia ya Ushirika nchini tangu wakati wa mkoloni hadi leo ni historia ya mapambano katika ya washirika na dola. Ushirika ni nguvu za wanyonge ambazo zikiwekwa pamoja katika mfumo rasmi unaowapa wanyonge uwezo wa kupambana na unyonge wao kiuchumi. Kwa namna hii NCCR-Mageuzi inaamini washirika si wakulima peke yao lakini pia wafanyakazi na wananchi walio katika sekta nyingine za jamii.
Kwa wafanyakazi; mifuko ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF, PPF na LLPF ni mifuko ya washirika, na wanaochangia mifuko hiyo wanastahili kupewa hisa kutokana na michango yao ili wapate gawio la faida ya shughuli za kiuchumi za mashirika hayo. Lakini kwa sasa serikali iliyoko madarakani imekuwa ikimiliki na kuchezea fedha za mashirika haya kana kwamba ni mali binafsi ya wakubwa serikalini. Mifuko hii ya washirika ilitosha kuwa ni benki za wanaochangia ili kuondoa unyonge na umaskini wao katika kutoa mitaji kwa sekta mbalimbali katika jamii.
Kwa upande wa wakulima; taasisi ya ushirika imenyanyaswa sana na kuogopwa na serikali. Imenyang’anywa nguvu yake kwa kuvunjwa mara nyingi na kupewa tafsiri na sheria ambazo zimeinufaisha serikali na viongozi wake zaidi kuliko wakulima wenyewe na sasa imeachwa bila mitaji wala nguvu ya kiutendaji.
Sera na malengo yake; Sera ya NCCR-Mageuzi ni Ushirika Wenye Manufaa . Nia ya NCCR-Mageuzi katika sera hii, ni kubadili mfumo wa kionevu na unyonyaji wa uliomo katika ushirika, ili kuwanufaisha zaidi wanaushirika. Ushirika ni hazina na nguvu ya taifa, haipaswi kunufaisha wakubwa na watawala tu katika jamii bali taifa na hasa wenye kuchangia.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itatunga sheria inayolinda ushirika na kukusanya nguvu za wanyonge na kuwapa hisa na umilikaji na utawala wa taasisi hizi na kuziachia uhuru ili zitoe mchango wa kimitaji kwa jamii yote kwa faida ya washirika na taifa kwa ujumla.
4.7 Sera ya Mifugo
Tathmini ya hali: Tanzania ni moja ya nchi zenye mifugo mingi katika Bara la Afrika. Kulingana na takwimu za mwaka 1999 Tanzania ina jumla ya ng’ombe 15,600.00, mbuzi 10,700,000 na kondoo 3,700,000, kuku 27, 000,000 na nguruwe 6,700,000. Mifugo hii inalipatia taifa sehemu kubwa ya maziwa na nyama zinavyotumika kwa chakula na pia kuuzwa nchi za nje. Pia mauzo ya ngozi na bidhaa nyingine zitokanazo na wanyama hao huliletea taifa pato kubwa.
Chini ya serikali iliyoko madarakani mpango wa huduma za mifugo kupitia mabwana-mifugo umekwama. Mabwana-mifugo hawana vitendeakazi, ujiria kwao ni duni na hivyo mazingira yao ya kazi hayatoi nafasi kuwa na ufanisi wowote. Ukosefu wa madawa ya mifugo, mbegu bora za mifugo, vyombo vya tiba ya mifugo na usafiri vimekithiri vijijini pote.
Inaelekea pia kwamba serikali ya sasa imeshindwa kabisa kuwalinda na kuwaendeleza wafugaji. Makabila ya wafugaji kama vile wamasai, wabarbaig na wagogo wameachwa nyuma kabisa kimaendeleo. Kwanza serikali haitambui haki zao za kumiliki ardhi wanamofugia mifugo yao . Hivi sasa makabila haya yanachukuliwa kuwa ni watangatangaji wasio na makazi ya kudumu. Ardhi yao imenyang’anywa na kufanywa mashamba ya kilimo ya serikali. Mfano hai ni mashamba ya NAFCO Hannang ambayo yalianzishwa kwa ajili ya kilimo cha ngano baada ya wafugaji wa kibargaig kuporwa ardhi yao kwa kuchomewa nyumba zao na watendaji wa serikali. Mfano mwingine ni wafugaji wa kimasai wa mkomazi. Hawa walifukuzwa kwenye mbuga za mkomazi ili serikali iunde Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi. Wafugaji hawa ambao kwa zaidi ya nusu ya karne wamekuwa wakiishi Mkomazi sasa hawana makazi kwa vile serikali imewafukuza kwenye mbuga hizo bila kuwapatia sehemu nyingine ya kuishi na kufuga. Hatma ya wafugaji hawa imeamuliwa na mahakama ya rufaa ya Tanzania kwamba hawana haki ila wanyama ndio wenye haki ya ardhi hiyo.
Sera na malengo yake: sera ya NCCR-Mageuzi katika mifugo ni Ufugaji unaozingatia maarifa ya wafugaji, maarifa ya Kisasa na Wenye Tija. Lengo ni kuhakikisha kuwa ufugaji unakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji na unakuwa na mchango mkubwa katika afya za wananchi, utoshelevu wa chakula na kuinua uchumi wa Taifa.
Mikakati ya kisera: Serikali itakayoundwa na NCCR-Mageuzi inakusudia kuthamini kazi ya mabwana-mifugo na kuwashirikisha katika mipango ihusuyo sekta hii.
NCCR-Mageuzi inatambua haki za wafugaji kumiliki ardhi wanamoishi na kufuga. Mbuga za mifugo lazima zipimwe na jamii ya wafugaji kumilikishwa mbuga hizi kwa makazi yao na shughuli zao za ufugaji. Ni kweli kwamba hata wakoloni walitambua haki hizi na walitenga mbuga za wafugaji ili wasibughudhiwe na wakulima au waporaji wa ardhi. Ni jambo la aibu na la kusikitisha kwamba serikali ya sasa imeshindwa kuwalinda na kuwaendeleza wafugaji.
Serikali ya NCCR-Mageuzi, itawasaidia wafugaji kwa kuwatafutia soko kwa bidhaa za mifugo
Itatenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya wafugaji na kuilinda isiingiliwe na/au kuporwa.
NCCR-Mageuzi kitahakikisha kuwa wafugaji wa Hannang na maeneno mengine wote walionyang’anywa ardhi, wanarudishiwa ardhi yao na pia kulipwa fidia wanayostahili. Vile vile wafugaji wa Mkomazi na wengineo watapewa ardhi nyingine ya kuishi na kufugia na kufidiwa wanayostahili.
Pia kutokana na umuhimu wa sekta hii NCCR-Mageuzi kitaweka mikakati madhubuti yenye lengo la kuondokana na ufugaji wa kuhamahama na kufanya sekta hii kuwa ya kitaalamu zaidi.
Vile vile NCCR-Mageuzi kina mikakati ifuatayo ya kuimarisha sekta ya mifugo:-
Kuboresha malisho ya mifugo kwa kutumia utaalam unaofahamika hadi sasa ili mifugo ipate malisho ya kutosha na bora na kupunguza adha ya kuhamahama.
Kuimarisha huduma za Ugani ili kuelimisha wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa.
Kuimarisha miundombinu ya sekta ya ufugaji vikiwepo vituo vya utafiti na tiba za maradhi ya mifugo, majosho, malambo ya maji vile vile.
Kupanua ufugaji wa mifugo kama vile sungura, kuku, ili kuinua ubora wa lishe kwa jamii za vijijini na mijini.
4.8 Sera Kuhusu Wanyamapori
Tathimini ya hali: Katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 ya uhuru sekta ya wanyamapori haijapewa umuhimu unaostahili na kutambuliwa kuwa hii ni rasilimali muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Sera na malengo yake; Sera ya NCCR-Mageuzi ina mtazamo kuwa Wanyamapori ni Utajiri Maalum. Vilevile, Sera ya NCCR-Mageuzi ni kuwashirikisha wananchi katika uongozi na utunzaji wa maliasili hizi.
Endapo wananchi wakitupatia ridhaa ya kuunda serikali, serikali ya NCCR-Mageuzi itatoa kipaumbele kwa sekta hii ya wanyamapori . NCCR-Mageuzi inatambua kuwa wanyamapori huvunwa kwa ajili ya chakula na huliingizia taifa fedha nyingi za kigeni kwa kuuza mawindo ya wanyama hawa. Vile vile mbuga zetu zimekuwa kivutio kwa watalii wanaokuja kutazama kupata fedha za kigeni kutokana na biashara hii.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itaweka utaratibu madhubuti kuratibu uwindaji bora ili kuondokana na hujuma za uwindaji holela kama inavyoendelea hivi sasa katika sehemu mbalimbali za nchi yetu. Hivyo serikali ya NCCR-Mageuzi itazingatia kuikuza na kuiendelea sekta hii ili itoe mchango wake katika uchumi wa Tanzania.
Kadhalika, serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kuwa watanzania wanapewa mafunzo ya utawala wa wanyamapori na utalii ili waweze kushiriki kikamilifu kulinda na kuitunza maliasili hii.
Kwa kuwa serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha inatambua na kujali watu wake itahakikisha wananchi wanaoishi kwenye mipaka au kandokando ya mbuga za wanyama wanafaidika kwa asilimia thelathini (30%) ya pato litakalotokana na wanyamapori. Kwa kufanya hivyo wananchi hawa watalinda wanyama hao wasiwindwe na majangili maana wananchi watakuwa wanajua kwamba wanyama hawa ni rasilimali yao wanayonufaika nayo moja kwa moja.
4.9 Sera ya Misitu
Tathmini ya hali: Tanzania ina utajiri mkubwa wa misitu ya asili na ya kupandwa. Misitu hii ina manufaa kwa taifa. Hata hivyo uendelevu wa misitu hiyo haujawa wa uhakika kutokana na shughuli za kibinadamu au nguvu za asili, hususani hali ya ukame katika baadhi ya maeneo.
Sera na malengo yake; NCCR-Mageuzi ingependa kuona kuwa katika misitu ya taifa letu, kunakuwa na mzunguko endelevu wa hifadhi misitu hiyo. Pia sera ya NCCR-Mageuzi juu ya mapori na misitu ni kuondokana na uchumi tegemezi unaotegemea wafadhili. Hivyo, misitu itapandwa na kuvunwa katika maeneo maalumu ili wananchi na taifa linufaike na miradi hiyo.
Viwanda vya mazao ya rasilimali hizi lazima vijengwe kwenye maeneo zilipo rasilimali zenyewe. Hii itarahisisha uvunjaji na usambazaji wa mazao yake. Vile vile wananchi wa maeneo zilipo rasilimali za misitu wajipatia ajira na hivyo kujiongezea kipato.
NCCR-Mageuzi itasimamia kikamilifu upandaji, ustawishaji na matumizi ya miti-dawa ili kukuza uwezo wa taifa kutengeneza dawa na tiba mbalimbali kutokana na miti-shamba.
