Thursday 17 January 2013

SUNGURA: OOH MTWARA, JIWE WALILOLIKATAA WAASHI…!


Ndugu Faustin Sungura
Mwishoni mwa mwaka 2012, baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mtwara walifanya maandamano ya amani na yaliyofuata utaratibu wa sheria zilizopo, kwa lengo la kufikisha ujumbe waliokuwanao kwa viongozi. Maandamano hayo yaliitimishwa kwa mkutano wa hadhara. Kati ya mengi yaliyozungumzwa kwenye mkutano huo, ni pamoja na suala la gesi iliyogundulika hivi karibuni mkoani humo. Baadhi ya wananchi Mkoani Mtwara, wanataka rasilimali hiyo ya gesi ifuliwe na kusambazwa kwa watumiaji ikitokea mkoani Mtwara. Wanapinga hatua ya serikali kuu ya kujenga njia (bomba) ya kuisafirisha gesi kutoka Mtwara na kwenda kufuliwa, kisha kusambazwa nchini ikitokea Dar es Salaam. Baada ya kutolewa kwa msimamo huo wa wananchi wa Mkoa wa Mtwara, upele umeota na kusambaa kwenye ngozi na sasa wakunaji wa upele huo wameingia kazini wakitokea sehemu mbalimbali na staili zao tofauti tofauti za ukunaji.

Kuna baadhi yetu watanzania, wanaona kuwa, gesi kufuliwa na kusambazwa kutokea Mkoa Mtwara hakuleti tija kwa afya ya ustawi wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Kwamba tumekuwa na utamaduni wa kutumia maliasili za taifa sote pamoja, siyo tu katika eneo moja ilikopatikana na au kugundulika kwa rasilimali fulani. Wanadai kwamba, miundombinu ya kufua umeme tayari ilishajengwa Dar es Salaam hata kabla ya kugundulika gesi ya Mtwara, hivyo ni  rahisi kusafirisha gesi kutoka Mtwara na kuifulia jijini, na kwamba walaji wakubwa wa zao la gesi wanapatikana jijini Dar es Salaam, lakini pia kwamba wakazi wa Mtwara hawajaachwa nyuma kwani nao watapewa mgao wa nishati hii nyeti.

Aidha, serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kupitia kwa waziri mwenye dhamana ya nishati na madini, alipata kutoa ufafanuzi wa ni kwa nini gesi isafirishwe kutoka Mtwara ili ifuliwe jijini Dar es Salaam. Alieleza vile vile kwamba, baadhi ya wananchi wa Mtwara waliondamana hawakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya kile wanachopinga na au walikuwa wanachochewa na watu wa kambi ya upinzani, yaani viongozi wa vyama vya upinzani vya  UPDP, CUF, TLP, Chadema, NRA, NCCR – Mageuzi,  na vingine.

Hatimaye muwasho wa upele huu ukafika hata kwa wazee wa Mkoa wa Tabora, walipotoa msimamo wao mbele ya mkuu wa nchi, ambaye pia ameungana na wazee hao kwamba, rasilimali ya gesi iliyogundulika Mkoani Mtwara ni mali ya watanzania wote bila kujali mwananchi anayekaa Kagera, Arusha, Dodoma, kwingine popote na hiyo Mtwara yenyewe.

Aina lukuki za ukunaji wa upele huu, ndizo zimenifanya nitenge muda kidogo, nifikiri ni chambue na kuandika haya. Hakika kutenga muda, kufikiri, kuchambua na kuandika juu ya jambo ni kazi ngumu sana, ni kazi inayohitaji utulivu,  staha na uvumilivu, lakini pia ni wajibu na hasa kwa watu makini.

Ninaandika makala haya nikiwa na ufahamu kuwa, wananchi (japo sio wote) wanajua kusoma na kuandika, ila sina uhakika kama wote tunaojua kusoma na kuandika tunapenda pia kusoma na kuandika.

Ninaandika makala haya, nikiwa mmoja wa watanzania wanaounga mkono maandamano na madai ya baadhi ya wanamtwara.

