Sunday 20 January 2013

NCCR-MAGEUZI YACHOMOA MWINGINE KUTOKA CHADEMA

Ndugu Moses J. Machali (Mb) Katibu wa Uenezi na Mahusiano ya Umma ya Chama  akimkabidhi kadi ya NCCR-Mageuzi Ndugu Edo R. Makata aliyejiengua CDM na kujiunga na NCCR-Mageuzi, leo tarehe 20.1.2013 Mkao Makuu ya Chama.



TAMKO LA NDUGU EDO R. MAKATA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA
 KUHUSU KUJIUNGA NA NCCR-MAGEUZI 20/01/2013
Ndugu wanahabari,
Salamu, na heri ya mwaka mpya!
Ndugu wanahabari,
Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunivusha hadi mwaka huu wa 2013 nikiwa imara na mwenye afya njema sana, maana bila yeye Mwenyezi tusingeiona siku ya leo.
Ndg wanahabari, Naitwa Edo Rashid Makata Mwamalala niliyekuwa katibu wa CHADEMA mkoa wa Mbeya tangu mwaka 2009 hadi 2013, Leo nimeona kuwa ni wakati mwafaka kuzungumuza nanyi ili niwafahamishe wanachadema kutoka mkoa wa Mbeya na watanzania kwa ujumla juu ya mustakabali wangu kisiasa baada ya kutangaza kujiuzulu uanachama wa CHADEMA pasipo kueleza bayana naenda wapi.
Wapendwa wanahabari, harakati zangu za kisiasa nilizianza tangu ujana wangu nikiwa ni muumini wa siasa za upinzani zenye tija na kweli, na rasmi nilijiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Machi 2005. Nikiwa CHADEMA, nilijituma kwa bidii na kwa moyo mkunjufu sana, nilikitumikia katika nafasi mbalimbali; ikiwamo Uratibu wa vijana jimbo la ubungo 2005/ 2007, ukatibu wa wilaya ya kinondoni, 2006/2007, ukatibu wa mkoa wa mbeya na ujumbe wa mkutano mkuu wa Taifa 2009/2013. Pia nimegombea nafasi za uwakilishi mbali mbali;  2005 udiwani kata ya mabibo Dar es salaam, na 2010 niligombea  ubunge jimbo la Kyela.
Ndugu wanahabari, mtakumbuka mwanzoni mwa mwezi huu, tarehe  03/01/2013, nilitangaza kujiuzulu nafasi zote za uongozi ndani ya CHADEMA ikiwa ni pamoja na kujivua uanachama wa chama hicho.
Kwa furaha kubwa kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwatangazia wana Mbeya na umma wa Watanzania kwa ujumla; kwa kuvunja ukimya, sasa  natangaza rasmi kujiunga na Chama Cha National Convention For Construction and Reform- Mageuzi (NCCR- Mageuzi). Aidha, niseme kuwa huu ni mwanzo tu, mimi nimetangulia na kuamini wengi watakuja au kufuata hatua kwa hatua.
Nimechukua uamuzi huu mzito na wa kihistoria wa kuhama nilikokuwa zamani na kujiunga na NCCR-Mageuzi kwa kuwa;
NCCR kwa matendo kimeonekana kuwa chama cha UTU na chenye misingi bora ya usawa, uheshimu wa haki za wanachama na watanzania wote, na chenye mshikamano wa kweli.

Aidha nimekerwa na kuchoshwa na CHADEMA sana kutokana na;
1.      Ufisadi mkubwa wa ukiukaji wa katiba na kanuni ndani ya chama,  ubabe wa Mwenyekiti Taifa Bwana Freeman Mbowe, ukabila, udini na matumizi mabaya ya ruzuku ambayo ni mambo ya kawaida ndani ya Chama kinachoitwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo.
2.      Ndani ya Chadema, pindi utakapotofautina kimtazamo au kimawazo na Freeman Mbowe au Dr wilbrod Slaa katika masuala ya msingi ya ujenzi wa chama, utasemwa umehongwa, Umetumwa au wewe ni pandikizi la CCM na au Masalia.  Viongozi hawa wanapenda sana sera za CCM za zidumu fikra za mwenyekiti na katibu mkuu wa CHADEMA hata kama ni mbovu au ni za kipuuzi, kwa mfano suala la kutangaza nia ya Urais na Mchumba wa Dkt Slaa, Josephine Mshumbusi anafanya ziara mikoani huku ikiwa haifahamiki ni nani ndani ya CHADEMA mbali na kuwa ni mwanachama wa kawaida, na iwapo watajitetea kuwa ni mwanachama wa kawaida; je, ni First lady au nani? Hali ambayo inakivuruga chama ilihali ikifahamika wazi kuwa CHADEMA wamekuwa wakipinga kwa nyakati tofauti suala la mke wa Mhe. Rais wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kufanya ziara mbalimbali nchini kwa kutumia gaharama za seriakali; ni vema sasa watanzania tukajiuliza CHADEMA ina tofauti gani na CCM? Suala la huyu mchumba wa Dr. Slaa kufanya ziara kwa kutumia gharama za CHADEMA pasipo baraka za vikao halali vya chama si ni ubadhirifu wa fedha na utoaji wa posho kinyemela? Ukihoji wanadai umehongwa, umetumwa, pandikizi au masalia. Haya ni matumizi mabaya ya fedha.