4.10 Sera ya Utalii
Tathmini ya hali: Nchi yetu imejaliwa kuwa na milima, mabonde ya kupendeza, mbuga za wanyama pori na vivutio mbalimbali kwa ajili ya utalii. Hata hivyo serikali ya sasa haikuipa sekta hii kipaumbele ili kuhakikisha kwamba taifa letu linafaidika kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazoandamana na sekta hii.
Sera na malengo yake: Sehemu ya sera ya NCCR-Mageuzi katika utalii ni; Utalii laini. Kwa kurejea katika itikadi yetu; mojawapo ya malengo ya itikadi ya UTU ni kuendeleza mahusiano mema kati ya binadamu. NCCR-Mageuzi tunasema, utalii siyo kutembelea mbuga za wanyama ama mahoteli makubwa tu bali hata watu kutembeleana na kujua mila na desturi za makabila mengine.
Hivyo, NCCR-Mageuzi itaamsha na kuimarisha utalii laini ambapo watalii wa nje watakaa na wenyeji majumbaji mwao. Hii itasaidia wananchi binafsi kujiongezea kipato na kufahamu mila za wenzetu na wageni nao watapata fursa ya kujifunza mila na desturi na ukarimu wetu.
Pia NCCR-Mageuzi itaendeleza na kusimamia ujenzi wa mfumo wa hoteli za utalii wa ndani zisizo za gharama kubwa. Katika hili ujenzi utakuwa wa kutumia zana za asili zinazopatikana kwenye maeneo husika. Kwa upande wa chakula, NCCR-Mageuzi itasisitiza upikaji wa vyakula vya asili na vinywaji vya maeneo hayo. Pia viwanda vyetu vitatoa huduma na mazao yenye kuvutia na kukuza utalii.
Kwa kuwa serikali ya NCCR-Mageuzi itatambua umuhimu sekta hii katika uchumi wa taifa, itaweka mikakati madhubuti ya kuiendeleza sekta hii kwa kuweka vivutio vya utalii hasa uboreshaji wa huduma mbalimbali kama vile kujenga barabara ziendazo katika sehemu watembeleazo watalii, kuweka mawasiliano, ujenzi wa mahoteli ya kisasa yenye mvuto wa kiafrika na viwanda vya bidhaa za kitalii. NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba mgeni mwekezaji yeyote atakayetaka kuwekeza katika sekta hii ni lazima ashirikiane na watanzania ili sekta hii itawaliwe na raia.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itawapatia raia mtaji kwa kwa njia ya mikopo na ruzuku ili kufanikisha ubia katika yao na wawekezaji wageni. NCCR-Mageuzi itahakikisha kuwa mchango wa raia katika ubia itakuwa ni pamoja na ardhi ambayo itakuwa na hati-miliki ya mwananchi.
Kuhusu huduma ya usafirishaji wa watalii ndani ya nchi, NCCR-Mageuzi kitahakikisha kwamba huduma hii inafanywa na raia peke yake bila wageni kushiriki. Katika usafiri wa anga na majini serikali ya NCCR-Mageuzi itaruhusu wageni kuwekeza kwa vile huduma hizi zinahitaji mtaji mkubwa na utaalamu katika kuziendesha.
4.11 Sera ya Nishati
Tathmini ya hali: Maendeleo yote ya kijamii na kiuchumi yanategemea nishati. Pamoja na umuhimu huo, sekta hii bado iko nyuma hapa nchini. Kwa mfano, asilimia tisini (90%) ya nishati yote itumikayo nchini hutokana na miti, yaani kuni na mkaa. Nishati itokanayo na mafuta ni asilimia nane (8%) na nishati ya umeme ni chini ya asilimia mbili (2%). Ni azma ya serikali ya NCCR-Mageuzi kubadilisha hali hii ili kuthibiti uharibifu wa mazingira utokanao na matumizi ya miti na wakati huo huo kuondoa adha ya matumizi ya kuni.
Utafiti uliofanywa na wanataaluma na NCCR-Mageuzi umegundua kwamba utawala uliopo umeshindwa kumiliki na kulinda mazingira na hasa kulinda vyanzo vya mito . Kwa kuruhusu uchimbaji holela wa dhahabu katika chanzo cha mto Ruaha, kula rushwa, kushindwa kutawala kujaa kwa tope kwenye bwawa la Mtera, na kushindwa kuthibiti miradi inayotumia maji yaingiayo kwenye bwawa la Mtera, hivi sasa bwawa hilo linaendelea kukauka. Hii ina maana kwamba matumaini ya kuendelea kupata nishati kutoka Mtera yanaendelea kufifia. Kulingana na ukweli wa utafiti huu Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba tatizo la nishati linatafutiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
Sera na malengo: Sera ya NCCR-Mageuzi ni Taifa linalojitegemea kwa nishati toshelevu.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba Taifa linajitegemea katika utoaji wa nishati kwa kuzingatia yafuatayo.
Vyanzo vipya vya nishati vitajengwa. Hivi ni pamoja na
- Gesi asilia,
- Nishati ya jua,
- Nishati ya Upepo,
- Makaa ya mawe,
- Gesi ya samadi, na
- Nuklia.
Pia Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba nishati ya mafuta ya taa inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu vijijini. Agenda ya NCCR-Mageuzi kuhusu nishati ni pamoja na kudhibiti utumiaji mzuri wa nishati kwa kutathmini matumizi ya machine zinazoingizwa nchini. Pia Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba suala la nishati linafanyiwa utafiti wa kitaalamu ili kuhakikisha kwamba Taifa linaendelea kulingana na viwango vya taaluma hii duniani.
4.12 Sera ya Madini
Tathmini ya hali: Nchi yetu ina utajiri mkubwa sana wa madini. Madini na vito vya thamani vinavyopatikana nchini ni pamoja na dhahabu, fedha, shaba, chuma, bati, platinum na nikeli. Vile vile Tanzania ina utajiri wa almasi, lulu, tanzanite, rubi, ganeti, emeradi, alexandrite and sapphire, kaolin, fosfeti, lime, gypsum, diatomite, bentonite, vermiculite, Nyerereite, chumvi, mchanga wa bahari, makaa ya mawe, gesi, madini ya urani na mengine. Hata hivyo, hadi sasa nchi haijaweza kunufaika vilivyo kutokana na utajiri huu. Sababu za kutonufaika ni pamoja na kutokuwepo kwa makampuni ya ndani au ya wazalendo yanayoshughulikia uchimbaji wa madini haya, utegemezi wa kiteknolojia kutoka nje, pamoja na mikataba ya uchumbaji madini isiyozingatia zaidi maslahi ya taifa.
Sera na malengo yake: Sera ya madini ya NCCR-Mageuzi ni Mmiliki, mchimbaji, muuzaji na mnufaika wa madini ni mwananchi. Lengo kuu ni kuweka uchumi wa madini mikononi mwa wanachi na kukuza pato la nchi linalotokana na sekta ya madini.
Mikakati: Ili kutekeleza sera hii na kufikia malengo, serikali itakayoundwa na NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba wananchi wanafahamishwa tawimu sahihi za hazina ya madini yote yaliyoko nchini na thamani yake. Utafiti wa hazina hii utakuwa endelevu ili kuendelea kubaini hazina ambazo hazijajulikana bado.
Vilevile serikali itatengeneza fursa kwa ajili ya watanzania kuanzisha na kumiliki makampuni ya uchimbaji wa madini, ili taifa liondokane na utegemezi kwa makampuni ya nje. Serikali itawezesha uanzishaji na uendeshaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini hapa nchini kabla ya madini kuuza.
Serikali itaendelea kuruhusu na kulinda kisheria shughuli za wachimba madini wadogowadogo (hawa ni raia wa Tanzania tu).
Serikali itaingiza katika mitaala sitahiki elimu na mafunzo juu manufaa, uchimbaji na biashara ya madini (mfano, mafunzo katika taaluma za uvunaji wa vito vya thamani, mafuta na gesi).
Aidha, serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba, uchimbaji wa madini unalazimika kufuata kanuni za utunzaji wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za nchi.
4.13 Sera ya Viwanda
Tathmini ya hali: Nchi yetu haijafikia maendeleo ya uchumi wa kiviwanda hadi sasa. Jitihada za awali za kuanzisha na kuendesha viwanda nchini mara baada ya uhuru, zilikwama kufuatia serikali ya sasa kuamua kubinafsisha juhudi zilizokwishafanyika kwa kuuza viwanda vilivyokuwepo. Taifa limeendelea kuwa mzalishaji wa bidhaa zisizosindikwa viwandani, na limezidi kuwa mtegemezi wa bidhaa zizalishwazo katika viwanda vya nchi mbalimbali. Hali hii huchangia kwa kiasi kikubwa uwiano wa biashara ya nje kuwa mbaya kwa upande wetu; tunaagiza bidhaa kutoka nje kuliko tunavyouza. Hivyo, ni muhimu sana Tanzania kuingia katika uchumi wa viwanda.
Sera ya NCCR-Mageuzi katika viwanda ni; Tuzalishe wenyewe zaidi kuliko tunavyoagiza bidhaa za viwandani. Kadhalika, uchumi mpana wa viwanda vya kisasa ni lazima kwa Tanzania. Suala hili la viwanda ni mtambuka kisera na kisekta. Itakumbukwa kwamba katika sera zetu hizi tumelitaja kwenye maeneo yafuatayo.
Mikakati: Kwamba serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha maendeleo ya viwanda yanazingatia utu, yasiwe na madhara kwa uhai wa watu na viumbe wengine. Kadhalika yazingatie kwa kiwango cha juu hifadhi ya mazingira.
Kwamba serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha sekta ya viwanda haiwi miliki ya wageni/wawekezaji wa kigeni tu waliouziwa vilivyokuwa vikiitwa viwanda vya umma, wazalendo nao sharti wamiliki viwanda.
Kwamba serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kunakuwepo uanzishaji wa viwanda kwa wingi, ili pamoja na mambo mengine viwanda viwe hakikisho la uwepo na upanuzi wa fursa za ajira nchini.
Kwamba serikali ya NCCR-Mageuzi itawapatia wamiliki wa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo nafuu ya uendeshaji wa viwanda hivyo katika kodi ili visaidie maendeleo ya kilimo nchini.
Kwamba serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha zilipo rasilimali ndilo eneo la kipaumbele la kuanzisha kiwanda kinachoshughulika na rasilimali husika.
Kwamba serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha viwanda vya tanzania vinakuwa kichocheo cha utalii nchini kwa kuzalisha bidhaa za kitalii.
Kwamba serikali ya NCCR-Mageuzi itaanzisha viwanda vya madawa nchini kwa ajili ya suala la afya.