Ninawaunga mkono huku nikiistaajabia kauli ya serikali kwamba, “waliondamamana hawakuwa na ufahamu juu ya mpango wa serikali wa kusafirisha gesi kutoka huko kuja Dar es Salaam kwa sababu hata wao watanufaika na mradi huo.” Ninastaajabu kwa sababu, idadi kubwa ya wenyeviti wa Vijiji, Mitaa, Madiwani na Wabunge wengi wa Mkoa wa Mtwara wanawawakilisha wananchi kupitia Chama Cha Mapinduzi. hawa nao (baadhi yao) walishiriki maandamano! Kwa kuwa serikali iliyo madarakani inatekeleza Ilani na sera za Chama Cha Mapinduzi, ninapata shida kuilewa vizuri dhana hii kwamba watu hawafahamu, kwa sababu, kama serikali inasema ukweli inakuwaje wawakilishi wa wananchi wa Mkoa wa Mtwara na ambao pia walishiriki kuzinadi  Ilani na sera za CCM hawakujua mipango ya serikali yao? KinyumeLabda serikali iweke wazi  kwamba Ilani na Sera za CCM zipo wizarani na siyo katika ngazi za vijiji, mitaa, kata na majimbo.

Katika hali ya kawaida ningetarajia kuona maandamano ya baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara yanahusisha tu na au kuungwa mkono na wale ambao hawajui Ilani na Sera za CCM. Inapotokea baadhi ya wenyeviti wa vijiji, mitaa, madiwani na wabunge wa CCM wanaunga mkono maandamano, basi ni vema tukajua kuwa ngozi hii inawasha zaidi tunavyoona kwa juu na wakunaji waliobobea wanahitajika sana.

Maadamano yaliyohusisha viongozi na au kuungwa mkono na viongozi hao ni kielelezo kizuri kuwa hawajui kile kinachofanywa na chama chao, wametengwa na au hawashirikishwi katika mambo ya msingi.Kama CCM tangu awali ilikuwa na mambo yalifanyika na kwa maslahi ya wanamtwara lilikuwa jambo jema kuwahusisha na kama hawakuhusishwa walistahili kufanya kile walichokifanya (maandamano).

Aidha ninaungana  na watoa hoja ya kwamba masuala ya gesi ya Mtwara yaamuliwe na wanamtwara kwa sababu, sikubaliani na mawazo kuwa huo ni ubaguzi na kwamba ni kurudisha nyuma maendeleo ya taifa kwa ujumla wake.

Serikali na baadhi ya watu, wana mtizamo kwamba, madini na au rasilimali inayopatikana eneo fulani, isitumike tu kwa ajili ya eneo hilo bali ipelekwe eneo lingine na au sehemu zingine za nchi kwa mgawo ulio sawia. Binafsi ninauona mtazamo huu kuwa wenye kasoro kubwa na pengine ndicho chanzo cha kuifanya nchi yetu na hasa raia wetu wengi waendelee kuishi katika hali ya umasikini na hasa ule mbaya kuliko umasikini wa kipato, yaani umasikini wa mawazo.

Ni makosa makubwa sana, nchi kuweka mayai yote kwenye kapu moja. Si jambo la afya ya ustawi wa taifa kufanyia kila kitu kwenye mji mmoja kwa hoja hafifu kuwa ni kurahisisha huduma. hatari ya kapu moja ina mifano dhahiri. Matharani, mikoa mingi ya Tanzania bara ikiondolewa tu ile ya kusini, inategemea daraja la mto Ruvu kuingia na kutoka Dar es salaam. Siku daraja hilo litakapoharibika na au kuhujumiwa ndipo tutaona umuhimu wa kuwa na zaidi ya barabara mbili au tatu za kuingilia na kutokea Jijini. Ninaandika makala haya nikiamini ya kuwa, kuwa na chanzo kingine cha umeme na nje ya mkoa wa Dar es salaam ni moja ya hatua chanya na ambayo kila aliye makini anatakiwa kuiunga mkono.

