Tuesday, 16 July 2013

HISTORIA YA TANZANIA NA CHIMBUKO LA NCCR-MAGEUZI



1.1 Dokezo

Uhifadhi wa historia ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya taifa letu la Tanzania hauna budi kuzingatia kina cha harakati za umma, hususan harakati zilizoanza katika karne ya kumi na tisa na kuendelea hata sasa.  Taifa lililostaarabika hutunza kumbukumbu ya pamoja, na litajitambua pale lilopo kwa kutazama lilipotoka na huko linapokwenda. Chama cha NCCR-Mageuzi kinatambua umuhimu wa kuhifadhi kwa usahihi kumbukumbu ya pamoja ya utaifa wa watu wetu kwa heshima ya wahenga wetu na kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo vya watanzania. Kwa mantiki hiyo, katika sura hii ya kwanza ya kitabu cha sera zetu, tunaeleza japo kwa ufupi historia ya nchi yetu na jinsi historia hiyo inavyohusiana na harakati za wanamageuzi ambao hatimaye ndilo chimbuko la chama chetu.

1.2 Historia ya Nchi

Katika historia ya binadamu, sisi waafrika wa Tanzania na kwingineko barani Afrika, tumepata kukumbwa na majanga matatu makuu, ambayo ni Utumwa, Ukoloni na sasa Ukoloni mamboleo.  Katika janga ya kwanza ambalo lilishamiri sana kati ya karne ya 14 na 18, waafrika walitekwa na kuuzwa utumwani kuwa vyombo vya uzalishaji mali vya mataifa ya ng’ambo kwa kisingizio kuwa sisi ni sawa na nyani au sokwe mtu.  Watu wa kutoka nje ya bara letu walimtazama Mwafrika kama mnyama yoyote yule na hawakumtambua kuwa ni binadamu wenye utashi na roho.

Wengi kati ya watu weusi walioko Amerika ya Kaskazini na Kusini, Uarabuni, bara la Ulaya na Asia leo, ni vizazi vya watu waliochukuliwa utumwani kutoka barani kwetu.  Zaidi ya waafrika milioni 12 waliuzwa katika Bara la Amerika na Visiwa vya Karebea katika biashara hiyo dhalimu ya utumwa.  Maendeleo ya sasa ya nguvu za kiuchumi za mataifa hayo ni matokeo ya nguvukazi ya watumwa wenye asili ya kiafrika.

Janga la pili, yaani Ukoloni; lilifuatia lile la Utumwa. Mabadiliko kutoka kulidhulumu bara la Afrika kwa njia ya Utumwa hadi njia ya Ukoloni kulitokana na mabadiliko ya uchumi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyopunguza mahitaji ya nguvukazi ya watumwa.  Ilibidi watumwa waachiwe huru ili kujenga uchumi wa soko la dunia. Ilionekana kuwa kuna faida kubwa kumtawala mwafrika katika bara lake la asili na kumtumia kuzalisha malighafi za kilimo, madini na nyinginezo kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vya Ulaya Magharibi. Hivyo pilikapilika za mataifa ya kigeni za kujitwalia makoloni barani Afrika zilibuniwa na kutekelezwa haraka kiasi kwamba ilipofika mwaka 1884 mataifa ya kibeberu yalikutana Berlin, Ujerumani kugawana bara letu.  Katika kilele cha mkutano huo wa Berlin nchi zilizojipatia makoloni barani Afrika ni pamoja na Ujerumani (mwenyeji wa mkutano), Uingereza, Ufaransa, Ubeligiji, Ureno, Hispania na Italia. Katika mgawanyo huo, Tanganyika iliangukia mikononi mwa utawala wa kijerumani.

1.2.1 Tanganyika chini ya utawala wa Ujerumani

Ukoloni uliingia Tanzania kuanzia nchi yetu ilipotawaliwa na Ujerumani kati ya mwaka 1884 na 1918, na ikapewa jina la Deutsch Ostafrika.  Koloni la Deutsch Ostafrika lilijumuisha eneo lote lililo kati ya maziwa makuu ya Tanganyika na Nyasa.  Eneo hilo sasa ndipo zilipo nchi za Rwanda, Burundi na Tanzania (bara).  Wakati wa uvamizi huo wa kikoloni mnamo mwaka 1884, sehemu ya ukanda wa pwani ya Tanganyika ilikuwa chini ya Sultani wa Zanzibar hivyo ilibidi Wajerumani wainunue kutoka kwa Sultani wa Zanzibar.  Hatimaye, mwaka 1890 visiwa vya Zanzibar viliwekwa chini ya himaya ya Uingereza.