Aidha serikali ya NCCR-Mageuzi itaanzisha programu ya kujenga viwanda vinavyoshughulika na uzalishaji wa bidhaa ambazo nchi imeendelea kuzipata kutoka nchi za nje. Jitihada zitafanywa kuona kuwa Tanzania inakuwa na mtaji, tekinolojia na rasilimali watu kwa ajili viwanda vya namna hiyo.
4.14 Sera ya Ajira
Ajira kwa Vijana: Mpaka sasa kuna uzembe wa wazi kabisa kuhusu kuwekeza katika elimu, ufundi na teknolojia. Matokeo yake ni kwamba vijana wetu hawana elimu ya kutosha ya nadharia na vitendo kuweza kuwa na sifa za kuajirika, kuajiriwa na au kujiajiri katika fani mbalimbali.
Chama cha NCCR-Mageuzi kinatamka yafuatayo: Kwamba mipango ya maendeleo ya taifa lazima izingatie hoja ya kuwekeza katika elimu. Vijana wapewe elimu ya nadharia na ufundi ili wamalizapo shule wawe tayari na upeo wa kutosha kuishi kwenye jamii yenye ustaarabu na wawe na ufundi na utaalam wa kutosha kuweza kupata ajira.
Kwamba elimu ya msingi ipanuliwe hadi kidato cha nne na vijana waanze mafunzo ya ufundi tangu darasa la saba.
Kipaumbele kiwekwe na serikali katika kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe ama mmoja au kwa vikundi vya uzalishaji mali.
Sekta ya kilimo ifufuliwe na kuimarishwa kama ilivyoelezwa awali ili iweze kuajiri vijana wengi.
Mafunzo kwa vijana yatolewe ili kuwahamasisha wawe na moyo wa kujenga nchi yao.
Vipaji vya watoto na vijana katika michezo na sanaa kama vile muziki na sanaa nyinginezo vitapewa uzito wa kipekee na wa hali ya juu kwa kuwa eneo hili limewakomboa na kuwatajirisha raia wa mataifa mbalimbali duniani. Serikali ya NCCR-Mageuzi itaweka mkakati madhubuti wa kuwanufaisha watanzania katika hili.
Ajira na Wafanyakazi: Kazi ni msingi wa maisha na utu wa mwanadumu (rejea itikadi yetu). Hivyo basi, kazi ni haki ya kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi kama inavyotamkwa katika ibara ya 22(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ni wajibu wa Chama tawala kupitia serikali yake kujenga mazingira yenye kuibua na kupanua ajira katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya watanzania. Hadi sasa hakuna sera ya ajira nchini.
Baada ya kufinya ajira kwa ubinafsishaji na urekebishaji wa sekta ya umma hakuna mipango makini ya uchumi yenye kuweza kuibua na kupanua ajira katika sekta za viwanda, kilimo, uchukuzi, uvuvi, na kadhalika. Kinachoendelea sasa ni kutoa vibali kwa wawekezaji vitegauchumi bandia ambao hawana mtaji na wanaoingilia sekta ambazo watanzania wanazimudu. Hivi sasa wageni wanaruhusiwa kuishi nchini na kufanya biashara ndogo ndogo kama vile migahawa, vioski, na kadhalika, na hivyo kuwapunguzia ajira watanzania.
Ahadi ya uongozi ulioko madarakani ya kuwamilikisha wafanyakazi na wakulima mashirika ya umma imekuwa maneno matupu hadi sasa. Wageni toka nje wanaruhusiwa kunyang’anya ajira wananchi.
Wawekezaji na wenye mitaji ambao wangesaidia kuibua na kupanua ajira wanakabiliwa na kitisho cha ama ushuru mkubwa wa forodha au kodi kubwa ya ardhi au kodi kubwa ya mapato au gharama kubwa za nishati. Ahadi ya kuondoa vikwazo hivyo imekuwa ahadi hewa. Wakulima wadogo wadogo hawawezi kuendeleza kujiajiri kwa sababu hawana tena uwezo wa kumudu zana, pembejeo na soko holela linaloendekezwa na serikali ya sasa linawaathiri.
Sera ya NCCR-Mageuzi ni; uhakika wa ajira na kazi yenye kipato toshelevu.
Mikakati ya kukuza ajira: Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha uchumi unakua kwa zaidi ya asilimia nane (8%) kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Ili kuweza kufikia lengo hilo yafuatayo yatazingatiwa:-
Kupunguza kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ili walipa kodi wavutike kulipa kwa hiari.
Kupunguza kodi ya ardhi ili kuchachamua kilimo cha mashamba makubwa hususan kilimo cha mkonge, chai, sukari, mpunga na mazao mengine.
Kupunguza ushuru wa forodha wa malighafi na gharama za nishati ili kupanua uzalishaji mali viwandani na kuziwezesha bidhaa za viwanda vyetu kushindana na bidhaa toka nje katika soko la ndani na nje ya nchi.
Kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi ili wastani wa uhai wa mtanzania ufike miaka 60.
Kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuzalisha zana na pembejeo nchini pamoja na kufufua viwanda vitumiavyo mazao ya kilimo kama vile viwanda vya nguo, korosho, na vingine na kudhibiti mwenendo wa soko huru.
Kuwawezesha wafanyakazi na wakulima kununua hisa katika mashirika na makampuni yanayorekebishwa au kubinafsishwa.
Kupanua na kuongeza ubora wa elimu katika ngazi zote.
Aidha serikali ya NCCR-Mageuzi itatoa/itaandika sera ya ajira yenye kuweka mfumo mpya wa ajira nchini, lengo likiwa ni kuongeza mapato na nafasi za ajira. Sera ya ajira ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba mishahara inazingatia gharama halisi ya maisha na mchango wa mfanyakazi.
NCCR-Mageuzi kitaimarisha utetezi wa maslahi ya wafanyakazi (pia wakulima na wafugaji) kwa kuwawezesha kuwa na wawakilishi bungeni kwa njia ya kuanzisha utaratibu wa uwakilishi wa uwiano na viti maalum vitakavyozingatia uwakilishi wa makundi mbalimbali maalum katika jamii yetu yakiwemo wafugaji, wafanyakazi na wakulima.
Wastaafu: Watumishi waliostaafu baada ya kufikia umri uliowekwa kisheria na wale ambao wamestaafishwa kutokana na ama urekebishaji au ubinafsishaji wa utumishi serikalini, mashiriki na makampuni ya umma wamekuwa serikalini, mashirika na makampuni ya umma wamekuwa wakilipwa mafao pungufu sasa na utaratibu wa kuyapata umekuwa wa usumbufu mkubwa. Mafao hayo hayalingani na gharama halisi ya maisha. Utaratibu wa serikali ya sasa wa kuwalipa kwa mikupuo baadhi ya wastaafu, licha ya kutoridhisha, umewaacha kama yatima na kuwasababishia kufa mapema.
Baadhi ya wastaafu Kama vile wale waliokuwa watumishi wa jumuiya ya Afrika Mashiriki iliyovunjika mwaka 1977 wamedhulumiwa haki zao kwa kulipwa mafao. Dhuluma hii ni kinyume na makubaliano yaliyofikiwa baada ya kuvunjwa kwa jumuiya hiyo na thamani halisi ya fedha ya wakati ule.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba unajengwa mfumo wa hifadhi ya jamii ambao utawaenzi wastaafu kwa kulitumikia taifa. Mfumo huo utatumika pia kuwaandaa kwa mafunzo ya uendeshaji miradi kabla ya kustaafu, na kuwaandalia taasisi za kuwapa huduma za mikopo na ushauri. Aidha wastaafu watapata mafao yanayoendana na gharama halisi ya maisha wakati wa kustaafu na watapata mafao yanayoendana na gharama halisi ya maisha wakati wote wa uhai wao.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itatumia taaluma, ujuzi na uzoefu wa wastaafu kwa kuwapa kazi za ushauri na usimamizi kwa mikataba badala ya kuwatumia wataalam na wastaafu wa nchi za nje.
Ili kuwawezesha wastaafu kutetea maslahi yao ya ustaafu, serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kuwa inawawezesha wastaafu kuunda chama au vyama vya kutetea maslahi hayo.
5.1 Dokezo
Lengo kuu la NCCR-Mageuzi kuhakikisha kwamba Mtanzania anakuwa binadamu bora, mwenye afya nzuri kimwili, kiakili na kimaadili. Mtanzania awe ni binadamu mwenye ustawi, anayemudu maisha yake kiuchumi awe na chakula, na malazi bora, na maisha mema ya amani na burudani.
Ili kufanikisha hayo lazima kujenga sekta ya huduma za jamii yenye nguvu. Zifuatazo ni sera za NCCR-Mageuzi zenye lengo la kujenga sekta ya huduma za jamii itakayotuhakikishia Tanzania yenye kupendeza.
5.2 Sera ya Elimu
Tathmini ya hali: Hali ya Elimu nchini kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu inasikitisha. Elimu ya awali, ambayo kwa kweli ni haki kwa watoto wote, kwa sasa inatolewa kwa pungufu ya Asilimia ishirini (20%) ya watoto wote wanaoanza darasa la kwanza. Shule nyingi za vijijini hazina mitaala iliyoandikwa, madarasa wala waalimu wa elimu ya awali. Hali hii inawasababisha wenye uwezo kuwapeleka watoto wao mijini au nje ya nchi kusoma. Hali hii inamaanisha kwamba watakaosoma ni watoto wa wazazi wenye uwezo na watoto wa watu wa kawaida watabaki bila elimu bora. Elimu ya msingi nayo inazidi kudidimia. Uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule wanaoandikishwa wanaomaliza darasa la saba ni pungufu ya asilimia arobaini (40%). Kwa mantiki hii mfumo wetu wa elimu unazalisha maelfu ya watanzania wasiojua kusoma na kuandika kama hazina ya nguvukazi ya Taifa. Hiki ni kiama. Elimu ya sekondari bado inaonekana kama ni kitu cha anasa kwa watanzania wengi. Watoto wanaopata nafasi katika shule za sekondari ni pungufu ya asilimia kumi (10%) ya wanaomaliza, siyo wanaoandikishwa darasa la kwanza.
Pamoja na kwamba idadi ya walimu wanaohitimu inaongezeka kwa kiasi kidogo, nafasi zao za ajira haziongezeki. Matokeo yake ni kuwa na shule ambazo hazina walimu. Walimu pungufu waliopo hawapati mafunzo ya mara kwa mara, na hawana nyumba za kuishi zenye hadhi na heshima. Vilevile walimu hawana vitabu vya kutosha vya rejea wala nyenzo muhimu za kufundisha. Mishahara yao haikidhi mahitaji ya kujikimu. Ukichanganya haya yote mwalimu anakuwa na morali ndogo ya kazi.
Majengo ya shule nayo yana upungufu mkubwa. Majengo mengi ya shule za msingi na sekondari yamechakaa, yanavuja na hakuna vyoo safi na vya kutosha. Madirisha na milango kama ipo havitamaniki. Majengo maalum kwa ajili ya maabara na maktaba sehemu nyingi hakuna. Kadhalika viwanja, vifaa vya michezo na samani nyinginezo muhimu havipatikani.