Wilaya, au Mikoa yote kusikopatikana na kunakopatikana rasilimali mbalimbali, kwa pamoja ndizo zinaunda nchi itwayo Tanzania. Tanzania inatumia rasilimali za wilaya A, B na C kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hizo lakini pia rasilimali hizo zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wilaya D, E, F nk. Huu ndio msimamo wa serikali, lakini pia baadhi ya wananchi ndio wanaounga mkono, sina hakikia kama kuunga kwao mkono kunatokana na mazoea, uelewa au kuamini kile wanachoelezwa na serikali

Hata hivyo, inapotokea madini x au rasilimali y yamengundulika kwenye eneo A na ambalo linakaliwa na wananchi, huwa serikali inawaondoa eneo hilo, lakini haiwafidii wananchi wa eneo B au C bali wale wale wa eneo A.

Tunapoendelea kuliangalia hili tujiulize pia kama ni sahihi kwa wananchi wanaokaa karibu sana na viwanda vya sukari kama Mtibwa Mkoani Morogoro, Kagera Mkoa Kagera na TPC-chama mjini Moshi, Mkoani kilimanajaro, wanafurahia kununua kilo moja ya sukari kwa shilingi x kama wanavyonunua wakazi wengine wanaokaa umbali wa kusafiri kwa masaa 12 kutoka eneo la viwanda hivi.

Sina hakika, kama mtanzania anayeishi mita chache kutoka kwenye kiwanda cha magari aina ya TOYOTA nchini Japani, ataacha kununua gari kwa bei nzuri, badala yake aje kununua gari kama hilo kwenye yadi zetu hapa ‘Bongo’ kwa bei ya kibongo eti kwa sababu tu… aagh!

Sina hakiki kama uamuzi wa serikali za awamu za nyuma wa kujenga viwanda kama Mutex, Ngozi, Magunia mjini Moshi nk, mbali na zinakopatikana malighafi nk ulikuwa unazingatia maslahi ya wananchi.

Sina hakika kama wakazi na au wananchi wanaokaa karibu na bahari, maziwa na mito mikubwa wanafurahia kununua mazao yatokanayo na maji hayo (hususan samaki) kwa bei kubwa kama wale wanaokaa mbali sana na maziwa, bahari na mito mikubwa.

Sina hakika kama bei za mazao ya wakulima zinazotolewa wakati wa ununuzi wa mazao hayo huko mashambani, zinaoana kwa ulali na bei ya mazao hayo kwenye masoko yetu ya Tandale, Kariakoo, Kisutu na kwingineko kwingi.

Sina hakika kama kutatokea muujiza kwamba kufulia umeme wa gesi ya Mtwara na kuusambazia Dar es Salaam kutamnufaisha mwananchi wa Mtwara, wakati mlaji wa umeme anaiyeishi Dar es Salaam ananunua umeme kwa bei ile ile kama anavyonunua mkazi Kidatu na Mtera yaliko mabwawa ya maji.

Ninarejea kauli yangu ya awali, ninaunga mkono wananchi wa Mtwara wawe na maamuzi ya rasilimal hiyo kwa sababu kadhaa,

Kabla ya kueleza sababu hizo moja kwa moja, ningalipenda wasomaji wa makala haya, waifananishe Tanzania na mmoja wa wazazi wa watoto x, y na z.

Kwamba, Tanzania kama baba analo kujukumu la kuwatunza watoto hawa kwa ulinganifu na bila ya upendeleo wowote. Hata hivyo, mzazi (Tanzania) anayo pia majukumu mengine mazito zaidi ya kuwatunza watoto wake. Matunzo ya watoto hawa yanahitaji gharama kubwa lakini pia kuna kazi na au shughuli nyingine zinazohitaji fedha na gharama kubwa ambazo zinamuangalia mzazi huyu (Tanzania).

Akili zangu ndogo zilizomo kwenye medula oblongata yangu, zinatosha kuona mantiki ya hoja ya wakazi wa Mtwara.

Mtwara kama moja wa watoto wa mzazi aitwaye Tanzania, anasema “Baba nimekuwa mtu mzima na sasa ninataka kujitegemea.” Watu makini wanatarajia baba awe mwenye furaha kwa kumlea mtoto wake hadi utu uzima, na sasa mzigo wa kulea unapungua, anapumua, anapumzika baadhi ya majukumu.


