Ilani za Uchaguzi

Ilani ya 2010

1.  0 UTANGULIZI

Mwaka 2010 ni mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania. Huu utakuwa ni uchaguzi mkuu wa nne tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe nchini Tanzania. Hivi sasa ni miaka 49 tangu tujipatie uhuru. Kwa maana nyingine nchi yetu imekuwa Taifa huru kwa miongo mitano kasoro mwaka mmoja tu. Tukilinganisha umri huo na umri wa binadamu, Taifa limekomaa sasa na lina watoto na wajukuu. Tunapojiandaa kupiga kura katika uchaguzi tarajiwa na tunapotafakari tulikotoka na tuliko, na tujiulize maswali kadhaa kuhusu utaifa wetu na kuyapatia majibu sahihi.

Swali: Tulipopata uhuru Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alibainisha maadui wa tatu wa Taifa letu. Je maadui hao ni nani?

Jibu: Maadui wa Taifa letu kama walivyoainishwa na Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere ni ujinga, umasikini na maradhi.

Swali: Je tumewashinda au bado tunao?

Jibu: Hapana, hatujawashinda, bado tunao tena wamezamisha mizizi yao ndani ya jamii yetu kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko miaka hamsini iliyopita tulipopata uhuru.

Swali: Je ni nani wa kulaumiwa?

Jibu: Wa kulaumiwa kwa kushindwa kutuongoza kushinda vita dhidi ya maadui hao watatu wa Taifa ni ‘viongozi wetu’.

Swali: Hao viongozi wetu ni kina nani?

Jibu: Tangu tupate uhuru viongozi wetu ni wana TANU na Afro Shirazi ambao baadaye walibadili jina la vyama vyao na kujiita Chama cha Mapinduzi (CCM)’.

Swali: Kwa nini tuwalaumu viongozi wana CCM na si vinginevyo?

Jibu: Kwa kuwa wamekuwa wakiomba ridhaa ya kutuongoza kwa ahadi kuwa watatuongoza tuwashinde maadui hao watatu lakini kila tulivyozidi kuwapigia kura waliendelea kujali masilahi yao binafsi na kutuacha katika ujinga zaidi, umasikini zaidi na maradhi zaidi.

Swali: Mbona wao wanasema tatizo si udhaifu wao kiuongozi bali ni umaskini wa Taifa letu?

Jibu: Si kweli, Taifa letu limejaliwa rasilimali zote, dhahabu, almasi, mafuta, wanyama pori, madini ya aina mbalimbali, maziwa makuu matatu, bahari ya Hindi, Mito, Milima na ardhi nzuri ya kilimo na ufugaji. Kutoliongoza Taifa kuzitumia rasilimali hizi kwa maendeleo ya wananchi wake ni udhaifu wa uongozi, na uzembe uliochanganyika na ubinafsi wa viongozi wetu ambao hivi sasa wengi wao sifa yao kuu ni ufisadi.

Swali: Ufisadi umeriathiri Taifa kwa kiasi gani, na tutaung’oa vipi?

Jibu: Ufisadi umelipasua Taifa na unaelekea kuliangamiza. Hatuna budi sote kwa pamoja kuunga mkono mabadiliko makubwa ya kiuongozi na kimfumo. Hii ni pamoja na kuwa na katiba mpya, sheria bora tena zenye kusimamiwa, na kuung’oa madarakani uongozi ulioshindwa kuondoa ufisadi nchini.

Aksante mwana wa nchi kwa majibu muafaka.



2.0 DHAMIRA YA NCCR-MAGEUZI

2.1 Historia fupi ya Chama
Mnamo tarehe 12 June, 1991 Wanamageuzi nchini Tanzania waliunda Kamati ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba (National Committee for Constitutional Reform) (NCCR). Lengo la kuundwa kwa kamati hii lilikuwa kuleta mabadiliko ya haraka kumkomboa mwananchi kiuchumi, kisiasa na kijamii kutokana na hali ya umaskini, ujinga, maradhi, rushwa na ukiritimba wa utawala wa chama kimoja cha siasa, iliyokuwa imeenea nchini chini ya utawala wa chama kimoja cha siasa.

Utawala wa chama kimoja cha siasa ulikuwa umegeuka kuwa utawala wa kidikiteta, usiojali kero za wananchi, na ilivyokuwa wakati huo, utawala huo ulikuwa umeshindwa kabisa kujali mahitaji ya kawaida ya wananchi kama vile chakula, sabuni, dawa ya meno, sukari, mafuta ya kupikia, nguo na bidhaa nyinginezo. Umma wa wananchi ulitaabika kupata mahitaji hayo yaliyokuwa yakihodhiwa na wafanyabiashara na kuuzwa kwa bei ya kuruka. Zilikuwa enzi za ‘bidhaa adimu’ zilizopatikana kwenye ‘maduka ya kaya’. Tanzania ilikuwa nchi ya taabu isiyokuwa na bidhaa muhimu kwa mahitaji ya wananchi madukani.

Katiba iliruhusu Chama kimoja tu cha siasa, kilichoitwa ‘Chama cha Mapinduzi’. Hicho ndicho chama kinachotawala hadi sasa. Wananchi waliothubutu kuwa na fikra mbadala, au waliokosoa hali ilivyokuwa walichukuliwa hatua ya kuwekwa kizuizini kwa amri ya Rais bila kufikishwa mahakamani. Haijulikani hadi leo ni wangapi walifanyiwa vitendo vya aina hiyo na ni wangapi walipoteza maisha yao wakiwa kizuizini. Hata hivyo wanaharakati wanawajua baadhi ya waliowekwa kizuizini kwa namna hiyo kwa amri ya Rais. Waliopata fursa, waliikimbia nchi na kuishi ughaibuni bila kuwa na matumaini ya kurejea nchini mwao. Wanaharakati wanaziita enzi hizo, enzi za giza.

Wanamageuzi walifaulu kushinikiza yafanyike mageuzi ya katiba, sheria na siasa za nchi. Serikali iliridhia kuvunja mfumo wa chama kimoja cha siasa na kuweka mfumo wa vyama vingi vya siasa tulio nao hivi sasa. Fungate la mageuzi haya lilishuhudia wanaharakati waliokuwa ndani ya Kamati ya Taifa ya Mabadiliko ya katiba (NCCR) wakitoka na kujiunda katika vyama vingi vya siasa na wale waliobakia ndani ya kamati wakijiunda kuwa chama cha siasa tarehe 15 Februari 1992 na kusajiliwa rasmi tarehe 21 Januari, 1993 kwa jina la National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi). Chama hiki kimebakia na historia hii, kama mama wa mageuzi ya vyama vingi nchini.

Chama cha NCCR-Mageuzi kimejikita katika mapambano dhidi ya ubeberu ukiwa katika sura ya ukoloni mamboleo na sura ya utandawazi. Hiki ni chama cha umma wa wanyonge chenye lengo kuu la kuleta mageuzi ya kidemokrasia na kijamii. Itikadi ya chama hiki ni demokrasia ya kijamii ambayo misingi yake ni kuheshimu haki za binadamu, umoja na udugu wa umma wa wanyonge nchini na duniani kote, Uhuru wa kitaifa na ustawi wa wanajamii wote kiuchumi, kiafya na kielimu.

2.2 Sifa za Kiongozi Mwanamageuzi
Chama cha NCCR – Mageuzi kinawaletea wapiga kura wagombea wake wa nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani. Hawa ni wagombea waliojitokeza na kuteuliwa kwao na chama chetu kunamaanisha kuwa chama kina imani kuwa ni wagombea wenye sifa za uongozi bora.  Ni muhimu kuliweka wazi suala la sifa za uongozi ili tunapokwenda kutekeleza jukumu letu la kupiga kura tuchague kiongozi mwenye sifa badala ya kushawishiwa kwa takrima na uongo.

Pamoja na sifa zilizowekwa na katiba ya nchi na katiba ya chama tunajua ya kuwa tatizo kubwa tulilonalo katika nchi yetu ni uongozi mbovu.  Maswali na majibu yaliyo kwenye utangulizi wa Ilani hii yanadhihirisha kuwa taifa limekuwa na maendeleo duni kutokana na ukosefu wa uongozi wenye upeo, uadilifu na ujasiri. Hiki ndicho kiini ya umaskini wa Taifa letu na kuporomoka mno miongoni mwa mataifa mengine kimaendeleo. Dawa ya changamoto hizi ni kukubali na kuwa makini kuwachagua viongozi bora wenye upeo, elimu ya kutosha, uadilifu na ujasiri wa kuthubutu.