Tokea enzi hizo, waafrika wenyeji wa Deutsch Ostafrika walipigana kuzuia uvamizi wa Wajerumani lakini kwa namna moja au nyingine baadhi ya viongozi wenyeji walijikuta wakigawanywa na kuanza kusaidiana na maadui kuisaliti nchi yao.  Mashujaa thabiti wa nchi yetu waliopambana na ukoloni ni pamoja na viongozi wa Wachaga, Mkwawa wa Wahehe na wanaharakati wa vita ya Majimaji. Bahati mbaya juhudi zao hazikufanikiwa kuzuia uvamizi wa wajerumani. Tunazidi kuuenzi na kuuheshimu moyo huo wa mashujaa wetu wa kipindi hicho.

1.2.2 Tanganyika chini ya Utawala wa Uingrereza

Mwaka 1919 baada ya Ujerumani kushindwa vita ya kwanza ya dunia, Deutsch Ostafrika ilitwaliwa na taifa la Uingereza chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa awali (League of Nations) na ikapewa jina jipya la Tanganyika.  Mnamo mwaka 1945, Umoja wa Mataifa wa awali ulivunjwa na kuundwa upya kuwa Umoja wa Mataifa wa sasa (United Nations Organisation).  Nchi zote zilizokuwa zimeshikiliwa chini ya Umoja wa Mataifa wa awali ziliwekwa chini ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa wa sasa, Tanganyika ikiwa mojawapo. Hivyo, Uingereza iliendelea na mkataba wa kuitawala Tanganyika kwa niaba ya Umoja wa Mataifa hadi itakapokuwa na uwezo wa kujitawala.

Wakati wa utawala huu wa mkoloni mwingereza, wanamageuzi wazalendo walianza harakati za kudai uhuru wa taifa letu. Harakati zao zilikuwa kwa njia ya kujikusanya pamoja katika vyama ama vya burudani au vya wafanyakazi. Hatimaye vikaanza kuibuka vyama vya siasa ambavyo lengo lake kuu lilikuwa ni kudai uhuru wa Tanganyika. Kwa mfano, mnano mwaka 1929 chama cha watanganyika kijulikanacho kwa jina la African Association (AA) kiliundwa jijini Dar es Salaam. Jitihada za vyama hivyo zilifanikiwa kumshinikiza mwingereza aone haja ya kukomesha utawala wake kwa Tanganyika.

Mnamo mwaka 1961, Uingereza ilifuta mkataba wa udhamini wa Umoja wa Mataifa na kuiweka chini ya himaya yake ili kuliwezesha Bunge lake kuwa na mamlaka ya kutoa uhuru kwa Tanganyika.  Kwa hiyo, katika kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe 9 Desemba mwaka 1961 hadi Tanganyika ilipokuwa Jamhuri mwaka 1962, Tanganyika ilikuwa sehemu ya himaya ya Uingereza.

1.2.3 Uhuru Kamili wa Tanganyika

Tarehe 9 Desemba 1962, Tanganyika ilijipatia uhuru kamili kwa kuwa Jamhuri.  Bunge la Tanganyika lilifuta sheria ya Bunge la Uingereza iliyokuwa imeiweka Tanganyika chini ya himaya ya Uingereza na kutunga katiba mpya ya Jamhuri.  Kwa jinsi hii, tarehe Tanganyika ilipokuwa jamhuri ndiyo tarehe halisi ya uhuru kamili wa Tanzania bara.

1.2.4 Utawala wa kigeni Zanzibar

Visiwa vya Unguja na pemba ambavyo ni sehemu inayounda taifa letu la Tanzania, vilipata kuwa chini ya utawala wa kigeni wa Sultani toka Uarabuni na baadaye mkoloni mwingereza  alitwaa utawala toka kwa Sultani kati ya mwaka 1890 hadi 1963. Katika kipindi hicho cha utawala wa kigeni, wazanzibar wenye moyo wa uanamageuzi walipinga kutawaliwa na wageni, hata wakaanzisha harakati za vyama vya siasa kwa ajili ya kutetea maslahi ya wazanzibari na kudai uhuru wa Zanzibar.