Mtwara (mtoto x) kati ya watoto watatu (y na z) wa mzazi wetu (Tanzania) anamwambia baba yetu kuwa, yeye amepata kazi, anaomba aruhusiwe kufanya kazi, bila shaka kufanya kwake kazi kutawanufaisha hata hao ndugu zake y na z na hata baba yetu mzazi (Tanzania).

Kama ingalitokea fursa nikapata hadhi ya kuwa mzazi wa watoto hawa (x, y na z) nisingalimzuia mmoja wao kufanya kazi ya kumuingizia kipato. Siyo kweli kuwa uchumi wa x unaweza kuathiri uhusiano wake na y au z dhidi ya mzazi wao.

Familia tatu za ukoo wa Uledi, kamwe haziwezi kuhatarisha uwepo wa ukoo eti kwa sababu familia mojawapo ya ukoo huo imepata fedha na au utajiri.

Hebu tuichukulie gesi kama bidhaa na au mazao mengine ya mashambani au viwandani.

Joel Mapunda ni mkazi na mkulima wa mahindi wilayani Songea, mazao yake yameiva shambani na sasa amevuna magunia mia moja ya mahindi. Mzee Mapunda ni baba wa familia ya mke mmoja na watoto wanne. Sina hakika kama Mzee Mapunda anawajibika kulima shamba kubwa ili awalishe jirani na au rafiki zake, kama vile Mzee Bernald Mbawala na wala Simioni Mhagama. Ninaandika makala haya nikiwa na uhakika wa asilimia zote kuwa, Mzee Joel Mapunda anaweza kutumia magunia yote mia moja, lakini siyo kwa kukoboa na kusaga kwa ajili ya kusonga tu ugali. Ninaandika makala haya nikiwa na uhakika wa asilimia zote kuwa, mahindi na au unga siyo mahitaji pekee ya lazima ya familia ya Mzee Joel Mapunda, familia hii itahitaji pamoja na mambo mengine au vitu vingine kama; Mchele, Unga wa ngano, Mafuta ya Alizeti au yale ya Mawese, Vitunguu, Nyanya, Mafuta ya taa, Sukari, Mavazi, Kusafiri, Ada kwa ajili ya shule, Michango ya harusi, misiba n.k, na vitu hivyo vitahitaji fedha.

Ninapoandika makala haya, japo akili zangu zimevurugwa na wakunaji upere kuukuna ndivyo sivyo, sina uhakika kuwa,  kuhitaji fedha za matumizi mengine kutaleta ubaguzi na kuacha kumuuzia mahindi yake Ndugu Jacob Malecela wa Dodoma, Hamis Mtolya wa Temeke, Anastazia Kimatuzi wa Kigoma, Daimoni Mwasampeta wa Mbeya, Khatibu Shaha Zaharani wa Ole Kisiwani Pemba nk.

Aidha, sidhani kama hawa wanaonunua mahindi ya Mzee Joel, wanalazimika kwenda Songea ndipo wapate mahindi hayo, lakini pia sina uhakika kama wanaonunua mahindi kwenye masoko ya Tandale, Kariakoo na hata Kibaigwa wanafahamu na au wanauliza jina la mkulima.

Kama ningekuwa na uhakika wa asilimia zote kuwa, watu wote wanaojua kusoma na kuandika, pia wanapenda kusoma na kuandika, mbali na kuandika juu ya mazao ya mahindi ya Mzee Joeli, pia ningeandika juu ya Mzee Anthony Massawe na zao la ndizi kule Kilimanjaro. Isack Masanja na mazao ya pamba na dengu kule Mkoani Shinyanga, Ndugu Pili Kumwembe wa Morogoro na zao la mpunga, Bi Mose Juma wa Michaweni na Asha Muhsini wa Chambani na zao la karafuu na muhogo kisiwani Pemba nk.

Kama ambavyo wakulima wa mazao ya Mahindi, Pamba, Korosho, Kahawa, Katani, Michikichiki, Mpunga, Alizeti, Karanga nk wanavyohitaji fedha za kununulia bidhaa nyingine, kadhalika na wakazi wa Mtwara hawawezi kula gesi, hawezi kuvaa gesi na wala kufanya kiwanda cha gesi kiwe makazi yao badala ya nyumba bora.

