Wednesday, 6 March 2013

MBATIA AMGOMEA PINDA

Mbatia amgomea Pinda

Ndg. James Francis Mbatia akiongea na waandishi wa Habari kuhusu kukataa kwake kushiriki katika Tume iliyoundwa na Mhe. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. (Picha kwa hisani ya IPP Media)

 

6th March 2013
 Ni kwenye Tume ya matokeo ya kidato cha IV   
Asema hataki kuwa sehemu ya kuua elimu

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia,  amesema amekataa uteuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwa mjumbe wa Tume ya kuchunguza chanzo cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2012.

Mbatia ambaye aliteuliwa katika tume hiyo yenye wajumbe 15 iliyotangazwa wiki iliyopita, amesema kwamba hayuko tayari kushiriki katika tume hiyo kwa kinachochunguzwa ni sehemu ndogo ya tatizo lililopo. Mbatia alitangaza uamuzi huo katika mkutano wa waandishi wa habari jana uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam.

Mbatia alitangaza uamuzi huo kwa kuonyesha barua aliyoiandika jana kwenda kwa Waziri Mkuu Pinda kuukataa uteuzi huo.

Alisema licha ya kwamba hajapata barua rasmi ya uteuzi huo, lakini ameona halitakuwa jambo jema kwake kushiriki katika tume hiyo kwa kuwa anaamini kwamba njia hiyo haitakuwa bora katika kupambana na tatizo lililopo katika mfumo wa elimu nchini.

Mbatia pia alisema kuwa anaamini kuwa hadidu rejea za tume hiyo zilizotajwa kupitia vyombo vya habari hazitashughulikia kwa upana udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini.

“Kwa heshima na kwa unyenyekevu mkubwa, napenda kukuarifu kwamba nimesikia habari za kuundwa kwa Tume ya kuchunguza chanzo cha kushuka kwa kiwango cha kutisha cha ufaulu wa mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2012 na kuteuliwa James Mbatia (Mb) kuwa miongoni mwa wajumbe wa tume ambao umewateuwa katika tume hiyo,” ilieleza sehemu ya barua ya Mbatia kwenda kwa Waziri Mkuu na kuongeza:

“Hizi ni habari nilizozipata kupitia vyombo vya habari mbalimbali vya hapa nchini, hadi ninapoandika ujumbe huu sijapokea mawasiliano kwa njia barua kutoka ofisini kwako (Pinda) kunijulisha kwamba nimeteuliwa katika tume hiyo na majukumu yanayonikabili ni yapi kufuatia uteuzi huo.”

 Aliongeza katika barua hiyo aliyaandika jana kuwa: “Pamoja na kutopokea barua rasmi ya uteuzi, ninapata wasiwasi kwamba kushirikishwa kwangu katika Tume hiyo kumezingatia vigezo vipi na kunaweza kujenga sura gani katika matokeo ya utafiti yatakayotolewa na tume mara baada ya kumaliza kazi yake.  Wasiwasi wangu huo unatokana na kwamba kushirikishwa kwangu katika tume tajwa kunaweza kuwa na mgongano wa kimaslahi (Conflict of interest).”

Aidha, Mbatia aliongeza kwamba kabla ya Pinda kuunda tume hiyo, chama chake kilimwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kumtaka aunde tume ambayo itaangalia namna ya kushughulikia kwa undani mfumo mzima wa elimu kama ile iliyoundwa na aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu, Marehemu Jackson Makwetta, siyo kuendelea kuchunguza kushuka kwa ufaulu jambo ambalo limekwishafanyiwa kazi na tume zilizopita.

Mbatia aliongeza kwamba hoja yake aliyoiwasilisha katika mkutano wa 10 wa bunge ilihusu udhaifu uliopo katika setka ya elimu nchini na kwamba maelezo aliyoyatoa juu ya chimbuko la udhaifu huo ni pamoja na Sera ya elimu iliyopo kutokuwa na andiko rasmi la mtaala wa elimu, kasoro nyingi katika mihtasari ya masomo, vitabu vya kiada na ziada visivyokuwa na ubora wa viwango vya kuridhisha na utaratibu wa kifisadi katika utayarishaji vifaa vya elimu hususani vitabu, hivyo  kuunda tume ya kuchunguza tatizo la kufeli ni sehemu ndogo sana ambayo haitasaidia.