Kuwa na upeo ni kuwa na fikra pevu na bunifu katika kuongoza ili kulivusha Taifa kwenye changamoto za kimaendeleo. Sifa ya elimu ya kutosha ni muhimu kwa kuwa katika dunia ya ushindani taifa la wajinga halina nafasi. Taifa lenye viongozi wasiosoma. Au ambao elimu yao ni duni haliwezi kushindana katika dunia ya sayansi, tekinolojia na weledi. Tuwakwepe Kama ukoma wagombea wenye elimu ya kubabaisha na vyeti feki. Hawa wataliangamiza taifa.

Sifa ya uadilifu ni sifa muhimu mno kwa kiongozi. Ni hatari kumkabidhi fisi wajibu wa kuuza nyama buchani. Viongozi walafi wa madaraka huutaka uongozi ili kuganga njaa zao. Hutumia fursa ya uongozi kupora mali za umma, kujilundikia mali na kila mara wataliingiza taifa mkenge kwa kujipatia rushwa kwenye mikataba ya serikali na manunuzi ya bidhaa na huduma kwa umma. Sifa hii inabeba uzito mkubwa kwani uadilifu unahusu usafi kiroho, ucha Mungu, utetezi wa haki na hivyo kutokuwa fisadi au mla rushwa.  Sifa hii inampa kiongozi uwezo mkubwa wa kuwa mtetezi wa wanyonge na kuheshimu binadamu wa aina zote, kutokuwa mbaguzi, mkabila, mdini au mnyanyasaji watu kwa misingi ya jinsia.  Hakika mgombea anayewapatia watu kitu chochote ili wampigie kura ni mla rushwa na kwa hiyo hafai kabisa kuwa kiongozi.  Mgombea wa aina hii hana uwezo wa kupambana na ufisadi au rushwa na hivyo asichaguliwe.

Sifa ya ujasiri wa kuthubutu huendana na upeo alionao kiongozi na kiwango chake cha kuipenda nchi yake. Kiongozi mwenye sifa hii hataogopa kubuni mikakati mipya ya kuliongoza taifa na kila mara ataliongoza taifa lake lipate kilicho bora. Atashangilia akiona taifa lake limefaulu na kuneemeka kuliko kuona yeye binafsi amefaulu na kuneemeka. Sifa hii humpa kiongozi haiba. Hii ni sifa inayotokana na utamaduni wa kistaarabu wa mtu binafsi, usafi, kujiheshimu, kujituma, unyenyekevu, kupenda kusikiliza wengine na kusaidia, kupenda kujiendeleza kielimu, kuwa na maarifa mapana kuhusu maisha ya binadamu, kuwatumikia na kuwapenda watu.

Kwa hiyo tunapozungumzia aina gani ya kiongozi tutakayempa dhamana ya kuongoza jamii, tunatazama wale miongoni mwetu wenye sifa hizi. Tuchague watumishi wa umma na sio mabwana wakubwa.

3.0 HALI YA NCHI 2010
Tunapoufikia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 hali ya uchumi wa Taifa letu ni mbaya kuliko ile ya mwaka 2005. Uchumi umeyumba, siyo tu kwa sababu ya kuyumba kwa uchumi wa dunia lakini zaidi kutokana na uongozi dhaifu tulionao kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Katikati ya kipindi cha miaka mitano ya awamu ya nne, wananchi walijionea wenyewe jinsi serikali nzima ya awamu ya nne ilivyolazimika kujiuzulu kutokana na ufisadi wa manunuzi yenye rushwa ya mitambo ya umeme katika kashfa ya Richmond. Pia wananchi wamesikia sana kuhusu jinsi ambavyo serikali ya awamu ya nne ilivyoshindwa kushughulikia ufisadi wa ununuzi ya ndege ya Rais, rada na helikopta za JWTZ, ujenzi wa jengo la minara pacha la Benki Kuu ya Tanzania, EPA na ufisadi mwingineo.

Katika medani ya siasa, Taifa letu liko hoi.  Utawala uliopo umekuwa goigoi katika kutetea masilahi yetu kwenye soko la pamoja la Afrika Mashariki kwa kutowaandaa wananchi wetu kuweza kushindana kwenye soko hilo.  Utawala umeshindwa kabisa kubadili katiba ya nchi iwe ya kidemokrasia zaidi na yenye uwezo wa kutetea haki za binadamu, haki za kiuchumi, kijamii na haki za kisiasa za wananchi wetu.

Hivyo makundi mbalimbali ambayo yamepoteza haki zao, tukianzia na wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wananchi waliopokonywa ardhi yao bila fidia inayostahili ili kujenga miradi ya maendeleo, wananchi waliohamishwa kupisha wawekezaji kwenye ardhi zao, malalamiko dhidi ya uchafuzi wa mazingira unaohatarisha afya za wananchi na kadhalika, yamekuwa yakiilalamikia serikali bila mafanikio ya kupata haki zao.

Chama chetu kimebaini kuwa kiini cha matatizo yote tuliyonayo ni udhaifu wa kiuongozi na dira zisizo sahihi za kiutawala zilizomo katika katiba, sheria mbovu na taratibu dhaifu.  Ili kuleta ufumbuzi wa matatizo haya chama chetu kinazipa kipaumbele ajenda zifuatazo katika uchaguzi huu.
4.0 AJENDA ZETU KATIKA UCHAGUZI WA 2010

4.1 AJENDA ZA KIUTAWALA

4.1.1 KATIBA MPYA
Katiba ya nchi ndiyo sheria kuu ya nchi. Sera za Serikali na Sheria za nchi lazima zitokane na kufungamana na katiba ya nchi. Kama taifa lina katiba mbaya isiyolinda haki za wananchi, basi sheria na mfumo wa utoaji wa haki utakuwa mbaya na usiotenda haki. Kama katiba ya nchi na sheria zake havilindi haki, basi watendaji wa vyombo vya dola hawatatenda haki kwa kuwa haki haipo kisheria.

Pia, Taifa ambalo katiba yake ni mali ya viongozi, kwa maana kwamba imetungwa na viongozi kwa ajili ya kujiweka madarakani na kulinda masilahi yao, halina demokrasia ya kweli. Katiba ya Tanzania ni ya aina hiyo, Ni katiba iliyotungwa na viongozi kupitia Bunge Jamhuri. Sote tutatambua kuwa kwa mujibu wa taaluma ya katiba, Bunge ni chombo cha kutunga sheria za kawaida za nchi lakini si chombo cha kutunga katiba. Katiba ya nchi hutungwa na Baraza la Taifa la Kutunga katiba.

Chama cha NCCR – Mageuzi kinatambua ukweli kwamba baraza la Taifa la Kutunga Katiba ndicho chombo halali cha kutunga katiba ya nchi. Chama chetu kinatambua pia kuwa tangu Taifa letu kuundwa, hatujawa na chombo hiki kwa mujibu wa katiba na sheria zetu za nchi.

Baraza la Taifa la Kutunga Katiba hujumuisha wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na wawakilishi wa sekta muhimu, vyama vya siasa, taasisi za kijamii, mashirika ya dini, vyama vya wafanyakazi, wakulima, taasisi mbalimbali za serikali na kadhalika.

Chama cha NCCR-mageuzi kitahakikisha kuwa Baraza la Taifa la Kutunga Katiba litaundwa na litatekeleza mchakato wa kutungwa katiba mpya.  Kwa mujibu wa mageuzi haya, lengo letu ni kuwa na katiba mpya ya nchi itakayofanya mambo yafuatavyo:

