Sunday 30 December 2012

Chama Chazidi Kuimarika Jimbo la Babati Vijijini

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimezidi kujiimarisha katika Jimbo la Babati Vijijini.
Mafanikio hayo yametokana na jinsi viongozi wa chama hicho wanavyofanya mikutano ya hadhara na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wa jimbo hilo.
Katika harakati za kujiimarisha zaidi, juzi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Danda Juju, Hemed Msabaha na Peterson Mshenyela, walihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Kijiji cha Galapo.
Katika mkutano huo, Danda alikemea tabia ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuendelea kuvisema vyama vingine vya upinzani kwa kile alichosema kuwa kitendo hicho kinadhoofisha upinzani nchini.
“Hii tabia haifai kabisa, CHADEMA wao ni wapinzani kama sisi, iweje wakisimama majukwaani waendelee kuisema NCCR. Kama wanadhani watachukua nchi kwa kuwasema wenzao au kwa kuwachukua baadhi ya wanachama wa upinzani, wajue wanajidanganya,” alisema Danda.
Kuhusu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho aliyehamia CHADEMA hivi karibuni, Laurent Tara, alisema kuondoka kwake hakuna madhara ndani ya chama kwa kuwa wananchi wanamfahamu ni kiongozi wa aina gani.
Naye Msabaha, alijikita zaidi kumzungumzia Tara na kufananisha kuwa kuondoka kwake kunafanana na ujio wa Yesu Kristo ambaye alikuja baada ya Nabii Musa kuondoka.
“Mwacheni aende CHADEMA, sisi NCCR ni kama safina, watu wanapanda na wengine wanashuka. Vile vile kuondoka kwa Tara ni njia ya wengine kuingia kwa sababu hata baada ya Nabii Musa kuondoka, Yesu Kristo akaja,” alisema

Habari hii imeandikwa katika gazeti la TanzaniaDaima

No comments:

Post a Comment