Friday 4 January 2013

ALIYEKUWA KATIBU BAVICHA AJIUNGA NA NCCR-MAGEUZI

 
 

Ndugu Deogratius Kisandu aliyeshika Kadi, Kulia kwake ni Ndg. Florian Rutayuga ( Afisa Utawala wa Chama) na Katikati ni Ndugu Faustin Sungura (Kaimu Katibu Mkuu)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UAMUZI WANGU WA KUJIUNGA NA NCCR – MAGEUZI

Ndugu wanahabari,
Mimi ninaitwa Deogratius Kisandu, nimehitimu katika  Chuo Kikuu  cha Sebastian Kolowa  huko Lushoto (SEKUCO) nina  Shahada ya Elimu Maalum, Siasa na Utawala.
Nilikuwa mwanachama na kiongozi wa CHADEMA katika nafasi za; Katibu wa Wilaya ya Lushoto na Katibu wa Vijana wa Mkoa wa Tanga (Bavicha).
Mwaka 2010 niligombea ubunge katika jimbo la Lushoto, nilishika nafasi ya pili kwa kupata kura 5000+ dhidi ya mgombea wa CCM aliyepata kura 14000+ .
Ndugu wanahabari,
Kwa muda mrefu nikiwa ndani ya CHADEMA, tumekuwa katika maelewano mabaya  na hata pengine kujengewa  chuki na fitina   pale nilipojaribu kuhimiza viongozi wenzangu kufuata katiba ya Chama chetu.
Mwishoni mwa mwaka jana (2012) niliamua kujivua uanachama ndani ya CHADEMA na kuahidi kujiunga na Chama kingine.Vile vile nilisema siku hiyo nitaeleza sababu za  msingi zilizonifanya nijivue uanachama na kukabidhi kadi ya Chama hicho.

1.    Mnamo mwaka 2012 nilitangaza nia yangu ya kugombea urais kupitia CHADEMA. Msimamo huo umenijengea chuki na uhasama kwa viongozi wakuu wa CHADEMA akiwemo muasisi wa Chama hicho Mzee Edwin Mtei, kupinga vijana kuonesha   dhamira zao.
Nimejiridhisha kwamba, CHADEMA ina watu wake inaowataka wagombee urais na hususan watu wa Kaskazini mwa nchi hii.
Yaliyonikuta mimi pia yamewahi kuwatokea  marehemu Chacha Zakayo Wangwe, Zitto Zuberi Kabwe  na John Magane Shibuda pale walipojaribu kuwania nafasi hiyo ndani ya Chama.
Inasikitisha  sana kwa watu wanaotaka kugombea urais wanasakamwa, wale ambao hawataki kugombea  na wala kutangaza kugombea urais ndiwo wanaolazimishwa kugombea nafasi hiyo.
Itakumbukwa kwamba, Dkt. Wilbroad  Peter Slaa hakuwahi kujitangaza kuwa anataka kugombea urais, bali amekuwa analazimishwa  kugombea urais, hata juzi Mwenyekiti wa CHADEMA ameonekana  kumlazimisha Dkt. Slaa kugombea urais (2015).
2.    Mnamo mwaka 2012, Dkt. Slaa ametangaza na kukiri kuwa anamiliki Kadi ya Chama Cha Mapinduzi na kwamba Kadi hiyo ililipiwa ada kwa miaka 20 hadi  mwaka 2017.
Ninajua kuwa Dkt. Slaa anayo haki ya kuwa na Kadi hiyo kwa sababu aliinunua kwa fedha zake na hivyo ni mali yake.
Binafsi siridhiki na vitendo vya Dkt. Slaa, amekuwa anahamasisha watu wanaotoka CCM wamkabidhi Kadi za CCM. Je, hao nao hawakununua kwa fedha zao? Je, hawataki nao kuwa na kumbukumbu kama yeye? Bila shaka kuna siri kubwa imejificha  nyuma ya pazia.
3.    CHADEMA haitaki kuona vijana wanaochipukia wanakuwa na umaarufu ndani ya Chama hicho. Kwenye ziara za M4C wamekuwa wanawatumia watu wasioijua CHADEMA, wanazunguka nao Mikoani, wanawaacha vijana waliokipigania  Chama hadi kikafika hapa kilipo.
Watu wanaopata nafasi nyeti ndani ya Chama hicho ni wale tu wenye udugu au uhusiano na viongozi wakuu wa Chama. Mfano mzuri ni mgawanyo wa vitu maalum vya ubunge.
Zaidi ya nusu ya viongozi wa juu wa Chama wamehakikisha ndugu zao au wake zao ndio wamepata nafasi hizo, zingine zinagawiwa kwa njia za kudhalilishana. Hivi sasa  kuna mmoja wa wabunge wa viti maalum ana ujauzito wa mmoja wa viongozi wakuu wa Chama.
Ndugu wanahabari,
Yapo mambo mengi na ambayo siwezi kuyamaliza  kwa  leo, ila kwa ufupi nianze na hayo ili yakikanushwa ndipo nitaeleza mengine.
Baada ya kusema hayo, ninatangaza sasa rasmi kuwa, kuanzia leo tarehe 04/01/2013 nitajiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi.

SABABU ZA KUJIUNGA NA NCCR-MAGEUZI
1.    Ni Chama kikongwe, waasisi na waanzilishi wa mageuzi hapa nchini. Ni Chama kilichopitia migogoro na misukosuko mingi  ambacho ninaamini kimekomaa.
2.    Ni chuo kizuri cha wanasiasa,watu wengi wamepitia hapa, wakafundwa na baadaye wakatamaniwa hata vyama vingine. Mifano michache  ni Dkt. Masumbuko Lamwai, Dkt. Festus Limbu, Steven Wasira (CCM) na Ndesamburo, John Mnyika, Joseph R. Selasini, Chiku Obwao, Suzana Kiwanga, Profesa Mwesigwa Baregu, Mabere Marando nk.
Ninaamini kwamba, kujiunga kwangu na Chama hiki nitajifunza mambo mengi.
3.    NCCR-Mageuzi ni Chama na kipimo cha demokrasia kwa vitendo. Ni Chama ambacho hakina mtu mmoja tu kwa ajili ya nafasi ya za uongozi, yeyote ana nafasi ya kugombea nafasi  anayotaka na mkutano mkuu wa Chama ndio uamue nani anafaa kuwa mgombea urais.
Mfano, Mwaka 1995 Chama kilimsimamisha ndugu A.L. Mrema kugombea urais. Mwaka 2000 Chama kilimsimamisha ndugu Edith S. Lucina kugombea urais. Mwaka 2005 Dkt. E.A. S. Mvungi aligombea urais na mwaka 2010 Chama kilimsimamisha ndugu Hashim  S. Rungwe aligombea urais. Hii ni tofauti na baadhi ya vyama vingine.
4.    Nilipotangaza kugombea urais kupitia CHADEMA, niliwekewa mizengwe, nikajengewa chuki. Nilitangaza kugombea urais, lakini sikutangaza kwa mwaka gani, kwani mwaka 2015 umri wangu wa kikatiba wa kugombea urais hauniruhusu, nilikusudia baada ya mwaka 2015, lakini kwa CHADEMA inaonekana wana wagombea  wao wa Kaskazini kwa miaka hamsini ijayo.
Ninaamini ndani ya NCCR-Mageuzi, umri wangu ukifika, mkutano mkuu ndio utaamua na siyo kiongozi mmoja.
Baada ya kusema  hayo, ninaomba sasa nikabidhiwe Kadi ya NCCR-Mageuzi.

----------------------------------04/01/2013
D. KISANDU 


No comments:

Post a Comment