i)    Itaainisha misingi na maadili ya utaifa kutokana na muafaka wa kitaifa, misingi ambayo itadumisha haki, maelewano, amani na umoja.
ii)  Itaweka mfumo mpya wa uchaguzi utakaowawezesha wananchi kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi huru na wa haki. Mfumo huo utaanzisha uwakilishi wa uwiano sambamba na uwakilishi wa majimbo  ulioko hivi sasa.
iii)Itaamuru kuwepo na tume huru ya uchaguzi na itaweka masharti ya uundwaji wake;
iv)  Italiamuru Bunge la Jamhuri kutunga sheria mpya ya uchaguzi inayoweka mazingira huru na sawa kwa wote kushiriki na kushindana katika uwanja ulio sawa.
v)   Itaweka misingi ya mgawano wa mamlaka katika mihimili ya dola itakayoondoa utaratibu wa hivi sasa wa mihimili hii kuingiliana katika utendaji wa wajukumu yake na itaondoa utaratibu usiofaa wa kuwapa watumishi wa mihimili hii kofia zaidi ya moja, matharani mbunge kuwa pia waziri au mkuu wa mkoa, jaji kuwa mwenyekiti wa Tume ya serikali, na kadhalika.
vi) Itaweka usawa wa kijinsia katika kutekeleza mfumo mpya wa uchaguzi.
vii)       Itatangaza rasmi utaifa wa Watanzania, kuweka vigezo vya uraia na kutaja wazi haki ya kila raia kupewa kitambulisho cha uraia.
viii)     Itaanzisha mahakama ya kudumu ya katiba itakayopokea na kusikiliza masharti ya kikatiba, raia binafsi au taasisi.
ix)         Italipa bunge nguvu ya kuwa chombo cha kutetea maslahi ya wananchi na kuwa na uamuzi wa mwisho katika utungaji wa sheria, uridhiaji ya mikataba na kuwa na mamlaka ya kupitisha au kukataa uteuzi wa viongozi muhimu wa dola.
x)           Itaainisha wizara na idadi ya kudumu ya wizara za Jamhuri ya Muungano.
xi)         Itapunguza baadhi ya madaraka ya rais kwa kuyaweka kwenye vyombo vingine vya maamuzi.
xii)       Italinda haki ya raia wa Jamhuri ya Muungano kumiliki ardhi na kulipwa fidia ya haki inayoendana na bei za soko ardhi inapochukuliwa na serikali kwa miradi ya umma.
xiii)     Itaweka muundo wa muungano wenye dola la shirikisho baina ya Tanganyika na Zanzibar.
xiv)     Itaainisha haki za binadamu kwa viwango vinavyokubalika kimataifa ikizingatia utu wa mwafrika na utamaduni wake.
xv)       Itaruhusu wagombea huru wa nafasi za uongozi (udiwani, ubunge, na urais).
xvi)     Itatambua sekta ya habari kama muhimili muhimu wa demokrasia yetu na kuliamuru Bunge litunge sheria ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari na haki ya raia kupata, kutumia na kutuma habari;
xvii)   Itaimarisha uhuru wa mahakama na kuamuru Bunge litunge sheria itakayorahisisha utoaji na upatikanaji wa haki kwenye vyombo vya maamuzi nchini;
xviii) Itahakikisha kuwa ardhi na maliasili vinaendelezwa, vinamilikiwa na vinawanufaisha Watanzania.

4.1.2 SHERIA ZINAZOSIMAMIA HAKI
Tunajua kuwa ipo hoja kuwa nchi yetu inaongozwa kwa katiba na sheria.  Lakini si kweli kwamba kila utawala unaofuata katiba na sheria ni utawala wa haki na wa kidemokrasia. Makaburu wa Afrika kusini waliendesha dola linalofuata ubaguzi wa rangi kwa kutumia katiba na sheria walizojitungia. Kwa kuwa tunayo katiba na sheria za nchi zinazopora haki na kuonea kama ilivyoelezwa kwenye ripoti za Tume ya hayati Jaji Mkuu Fransis Nyalali na Tume ya Jaji wa Rufani Robert Kisanga, kusisitiza kutawala kwa katiba na sheria hizi ni kuendeleza utawala usio wa haki wala wa kidemokrasia.

        Kutokana na mageuzi yatakayoletwa na katiba mpya ya nchi, chama cha NCCR-mageuzi kitasimamia mabadiliko ya sheria na mfumo wa utoaji haki nchini kama ifuatavyo:
(i)          Kufuta sheria zote za kikoloni (zinazoendelea kutumika nchini) na kutunga sheria mpya zinazolinda haki za binadamu na kuweka misingi mpya ya utoaji haki.
(ii)        Kufuta au kurekebisha sheria zinazokandamiza na kuonea wananchi, kwa mfano, Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985, sheria ya kuweka watu kizuizini, Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976, na nyinginezo.
(iii)      Kutafsiri sheria zilizopo, na zitakazotungwa kuwa katika lugha za Kiswahili.
(iv)       Kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya mahakama sambamba na Kiingereza.
(v)         Kurasimisha sheria bora za kimila.
(vi)       Kubadili mfumo wa serikali za mitaa ili kuimarisha madaraka ya umma na kuondoa rushwa na uonevu.
(vii)     Kuunda upya mfumo wa mahakama na kuweka mahakimu wenye taaluma ya kutosha ya sheria katika mahakama za mwanzo ili kulinda haki za raia vijijini, mitaani na kwenye kata.
(viii)   Kubadili utaratibu wa uteuzi wa majaji na mahakimu ili kudhibiti wale wasio waaminifu na wasio na weledi wa kutosha kutoteuliwa.

4.1.3 MUAFAKA WA KITAIFA

Ili kuleta maelewano, kudumisha amani, na kuleta utawala bora, chama cha NCCR-Mageuzi kitaanzisha mchakato wa kupata kwanza muafaka wa kitaifa. Muafaka wa kitaifa unajumuisha maridhiano kuhusu maadili ya kitaifa, na makubaliano katika mambo ya msingi yenye maslahi kwa taifa.  Aidha katika hoja hii wana NCCR-Mageuzi tunapendekeza taifa letu liwe na muafaka kuhusu misingi mikuu ya utaifa wetu.  Misingi hiyo itatokana na mambo ambayo yatakuwa yamekubaliwa na jamii bila kujali chama, dini, kabila, nasaba au jinsia.


Muafaka wa kitaifa utatusaidia kupanua wigo wa fikra zetu kuhusu maadili ya viongozi na ya wananchi. Hivi sasa mjadala kuhusu maadili ya taifa umejali tu suala la ufisadi, lakini hoja hii ni pana kuliko ufisadi. Lazima tuzungumzie malezi ya taifa, misingi na maadili ya malezi hayo, uzalendo wetu na masuala mengineyo.

Vilevile, muafaka wa kitaifa utatuwezesha kuondokana na mfumo wa utawala wa chama dola. Kwa sasa chama kilichopo madarakani ni chama dola kinachotawala kijeshi kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama tangia ngazi ya wilaya hadi taifa. Kwa mfano, bado wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama zinazojumuisha wakuu wa vyombo vya dola vya ulinzi na usalama kama vile Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Usalama wa Taifa na Jeshi la Mgambo. Wakuu haohao wa Mikoa na Wilaya ni makada wa chama tawala na wakuu wa kamati za siasa za chama tawala katika ngazi zao.

Mfano mwingine ulio hai ni jinsi Tume ya Uchaguzi ya Taifa ilivyofumbikwa na mfumo wa chama kimoja, hali ambayo inaifanya tume isiwe huru.  Licha ya kuwa wajumbe wa tume hii walio wengi ni wanachama wa chama cha kilichoko madarakani kwa sasa, watumishi wa tume ni watendaji wa Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI). Hawa wanawajibika kwa wakuu wao na wala si kwa Tume ya Uchaguzi. Muafaka wa kitaifa utatuletea Tume huru ya Uchaguzi.

Hatuna budi kuafikiana (kuwa na muafaka) kwamba licha ya tofauti zetu za kiitikadi yapo musuada ambayo chama chochote kitakachoshika madaraka lazima kiyaheshimu maana hayo ni yetu sote kama taifa.

4.1.4 KUTOKOMEZA UFISADI NA RUSHWA

Tangia mwaka 1995, maudhui ya ilani za uchanguzi za NCCR-Mageuzi kila mara yameelezea kuwa Rushwa ni balaa na tishio kubwa kwa taifa letu. Kwa Sasa hali ni mbaya zaidi, tunakabiliwa na janga la Ufisadi!

Ufisadi kwa tafsiri yetu, ni uozo na uvundo wa dola na utawala wa nchi. Uozo huu unaambatana na Rushwa inayoliguguna taifa na kuliangamiza. Dola limegeuka na kuwa la kifisadi kwa kuwa taratibu zake za kiutendaji, sera na kanuni zake zinajenga ufisadi. Watendaji wa serikali na watumishi kadhaa wamegeuka mafisadi, kwa kuwa upofu unaoandamana na rushwa umewaondolea uwezo wao wa kuona, kufikiri au kutenda mambo yasiyo ya kifisadi.

Hivi sasa Tanzania imekuwa Taifa lenye sifa chafu ya rushwa na ufisadi uliokithiri. Chama cha NCCR-mageuzi kinatangaza rasmi kuwa rushwa na ufisadi ni adui wa nne wa taifa. Hivyo tuzungumzie sasa maadui wanne, na si watatu tena kama tulivyobaini hapo zamani.
Rushwa ni utoaji na upokeaji wa hongo au mlungula ili kuishinda haki. Rushwa imezidi kushamiri miongoni mwa watendaji wakuu wa dola katika utoaji wa huduma ya uongozi na utumishi kwa umma.

Chama cha NCCR – Mageuzi kimedhamiria kutokomeza ufisadi na rushwa kwa kutekeleza mkakati ufuatao:-

1)          Kutengeneza vyombo vyenye nguvu kubwa na mtandao ulioenea hadi kona zote za nchi, vyombo vyenye meno makali ya kutokomeza ulaji rushwa.
2)          Kuunda dola kwa kuzingatia weledi, uwezo kitaaluma na maadili ya uongozi kwa watendaji na viongozi wa umma.
3)          Kuvipa uhuru mkubwa vyombo vya habari ili viandike bila hofu ufisadi vitakaoubaini katika taasisi yoyote nchini. Vyombo hivi na waandishi wake watapewa ulinzi wa kisheria
4)          Kulinda haki ya kila raia kupata na kutoa habari ili kwa kufanya hivyo uwezekano wa kuficha siri za kifisadi uondolewa, na kuhakikisha kwamba serikali inatoa taarifa za uendeshaji wa shughuli za umma kwa vyombo vya habari na asasi za kijamii zinazolinda na kutetea haki.
5)          Kuelimisha, kulea na kufunda watumishi na viongozi katika misingi ya uadilifu na uongozi bora. Hili litaendana na kujenga taifa adilifu kwa njia ya elimu kwa watanzania tangia wakiwa na umri mdogo na kuwakuza katika maadili hayo
6)          Kurahisisha mfumo wa ulipaji kodi na kupunguza kiwango cha kodi ili kuwahamasisha wananchi kulipa kodi, ili waondokane na kishawishi cha kutoa rushwa badala ya kodi.
7)          Kufuta umangimeza, kurahisisha taratibu za utoaji wa haki na huduma kwa umma kutoka taasisi za serikali.
8)          Kuwafikisha mara moja mbele ya sheria watuhumiwa wote wa vitendo vya kifisadi.
9)          Kuandaa mswada wa sheria itakayotoa adhabu kali zaidi kwa walaji na watoa rushwa.
10)      Kufuta mara moja mikataba yote iliyosainiwa katika mazingira ya kifisadi.
11)      Kutengeneza utaratibu wa kusaini mikataba ya serikali utakaokuwa wazi kabisa mbele ya umma wa watanzania.


4.2 AJENDA KATIKA SEKTA ZA KIUCHUMI

4.2.1 Uchumi, Uwezeshaji na Ajira
Mabadiliko ya masuala ya kiutawala tuliyoyaeleza yanalipa taifa fursa na uwezo wa kutekeleza mageuzi ya kujikomboa kiuchumi.  Tunapozungumzia uchumi tunamaanisha jumla ya shughuli zote za kuzalisha mali na utoaji wa huduma mbalimbali katika jamii, maadam vyote vina thamani inayoweza kupimwa kwa fedha.  Matokeo ya shughuli za kiuchumi ni upatikanaji wa mahitaji ya wanadamu katika jamii husika.  Katika kila jamii mgawanyo wa mafao au mahitaji huzaa matabaka ya walionacho na wasionacho.  Kipimo cha maendeleo ya jamii yoyote ile ni uwezo wake wa kukidhi mahitaji ya lazima ya wanajamii walio wengi katika jamii husika.

Tanzania ni taifa tajiri kirasilimali lakini masikini kimaendeleo kwa sababu asilimia kubwa ya wananchi wake ni mafukara wanaoishi kwa kipato cha chini ya shilingi mia tano kwa siku.  Asilimia 44 ya Watanzania wana uwezo wa kujipatia mlo mmoja kwa siku na asilimia ndogo zaidi ndio wenye uwezo wa kupata milo mitatu kwa siku.

Tunayo makundi mawili makubwa ya umma wa Tanzania.  Kundi la wafanyakazi ni la pili kwa ukubwa kufuatia kundi la wakulima na wafugaji.  Makundi haya yameathiriwa sana na uchumi duni tulionao.  Utafiti wa nguvukazi uliofanyika hapa nchini katika ya mwaka ya hivi karibuni unaonyesha kuwa katika sekta ya ajira kati ya watu milioni 17, 800,000 wenye uwezo wa kufanyakazi nchini, watu 2,300,000 hawana kazi na asilimia kubwa kati yao ni vijana wenye rika kati ya miaka 18  hadi 34.
Utafiti huo unaonyesha pia kuwa jumla ya vijana 650,000 hadi 750,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka.  Kati yao 84% hujiariji wenyewe katika sekta ya kilimo, 6% katika sekta isiyo rasmi, 4% katika sekta rasmi binafsi, 3.5% katika kazi za nyumbani, 2% serikalini na 0.5% katika mashirika ya umma.  Kwa ujumla ukuaji wa ajira viwandani na kwenye sekta ya huduma ni mdogo sana. 
Ili kuleta Mageuzi ya kiuchumi nchini, serikali itakayoongozwa na chama cha NCCR – Mageuzi itafanya mambo yafuatayo:

(a)  Kuinua Uchumi
1)   Itakuwa na mkakati wa makusudi wa kuimarisha shilingi ya Tanzania

2)   Itahakikisha kwamba mauzo ya bidhaa nchi za nje yanaongezeka sana, ilihali manunuzi ya bidhaa kutoka nje yanadhibitiwa na kuondoa yale yasiyokuwa ya lazima

3)   Itaongeza thamani ya rasilimaliwatu (raia wa Tanzania) kwa kuwapatia maarifa na ujuzi mkubwa

4)  Itajenga mfumo wa ubunifu (innovation) utakaoambatana na kuinua shughuli za utafiti nchini ili kuibua maarifa yenye manufaa kwa sekta mbalimbali. Yaani, maarifa ya kitaalam yawasaidie moja kwa moja watendaji katika sekta za kiuchumi na wananchi wa kawaida.

5)  Itafanya tathmini ya kina ya utajiri wa rasilimali tulizonazo na kuziwekea mkakati endelevu wa kuzitumia ili kuinua uchumi wa nchi.


(b)  Kuwezesha wananchi 

1)     Itawezesha kimtaji wahitimu kutoka vyuoni/mashuleni pamoja na wananchi kwa ujumla kuanzisha miradi mbalimbali ya uchumi ndani na nje ya nchi.

2)     Itawahamasisha wananchi kujiamini, kutambua na kutumia uwezo wao wa kufanya kazi na kukabili changamoto ya sayansi, teknolojia na utandawazi.

3)     Itawawezesha wananchi kushiriki katika soko la dunia kwa kutoa vivutio, vishawishi na motisha mbalimbali kwa washiriki wa soko la nje.
       
4)          Itatetea vyema maslahi ya taifa katika mazungumzo ya kuweka kanuni na mikataba ya kibiashara na uchumi kwenye soko la pamoja la Afrika mashariki na kwenye medani za kimataifa.

5)          Itaweka sheria itakayoiamuru serikali kutoa zabuni za ununuzi wa mahitaji yake kwa wananchi au kampuni ambazo asilimia isiyopungua 60 ya hisa zake zinamilikiwa na wananchi.

(c)  Ajira/ Wafanyakazi

1)  Itahakikisha kuwa viwango vya mishahara nchini vinawiana na gharama za maisha.

2)  Itaandika upya sheria za kazi nchini ili kulinda haki za wafanyakazi na haki ya kufanya kazi.  Sheria hii itaiwajibisha serikali kudhibiti na kulinda ajira ya wafanyakazi kwa kuanzisha taasisi za mafunzo ya uhaulishaji wa ajira na utafiti wa ajira mbadala pale ustaafishaji wa lazima unapotokea.

3)  Itaandika upya sheria ya vyama vya wafanyakazi ili kuvipa vyama hivyo uhuru zaidi wa kulinda na kutetea maslahi ya wafanyakazi, kupanua ushiriki wake katika uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

4)   Itaongeza pensheni ya wastaafu ili wastaafu wapate kiwango cha 80% ya mishahara yao na pia kuhakikisha kuwa serikali inachangia mifuko hiyo badala ya kuitumia tu kama chanzo cha mikopo kwa miradi ya serikali.

5)  Itahakikisha kuwa wastaafu wanalipwa pensheni zao mara tu wanapostaafu. Hii ni pamoja na kuwarejesha katika malipo ya pensheni wanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii wa mashirika ya umma walioondolewa baada ya marekebisho ya sheria ya mfuko huo.

6)  Itatoa kipaumbele kwa wataalamu na wastaafu wenyeji badala ya wageni katika kazi za mikataba na huduma za ushauri.