Ukaguzi wa shule nao umesahaulika. Wakaguzi ni pungufu. Hawapati mafunzo wala hawapati vitendea kazi muhimu. Kama walimu, wakaguzi hawana nyumba za kuishi na vipato vyao ni duni. Kwa watu wa aina hii huwezi kutegemea watafanya chochote kusaidia elimu yetu.
Katika baadhi ya shule za bweni za sekondari lishe ni duni kiasi cha watoto wetu kupatwa na utapiamlo. Wakati mwingine masomo hukatishwa kwa ukosefu wa chakula. Yaliyopangwa katika mihitasari ya masomo hayakamilishwi katika ufundishaji kutokana na kukatishwa kwa masomo.
Masomo yanafundishwa kwa nadharia zaidi kuliko vitendo. Hii hutokana na ukosefu wa nyenzo za elimu za utekelezaji mitaala.
Kuna tatizo kubwa la kuwafunza wakuza mitaala wetu ili waende na wakati. Nyenzo zao za utendaji kazi ni hafifu. Taifa lina upungufu mkubwa wa wataalam hawa.
Mitihani yetu sasa imekuwa haina usimamizi na udhibiti wa kutosha na hivyo kuongeza mianya ya mitihani kuvuja. Mara kadhaa Taifa lilitumia mamilioni ya fedha za walipakodi kurudia mitihani ya kidato cha nne iliyovuja. Hali hii inafanya shahada zitulewazo katika vyuo vikuu nchini ziwe katika hatari ya kutoaminika hapa nchini na nje ya nchi. Hii ni hatari kubwa.
Elimu ya juu inaonekana si muhimu kama elimu ya msingi na sekondari. Ndiyo sababu uboreshaji wa elimu ya juu umepuuzwa. Katika nchi za jumuiya ya Afrika Mashiriki Tanzania ndiyo nchi yenye wanachuo pungufu katika vyuo vya elimu ya juu kuliko Kenya na Uganda . Mnamo mwaka 1995 Kenya ilikuwa na wanachuo 67,371 katika vyuo vikuu. Uganda ilikuwa na wanachuo 30,266 wakati Tanzania ilikuwa na wanachuo 12,776 tu. Hata leo bado hatujaweza kufikia kiwango cha majirani zetu.
Pamoja na uboreshaji usioridhisha vyuo vyetu vikuu hutoa maslahi duni zaidi kwa wahadhiri wake. Huduma za maktaba vyuoni ni duni na hali ya maidha ya wanafunzi ni duni. Nyenzo muhimu za kufundishia hazipatikani kwa kiwango cha kuridhisha.
Wataalam wanatutahadharisha kuwa leo, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya binadamu, utajiri au umaskini wa nchi utapimwa siyo kwa kiasi cha viwanda, ardhi, mitambo na zana nchi iliyonayo, bali kwa kiasi cha watu walio na utaalam na ujuzi. Tusitegemee kwamba mafuta, almasi, dhahabu, wanyamapori na kadhalika, peke yake vitatuhakikishia nafasi yeyote hapo ulimwenguni ikiwa hatutakuwa na ujuzi na utaalam kama wenzetu. Kupuuza elimu ya juu, sayansi na teknolojia ni kujichimbia kaburi. Wakati wenzetu kwa mfano, Kenya bajeti ya elimu imekuwa ikipanda hadi kufikia asilimia 30 ya bajeti yote, sisi ya kwetu imeendelea kushuka hadi kufikia asilimia 6.
Sera ya Elimu ya NCCR-Mageuzi: ni elimu bora kwa kila mtoto wa kitanzania. Elimu yenye vionjo vya utamaduni wetu, elimu ya kazi na maendeleo ya mtu mmojammoja. Elimu hii isingatie pia maendeleo Sayansi ya asili, sayansi ya jamii na Tekinolojia.
Malengo ya Sera: Elimu itolewayo imwezeshe mtanzania kumudu mazingira yake popote awapo kwa sasa na baadae pia kumletea usitawi wa maisha yake na ya taifa. Ili kufanikisha lengo hilo hatuna budi kujenga na kudumisha elimu madhubuti yenye mwelekeo wa kuleta mapinduzi ya Kisayansi na kitekinolojia kwa kuigeuza Tanzania kuwa kitovu cha elimu katika bara la Afrika.
Mikakati ya kufanikisha Sera ya Elimu: Hatua zifuatazo zitachukuliwa ili kufanikisha sera hii ya NCCR-Mageuzi:-
Kiwango kisichopungua asilimia thelathini (30%) ya bajeti ya taifa ama asilimia moja (1%) ya pato la taifa kutegemea ni ipi kubwa, kitatumika kwa ajili ya elimu. Ili kuhakikisha kuwa elimu haitatelekezwa tena miaka ijayo, itarekebishwa na kiwango hiki kitahifadhiwa.
Mfuko maalum utakaochangiwa kwa utaratibu rasmi na mashirika, viwanda, makampuni na wafanya biashara utaanzishwa ili kuboresha mafao ya waalimu na mahitaji mengine muhimu ya sekta ya elimu.
Sera za mambo ya nje kuhusu elimu zitalenga katika kukuza uchumi wa taifa, kulinda sera za ndani, kulinda, kuendeleza na kuimarisha utamaduni wa Mtanzania, na kupata tekinolojia na maarifa toka nchi za nje kwa ajili ya maendeleo na umaarufu wa Mtanzania. Sera hii itajumuisha pia mambo yafuatayo:
Uhusiano na nchi nyingine utatoa kipaumbele katika elimu, sayansi, tekinolojia na utamaduni.
Ofisi za balozi zitafunguliwa hususan katika nchi zenye biashara kubwa na Tanzania ama zenye kuleta faida ya kisayansi na kitekinolojia kwa Tanzania .
Uhusiano maalumu utajengwa na nchi maarufu kisayansi na kitekinolojia zikiwemo Japan , mataifa ya Ulaya , India , Korea , Marekani , Brazil , Taiwan na China .
Balozi za Tanzania nchi za nje zitapewa jukumu la kuleta tekinolojia Tanzania .
Utoaji wa nafasi za mafunzo kwa watanzania nchi za nje utapewa nafasi ya kwanza katika mazungumzo yote ya mahusiano ya kimataifa.
Ujumbe wowote wa watanzania nchi za nje ni lazima ujumuishe mabingwa na watafiti wa sayansi na tekinolojia wakiwa na jukumu la kuchangua tekinolojia, kuikariri na kuileta Tanzania .
Sera za ndani za elimu, sayansi na tekinolojia zitalenga kujengeka kwa kundi la wanasayansi na wanatekinolojia watendaji katika fani zote. Sera hizi zitajumuisha yafuatayo:
Uhamiaji wa wanasayansi na wanatekinolojia mabingwa utarahisishwa.
Uhamaji wa wanasayansi, wanatekinolojia na wataalamu wote wa fani mbalimbali utashuka kutokana na hatua za NCCR-Mageuzi za kuboresha mazingira ya utafiti kwa wataalam.
Shule na vyuo vyote vya elimu vitakarabatiwa ili zistahili kuitwa shule au vyuo, na pia kuvifanya viwe vivutio kwa wanafunzi na wananchi.
Vyuo vikuu, vyuo vya Ualimu na Vyuo vya elimu ya juu vitaongezwa kwa kiwango kikubwa ili vitosheleze mahitaji ya ndani ya elimu ya juu, na kutoa huduma kwa wanafunzi toka mataifa mengine, na ili kukidhi pamoja na mambo mengine, mahitaji ya uchumi utakaopanuka chini ya serikali ya NCCR-Mageuzi.
Elimu ya sayansi na tekinolojia, na elimu ya misingi ya uchumi, biashara na menejimenti, itapewa umuhimu maalum Shule na vyuo vya ufundi vitaongezwa na vijiji vya sayansi vitajengwa angalau katika kila mji mkuu wa mkoa.
Jamii itashirikishwa katika uendeshaji wa elimu. Ujenzi na uendeshaji wa shule na vyuo vya watu utaimarishwa na kupewa msukumo maalum.
Juhudi zitafanywa kuendeleza na kuimarisha elimu ya awali kwa watoto wote wa Tanzania. Elimu ya msingi itakuwa ya lazima kwa watoto wote mara tu NCCR-Mageuzi itakapoingia madarakani na lengo ni kutoa elimu ya sekondari kwa watanzania wote katika kipindi cha miaka kumi.
Kodi kwenye vitabu na vifaa vya kufundishia itafutwa, na utengenezaji wa vitu hivi hapa Tanzania utapewa kipaumbele. Shule na vyuo binafsi vitasamehewa kodi ili kupunguza malipo watakayotozwa wanafunzi na hivyo kuwawezesha wananchi wa kawaida kupeleka watoto wao katika shule na vyuo hivyo.
Utafiti
Mfuko maalum wa kugharamia utafiti katika vyuo na taasisi za uchunguzi utaanzishwa ili kukomboa wataalam wetu kutoka kwenye vishawishi vya kuuza utaalam wao kwa manufaa ya nchi za nje. Lengo ni kuwawezesha (kwa kugharimia tafiti) wataalam hawa kufanya utafiti kwenye matatizo yanayowakera wananchi, na kujijengea heshima na utii kwa taifa lao.
Wafadhili wote wanaotaka kusaidia utafiti Tanzania watatakiwa kutoa misaada yao kupitia kwenye mfuko uliotajwa hapo juu.
Makampuni yote makubwa yatalazimika kuwa na vitengo vya utafiti au maabara kama sharti mojawapo la kupata leseni, lengo likiwa ni kuinua ubora wa bidhaa zetu kugundua vitu vipya na kuongeza ajira.
Elimu kwa Makundi Maalum
Elimu kwa wenye mtindio wa akili na wenye udhaifu wa viungo itakuwa bure kwa watanzania, katika viwango vyote vya elimu.
Elimu kwa wenye vipaji maalum ambao itathibitika kuwa vipaji vyao vinahitaji mafunzo ya namna ya kipekee itatolewa katika shule na vyuo maalum na kulipiwa na mfuko utakaonzishwa kwa ajili hiyo. Hata hivyo serikali ya NCCR-Mageuzi itazingatia kuwapatia watanzania, elimu katika mazingira shirikishi (inclusion).
Vifaa maalum kwa ajili ya kufundishia wenye mtindio wa akili, wenye udhaifu wa viungo na wenye vipaji vitatolewa katika shule na vyuo vyote vinavyohusika na elimu hiyo, na utengenezaji wa vifaa hivyo hapa Tanzania utapewa kipaumbele.
Elimu kwa Jamii/ lifelong learning
Elimu ya watu wazima itafufuliwa na kuendelezwa ikiwa ni pamoja na elimu ya kujiendeleza. Pia elimu kazini itapewa kipaumbele. Maktaba za umma zitaongezwa na kuendeshwa kitaalam, ikiwa ni pamoja na kuzipatia mahitaji yanayotakiwa.
5.3 Sera ya Afya
Tathmini ya hali: Tangu Tanzania ipate uhuru iliwatambua maadui zake wa maendeleo ambao ni pamoja na maradhi. Kwa miaka yote hii hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu zimekuwa zikitoa huduma duni sana kutokana na ukosefu wa vifaa vya uchunguzi vya kisasa. Uwezo wetu wa kutoa huduma za tiba umekwisha. Tumebakia tu kutoa huduma ya kwanza, mgonjwa mwenye matatizo yanayohitaji uchunguzi wa kina inabidi apelekwe nje ya nchi. Hao wanaobahatika hivyo ni wachache sana mara nyingi ni viongozi wakubwa tu.
Toka enzi za ukoloni huduma za huduma za afya zilikuwa zinazingatia tiba zaidi kuliko kinga. Mfumo huu uliendelezwa na serikali iliyofuata. Serikali iliyoko madarakani inatilia mkazo huduma za tiba ambayo imeshindwa kabisa kuzitekeleza kikamilifu kutokana na gharama zake kuwa kubwa. Serikali ya sasa imetekeleza huduma za uzazi wa mpango, mradi wa kudhibiti ukimwi na huduma nyingine za afya kwa mahitaji yetu na kufifia kwa huduma za kinga.
Sera ya NCCR-Mageuzi: NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa afya bora inaambatana na kuinuka kwa hali ya maisha ya wananchi. Pia inaamini kuwa lishe bora, mazingira safi , kinga ya tiba ni nguzo kuu za afya.
NCCR-Mageuzi kitahakikisha kwamba huduma za afya zinaboreshwa kufikia viwango vya kimataifa kwa kujenga hospitali zenye vifaa vya uchunguzi, wataalam mabingwa ili kuweza kutoa huduma zinazokidhi haja za wananchi.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikishwa kwamba;
Viwanda vya madawa ya binadamu vinajengwa nchini na vilivyopo vinafufuliwa na kuimarishwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana kwa urahisi, kwa viwango vinavyokubalika kitaalam na kwa bei nafuu.
Dawa za asili zitaendelezwa na matumizi yake yatatiliwa mkazo.
NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa kinga ni bora kuliko tiba hivyo basi katika utekelezaji wa sera zake za afya serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba huduma za kinga ya magonjwa zimepewa kipaumbele kwa kutoa elimu ya afya kwa umma kwa kutumia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara, kampeni za afya na njia nyinginezo.
Wakati huo huo NCCR-Mageuzi kinatambua mchango mkubwa wa madaktari wauguzi na watumishi wengine wa sekta ya afya. Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba watumishi wa sekta hii wanalipwa mishahara na marupurupu wanayostahili na kuthaminiwa kulingana na umuhimu mkubwa wa sekta hii katika jamii ya watanzania.
Aidha chama kitahakikishwa kwamba serikali inabuni mfumo bora wa bima ya afya kwa Taifa zima.
NCCR-Mageuzi pia kinatambua mchango wa waganga na wakunga wa jadi. NCCR-Mageuzi kinatambua kuwa watu hawa ni maarufu na mashuhuri katika jamii, na watu wanaoaminika. Kwa kutambua ukweli huu serikali ya NCCR-Mageuzi itawashirikisha waganga wa jadi na wakunga katika mipango ya afya kama hatua ya mpito hadi hapo tutakapoweza katoa huduma za kisasa na kitaalam nchini pote. Waganga na wakunga wa jadi wanaoweza kuendelezwa wataendelezwa.
5.4 Sera ya Mazingira
Tathmini ya hali: Utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa uhai na afya ya jamii. Mazingira yetu yanasikitisha sana . Miji yetu inanuka kutokana na marundo ya takataka kila kona, maji machafu toka viwandani na majumbani yanazagaa ovyo ovyo mitaani, mikojo na vinyesi vya binadamu na mifugo vimetapakaa kila kichochoro. Miji yetu imechafuka kwa mifuko na chupa za plastiki, magari makuukuu, makaratasi, moshi na vumbi toka viwandani. Vijijini pia tunashuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira, kupotea, kupungua kwa misitu na mbuga zetu, kuongezeka kwa ukame na hali ya jangwa kutishia sehemu kubwa ya nchi yetu.
Serikali imeshindwa kudhibiti shughuli za uchumi zinazoathiri mazingira, kama vile njia haramu za uvuvi, uchomaji moto, mbinu duni za kilimo na ukataji holela wa miti kwa ajili ya makazi, nishati, mbao na kadhalika. Baa la njaa, ukosefu wa maji safi na salama, mlipuko wa magonjwa ya mara kwa mara, ukame, kupotea au upungufu wa viumbe hai waishio majini na porini ni matokeo ya uharibifu wa mazingira.
NCCR-Mageuzi kimebaini kuwa matatizo ya uchafuzi wa mazingira yameshamiri kutokana na utawala mbovu wa serikali ya sasa unaoambatana na vitendo vya rushwa. Hivyo, Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba vitendo hivyo vimekomeshwa na itatunga sheria na kanuni madhubuti za kulinda na kuhifadhi mazingira mijini, vijijini na kwenye mbuga za hifadhi zote za kitaifa. Pia itashirikisha vyombo vya dola, taasisi za umma, sekta binafsi, mashirika ya umma, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) na taasisi za kimataifa katika zoezi zima la kuhifadhi mazingira.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba ujenzi wa viwanda, njia za mawasiliano, migodi, na shughuli nyingine zote za kiuchumi na kijamii zinazoathiri mazingira zinadhibitiwa. Itahikikisha kwamba vitendo vinavyoharibu mazingira kwa hila vimekomeshwa na itahakikisha kwamba viwanda vinavyoleta uchafuzi wa mazingira vimepigwa marufuku. Serikali ya NCCR-Mageuzi itasisitiza uanzishaji wa viwanda ambavyo vitatumia teknolojia bora na mbinu sahihi za kuhifadhi mazingira.
Ili kuhakikishwa kuwa nchi yetu haiharibiwi na mazingira hayachafuliwi, miradi yote ya viwanda, uchimbaji madini hautaanza kabla ya kufanya tathimini ya athari za miradi hiyo kwa mazingira (Environmental Impact Assessment). Itakuwa ni marufuku kuendeleza ujenzi wa miji na vijiji bila kuzingatia kanuni za hifadhi ya mazingira.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itazingatia matumizi ya nishati mbadala kama vile nishati ya jua na nguvu za upepo katika shughuli za uzalishaji ili kuyanusuru mazingira. Itawekeza katika teknolojia ya matumizi ya nishati ya gesi kutoka katika kinyesi cha binadamu na wanyama na matumizi ya mbolea na maji yanayozalishwa katika mitambo hii kutumika katika kuotesha mimea. Serikali ya NCCR-Mageuzi itawekeza pia katika teknolojia ya nishati ya mionzi ya jua kwa matumizi ya nyumbani na uzalishaji viwandani. Mkazo pia utatiliwa katika matumizi ya gesi ya Songosongo, na kwingineko hususan, kusini mwa Tanzania. Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba pale ambapo mazingira yameathirika hatua mbalimbali zikiwemo za kisheria zitachukuliwa haraka kuyaponya mazingira. Aidha serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba wananchi wanahamasishwa kupanda miti. Serikali yenyewe itaanzisha mipango madhubuti ya kupanda na kuvuna miti, na zoezi la upandaji miti litakuwa la kudumu.
5.5 Sera ya Hifadhi na Maendeleo ya Jamii
Wanawake: Historia imembagua mwanamke, kumdharau na kumtweza. Hakupewa nafasi ya kujiendeleza kielimu, kiajira na katika kumiliki mali na uchumi wa familia na wa nchi. Mwanamke alidunishwa kwa vile tu yeye ni mwanamke. Ubaguzi huo wa kijinsia si halali na ni kashfa kubwa kwa binadamu. Lazima utamaduni mzima unaoshikilia dhana kwamba mwanamke ni kiumbe duni na dhaifu ubomolewe na kufutwa.
Wanawake kama wanaume wana haki ya kuongoza kwenye fani zote ndani ya jamii. NCCR-Mageuzi kinaota mwito kwa wanawake wote nchini kuungana; “unganeni, hamtapoteza kitu chochote ila itakuwa ndio mwisho wa unyonge wenu.”
Changamoto kwa wanawake wote wa nchi hii ni kuelewa kuwa sasa ndio wakati wa kusimama na kusema “nataka kuwa kiongozi wa siasa! nataka kuongoza nchi!”
Chama chetu kitaandaa mazingira mazuri ya kumuendeleza mwanamke. Upendeleo kwenye huduma za kijamii zenye lengo la kumnyanyua mwanamke utatiliwa mkazo. Usawa kwenye ajira, haki ya miliki ya mali , na haki ya uongozi ni msingi ambao wanamageuzi wa kweli lazima waheshimu na kuzingatia katika vita vya kuikomboa jamii nzima ya watanzania kutoka katika ubaguzi wa kijinsia.
Watoto: Kuhusu suala la watoto na haki zao mbele ya sheria, NCCR-Mageuzi inathamini watoto kwa kuwa watoto ni sehemu ya taifa la leo na kesho.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha sheria zinatungwa za kulinda haki za watoto kama vile kupata elimu bora, kuwa na afya njema, malezi bora, tiba yenye uhakika, lishe bora, upendo kutoka kwa jamii na kuzuia ajira na unyonyaji wa watoto.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikishwa pia katika sheria hiyo inawabana wazazi na jamii kuwajibika katika kuwalinda watoto dhidi ya uonevu na unyanyasaji wa aina zote.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha inatenga maeneo kwa ajili ya burudani kwa watoto na michezo ili kukuza vipaji vyao.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha inaanzisha vituo vya kulelea watoto (day care centers) pamoja na vituo vya kulelea watoto yatima.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha matumizi ya lugha yanakuwa ya ufasaha na yenye maadili.
NCCR-Mageuzi italinda haki za kiuchumi za watoto kwa kupata malipo halali hasa pale mtoto anapofanya tendo fulani kwa faida ya taifa mfano; Kuwatumia watoto katika matangazo ya biashara; na kuwatumia watoto kuitangaza nchi kwa njia ya ngoma na nyimbo.
Wasiojiweza: Aidha serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba wazee, wasiojiweza na walemavu wanapatiwa huduma za lazima za kijamii kama vile makazi, chakula, mavazi, matibabu, burudani, na nyinginezo.
5.6 Sera ya Maji
Tathmini ya hali: Maji ni rasilimali muhimu kiuchumi na ni uhai wa taifa. Licha ya shughuli za kilimo ya maji majumbani na kwenye shughuli za kilimo na viwanda, sekta ya maji ni chanzo cha sehemu kubwa ya nishati inayotumika nchini. Licha ya ahadi za watawala wa sasa za kueneza huduma za maji kwa wote, tathmini ya sekta ya maji inaonyesha kuwa karibu nusu ya watanzania hawapati maji safi na salama. Kwa upande wa vijijini ni watu milioni kumi tu kati ya wakazi milioni ishirini na mbili wanaopata maji safi na salama.