1.2.4 Uhuru wa Zanzibar

Mnamo Oktoba, 1963 Uingereza ilifuta mkataba ulioipa jukumu la kuilinda himaya ya Sultani wa Zanzibar.  Tangu hapo Zanzibar ikawa imerejeshwa chini ya sultani wa Zanzibar ambaye alikuwa ndiye mkoloni wa kwanza wa visiwa hivyo.  Ilibidi wenyeji wa Zanzibar kuendeleza harakati za kupigania uhuru ili kuung’oa ukoloni wa kiarabu visiwani.  Harakati hizo zilifaulu tarehe 12 January, 1964 pale wazalendo wakiongozwa na chama cha Afro Shirazi walipompindua Sultani Jamshid; ambaye alifanikiwa kutoroka na kukimbilia Uingereza.  Kwa jinsi hii, tarehe ya uhuru kamili wa Zanzibar ni 12 January, 1964.

1.2.5 Kuzaliwa kwa Taifa la Tanzania

Taifa la Watanzania lilizaliwa tarehe 26 April, 1964, siku Zanzibar na Tanganyika zilipoungana na kuwa nchi moja yenye dola moja la Jamhuri.  Ikumbukwe kuwa japokuwa zilikuwepo sababu nyingi za nchi hizi mbili kuungana na kuwa moja, ukweli ni kuwa muungano wa nchi hizi mbili ni mfano hai na uthibitisho kuwa lengo la umoja wa Afrika linaweza kufanikiwa.

1.2.6 Mfumo wa Siasa Chama Kimoja

Baada ya kuzaliwa kwa Tanzania, yaliibuka matatizo kadhaa yaliyo kinyume na haki, hususan tatizo la udikteta na ukiritimba ya chama kimoja uliojitokeza katika nchi yetu tangu ilipojipatia uhuru wake kamili wa kisiasa mwaka 1962 (kwa upande wa Tanganyika) na mapinduzi mwaka 1964 (kwa upande wa Zanzibar). Tatizo hili ni moja tu ya sura zilizojitokea za utawala wa kibeberu ambao sasa ulikuwa katika enzi ya ukoloni mamboleo.

Kama ilivyoelezwa awali, vilikuwepo vyama mbalimbali vya siasa vilivyoshiriki harakati za kudai uhuru wa taifa letu. Hata hivyo, vyama vya siasa vilivyofanikisha hasa harakati hizo za uhuru ni Tanganyika African National Union (TANU) kwa upande wa Tanganyika, na Afro Shirazi Party (ASP) kwa upande wa Zanzibar.  Baada ya hatua hii ya harakati za ukombozi, vyama hivi viwili viliingia katika njia potofu ya utawala wa kiimla na ukiritimba.  Vilianza ukandamizaji wa umma, na mnamo mwaka 1965 vikapiga marufuku vyama vingine vya siasa na kujenga dola ya chama kimoja kimoja kila upande wa muungano.  Utawala wa nchi tangu nyakati hizo ulikuwa mbaya kwa kuwa haukufuata sawasawa katiba ya nchi wala kulinda haki za binadamu ipasavyo.

Wakati huo huo, wakoloni wetu wa zamani waliibuka na njia mpya za kulinyonya bara la Afrika, yaani Ukoloni mamboleo (janga kuu la tatu kwa Afrika). Utawala wa chama kimoja ulishindwa kabisa kubaini mikakati na mbinu dhidi ya ukoloni mamboleo.  Badala yake taifa likaingizwaa katika sera za utaifishaji wa mali binafsi na kujenga sekta kubwa ya dola (sio umma, kama ilivyodaiwa) katika uchumi na huduma za jamii badala ya kuwawezesha wenyeji wa nchi hii (umma wenyewe) kuingia katika shughuli kuu za kiuchumi na kuongoza uchumi wa nchi yao wenyewe.

Matokeo ya upotofu huo wa kisera na kiutawala yalidhihirika miongo miwili baadaye pale mashirika yaliyohodhiwa na dola yaliposhindwa kutimiza malengo yake na kuanza kufilisika.  Hali ya maisha ya wananchi ilizidi kuwa duni kiuchumi vijijini na mijini. Hali hii iliandamana na kuporomoka kwa huduma za jamii kama vile elimu, afya na miundombinu ya usafirishaji, nishati na mawasiliano.