Ninaandika makala haya, nikiwa na kumbukumbu za maneno ya baadhi ya wanachama, makada na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwamba “Serikali ya CCM ni serikali sikivu

Nimerejea maneno haya, siyo kwa sababu nyingine yoyote bali kwa sababu, matakwa ya watu wa Mtwara yanaweza yasiwe na maana yoyote kama Serikali ya CCM itaamua kushikilia msimamo wa kuendesaha nchi kwa mazoea badala ya hoja kama zinavyojitokeza kwenye baadhi ya mambo ya msingi.

Ninaomba pia usikivu wa serikali siyo kwa sababu nyingine yoyote, bali kwa sababu zinaanza kujionesha baadhi ya dalili za uchafuzi wa amani unaotokana na kupuuzwa, na kudhaurauliwa kwa muda mrefu kwa watu wa kusini, na ndiko kumewafanya wakakata tamaa.

Ulifika wakati, mfanyakazi au mtumishi wa serikali, kuhamishiwa na au kutishiwa kupelekwa Mtwara, kama moja ya adhabu halali ya kosa alilolifanya katika utendaji wake kazi wa kila siku.

Ninaandika makala haya, kama mmoja wa watu waliowahi kufuga mmoja wa wanyama wa ndani, mnyama huyu hutokea akawa rafiki wa mfugaji,wakapendana na hata wakati mwingine tofauti za unyama wao zikapotea na wanyama hawa wakawa kama ndugu. Siku isiyo jina, mmoja wao anapomkosea mwenzake, na hata aliyekosewa akaona na kuhisi kudharauliwa, kunyanyasika, urafiki wao hupotea na nafasi yake ikajazwa na uadui.Hapa ndipo panaponifanya niiomba serikali ya CCM kuwa wasikivu.

Mbali na busara za wazee wa CCM na Serikali yake, panahitaji pia na nia njema ya kuwatendea mema wakazi wa Mkoa wa Mtwara.

Ninapoandika makala haya, zao la Korosho linalolimwa kwa wingi Mkoani Mtwara, halijawahi kuwa na bei ya hovyo kwenye soko la dunia, zao hili limeliingizia taifa fedha nzuri za kigeni kama yalivyo mazao ya Kahawa na Pamba.

Ni mtu yule tu ‘aliyetokwa na akili’ kama mimi, na ambaye hakuwahi kuitembelea miji ya Moshi, Mwanza na Mtwara, atakayesadiki na kuamini kuwa miji hiyo inafanana kwa majengo yake, barabara zake, huduma na hata maendeleo ya wakazi na wenyeji wa mijji hiyo mitatu.

Kama wale ambao ‘hawajatokwa na akili’ kama mimi, ambao ‘wana akili zao’ siku zote, wataona moja ya miji ya Moshi, Mwanza na Mtwara haifanani na wala kukaribiana na miji mingine. Inapotokea wakazi  au wenyeji wa mji ule wakaanza kulalamika na wakaambiwa kwamba malalamiko yao hayana msingi, kwa usemi wa siku hizi, basi hapo sharti pakachimbika bila jembe.

Kutorejewa kwa akili zangu za kawaida wakati ninaandika makala haya na ili kuomba pasichimbike bila ya jembe, kumenifanya niyakumbuke maneno ya aliyepata kuwa mwandisi mashuhuri wa vitabu katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki, Shaaban Robert aliyepata kusema wakati wa uhai wake kwamba, “Busara kubwa kichwani haina faida, kama moyoni hakuna chembe ya wema

Baada ya kusema haya, ningalipenda kufahamu madhara yatakayolipata taifa, kama serikali na hususani wizara, itaamua kufua gesi na kusambaza umeme kutokea Mtwara badala ya Dar es Salaam.

Watanzania ‘waliohamwa na akili’ kama mimi, tungalipenda kujua gharama halisi za kufuliwa na kusambazwa umeme kutokea Mtwara kwenda Dar es Salaam na kwingineko. Aidha, tungalipenda kujua gharama halisi za mradi wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara na kufulia gesi hiyo Dar es Salaam.