3.      CHADEMA na siasa za ulaghai bungeni kutafuta umaarufu; Kimsingi haiingii akilini kumuona na kumsikia Mwenyekiti wa CHADEMA taifa akisimama Bungeni na kutamka kuwa anapinga kwa nguvu zote suala la matumizi makubwa ya fedha za serikali kwa kununulia magari ya kifahari ya takribani shilingi 300 milioni na vinginevyo (vx v8) halafu anatenda kinyume cha kauli zake. Kwa mfano Mwaka 2011 wakati wa bunge la bajeti aliutangazia umma wa Watanzania kuwa ameamua kulirudisha gari la kiongozi wa upinzani bungeni aina ya VX V8 lenye namba za usajili KUB kama sehemu ya kupinga matumizi mabaya ya fedha katika ununuzi wa magari, jambo hilo lilitufurahisha sana na kumuona huyu ni kiongozi mzalendo. Lakini cha ajabu Mbowe ameendelea kulitumia gari hilo na akiulizwa na kuelezwa kuwa anatusaliti, kutudhalilisha wapinzani anakuwa mkali. Je, huo siyo unafiki na utapeli wa kisiasa? Viongozi wa CDM taifa ni walaghai kwa sehemu kubwa kutafuta umaarufu usiokuwa na tija kwa taifa na hii ni kutudhalilisha wanasiasa wazalendo wa aina yangu.
4.      Matumizi mabaya ya ruzuku: yapo matumizi mabaya ya ruzuku katika chama hicho, kwa mfano Dr. Slaa kulipwa zaidi ya shilingi milioni saba kwa mwezi kama posho ya kujikimu. Hivi hii ni sahihi kweli ilihali huko mikoani na wilayani wakiachwa kama yatima na kwamba wachangishane hadi kieleweke? Binafsi hainingii akilini na nimehoji sana nikaambiwa nimetumwa; ni mamluki na masalia, ninajiuliza, mimi ni masalia? na kama ni masalia je, ni masalia ya nani au nini? Na kama dhana ya masalia ina maana ni mabaki ya kitu fulani, kwa hiyo Dr. Slaa mwenye kadi za CCM na CHADEMA ndiye masalia namba moja. Hivi hii ni haki kweli? Wakati huo huo dereva wake analipwa na chama; mafuta ya gari anapewa na chama, ana ulinzi kwa gharama za chama. Yote haya ni mwenendo mbaya wa uongozi wa CHADEMA kifaifa na nimesikitishwa sana kwa kusikia kuwa amejikopesha zaidi ya shilingi milioni mia moja arobaini kupitia ruzuku ya chama inayotokana na kodi za watanzania  huku mikoani na kwengineko wakiwa na njaa kali.

Upendeleo wa ruzuku kwenye majimbo, mfano jimbo la kyela linapewa tsh. 100,000/= wakati jimbo la ubungo kwa mnyika linapewa tsh. 800,000/=
Mwisho kabisa:Wakati akina Juju Danda, Moses Machali, Mkosamali Felix, David Kafulila  na wengine walipoondoka CHADEMA kwa nyakati tofauti hasa mwaka 2009 /2010, mimi na wenzangu tulibaki CHADEMA tukiamini tutapambana humohumo hadi hali itengemae lakini ukweli CHADEMA siyo chama cha watu wenye dhamira njema katika kuleta mabadiliko hapa nchini. Utafiti rahisi unaonesha kuwa siyo rahisi watu kuwa wanaondoka na kukalia kuaminishwa kuwa viongozi wa CHADEMA unaonewa na kwamba wapo  sahihi Slaa na wenzake.
Ndg. Wanahabari na watanzania wote, CHADEMA ni kama kampuni ya watu fulani kiutendaji. Hakuna Demokrasia ndani ya CHADEMA ndugu zangu. Naomba mrejee suala la Zitto na wengineo kutangaza nia ya kugombea urais. Kwa mfano, Zitto anapingwa sana, na hata Kisandu alipingwa sana hali kadhalika Ndg. John Shibuda (MB) kwa nyakati tofauti wameitwa waleta vurugu ndani ya CHADEMA. Lakini Mbowe kamtangaza Dr. Slaa kuwa mgombea wa urais mwaka 2015 ilihali akijua kuwa mtu yeyote kutangaza nia siyo tatizo kidemokrasia, je lini kamati kuu na baraza kuu la CHADEMA vilikaa na kumpitisha Slaa atangazwe kuwa mgombea wa mwaka 2015? Je, hiyo ndiyo demokrasia au Domokrasia?  Ni dhahiri ubaguzi upo wazi kwa kuwa akina Zitto, Shibuda na wengineo wakitangaza nia wanaitwa majina mbalimbali lakini Mbowe akitangaza, aaaaah; shwari. Siyo siri huu ni uhuni katika misingi ya demokrasia ndani ya CHADEMA na kokote miongoni mwa vyama vya siasa.


Imetolewa na
Ndg. Edo R. Makata





No comments:

Post a Comment