Mikakati ya chama: Ili kuongeza upatikanaji wa maji, serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya yafuatayo;
Itawekeza katika tekinolojia ya uvunaji wa maji ya mvua na hifadhi ya maji ya matumizi majumbani, kwenye taasisi, viwandani na mashambani. Aidha, itahakikisha kwamba jamii zetu zinajijengea uwezo wa kuvuna na kutumia maji ya mvua.
Itahakikisha kwamba maji ya mito na maziwa yatumika na kuhifadhiwa kwa utaalamu wa kisasa ili yakidhi mahitaji ya jamii.
Itahakikisha kwamba vyanzo vya maji vinahifadhiwa kisheria na kupewa hadhi ya hifadhi ya taifa. Hii ni pamoja na kuchukua hatua za kuyaponya mazingira pale ambapo yameharibiwa.
Itaweka mkazo katika uanzishaji, uendelezeji na udumishaji wa miradi ya maji vijijini. Itazingatia maoni na matokeo ya utafiti wa kitaalamu ili tahadhari ziweze kuchukuliwa kwa lengo la kuzuia sekta hii isiendelee kuathirika.
5.7 Sera ya Habari
Tathmini ya hali: Habari ni uhai na nguvu za Taifa. Taifa lolote lisilo na uwezo wa kupata, kutumia na kutuma habari litashindwa, kudhoofika na hatimaye kusambaratika. Habari ni bidhaa ambazo huzalishwa katika viwanda vya habari kama vile bidhaa nyingine zozote zinazofikishwa kwenye soko ili mlaji anunue.
Hivyo basi vyombo vya habari ambavyo kwa kweli ndivyo viwanda vya habari ni muhimu sana kwa maendeleo, maelewano, umoja na amani ya taifa. Mageuzi nchini Tanzania kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda demokrasia vya vyama vingi ni matokeo ya mchango mkubwa na kujitoa muhanga kwa waandishi wa habari Watanzania. Hawa ni wanamageuzi na mashujaa wasio na jina katika historia ya Mageuzi nchini mwetu.
Mazingira ya kisheria nchini yanaminya uhuru wa vyombo vya habari. Mathalani, ipo sheria ya magazeti ya mwaka 1976 inayoipa serikali mamlaka ya kupiga marufuku magazeti kama inavyotaka. Sheria hii ni moja katika ya sheria 40 za kikandamizaji iliyoainishwa na tume ya aliyekuwa Jaji Mkuu Francis Nyalali (Kwa sasa marehemu). Sheria hii inawapa polisi mamlaka ya kuingia kwenye viwanda vya habari na kuwanyanyasa waandishi wa habari na wapiga chapa kwa kuwapekua na kupora makala, kazi au maandishi.
Vile vile ipo sheria inayoviwekea mipaka vyombo vya utangazaji visizidishe eneo la zaidi ya robo ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Huu ni ukiritimba wa dola katika usambazaji wa habari na ni sheria inayokiuka ibara ya 18(1) na (2) ya katiba ya nchi.
Sera ya chama: NCCR-Mageuzi kinatambua kwamba, kuwepo kwake kama chama cha Mageuzi ni matokeo ya uthubutu wa vyombo vya habari. Kwa sababu hiyo na nyinginezo, NCCR-Mageuzi kitapigania uhuru wa waaandishi wa habari wa kukusanya, kuandika na kusambaza habari ndani na nje ya Tanzania . Pia tunapigania na kulinda haki ya kupata habari kutoka vyombo vya serikali vinavyoendesha shughuli za umma ili kuhakikisha kwamba serikali inatawala kwa uwazi na kwa kuwajibika kwa umma.
NCCR-Mageuzi kinatetea kulindwa kwa wanahabari na sheria za nchi, hii waweze kutekeleza wajibu wao wa kukusanya, kuandika na kusambaza habari. Vile vile NCCR-Mageuzi kinapinga kwa nguvu zetu zote sheria zinazowabana wanahabari na kuwazuia kukusanya, kuandika na kusambaza habari.
NCCR-Mageuzi kinapinga pia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 inayoipa serikali mamlaka ya kupiga marufuku magazeti kama inavyotaka.
NCCR-Mageuzi kinatamka kwamba uhuru wa habari ni uhai na nguvu za Taifa. Ukandamizaji na unyanyasaji wa wanahabari ni kulipiga vita taifa na kudhoofisha misingi yake ya kidemokrasia. Chama chochote kinachofurahia kuyafanya hayo, basi ni adui wa wanahabari na hakistahili kupigiwa kura kuendelea kutawala.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itatambua kisheria Baraza Huru la Habari lililoundwa na linaloendeshwa na wanahabari wenyewe ili kujiwajibisha na kupandisha viwango vya utendaji kazi wao kitaaluma.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itafuta sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari hususan sheria inayozuia vyombo vya utangazaji kutangaza habari katika eneo lote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
5.8 Sera ya Utamaduni na Burudani
Tathmini ya hali: Serikali iliyoko madarakani imeshindwa kulinda utamaduni wetu. Sasa unaharibiwa na utamaduni wa kigeni kupitia vitabu, magazeti, televisheni, kanda za video, sinema, mtandao wa kompyuta duniani, na njia nyinginezo. Hata nchi zilizoendelea kiuchumi duniani hulinda tamaduni zao kwa sheria za kuchuja mambo mabaya ili yasiingie katika tamaduni zao au kusimamia taratibu za usambazaji na kuhakikisha kwamba mambo yenye kuweza kuharibu maadili hayawafikii wananchi hususani watoto na vijana.
Mpaka sasa nchi yetu haina mwelekeo maalumu kuhusu utamaduni na michezo. Serikali imeshindwa kabisa kuendeleza utamaduni na michezo nchini. Nchi yetu haiko katika mataifa maarufu katika fani ya utamaduni na michezo. Wanamichezo wetu wanashindwa kila mara katika michezo ya kimataifa kutokana na kuwa na viwango vya chini. Kwa mfano, muziki haujapewa umuhimu wowote katika mfumo wetu wa elimu nchini. Watawala wanautumia utamaduni na michezo kama chombo cha kustarehesha viongozi wa siasa na pale ambapo wananchi wanahusika, fani hizi zimetumiwa kama chombo kueneza propaganda za chama kimoja nchini.
Nchi yetu haina umaarufu katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Aidha haijulikani katika nyanja za lugha, michezo, muziki na maadili kwa sababu haina mchango maalum katika nyanja hizo licha ya kuwa na watanzania wenye vipaji na uwezo katika mambo hayo.
Sera: NCCR-Mageuzi kinatambua kuwa utamaduni na burudani ni sehemu muhimu katika maisha ya binadamu na ni matokeo ya maendeleo. Pia, NCCR-Mageuzi kinaichukulia sekta ya utamaduni kama eneo la ajira.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya yafuatayo;
Italinda na kuimarisha utamaduni wa kitanzania kwa nguvu zote.
Itahakikisha kwamba Kiswahili ambacho ni lugha ya taifa kinakuwa lugha ya ukombozi kwa kuistawisha ili iwe utambulisho wa mtanzania duniani, iwe lugha ya mawasiliano katika fani mbalimbali za maisha; iwe nyenzo ya kukita na kusheheneza sayansi na teknolojia katika jamii ya Tanzania, iwe chombo cha kutangaza na kueneza utamaduni wa mtanzania, kuchangia katika mapato ya taifa na kujenga mahusiano mema ya kimataifa.
Lugha za makabila na mazuri yote katika mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania vitahifadhiwa na kustawishwa ili viendelee kuwa kisima ambamo yatochotwa mambo ya kudumishwa kwa ajili ya kuimarisha utaifa wa watanzania.
Itahakikisha kuwa kumbukumbu za historia ya taifa na makabila zinahifadhiwa.
Itahakikisha kuwa utalii wa ndani unaimarishwa na kukuzwa ili wananchi wetu waweze kuona na kufurahia nchi yao inayopendeza. Kwa kuwa suala la burudani ni la lazima kwa jamii, raia watahamasishwa kuwekeza katika sekta hii kwa kupatiwa elimu na mtaji.
Wasanii wataimarishwa na kusaidiwa ili waweze kustawisha biashara ya burudani nchini.
Hakimiliki ya kazi za sanaa italindwa bila suluhu na waporaji wa haki hiyo.
Serikali ya NCCR-Mageuzi
Itasimamia ujenzi wa mabwalo (halls) ya kisasa ya starehe na pia zitatengwa sehemu maalum katika maeneo ya makazi vijijini na mijini kwa ajili ya aina mbalimbali za starehe, burudani na michezo. Bustani za mapumziko zitaanzishwa na kuendelezwa ili miji yetu na vijiji vyetu viwe maskani ya kupendeza ya binadamu.
Itaimarisha huduma za burudani.
Michezo na muziki vitapewa kipaumbele katika mfumo wa elimu na katika maisha ya jamii. itahakikisha kwamba utamaduni wa Taifa, na michezo vinapewa kipaumbele katika mfumo wetu wa elimu na sekta mbalimbali za jamii.
Itahakikisha kwamba nyenzo na vifaa vya michezo na muziki vinazalishwa hapa nchini na kuagizwa toka nje ili viweze kupatikana katika mashule, vyuo na jamii kwa bei nafuu.
Lengo la NCCR-Mageuzi ni kujenga upya utaifa wa watanzania, kujenga taifa lenye watu wenye afya na nguvu kimichezo, kuendeleza lugha ya Kiswahili na maadili ya taifa, kuimarisha huduma za burudani na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa.
6.1 Dokezo
Katika sura hii tunaelezea umuhimu wa ulinzi na usalama katika taifa na kubainisha sera za chama cha NCCR-Mageuzi kuhusu masuala hayo nyeti. Tunaeleza pia mikakati ya utekelezaji wa sera kama itakavyozingatiwa na Serikali itakayoundwa na chama hiki, endapo tutapata ridhaa ya kuongoza nchi.
6.2 Majeshi
Majeshi yana umuhimu wa pekee katika ulinzi na usalama wa nchi.
Sera ya NCCR-Mageuzi: ni majeshi kwa usalama wa kila mwananchi na kila mali ya Tanzania.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kuwa;
Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la kujenga taifa, pamoja na usalama wa taifa vitakuwa chini ya serikali kuu.
Jeshi la ulinzi litakuwa jeshi la kisasa. Jeshi letu lazima lifikie viwango vya kimataifa katika sayansi ya ulinzi na uwezo wa kulinda taifa. Serikali ya NCCR-Mageuzi itawashirikisha wanajeshi kikamilifu katika zoezi la kuboresha jeshi, kuinua kiwango cha taaluma na kulishirikisha ili litoe mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Jeshi la kujenga taifa litapewa mwalekeo wa mafunzo ya ufundi na utaalamu, hii ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na tatizo la ajira, na ongezeko la vijana wanaozunguka bila kazi mijini.