Tunataka kujua ukweli kwani, kwa uchache wa akili tunadhani njia ya sasa ya kusafirisha gesi imefikiwa kwa sababu ya maslahi ya baadhi ya maafisa wa serikali. ninapoandika makala haya, halmashauri ya Jiji la Dar es salaam tayari inawahamisha baadhi ya wafanyabiashara wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo na kutoka nje ya Jiji la Dar es salaam kwa maelezo ya kupisha barabara za magari ya mwendo kasi. Hatua hii inanialika niwe na mawazo kuwa, Serikali yetu haina mipango ya muda mrefu wala ile ya muda mfupi. Tunaendesha mambo kwa kukurupuka. Kuna watu wanadhani kuwa, uwepo wa magari yaendayo kwa kasi kutapunguza msongamano wa magari jijini.

Lilikuwa jambo jema, napengine muhimu sana, kujiuliza na au kujua ni kwanini watu wanapenda kuja kuishi Dar es salaam. Njia sahihi na pengine ya suluhisho la muda mrefu ya kupunguza msongamano wa magari na watu, ni kuhamisha baadhi ya vitu vinavyowafanya watu wapende kuishi Dar es salaam kwenye mikoa mingine.

Watu hawaji Dar es salaam kufuata joto, majengo marefu, barabara za njia mbili, la! wana jambo na au mambo fulani. Mambo na au jambo hilo ndilo linatakiwa kushughulikiwa ili sasa lipatikane Mtwara, Lindi, Singida, Mara, Manyara, Kaskazini Pemba, Kusini Unguja nk. Tukiliweka jambo hilo kwenye mikoa hiyo, serikali haitawaambia watu wahame Dar es salaam na wala mabondeni, wataondoka wenyewe na Jiji litapumua vizuri.

Hatuwezi kuondoa msongamano wa magari, kama watu wanaendelea na hata kushindania kupata fursa ya kuja kuishi Jijini”.Haya ni mawazo yangu ya kijinga na ambayo hayanikeri kuwa nayo na wala kutamani na kuwa na zaidi ya haya.

Nimeandika makala haya nikiamini kwamba, kuacha gesi ya Mtwara ikaamuliwa na wanaMtwara, hakuwezi kuwa sababu ya kuondoa umoja, upendo na mshikamano miongoni mwetu.

Ninaamini kwa sababu, wakazi na au wenyeji wa Mtwara watahiji baadhi ya bidhaa na au huduma ambazo hazipatikani Mtwara, watalazimika kama ilivyokuwa kwa Mzee Joel Mbawala wa Songea kuuza mahindi yake, kuuza umeme unaotokana na gesi yao kukidhi mahitaji mengine.

Ninapoandika makala haya, sina uhakika kuwa kuna mkoa ambao hauna rasilimali zake na umefika wakati sasa inabidi serikali ikubali kupunguza matumizi yake na hasa yale yasiyo na tija, ijiendeshe kwa kupata ruzuku kutoka mikoani badala ya yenyewe kutoa ruzuku mkoani.

Hivi sasa Tanzania in mikoa 30 kati ya mikoa hiyo, mitano ipo Zanzibar na iliyobakia ipo upande wa pili wa Muungano. Dhana kwamba rasilimali zinazopatikana Mkoa fulani zisitumiwe tu na mkoa huo bali pia kwa mikoa mingine, ina siri kubwa nyuma ya pazia, dhana hii inatumiwa na wanyonyaji na wavivu wa kufikiri na hata wale wa kufanya kazi.

Tunapozumzia rasilimali, hautuzungumzii tu madini, mbunga za wanyama, maziwa, mito na bahari tu, bali pia watu, vipaji, ardhi nk.

Ninaandika makala haya, Mkoa wa Kilimanjaro ukiongoza kwa kuwa na shule za sekondari na nyingi zazo zikiwa za binafsi, lakini pia na ambazo hazikosi kutoa shule 2 – 4 katika shule kumi (10) bora kila mwaka. Wenyeji wa mkoa huu ni wachagga, lakini shule hizi hazipokei wanafunzi kwa kigezo cha ukabila, yeyote anayejihisi ana uwezo wa kugharamia ada ya mwanaye anao uhuru wa kutafuta nafasi ya kumsomesha mwanae.