7)  Itaruhusu, itahalalisha na kuzijengea mazingira mazuri shughuli zote ambazo wananchi watazibuni kwa ajili ya kujipatia riziki.

4.2.2 Mageuzi ya Kilimo, Ufugaji, Chakula na Ushirika

Kwa kuwa ukulima na ufugaji ni shughuli zinazoajiri takribani asilimia 87 ya nguvukazi ya taifa na kwa kuwa asilimia 44 ya pato la taifa inatokana na sekta hii, ni lazima wanamageuzi tulenge kuendeleza kilimo na ufugaji viwe vya kisasa kabisa ili maisha ya mkulima yawe ya hali ya juu na uchumi wetu upate kuimarika.  Hivi sasa sekta hii imebakia nyuma kitekinolojia na uwezeshwaji wa wananchi wanaoshiriki katika uzalishaji mali katika sekta hii ni mdogo mno.

Wakulima walio wengi hutegemea jembe la mkono na mvua.  Wafugaji huchunga mifugo yao badala ya kufuga kwa kutumia mbinu za kisasa zenye tija kubwa zaidi.  Ili kukabiliana na hali hii isiyoridhisha, serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya yafuatayo:

1)          Itawezesha nchi kupata zana bora za kilimo kwa kuwekeza kwenye machimbo ya chuma ya Liganga na machimbo ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na kiwanda cha kuyeyusha chuma ili viibuke viwanda vya uhandisi vinavyozalisha mashine na mitambo ya uzalishaji wa bidhaa za kilimo na chakula kwa ajili ya soko la ndani na nje.

2)          Itawezesha wananchi kujasiriamali katika sekta hii ili waanzishe miradi mbalimbali ya kuzalisha bidhaa za kilimo na mifugo pamoja na viwanda vya kusindika bidhaa zilizo tayari kwa matumizi ya binadamu kwa ajili ya soko la ndani na nje.

3)          Itatengeneza mpango imara na endelevu wa huduma za ughani katika kilimo na mifugo.

4)          Itafufua na kupanua vyuo vya kilimo na utafiti kuhusu mbinu za kilimo, ardhi, mbegu bora na udhibiti wa maradhi ya mifugo na mimea.

5)          Itaanzisha masoko yenye hadhi na mvuto wa kimataifa katika miji ya mipakani ili kuimarisha biashara na nchi jirani.

6)          Itafuta kodi kwa wakulima na wafugaji kufidia gharama za pembejeo, madawa na pia itafuta kodi ya mazao ya kilimo na mifugo.

7)          Itatunga upya sheria ya ushirika ili kutoa uhuru kamili kwa vyama vya ushirika kuendesha shughuli zake na kuwezesha vyama hivyo kujasiriamali katika mifuko ya hifadhi ya jamii ya wakulima na wafugaji.

8)          Itaanzisha taasisi za bima na usalama wa kipato cha mkulima na mfugaji hasa kwenye matukio ya ukame, mafuriko, maradhi ya mifugo, na matukio ya nzige na viwavi jeshi.

4.2.3 Maliasili, Maji na Nishati
Tanzania inao utajiri mkubwa wa rasilimali kama vile ardhi, maziwa, mito, wanyamapori, ndege, milima, misitu na madini ya aina mbalimbali.  Baadhi ya rasilimali  kama vile Mlima Kilimanjaro ambao ni wa pili kwa urefu duniani na Ziwa Tanganyika ambalo ni la pili kwa kuwa na kina kirefu duniani, madini ya tanzanite na vyura wa kihansi ambavyo havipatikani popote duniani isipokuwa Tanzania.

Umaskini wa Tanzania unatokana na ukweli kuwa kwa miaka 49 tangu tupate uhuru rasilimali hizi zimekuwa zikitumika vibaya.  Chama cha NCCR-Mageuzi kinataka sasa kuleta Mageuzi makubwa katika namna/jinsi tunavyodhibiti na kutumia rasilimali za taifa.  Tunatangaza wazi kuwa maliasili zote hizi ni urithi na mali ya Watanzania na hivyo si halali wageni kupewa haki ya kuvuna au kutumia rasilimali hizi kwa manufaa yao huku Watanzania wakiendelea kubaki katika ufukara.

Kwa hiyo basi, serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya yafuatayo:

1)          Itaandika upya sheria ya madini ili kuhakikisha kwamba madini na rasilimali nyingine za asili ni mali ya taifa na hivyo kutomilikishwa kwa mtu binafsi.  Haki ya kutumia au kuvuna rasilimali za asili itakuwa ni kwa raia na serikali yao na ushiriki wa wageni utakuwa kwa mikataba ya ukandarasi.

2)          Itatoa kipaumbele katika kuwawezesha wananchi kujasiriamali katika sekta ya maliasili, maji na nishati na kutenga sekta hii kwa uwekezaji wa wananchi kutokana na unyeti wa sekta yenyewe kwa uchumi wa taifa.

3)          Itaweka utaratibu wa kuwawezesha wananchi kunufaika kutokana na madini na maliasili zinginezo zilizopo katika maeneo yao na hasa kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye rasilimali za asili wanapata pato la kutosha kutokana na uvunaji wa rasilimali zilizo kwenye eneo lao. Fidia ya mazao na vifo vinavyo sababishwa na rasilimali zenyewe kama vile wanyamapori au uchafuzi wa mazingira wakati wa machimbo ya madini lazima ipewe uwiano wa bei ya soko.

4)          Itahakikisha kuwa uvunaji wa maji ya mito, mvua na maziwa unafanywa kwa makini kulingana na tekinolojia ya kisasa ili kutosheleza mahitaji ya kilimo, viwanda, wanyama na binadamu.

5)          Itabadili miundombinu ya uzalishaji wa nishati kutoka vyanzo mbalimbali ili kuwa na nishati nafuu kwa matumizi ya nyumbani na kwenye shughuli za uzalishaji mali, vyanzo hivyo ni pamoja na nguvu za jua, maji, upepo, gesi asilia, na makaa ya mawe

4.2.4 Utamaduni na Utalii

Kwa mujibu wa sera za NCCR – Mageuzi utamaduni na utalii ni sekta muhimu katika kukuza ajira na pato la taifa.  Serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya yafuatayo kuendeleza sekta ya utalii:

(a) Utamaduni
1)          Itatunga sheria ya kulinda na kuendeleza utamaduni wa taifa ikiwa ni pamoja na kukamilisha ubunifu juu ya vazi la kitaifa lenye heshima.
2)          Itakipa kiswahili hadhi inayostahili kama lugha rasmi ya taifa na kuunda taasisi ya kuendeleza kiswahili na utamaduni wetu ndani na nje ya nchi.

3)          Itawezesha na kuimarisha miradi ya raia ya kuendeleza fani zinazoelezea utamaduni kama vile muziki, michezo, ngoma, filamu, uchoraji, ufinyanzi, uchongaji na sanaa nyinginezo. Hii ni pamoja na kuwawezesha wasanii na kulinda haki ya kazi zao.

4)          Itaanzisha vyuo vya kuendeleza utamaduni wa taifa na fani zinazoelezea utamaduni wa taifa

5)          Itaanzisha programu maalumu ya kuwezesha vijana wenye vipaji katika kila fani zinazoelezea utamaduni wa taifa, ili kukuza ajira kwa vijana, uzalishaji wa bidhaa za utamaduni na kuinua pato la taifa.

6)          Itaimarisha ushirikiano kati ya serikali za mitaa, taasisi za kidini na jamii katika kujenga maadili na utamaduni wa taifa.

7)          Itajenga miundombinu ya michezo, ili kuiwezesha sekta hii kuajiri vijana wanamichezo ndani na nje ya nchi.  Kwa jinsi hii Tanzania itajiunga katika orodha ya mataifa mashuhuri katika medani ya michezo duniani na itajiongezea pato la taifa.

  (b) Utalii

1)   Itahifadhi katika hali ya kudumu na ya kuvutia watalii rasilimali za utamaduni kama vile sehemu zenye mambo ya kale yaani majengo, vifaa vya kutenda kazi, kumbukumbu za mashujaa na viongozi wakuu wote wa zamani (watemi), na sehemu za nchi zenye uasili wa kuvutia.

2)   Itajenga vyuo vya kutoa elimu inayohusiana na utamaduni na utalii na pia kuviwezesha vyuo vikuu vilivyopo kuanzisha vitivo vyenye kutoa elimu kuhusu utamaduni, utawala wa hoteli na huduma za utalii.

3)   Itawezesha wananchi kuwekeza katika ujenzi wa mahoteli, nyumba za kufikia wageni na utoaji wa huduma (mf. Usafirishaji na uongozaji) kwa watalii.