Jeshi la polisi litawekwa chini ya serikali za Tanganyika na Zanzibar. Hata hivyo utajengwa uhusiano wa karibu ambao utawezesha polisi katika sehemu hizi mbili kushirikiana kwa karibu.
Idara ya Usalama wa Taifa itaundwa upya chini ya mfumo mpya na sheria ya Bunge itakayohakikisha kwamba shughuli za idara hii zinadhibitiwa na Bunge. Aidha mtizamo wa usalama wa Taifa utapewa tafsiri pana zaidi na kuendelezwa kisayansi, teknolojia na kiuchumi. Itakuwa ni marufuku kwa idara ya usalama wa taifa kuathiri uhuru wa raia au kutumiwa ili kudhibiti upinzani halali wa kisiasa na kuonekana kama chombo cha kulinda maslahi ya wachache tu badala ya taifa kwa ujumla wake. Wajibu wa idara hii utakuwa ni kuchangia katika ulinzi wa taifa, na kutetea maslahi ya taifa.
6.3 Uraia na Uhamiaji
Tathmini ya hali: Nchi yetu imegeuzwa jalala la kimataifa ambapo matapeli na wahalifu wa kimataifa wanaingia na kutoka nchini bila kudhibitiwa. Wageni wamefanya nchi hii ni shamba lao na imefikia kiwango kwamba hata sheria ya uraia haziheshimiwi. Serikali iliyopo imeruhusu wahalifu, watu wasio na manufaa yoyote kwa Taifa, kupokelewa na kupewa uraia wa Tanzania . Hivi sasa kuongezeka kwa idadi ya wageni hohehahe na majambazi wanaoshiriki katika biashara haramu ikiwa ni pamoja na madawa ya kulevya kumekithiri.
Mtazamo wa kisera: NCCR-Mageuzi kinasema kwamba uraia wa Tanzania si wa kunadiwa sokoni. Tutaruhusu wageni maalum tu kuhamia nchini. Wageni watakopewa uraia ni hasa wale ambao taifa linawahitaji. Hawa ni pamoja na wanasayansi, wasanii, wanamichezo maarufu na wale ambao uwezo wao wa kiuchumi utalinufaisha taifa.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba;
Sheria ya uraia inatungwa upya kuzingatia misingi iliyotajwa hapo juu.
Wageni ambao wana historia ya uhalifu watadhibitiwa kwa kufuata sheria za kimataifa na wahalifu hawataruhusiwa kuingia au kuhamia Tanzania . Wale wote waliodanganya kuhusu uraia wao na ambao wanaishi na kufanya kazi au biashara, serikali ya NCCR-Mageuzi haitakuwa na jinsi nyingine bali kusitisha kukaa kwao nchini.
Kila Mtanzania atakapotaka atapatiwa hati ya kusafiria nchi za nje (passport) bila kipingamizi chochote.
Sheria ya uraia inazingatia maslahi ya taifa.
6.4 Maafa na Dharura
Tathmini ya hali: Maendeleo ya nchi ni pamoja na kukua na kukomaa kwa uwezo wa taifa kutabiri na kujikinga na maafa na dharura. Hivi sasa uwezo wa nchi katika kukabili majanga ni mdogo na idara zinazohusika hazina ufanisi kwa sababu ya uduni wa vifaa na miundombinu.
Sera ya NCCR-Mageuzi; ni Tahadhari makini kabla ya janga, utendaji wa papo hapo (immediate) litokeapo janga.
Mikakati: Serikali ya NCCR-Mageuzi itafanya yafuatayo;
Itahakikisha kwamba vyombo maalum vya kukabiliana na maafa na dharura vinaundwa. Itaunda mfuko maalum wa taifa wa dharura na maafa pamoja na hifadhi ya chakula kwa ajili hiyo.
6.5 Ushirikiano na Nchi za Nje
Tathmini ya hali: Tanzania ni sehemu ya jumuiya ya kimataifa ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali za mabadiliko yanayotokea kwa kasi. Hivyo, sera zetu za mambo ya nje lazima zizingatie mabadiliko yanayoendelea katika hali ya kisasa, kiulinzi, kiuchumi na kijamii duniani. Madhumuni ya kuzingatia hayo ni kukabiliana na matatizo mapya, na kuliwezesha taifa kutumia kwa manufaa yake kila mwanya unaojitokeza katika uchumi wa dunia. Ni wazi kwamba sera ya nchi za nje ni kioo cha ufanisi au kushindwa kwa sera za ndani. Kulingana na ukweli huu, sera zinazotumika nchini kwa sasa kuhusu mambo ya nje zimeparanganyika. Tanzania siyo tena Taifa lililo mstari wa mbele katika harakati za kuwakomboa wanyonge duniani. Sifa na nafasi ya taifa letu miongoni mwa mataifa yasiyofungamana na upande wowote, mataifa ya dunia ya tatu imedharirika kutokana na msimamo legelege wa watawala wa sasa kuhusu masuala muhimu yanayowakabili wanyonge katika jumuiya ya kimataifa.
Sera ya NCCR-Mageuzi ni; mahusiano ya kimataifa yenye tija na ya heshima kwa Taifa.
Mikakati: Serikali itakayoundwa na NCCR-Mageuzi;
Itachukua mwelekeo mpya wa sera za taifa katika mambo ya nje.
Italishirikisha taifa katika kutoa mchango wake kwenye masuala muhimu yanayoikabili jumuiya ya kimataifa kwa kuzingatia maslahi ya taifa. Msimamo wa Tanzania utakuwa ni kuwatetea wanyonge na kimataifa. Barani Afrika, Tanzania itakuwa mstari wa mbele katika kupigania umoja, amani na ushirikiano wa kiuchumi baina ya mataifa ya Afrika.
Serikali itashirikiana na nchi zote, itaimarisha, kudumisha na kuendeleza urafiki uliopo baina ya Tanzania na nchi zilizo marafiki wa Tanzania , barani Afrika na nje ya bara la Afrika.
Itadumisha ujirani mwema wa Tanzania na majirani zake; Tanzania itakuwa mwanachama mzuri wa Umoja wa mataifa, mashirika yake na Umoja wa Nchi za Afrika (A.U) vile vile tutashiriki kikamilifu katika umoja wa watu weusi (Pan African Movement). Tanzania itashiriki kikamilifu katika jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC) na itaheshimu mikataba ambayo Tanzania imetia saini mradi tu mikataba hiyo haipingani na maslahi ya Taifa. Tanzania itaendelea kuwa mwanachama makini wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Vile vile, mtizamo wa NCCR-Mageuzi kuhusu mambo ya nje ni kuhakikisha kwamba watendaji wa mambo ya nje nchini na nje wanazingatia suala la kulipatia Taifa uwezo wa maendeleo ya kiuchumi katika nyanja za viwanda, biashara, sayansi, teknolojia na mambo ya utamaduni. Uwakilishi wetu nchi za nje utateuliwa kwa kuzingatia misingi ya uwezo kielimu na ujuzi katika fani muhimu za uchumi, sayansi,na teknolojia. Fursa za Tanzania kwa nchi za nje zitafunguliwa kwa kuzingatia maslahi ya Tanzania kiuchumi na hasa katika fani ya biashara, elimu, sayansi na teknolojia.
Kadhalika, Sera ya serikali ya NCCR-Mageuzi ya mambo ya nje itazingatia kuwapa wataalamu wetu motisha ili wasihame nchi, na kuwavutia wataalamu muhimu wageni kuhamia Tanzania .
7.1 Dokezo
Katika sura hii kuna tafakuri ya matatizo mbalimbali yanayolikabli taifa na namna ya kuyashughulikia kisera. Hivyo, sura hii inaeleza sera za chama dhidi ya matatizo hayo ambayo ni pamoja na dhuluma, maonevu, ufisadi na rushwa.
7.2 Dhuluma na Maonevu
Mfumo na misingi ya dhuluma na maonevu ilijengeka nchini tangu ukoloni. Baada ya uhuru, misingi hiyo iliendelezwa katika dola la chama kimoja. Mshikamano ulijengeka kati ya viongozi chama na watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya shina kitongoji, kijiji, mtaa, wilaya, mkoa hadi taifa. Chama dola kilijengeka kwa kuainishwa kikatiba, kisheria na kiutendaji. Dhana ya chama kushika hatamu za dola ilifuatwa. Tamko la chama lilipewa nguvu za kisheria kama sheria ya Bunge. Viongozi wa chama walipewa wadhifa wa kuwa wajumbe wa vyombo vya kiutawala vya dola. Mfano hai ni ushiriki wa makada wa chama tawala katika kamati za maendeleo za kata, wilaya, mkoa na taifa na vivyo hivyo kwenye kamati za ulinzi na usalama za wilaya, mikoa na taifa.
Kwa kuwa wakuu wa wilaya na mikoa ni makatibu wa kamati ya siasa ya chama dola katika ngazi hizo, ushiriki wao katika vikao vya utendaji serikalini unawapa kofia mbili na matumizi ya kofia hizo yaliwageuza watendaji wa serikali walio chini yao kuwa watumishi pia wa chama bila wao kujijua. Madaraka ya namna hii yametoa mwanya kwa walionayo kudhulumu na kuwaonea wanyonge badala ya kutumia sheria kuwalinda.
Dhuluma na maonevu yanajishihirisha kwa wananchi kukamatwa na kupekuliwa hovyo na polisi bila kufuata kanuni za sheria ya nchi. Wengi wanaokamatwa na polisi katika mazingira haya hujikuta wamepoteza mali zao binafsi kama vile fedha, simu za mikononi na vitu vingine vya thamani. Aidha, Chama cha NCCR-Mageuzi kinayo mifano mingi ya wanachama wake waliosingiziwa uhalifu ili kuwanyanyasa na kuwatisha wananchi wengine wasiunge mkono wanamageuzi.
Sera ya NCCR-Mageuzi kuhusu dhuluma na maonevu ya dola dhidi ya umma ni kusimama kidete dhidi ya maovu hayo bila kukata tamaa. Maovu hukomeshwa na moyo usioyumba wala kukata tamaa; moyo wa wapigania haki.
Serikali itakayoundwa na NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba hakuna muingiliano kati ya shughuli za kiserikali na shughuli za kichama. Uadilifu wa hali ya juu utajengwa katika jeshi la polisi na vyombo vingine ili pamoja na mambo mengine, maonevu dhidi ya raia yakomeshwe.