Lushoto ni moja ya wilaya za Mkoa wa Tanga, wenyeji wa wilaya hii ni wasambaa, taasisi moja isiyo ya kiserikali inamiliki shule moja ya Kifungilo, ni shule nzuri kwa maana ya kuwa na walimu wanaolipwa vizuri, wenye wito na karama ya ualimu, ipo kwenye mazingira mazuri kwa mwanafunzi kujisomea. Wakati wa kufunga au kufungua shule na hata wakati wa usaili (Interview) ya wanafunzi wapya, shule hii huwa na magari mengi ya wazazi wa wanafunzi wasio wa wilaya hii na wala Mkao wa Tanga kwa ajili ya kuwasindikiza watoto/wanafunzi.

Mkoani Arusha kuna mgodi wa machimbo ya madini huko Mererani, wachimbaji wadogo kwa jina la Nyoka wapo wengi na wanatoka mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Manyara, Singida nk. Moja ya sifa ya kupata kazi ya unyoka ni uvumilivu,  nguvu na sanaa ya kuongea au namna ya kutumia akili na ulimi na wala siyo uenyeji wa mkoa wa Arusha.

Shule za Kilimanjaro, ile ya Kifungulo na nyingine nyingi na nzuri pamoja na machimbo ya Mererani, huwa haziiti watu, bali watu wenyewe ndio hufuata kilicho bora.

Mbali na wafanya biashara wengine na wazuri sana, Wachagga ni watu wanaojua na kupenda biashara, hakuna mkoa hata mmoja ukiacha mikoa miwili ya Kaskazini na kusini Pemba ambayo haina biashara ya wachagga, pia wapo kwenye ofisi nyingi za serikali kuu na hata serikali za mitaa, hawa wanafuatiwa kwa karibu na Wahaya, Wasukuma, Wanyamwezi, Wanyakyusa nk.

Ninapoandika makala haya, kuna hatari katika miaka hamsini ijayo, Mkoa wa Dar es Salaam hautakuwa na mwenyeji wa asili, hii inatokakana na wengi wa wenyeji wa mkoa huu kuuza viwanja na mashamba kwa fedha wanazoona ni nyingi sana kwao na kuanza kutafuta maeneo sehemu mbalimbali za mkoa wa Pwani.

Nimelazimika kuyaeleza haya kuonesha kuwa, hakuna mradi wowote unaoweza kuanzishwa na mkoa wowote na mradi huo ukawanufaisha tu watu na au wenyeji wa mkoa huo tu.

Ninapoandika makala haya, baadhi ya makampuni ya usafirishaji wa abiria na yanayomilikwa na matajiri wa makabila mbalimbali, tayari yamejipatia sifa na wateja wa mikoa mingine kutokana na huduma zao na siyo kwa sababu ya kampuni ya  mfanyabiashara wa kabila fulani.

Pamoja na kwamba akili zangu hazijarejea, ninafajirika sana kusikia kwamba; Mtwara kuna rasilimali ya gesi; kwamba harufu nzuri ya mchele wa Kyela, haitokani tu na mbegu bali udongo wake na ambao haupatikani kokote zaidi ya Kyela; Kwamba mazao ya Karanga, Alizeti na Michikichi yakiongezewa nyenzo na kutiliwa mkazo, nchi haina haja ya kuagiza mafuta ya kupikia tusiyoyajua yanatokana na nini; kwamba Nazi ni kiungo pekee cha Mboga, Kitoweo na Chakula tunacho; kwamba Dagaa wa Kigoma wakipata mpishi mzuri, basi nyama ya kuku na samaki vitadoda; kwamba nguo zilizotengenezwa kwa pamba, zina bei kubwa kwenye soko la dunia kuliko zile za sufi; kwamba wakazi wa Moshi wanashangaa kusikia eti maji yasiyochemshwa yana madhara; kwamba Mananasi ya Chalinze huliwa takribani na makabila 80 – 90 wapitao Chalinze kwenda mikoani kila siku; kwamba ni Samaki tu anayewezwa kufanywa kitoweo hata siku 20 baada ya kuvuliwa tofauti na kitoweo cha mnyama mwingine na hasa kwa maskini tusio na mojokofu, na samaki tunao tanzania; na kwamba Senene ni mdudu anayeweza kuhifadhiwa kwa kipindi kirefu na bado akaliwa kwa ladha ile ile.