4)   Itahamasisha na kuwezesha huduma za utangazaji wa biashara na sekta ya utalii nje ya nchi ili kuwafikia na kuwavutia watalii kuitembelea Tanzania.

5)   Itatunga sheria inayoweka masharti ya kudhibiti uuzaji holela wanyama pori kwa nchi za nje, ndege na mimea ya asili isipokuwa kwa matumizi ya utafiti wa kisayansi.

6)   Itawekeza katika miundombinu na maendeleo ya mbuga za hifadhi ya wanyama pori, ndege na mimea ya asili.

4.2.5 Viwanda na Biashara
Sera za NCCR – Mageuzi kuhusu viwanda zinalenga kuliondoa taifa kwenye utegemezi wa bidhaa zilizosindikwa au kutengenezwa viwandani kwa matumizi ya binadamu kutoka nje.  Serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya mambo yafuatayo katika sekta ya viwanda na biashara:-

1)     Itawahamasisha wananchi na kuwawezesha kujasiriamali katika sekta hii kwa kubuni na kujenga viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya binadamu.  Wajibu wa serikali ni kuhakikisha kuwa mtaji unapatikana na wananchi wanakopeshwa mtaji huo kwa riba nafuu na masharti rahisi.
  
2)     Itahakikisha kuwa kunakuwa na uwiano bora kati ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, na kuwa ujenzi wa viwanda unazingatia misingi ya kuhifadhi na kulinda mazingira.

3)     Itahakikisha kuwa viwanda vinavyojengwa ni vya kisasa kitekinolojia ili bidhaa zetu ziwe na ushindani kwa ubora na bei nafuu kwenye soko la pamoja la Afrika Mashariki, Jumuiya ya Uchumi ya SADC, bara la Afrika na duniani kwa ujumla.

4)     Itaimarisha vyama huru vya wenye viwanda na wafanyabiashara ili kuvipa uwezo wa kutoa huduma za ushauri kwa wanachama wao kuweza kupata wabia na soko la bidhaa nje ya nchi.

5)     Itaanzisha bandari huru, bandari ya Tanga kwa ajili ya soko la Afrika Mashariki, Bandari ya Mtwara kwa ajili ya soko la Kusini mwa Afrika na Bandari ya Dar Es Salaam na Zanzibar kwa ajili ya soko la dunia.

6)     Itatenga maeneo maalumu katika mipaka ya nchi yetu kwa ajili ya kujenga masoko ya kimataifa ili kuchochea biashara baina ya nchi yetu na nchi za jirani.

4.2.6 Mawasiliano na Uchukuzi
Sekta ya mawasiliano na uchukuzi ni uhai wa uchumi wa taifa inayoweza kulinganishwa na mishipa ya fahamu katika mwili wa binadamu.  Serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itaendeleza sekta hii kwa kufanya mambo yafuatayo:
       
1)          Itajenga barabara kwa kiwango cha lami ili kuhakikisha kuwa kila makao ya halmashauri yanafikika kwa barabara ya lami.

2)          Itajenga mfumo mpya wa usafiri wa barabara na reli katika miji mikubwa ikianzia Dar Es Salaam ili kuondoa kero ya msongamano wa magari, uhaba wa usafiri na ajali zinazosababishwa na barabara mbovu na nyembamba.

3)          Itaanza ujenzi wa mfumo mpya wa reli za umeme nchini

4)          Itahamasisha na kuwawezesha wananchi kujasiriamali katika sekta hii hasa kuanzisha viwanda vya bidhaa za mawasiliano na makampuni ya kutoa huduma ya mawasiliano kwa elektroniki badala ya kuiacha sekta hii imilikiwe na makampuni ya kigeni peke yake.

5)          Itahamasisha na kuwawezesha wananchi kumiliki na kuendesha vyombo vya usafiri wa anga na baharini.
4.2.7 Uhalalishaji wa Mali za Watu Binafsi

Kutokana na historia isiyopendeza ya serikali kutaifisha mali binafsi kwa jazba badala ya kuongozwa na sera makini na kisha kubinafsisha holela mali ya umma bila sera makini, serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itakabiliana na athari zilizotokana na matukio hayo na kurejesha imani ya wananchi katika serikali yao kwa  kufanya mambo yafuatayo:

1)          Itaweka masharti kwenye katiba ya nchi ili kuzuia utaifishaji wa mali ya watu binafsi.

2)          Itatunga sheria inayoiwajibisha serikali kulipa fidia inayokidhi thamani ya mali iliyotaifishwa bila ucheleweshaji wa malipo na pia kuwalipa fidia wenye mali iliyotaifishwa bila kulipwa fidia.

3)          Itaanzisha mjadala kuhusu ubinafsishaji wa nyumba za serikali ili kuangalia upya uhalali wa tendo hilo.

4)          Itafuta sheria iliyopo inayoipa serikali mamlaka ya kuchukua ardhi ya wananchi bila kushauriana nao na kutunga sheria mpya inayoweka masharti ya kuiwajibisha serikali kushauriana na wananchi kabla ya kuchukua ardhi, kufanya uthamini wa ardhi inayochukuliwa na serikali kwa bei ya soko, kulipa fidia na kuhakikisha kuwa wananchi husika wamepata makazi mbadala kabla ya bomoa bomoa kufanywa.

4.2.8 Uwekezaji wa Kigeni
Wawekezaji wa kigeni ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi wa nchi.  Hata hivyo siyo sera nzuri kwa taifa kuruhusu uwekezaji holela hadi kuwaruhusu wageni kuwekeza katika kuuza mishikaki na chipsi.  Hali kama hiyo huzua hisia za chuki miongoni mwa wananchi ambao wanaona kama uchumi wa nchi yao umeuzwa kwa wageni.  Ili kuondoa chuki dhidi ya wawekezaji wa kigeni na kuweka mazingira ya amani, maelewano ni utulivu, serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya mambo yafuatayo:

1)          Itaainisha na kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya wageni na kuhakikisha kuwa wageni hawawekezi katika sekta zilizotengwa kwa ajili ya wananchi.

2)          Itaweka masharti na kudhibiti ubora wa uwekezaji wa wageni nchini ili kukinga taifa lisivamiwe na matapeli, wezi na majangili waliojificha kwenye ngozi ya uwekezaji.

3)          Itaweka masharti ya uwekezaji yanayohakikisha kuwa wawekezaji wageni wanakuza ajira, uzoefu na tekinolojia kwa wananchi na pia wanabakiza kiasi cha kuridhisha cha pato nchini kwa kuwekeza upya faida yao katika miradi mingine mipya.

4)          Itawashawishi wawekezaji wa kigeni waliopo chini kuingia ubia na Watanzania kwa manufaa yao na ya Watanzania.

5)          Itawawezesha wananchi wajasiriamali kuingia ubia na wawekezaji wa kigeni.


4.3 HUDUMA ZA JAMII

4.3.1 ELIMU NA MALEZI YA TAIFA
Uhai wa taifa lolote hutegemea sana misingi ya kielimu na kimaadili inayowaunganisha wananchi wake kuwa taifa moja lenye utamaduni mmoja.  Ili kumjenga Mtanzania kiroho na kiakili, ili tuwe na mafanikio ya kiuchumi na kisiasa, na ili tuwe na taifa lenye utamaduni mmoja, hatuna budi kuwa na mfumo wa elimu na malezi ya taifa wenye maudhui na vionjo vya Kitanzania.

Lazima pia tuwe na mfumo wa elimu na malezi ya taifa utakaotupatia Mtanzania wa aina mpya mwenyewe taaluma ya kisasa ya kufanya kazi na kukabiliana na utandawazi wakati huo huo akiwa binadamu mwenye uadilifu, nidhamu, utaifa na moyo wa kujiamini na kuthubutu. 
Elimu yetu lazima imjenge Mtanzania anayejiamini na mwenye kuweka mbele utaifa wake.  Mtanzania wa aina hii atakuwa mshiriki mkamilifu na mshindani mzuri katika uchumi wa taifa na soko la dunia kwa ujumla.

Elimu hii isitujengee mlarushwa, goigoi, tapeli na msaliti wa maslahi ya Watanzania. Vijana wetu wamalizapo elimu ya msingi lazima wawe wamekamilika siyo tu katika elimu ya kinadharia bali pia kwa stadi za maisha ili waweze kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe na au kuajirika (watimizapo umri).  Haya ni mageuzi makubwa ya kielimu yatakayoliondoa taifa kwenye misingi ya elimu iliyowekwa na utawala wa kikoloni kwa manufaa ya ukoloni, na kuliingiza taifa katika mfumo mpya wa elimu inayolenga kuzikomboa fikra ili kutufanya kuwa binadamu huru waliokamilika.

Ili kufanikisha mageuzi hayo, serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya mambo yafuatayo:

(a) Maudhui ya Elimu
1)     Itabadili mitaala ya elimu kwa kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu ili kuipa ubora wa hali ya juu na maudhui na vionjo vya Kitanzania.

2)     Itahakikisha kwamba mitaala yote nchini ni ile tu yenye manufaa na maana katika maisha halisi ya mtu mmoja mmoja.

3)    Itaanzisha mpango kabambe wa elimu ya uraia na elimu ya maisha kwa jamii, mahali pa kazi na katika makazi ya watu.

(b) Mfumo wa Elimu

1)     Itahakikisha mfumo wa elimu ya awali (chekechea) unaenea nchi nzima katika maeneo ya makazi, maeneo ya kazi na kwenye kila shule ya msingi ili kuwa na malezi makini kwa watoto na kuwapa fursa wanawake wazazi kushiriki katika shughuli za kila siku za uzalishaji mali.

2)     Itaanzisha mfumo mpya wa elimu ya msingi yenye masomo ya stadi za maisha itakayoishia kidato cha nne ambayo itatolewa bure (bila malipo ya ada) kwa watoto wote wa Kitanzania.
       
3)     Itaanzisha elimu ya sekondari itakayochukua miaka miwili ya kidato cha tano na sita kuandaa vijana kuingia vyuo vikuu.  Elimu hii itatolewa kwa lugha ya Kiswahili sambamba na masomo ya lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa kuwa ya lazima.
       
4)     Itaanzisha vyuo vya ufundi na mafunzo kwa vitendo kwa wali ambao hawakuchaguliwa kwenda kidato cha tano na sita ili kuwaandaa kwa ajira na pia kujiunga na vyuo vya elimu ya juu vya ufundi na teknolojia.

5)     Itapanua elimu ya vyuo vikuu kwa kuanzisha vyuo vikuu vipya visivyopungua vitatu katika miaka mitano ijayo ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kuupatia kila mkoa angalau chuo kikuu kimoja.

6)          Itapanua vyuo vikuu vilivyopo na kuboresha viwango vya taaluma, mazingira ya kusoma kwa wanafunzi na mazingira ya kazi kwa wahadhiri.

7)          Itaboresha mishahara, marupurupu na pensheni za walimu wa shule za msingi, sekondari, wakufunzi wa vyuo na wahadhiri wa vyuo vikuu iwiane na gharama halisi za maisha na viwango vya taaluma zao.

8)          Itaanzisha vyuo vipya vya waalimu kulingana na mahitaji ya waalimu wa fani mbalimbali za elimu, ufundi na tekinolojia.

9)          Itapanua vyuo vya walimu vilivyopo na kuboresha elimu inayotolewa kulingana na mahitaji mapya ya mfumo mpya wa elimu utakaoanzishwa.

(c)  Sera ya Elimu

1)          Itabadili sera ya elimu ya taifa kwa kuipa maudhui, na upeo kulingana na mahitaji ya kimaadili na kimaendeleo ya taifa.

2)          Itaweka asilimia 30 kuwa kiwango cha chini cha bajeti ya taifa kila mwaka kwa ajili ya elimu.

3)          Itaanzisha utaratibu wa shule za bweni za wasichana ili kuwawezesha wasichana wengine kusoma pasipo kusumbuliwa na shughuli za nyumbani ambazo zimekuwa zikiathiri vibaya maendeleo yao ya kitaaluma.

4)          Itaweka uwiano mzuri kati ya wanafunzi wa kiume na wa kike wanaojiunga na masomo vyuoni na kuzipa nafasi katika mitaala hoja za jinsia, uraia, haki za binadamu na utaifa.

5)          Itaanzisha chuo cha taifa cha kufundisha viongozi kutoka sekta mbalimbali za jamii nchini ili kuipa nchi yetu mwelekeo maalum wa kudumu wa utamaduni wa kisiasa na demokrasia huru na maadili ya taifa.

6)          Itaondoa kodi kwenye vifaa vya elimu na kuzipa ruzuku taasisi binafsi zinazoshiriki kutoa elimu rasmi ili kuziongezea uwezo wa kutoa huduma ya elimu kwa jamii inayofanana na ile ya taasisi za serikali.

7)          Itahamasisha, itawezesha na kutoa vivutio na motisha kwa watafiti na wanasayansi na pia kutunza na kulinda uvumbuzi wao.

4.3.2 AFYA NA MAZINGIRA
Afya ya binadamu hubebwa na mazingira anamoishi.  Watanzania tumo katika matatizo makubwa sana kiafya, jambo ambalo linathibitishwa na magonjwa mengi ya mlipuko na kushindikana kufutika kwa magonjwa kama kipindupindu na homa za matumbo ambayo yanaashiria mazingira machafu.  Mazingira machafu ni chanzo kikubwa cha maradhi nchini.

Huduma za tiba zimeporomoka mno kiasi kwamba hospitali zinazoaminika sasa ni zile zinazoendeshwa na sekta binafsi.  Hali hii ni hatari kwa kuwa huduma za hospitali binafsi hazipatikani vijijini isipokuwa pale ambapo zipo zahanati za mashirika ya kidini.

Mijini pia hali si nzuri na wakubwa serikalini hujitibia nje kwa fedha za kodi ya wananchi.  Gharama za dawa ni kubwa mno hata kwa dozi ya kawaida ya malaria.  Hivyo tumefikishwa pabaya na kifo kinatukodolea macho kila mara tunapojihisi ni wagonjwa.

Ili kuweza kupambana na maradhi na kuwa na jamii yenye afya njema serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya mambo yafuatayo:

(a) Afya

1)          Itaanzisha programu za kudumu za kudhibiti vyanzo vyote vya magonjwa nchini, na kuzuia maambukizi. Mpango huu utajumuisha elimu ya afya kwa watu wote, na uangamizaji wa mazalia ya wadudu wanaoeneza maradhi.

2)          Itaanzisha mfumo wa tiba utakaohakikisha kuwa huduma ya afya ya msingi hutolewa kwa raia wote.

3)          Itaimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto ili kuhakikisha uzazi salama na kujenga taifa lenye watu wenye afya bora na maisha marefu.

4)          Itaanzisha mpango shirikishi na endelevu wa kuthibiti kasi ya maambukizi ya Ukimwi, kuboresha huduma kwa waathirika ili kuzipunguzia mzigo familia za wagonjwa, kuwezesha ununuzi na utengenezaji wa dawa za kurefusha maisha kwa waathirika na kuwezesha utafiti wa tiba ya UKIMWI.
5)          Itawezesha sekta ya tiba za jadi kwenda na wakati uliopo na kuchangia zaidi ya ilivyo sasa katika huduma ya kuzuia na kutibu maradhi nchini.

6)          Itazipa ruzuku taasisi binafsi zinazoshiriki katika utoaji wa huduma ya tiba ili kuziongezea uwezo wa kutoa huduma ya tiba kwa jamii na kuondoa ushuru kwa vifaa vya hospitali.

7)          Itawawezesha madaktari na watafiti wananchi katika sekta ya afya kuwekeza kwa kuanzisha hospitali za kisasa zenye uwezo wa kutibia maradhi yote ikiwa ni pamoja na yale nadra kupatikana.

8)          Itawahamasisha na kuwawezesha wafamasia wananchi na wawekezaji wengine wananchi kuanzisha viwanda vya utengenezaji wa dawa za binadamu na vifaa vya hospitali.

(b) Mazingira na Makazi
Kwa kuwa ni haki ya binadamu na msingi mkuu wa afya ya binadamu kuishi katika mazingira safi na salama, serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itafanya mambo yafuatayo kuhusiana na suala la mazingira:
       
1)          Itatunga sheria ya makaazi inayotenganisha makazi ya binadamu na viwanda.  Sheria hiyo itaweka masharti yanayopiga marufuku ujenzi wa viwanda vinavyochafua mazingira au kuhatarisha afya za binadamu na itazuia pia utengenezaji wa bidhaa zinazochafua mazingira kama vile mifuko ya plastiki.  Sheria hii itadhibitiwa utupaji hovyo wa taka na kuweka kanuni za usafi mijini na vijijini.

2)          Itatunga sheria ya vyakula, madawa na usafi wa mazingira ambayo itazuia uingizaji nchini bidhaa zisizofikia viwango vinavyokubalika kitaalamu na kisheria nchini.