7.3 Ufisadi/Rushwa
Watanzania wanakiri kuwa nchi imekumbwa na janga la rushwa. Rushwa ni saratani inayokula na kuua utawala bora. Kwa kuwa janga hili lipo, si suluhisho tena kusaka mla rushwa mmoja mmoja. Suluhisho sahihi ni kutafuta na kushughulikia sababu za kuzuka na kuenea kwa rushwa katika jamii. Kurejea kila mara msemo unaosema kuwa rushwa ni adui wa haki hakusaidii kuondoa ufisadi ulionenea kwenye kila pembe ya dola. Kwa mfano haitafanikiwa vita dhidi ya rushwa ikiwa watendaji wa serikali wataendelea kulipwa ujira duni usiokidhi gharama za maisha. Mazingira kama haya ni kiini cha rushwa. Taifa limeshuhudia jinsi tabia ya kuruhusu watendaji wa serikali waishi kwa kubangaiza kupokea bakshishi kutoka kwa wanajamii wanowahudumia, kutumia vibaya kwa matumizi binafsi huduma na rasilimali za kiofisi kufidia pengo la kipato kulivyojenga na kuimarisha rushwa ndani ya serikali. Tabia hii na nyingine nyingi zilizotajwa kwenye Ripoti ya Tume ya jaji Joseph Sinde Warioba hazijatafutiwa ufumbuzi hadi leo.
Chama cha NCCR-Mageuzi kimebaini pia kuwa utaratibu wa kuwaajiri na kuwalipa wageni ujira mkubwa kuliko wenyeji wenye ujuzi unaofanana ni kiini kingine cha rushwa nchini. Katika mazingira kama haya, Mtanzania yuko tayari kuruhusu sera, sheria na maamuzi yanayolingang’anya taifa masilahi yake kwa zawadi au hongo mradi anajinufaisha yeye binafsi na familia yake. Utamaduni huu umetia nanga katika jamii yetu kiasi kwamba viongozi na maofisa wa serikali wanashindana sasa kuiba mali ya umma. Mwenye sifa ni yule anayeiba na anayechelea kuiba huchekwa na kubezwa kwa kuwa mpumbavu.
NCCR-Mageuzi kinaamini kuwa rushwa ni chanzo kikubwa cha kukwama na kudidimia kwa nchi na maendeleo ya nchi yetu. Taifa halijatendewa haki kufuatia kupitishwa kwa sheria na taratibu zinazohalalisha rushwa kwenye uchaguzi (kwa mfano kuiita rushwa takrima).
Kisheria, rushwa ni kosa la jinai na kimaadili rushwa ni dhambi. Hivyo chama cha NCCR-Mageuzi kitasimamia ukweli huu. Kitawaomba wananchi kutopokea takrima kwenye uchaguzi kwa kuwa kura ni risasi aliyonayo mpiga kura dhidi ya rushwa. NCCR-Mageuzi inaahidi kuwa itapiga vita rushwa kwa nguvu zake zote. Hakika ni dhumuni la NCCR-Mageuzi kupambana dhidi ya vitendo viovu vya ulaji rushwa, wizi wa mali ya umma, uporaji wa rasilimali za taifa, biashara haramu ya madawa ya kulevya na matumizi mabaya ya vyombo vya dola.
Mkakati wetu wa kupiga vita rushwa utaanza kwa kudhibiti ajira katika sekta ya umma ili sekta hiyo iwe bora na iwape waajiriwa maslahi yanayoendana na uwezo wa nchi kiuchumi, na kisha tutaoanisha ajira, kipato na gharama za maisha ili kupunguza vishawishi vya rushwa kwa watumishi wa sekta ya umma. Tutaimarisha taasisi ya kupambana na rushwa. Itawajibika kwa bunge badala ya kuwajibika kwa rais kama ilivyo sasa.
8.1 Dokezo
Katika sura hii kuna majumuisho ya mkakati wa namna ya kutekeleza sera zilizotajwa katika kitabu hiki. Itazingatiwa pia kuwa katika sera mbalimbali zilizoainishwa katika sura zilizotangulia, mikakati ya kutekeleza sera husika imetajwa pia. Sura hii ya mwisho inajikita zaidi katika kutoa mwongozo zaidi wa utekelezaji. Katika kuleleza haya tunazingatia kwamba, sera za chama chochote cha siasa hazina maana yoyote kama hazitekelezeki. Kwa kuzingatia hilo, Chama chetu kinapotoa Ilani zake za uchaguzi hubainisha mambo muhimu ya lazima na ambayo yako katika uwezo wa taifa letu kuyatekeleza. Ili Ilani za chama zinazotokana na sera zetu ziweze kutekelezeka, NCCR-Mageuzi kitahitaji ridhaa ya taifa, na ushirikiano wa kila mwananchi bila kujali dini, kabila, chama au rangi.
8.2 Kuchambua na kupanga Mahitaji ya Taifa
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba mambo yaliyotajwa kwenye kila eneo la sera zilizomo kwenye kitabu hiki yanawekwa wazi kwa wananchi ili kuomba ushirikiano wa kila mwananchi katika zoezi la kuchambua na kupanga mahitaji muhimu ya taifa. Wataalamu Wazalendo wa nchi hii watashirikishwa kikamilifu katika hatua zote za uchambuzi wa kupanga mahitaji na vipaumbele vya taifa. Yale tutakayokubaliana kwa pamoja ndiyo yatakayopewa umuhimu wa kwanza kutekelezwa. Hii ni kwa kuzingatia ukweli kwamba uwezo wa taifa una kikomo chake.
8.3 Kuchambua na Kupanga Uwezo wa Taifa Kuyakabili Mahitaji Muhimu ya Taifa.
Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna taifa lisiloweza kuendelea, likiamua kufanya hivyo. Inafahamika pia kwamba suluba na kazi ya maendeleo ni ngumu na inahitaji moyo, ujarisiri, utaalamu, mbinu, moyo wa kujitolea na uzalendo.
Ni kweli pia kwamba Tanzania inazo rasilimali zote za lazima kwa maendeleo. Kwa mfano tunayo ardhi nzuri kwa kilimo, tunayo madini ya aina nyingi, tunayo mito , maziwa na bahari, tunazo bandari kubwa, maliasili tele na watu wenye ujuzi na taaluma ya kutosha. Kushindwa kwetu kutambua na kuzitumia ipasavyo kuleta maendeleo limekuwa ni chimbuko la umaskini wa taifa letu.
Serikali ya NCCR-Mageuzi kwa kuzingatia ukweli huu itatekeleza zoezi la kuchambua na kutathmini rasilimali za taifa na uwezo wetu wa kuzitawala na kuzitumia ipasavyo ili kuleta maendeleo ya haraka kwa taifa letu.
8.4 Mbinu za Utekelezaji
Ili kutekeleza sera hizi serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba uchumi wa nchi unajengwa, kukua na kuliletea taifa pato halisi mwaka hadi mwaka.
Serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba utaratibu madhubuti wa kulipa kodi na ukusanyaji wa kodi unajengwa na kuimarishwa. Pia serikali itahakikikisha kwamba mapato ya serikali yanatumika ipasavyo kuleta huduma na maendeleo ya jamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba ufanisi unapatikana siyo tu katika ukusanyaji kodi na mapato, bali pia katika kudhibiti matumizi ya serikali. Kwa vyovyote vile serikali ya NCCR-Mageuzi itahakikisha kwamba wananchi wenyewe wanahusishwa na kushirikishwa katika kufikia maamuzi muhimu ya kujenga upya uchumi wa taifa.
NCCR-Mageuzi kinatambua wazi kwamba serikali ya sasa imejenga utamaduni wa utawala wa mabavu, uongozi wa rushwa na utoaji wa amri. Serikali itakayoundwa na NCCR-Mageuzi itaongozwa kwa kutegemea nguvu ya hoja badala ya hoja ya nguvu, na itarejesha hadhi ya wasomi wetu ili tuwatumie katika kuling’oa taifa letu katika hali ya kutoendelea na kuliongoza katika karne ya 21 likiwa na ustawi na maendeleo makubwa ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
THE GREEN AGENDA
Green Agenda is one of our prime policies. It is for this reason that the agenda is highlighted in our party constitution.
The NCCR-Mageuzi party’s green agenda is stated in article 8(12) of the party constitution as follows:
“to have clean and safe environment for the sustenance of human life and the existence of other living organisms”.
The ecological wisdom as our philosophical outlook underpinning the agenda is as follows.
NCCR-MAGEUZI Party considers mother earth as a common human kind heritage and resource to which every people have a right to and is accountable for its protection and improvement. Our party acknowledges that human beings are part of the natural world and we respect the specific values of all forms of life, including nonhuman species. Mother earth is our common heritage and all humans have a common future. Our ecological wisdom is to respect
mother earth and the life of all living species.
In relation to the Agenda, we also recognize the following;
In relation to the Agenda, we also recognize the following;
SUSTAINABILITY
We recognize the scope for the material expansion of society within the biosphere, and the need to maintain biodiversity through the use of renewable resources. Any global or even cosmic disaster that is a consequence of human activity is the responsibility of the human kind as a whole. If the ozone layer perishes as a result of human activities, or if global warming results into uncontrollable disasters, humankind is to blame. In order to stand up and be counted on these important issues, we need common action based on a common global green agenda.
RESPECT FOR DIVERSITY
We honour and value equally the Earth's biological and ecological diversity together with the context of individual responsibility toward all beings. We believe in a balanced eco-system. Our environment has to have a reasonable balance between what nature can offer for human needs and what humans have to do to protect and improve nature’s capacity to sustain healthy human life and the lives of other living organisms. We therefore reject over-exploitation of nature, damage to natural environment and deployment of practices that cause irreversible damage to nature.
SOCIAL JUSTICE
We assert that justice is social and equitable. The key to social justice is the equitable distribution of resources to ensure that all have full opportunities for personal and social development. In Tanzania our concern and commitment is to secure for all our people acceptable standard of education, a healthy society in which all have access to effective and efficient medical care and sustainable standard of livelihood which assures the basics of life for all.
NON-VIOLENCE
We believe that peace is a fruit of social justice, equity and solidarity amongst humans. We are therefore committed to the achievement of these objectives and peace through the principle of non-violence and shall strive for achievement of a culture of peace and cooperation between states.
PARTICIPATORY DEMOCRACY
We strive for a democracy in which all citizens have the right to express their views, and are able to directly participate in decisions which affect their lives. Sovereignty resides in and belongs to the people. Therefore not only must the constitution of the state be made by the people but the people should be seen participating from grassroots to national level in all governance processes.
THE GREEN AGENDA IN OUR PARTY MANIFESTO
Our political manifesto aims at achieving the above agenda through the following measures:-
(i) Creating awareness among our people in general and our party members in particular, of global issues that surround the green agenda.
(ii) To link with the global green movement in its entirety in political, economic and social fields.
(iii) In education: to struggle for the introduction of alternative education curricula that takes on board an integrated education formation that integrates Tanzanian needs and interests
(iv) In health: to struggle for the establishment of a bi-pillar national health care system founded on traditional and modern medicine.
(v) In Housing: to develop a green habitat agenda that includes green towns, cities and villages;
(vi) In economic development: to implement an economic empowerment policy aimed at including all the people in the national economy. Exploitation of natural resources should be put under permanent sovereignty of the people while all economic activities should be friendly to the environment.
No comments:
Post a Comment