Ninasikitika kwamba, yapo mengi ya kuonesha rasilimali tulizo nazo, lakini muda siyo rafiki bali tu kwa ufupi, umefika wakati sasa tuambiwe ni mkoa upi usio na rasilimali ili sasa tuwe na sababu chanya ya kuzuia gesi ya Mtwara isifuliwe na kusambazwa kutokea Mtwara bali Dar es Salaam.


Ninaandika makala haya nikiamini ya kuwa, mbali na wenyeji wa Mkoa wa Mtwara, kuna wakazi wa mkoa huo na ambao siyo wenyeji wa asili (kabila) wa Mkoa huo, hawa ni watu kutoka mikoa ya Lindi, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro nk.


Kiwanda cha kufua gesi na kusambaza umeme kitajengwa na kusimamiwa na wataalam wa mambo ya ujenzi, wafanyakazi watahitajika na ukabila haitakuwa sifa ya kupata kazi, umeme utakaozalishwa hauwezi kuwa ndiyo hitaji pekee la wenyeji na wakazi wa Mtwara, itabidi wauze umeme nje ya mkoa wa Mtwara, wakazi wa Mtwara wakiwa na uwezo mzuri wa kifedha wanaweza kama wakipenda kuhama Mtwara na kwenda kuwekeza kwenye mikoa mingine kama walivyofanya watu wa makabila mengine.


Ninamalizia makala yangu nikiamini ya kwamba, wasomaji wa makala haya hawatajali sana kuhama kwa akili zangu, bali uzito na au wepesi wa hoja zinazobeba makala haya.


Ninamalizia makala haya katika ukweli kwamba “hakuna fedha inayoweza kukosa matumizi na hasa inapokuwa mfukoni mwa mmiliki wake


Ninamalizia makala haya, huku serikali kuu ikiwa ni mkusanyaji mkuu wa kodi, ushuru na mpokeaji wa misaada mikubwa na mikopo kutoka nje ya nchi, ndiyo inayotoa ruzuku mikoani, kwenye wilaya na halmashauri nchini.


Ninaamini kuwa, matumizi mabaya na hata ufujaji wa fedha za serikali unatokana na jinsi inavyopata fedha kwa urahisi sana.


Kuweka viwango vikubwa vya kodi ni moja ya kielezo cha kuonesha jinsi serikali isivyotaka kujihangaisha katika kutafuta kodi halali inayotakiwa  kupatikana kwa kila anayestahili kulipa kodi.


Siyo jambo la kujivunia, wala lenye tija, afya na ustawi wa ulipaji kodi kwa serikali kukusanya shilingi milioni moja kutoka kwa walipa kodi kumi. Ni jambo la kujivunia na lenye tija kwa afya na usitawi wa ulipaji kodi kwa serikali kukusanya shilingi milioni moja kutoka kwa walipa kodi hamsini” kwani, serikali huonesha jinsi ilivyo waandaa raia na kuwa na ufahamu wa wajibu badala ya kuonekana kuwa kodi ni adhabu.


Kadiri serikali itakavyoshusha viwango vya kodi, ndivyo watu wengi watakavyolipa kodi, kadiri serikali itakavyopata kodi kwa taabu, ndivyo nidhamu ya matumizi ya fedha za umma itakavyoimarika.


Makala haya yameandaliwa na Faustin Sungura, mwanachama, na mmoja wa waanzilishi wa NCCR – Mageuzi. Wakati ninaandaa makala haya nilikuwa ninakaimu nafasi ya Ukatibu Mkuu. Hata hivyo haya siyo mawazo ya chama bali yangu binafsi0659 -643191

No comments:

Post a Comment