3)          Itaweka wazi kwa wananchi, ramani za mipango miji ili watambue ni wapi wajenge na wapi hawapaswi kufanya hivyo. Hii itaambatana na kukomesha kabisa ujenzi holela.

4)          Itashawishi vyombo vya fedha, taasisi za serikali na za binafsi kuwekeza katika ujenzi wa makazi bora ya watu (ujenzi wa nyumba bora na nafuu).



4.3.3 Ulinzi na Usalama
Wanamageuzi tunatambua kwamba mojawapo ya mahitaji muhimu ya mwanadamu ni usalama wa nafsi yake, jamaa zake na mali zake. Katika taifa letu kwa sasa usalama huu si wa hakika sana. Bado tunashuhudia uwepo wa tishio la vitendo vya ujambazi, unyang’anyi, ubakaji, mauaji ya watu wasio na hatia, na maovu mengineyo.
Ili kuwahakikishia wananchi usalama, serikali ya NCCR-Mageuzi, pamoja na mambo mengine itafanya yafuatayo.

1)  Itahakikisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinapatiwa zana za kisasa kabisa ili viweze kumudu kudhibiti vilivyo uhalifu.

2)  Itaweka utaratibu wa kudumu wa kuwapatia askari wetu mafunzo kazini ya mbinu bora zaidi, na kuhakikisha kuwa wamejengeka na kuwa waadilifu wa hali ya juu.

3)  Itaweka vituo vya ulinzi karibu sana na wananchi, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinapatiwa vituo vya ulinzi na usalama.


4.4 MAKUNDI MAALUMU
Kila taifa lina walemavu na wanajamii wengi ambao wanahitaji uwezeshwaji wa ziada.  Serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itatekeleza sera zifuatazo kuhusu makundi haya maalumu:

(a)    Walemavu
1)     Itatoa nafasi maalumu katika mabaraza ya uwakilishi kwa ajili ya walemavu

2)     Itatunga sheria za kusimamia maslahi ya walemavu katika huduma za umma na kuwawezesha kufanya shughuli za kujipatia kipato.

(b)    Yatima na watoto walio katika mazingira magumu
1)                          Itakabiliana na chimbuko la watoto yatima na watoto walio katika mazingira magumu

2)                          Itatoa ruzuku kwa asasi zisizo za kiserikali zinazohudumia watoto yatima na watoto walio katika mazingira magumu.

( c)    Makabila yaliyo katika hatari ya kutoweka
Itashirikiana na asasi zisizo za kiserikali kuainisha na kukabiliana na hali inayotishia uwepo wa makabila hayo.


4.5   VYOMBO VYA HABARI NA ASASI ZISIZO ZA
        KISERIKALI
Sera za NCCR – Mageuzi kuhusu vyombo vya habari na taasisi zisizo za kiserikali zinatoa kipaumbele maalumu kwa taasisi hizi kwa kuwa zimekuwa zikitoa mchango mkubwa sana katikamageuzi ya kidemokrasia nchini na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Ili kuviwezesha vyombo vya habari na asasi zisizo za kiserikali kuwa huru na kufanya kazi vizuri kwa manufaa ya wananchi serikali itakayoongozwa na NCCR – Mageuzi itachukua hatua zifuatazo:-

1)          Itatunga sheria ya uhuru wa vyombo vya habari na haki ya vyombo hivyo kupata habari kutoka taasisi za umma na idara za serikali.

2)          Itapunguza kodi kwa vyombo vya habari vitakavyotoa huduma vijijini na kuendesha programu za elimu na maendeleo na pia kupunguza kodi za karatasi.

3)          Itapanua mafunzo ya uandishi wa habari na utangazaji.

4)          Itarahisisha utaratibu wa usajili wa asasi zisizo za kiserikali.


4.6 USAWA WA JINSIA
Ili kujenga usawa baina ya jinsia ya kiume na ya kike na kutokomeza maonevu ya kihistoria na mila potofu zinazomdhalilisha mwanamke, wanawake watapewa nafasi na fursa maalum ili kurekebisha athari za maonevu waliyoyapata katika historia kama ifuatavyo:

1)     Kuwezesha matumizi ya vifaa vya kisasa majumbani ili kiwe rahisi kwa jinsia zote kushiriki katika kazi za hudumia familia

2)     Kuwa na idadi iliyo sawa ya wanaume na wanawake katika vyombo vya uwakilishi na kupanua mfumo wa uwakilishi wa uwiano.

3)     Kuridhia na kutekeleza mikataba yote ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afirka kwa manufaa ya Watanzania ili kujenga jamii yenye kutamalaki haki za binadamu na yenye kufurahia usawa kati ya wanaume na wanawake.

4)     Kuwapo kwa wanawake katika ngazi mbalimbali muhimu za uongozi wa   nchi kama ifuatavyo.

5)          Kuwepo kwa kiongozi mwanamke miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya nchi yetu ambao ni pamoja na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

6)          Kuwa na Spika wa Bunge au Baraza la Wawakilishi mwanamke na Naibu Spika atakuwa mwanaume au kinyume chake.

7)          Kuzingatia usawa wa jinsia katika nafasi mbalimbali za kiutawala  kama vile mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, mabalozi, makatibu wakuu wa wizara, makamishna, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wenyeviti na wajumbe wa bodi za mashirika ya umma.

8)          Kuwa na Meya wa jiji/Mji au Mwenyekiti wa Halmashauri mwanamke na Naibu Meya au Makamu Mwenyekiti mwanamke au kinyume chake.


MWITO KWA WANANCHI
Katika uchaguzi huu tayari tumeshuhudia matumizi makubwa ya fedha kununua wapiga kura yanayofanywa na wagombea wa Chama cha mapinduzi. Hii ni pamoja na kuwa ipo sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi na TAKUKURU kuhamasishwa ichukue hatua kali kwa wahalifu wa sheria za uchaguzi.

Wengi wetu watakuwa wamesoma na kuona katika vyombo vya habari vya serikali matangazo ya kuwasifu na kuwapongeza wagombea wa chama kilichoko madarakani. Haya ni matumizi mabaya ya taasisi hizo kwa manufaa ya chama kimoja dhidi ya vyama vingine vya siasa, ni uvunjaji wa sheria za uchaguzi, na vitendo hivyo haviweki uwanja sawa kwa wote.
Watanzania wameona jinsi miaka mitano iliyopita ilivyogeuka kuwa miaka ya kero, mateso na ufukara. Waliahidiwa maisha bora kwa wote na wameshuhudia maisha bora kwa viongozi wa serikali na CCM na dhiki kwa waliowengi. Tusifanye makosa kuwachagua viongozi wa aina hii. Tuwe jasiri na tuthubutu kuwapigia kura wanamageuzi.

Tukubali kubadilika, tuchague wagombea wanamageuzi walioletwa kwenu na NCCR – Mageuzi ili tupate fursa ya kulitendea taifa haki.  Tupeni kura zote na sisi tutawapa uwezo wetu, nguvu zetu na maarifa yetu yote ili tufike katika Tanzania inayopendeza.

Tunaomba kura zenu bila kujali dini, kabila, chama au rangi.  Kura yako ina thamani ya heri, amani na matumaini kwa miaka mitano. Ukipiga kura watawala wa sasa ni kutufunga minyororo ya umaskini, tabu na kero kwa miaka mingine mitano.  Sisi tunaahidi kutekeleza hoja na matakwa yenu kwa uaminifu na kwa umakini kama yalivyoainishwa katika ilani hii.

Fanya mageuzi kwa kutumia kura yako!

Pamoja Tutashinda!

1 comment:

  1. Je Need haraka fedha mkopo mikopo?
    * Sana haraka na ya haraka uhamisho wa akaunti ya benki yako
    * Ulipaji kuanza miezi nane baada ya kupata fedha
    akaunti ya benki
    * Low riba ya 2%
    * Ulipaji muda mrefu (miaka 1-30) Length
    * Flexible mkopo sheria na malipo ya kila mwezi
    *. Muda gani kuchukua ili fedha? Baada ya kuwasilisha maombi ya mkopo
    Unaweza kutarajia jibu awali chini ya masaa 24
    fedha katika masaa 72-96 baada ya kupokea habari wanahitaji
    kutoka kwenu.

    Wasiliana halali na leseni kampuni uaminifu mamlaka
    kwamba misaada ya kifedha kwa nchi nyingine.
    Kwa habari na mkopo zaidi fomu ya maombi ya pamoja ya biashara, kwa njia ya

    email: cashfirmarena@gmail.com

    SIR Eva Demeter
    Mkurugenzi Mkuu
    CASHFIRM

    ReplyDelete