Kadhalika taifa liliingizwa katika shimo la ubadhirifu wa mali iliyopaswa kuwa ya umma, ukiritimba, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na udikiteta.  Tarehe 5 February, 1977 vyama vya TANU na ASP viliungana na kuwa chama kimoja kiitwacho “Chama cha Mapinduzi” kwa kifupi CCM.  Sambamba na matukio haya katiba ya nchi ilitungwa upya kuhitimisha matakwa ya muundo wa dola ya chama kimoja cha siasa.  Hii ndiyo katiba inayotumika hadi leo ambayo imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara badala ya kuandikwa upya ili iwe katiba ya kudumu kama zilivyo katiba zinazoheshimika duniani.

1.2.7 Harakati za Kurejeshwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa

Kwa kuwa utawala wa chama kimoja ulijidhihirisha kuwa mbaya kiasi cha kuwa karibu kufanana na ule wa kikoloni wanamageuzi wazalendo walibuni mbinu mpya za ukombozi.  Hatua ya awali ilikuwa ni kuleta ukombozi wa kisiasa utakaoliwezesha taifa kuondokana na mfumo wa siasa na utawala wa chama kimoja.  Hii ilipelekea kuundwa kwa Kamati ya kupigania Mageuzi ya kikatiba nchini iliyoitwa National Committee for Constitutional Reforms (NCCR).  Kamati hii iliundwa mnamo tarehe 11 na 12 Juni 1991 na wanamageuzi waliotoka kwenye sekta mbalimbali za jamii nchini.

Harakati dhidi ya mfumo wa chama kimoja nchini ziliungana na vuguvugu dhidi ya udikiteta na ukiritimba wa kisiasa kwingineko duniani.  Mnamo 1992 serikali ya Tanzania ililazimika kuridhia kubomolewa kwa mfumo wa chama kimoja na kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vyingi nchini.  Katiba ya nchi ilirekebishwa na kufuta mfumo wa Chama kimoja na kufungua milango kwa mfumo wa vyama vingi.

Baada ya mafanikio hayo, baadhi ya wanamageuzi waliokuwa katika kamati ya NCCR walitumia fursa ya uwepo wao katika kamati hiyo, wakuunda vyama mbalimbali vya siasa. Hatua hiyo wapo waliodhani kuwa ni mbaya kwa kuwa kwao iliashiria kuzaliwa kwa ‘utitiri’ wa vyama.  Mtazamo huo hauzingatii ukweli kuwa vyama vya siasa ni vyombo vya uainishaji wa fikra mbalimbali za kisiasa zenye misingi katika falsafa mbalimbali za jinsi gani binadamu anaiona jamii, uchumi na siasa.  Ni vyombo vinavyowapa wananchi uhuru wa kufuata mitazamo ya kisiasa wanayoitaka. Kila chama ni chombo cha kiitikadi na hivyo ni jambo lililokuwa la kutegemewa kuwa mara itakapokuwa halali kuunda vyama, basi vitaibuka vyama vingi kulingana na itikadi zinazoshindania fursa ya kuongoza dola.

1.3 Kuzaliwa kwa Chama cha NCCR- Mageuzi

Wanamageuzi ambao hawakuondoka ndani ya kamati ya NCCR kwa ajili ya kwenda kuunda vyama vingine, waliamua kuibadilisha kamati hiyo na kuunda chama cha Mageuzi kwa jina la NCCR-Mageuzi, mnamo tarehe 15 Februari 1992.  Neno NCCR lilipewa maana mpya, yaani; National Convention for Construction and Reform.  Tafsiri rasmi ya jina hili ni Chama cha Mageuzi na Ujenzi wa Taifa.

Hivyo, NCCR-Mageuzi ni chama cha siasa kilichosajiliwa mnamo tarehe 29 Julai, 1992 kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.  Kwa ujumla Chama hiki ni matokeo ya juhudi za wananchi wa Tanzania kujikomboa kutokana na ubeberu ambao umejikita katika nchi yetu tangu mwaka 1884.

No comments:

Post a Comment