“Ikumbukwe kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) iliunda tume ya kuchunguza chanzo cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2010 na kutoa ripoti Juni 2011 ambayo Waziri Shukuru Kawambwa aliiwasilisha.  Kwa mantiki hiyo, haitakuwa jambo jema kwangu kushiriki katika tume hiyo kwa sababu hailengi kushughulikia kwa upana udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini,” alisisitiza.

“Litakuwa ni jambo jema kama maafisa wa serikali hususani kutoka katika ofisi yako wataona haja ya kusoma taarifa mbalimbali za tafiti juu ya suala husika mathalani zilizoko katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wizara ya elimu na Mafunzo ya ufundi, Hakielimu, Twaweza,” ilieleza sehemu ya barua ya Mbatia kwenda kwa Pinda. Pia Mbatia aliishauri serikali kwamba endapo kuna umuhimu wa kuunda tume, jambo muhimu la kulifanyia kazi ni ulinganifu wa uzito wa sababu zote nzito za elimu kwa kufuata viwango vya kitaifa, kimataifa na uwezo wa kirasilimali uliopo.

Pinda aliteua wajumbe wa tume hiyo Machi 2,  mwaka huu, ambao  kwa mujibu wa hadidu za rejea, watatakiwa kuangalia ni sababu zipi zimechangia kuwapo kwa matokeo hayo mabaya, sababu zinazochangia kushuka kwa kiwango cha elimu, usimamizi wa elimu katika halmashauri, ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya elimu kwenye Wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (Tamisemi) umechangiaje kushuka kwa kiwango cha ufaulu.

Vile vile Waziri Mkuu alisema wajumbe wa tume hiyo watatakiwa kuangalia mitaala na mihtasari ikoje, kuangalia uwiano uliopo kwenye mitihani inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani hiyo, kuangalia mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji, usimamizi na uendeshaji, na kutokuwapo kwa chakula shuleni kunachangiaje kushuka kwa utendaji mbaya wa wanafunzi katika masomo yao. Tume hiyo ilipewa muda wa wiki sita kuanzia Machi Mosi iwe imekamilisha kazi hiyo na kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu.

Tume hiyo inaongozwa na Profesa Sifuni Mchome kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) na Makamu wake ni  Bernadetha Mushashu ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera.
Wengine ni James Mbatia; Abdul  Marombwa (Mbunge wa Kibiti); Profesa Mwajabu Possi (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;  Honoratha Chitanda kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT); Daina Matemu kutoka Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa) na Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).

Wajumbe wengine ni Rakhesh Rajani (Twaweza); Peter Maduki (CSSC), Nurdin Mohamed (Bakwata); Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi);  Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu cha Suza); Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Zanzibar na  Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala).

Mbatia aliwasilisha hoja binafsi katika mkutano wa 10 wa bunge kuhusu udhaifu uliopo katika mitaala huku akibainisha mambo makuu yanayochangia kudidimiza elimu nchini kuwa ni mitaala ya elimu, udhaifu katika vitabu vya ziada na kiada, sera iliyopitwa na wakati na kasoro zilizopo katika mihtasari ya masomo.

Hata  hivyo,  hoja hiyo iliibua mjadala mzito bungeni baada ya serikali na wabunge wa Chama Cha mapinduzi kuikataa.

Baada ya hoja hiyo ambayo Mbatia pamoja na mambo mengine alitaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza, wabunge wote wa upinzani walisusia kikao na kutoka nje kama njia ya kumuunga mkono Mbatia.

Baadaye serikali iliwasilisha vitabu vya mitaala na baadaye iliunda kamati ya wabunge akiwamo Mbatia kuchunguza kama mitaala hiyo ni halali. Kamati hiyo iliwahusisha Margareth Sitta (Viti Maalum CCM); Mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Malombwa; Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa, Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse; Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa na Mbunge wa Viti Malum (CCM), Bernadeta Mashashu.

Kamati hiyo baadaye iliwasilisha taarifa yake bungeni ikieleza kuwa mitaala hiyo ni halali, ingawa Mbatia aliendeleza msimamo wake wa kupinga.  Serikali imeunda tume hiyo kufuatia matokeo hayo mabaya ambayo yalitangazwa Februari 18 na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, yakionyesha kuwa asilimia 60 ya watahiniwa wamefeli.

Wanafunzi waliofeli kwa maana ya kupata sifuri ni 240,903. Waliopata daraja la nne ni 103,227, waliopata daraja la tatu na 15,426, waliopata daraja la pili ni 6,4,53 na waliopata daraja la kwanza ni 1,641.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment