Friday 14 December 2012

Cheyo, Mbatia wapinga wafugaji kufukuzwa Moro


14th December 2012

Mbunge wa kuteuliwa na Rais, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia, na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo, wamemuomba Rais Kikwete aamuru kusitishwa mara moja zoezi kla kuhamisha mifugo linaloendelea mkoani Mororogo.

Walitoa kauli hiyo jana jijini  Dar es Salaam, wakati wakizungumza na waandishi wa habari wakati wakizungumzia zoezi la kuwahamisha wafugajia kutoka maeneo ya Wilaya za Kilombero na Ulanga.

Walisema kitendo cha kuwafukuza kwa nguvu wafugaji mkoani Morogoro,  na kuwataka warudi walikotoka ni kinyume cha taratibu za nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia na ni uvunjifu wa haki za binadamu.

“Mwalimu Nyerere alitutengenezea taswira kwamba Tanzania ni yetu sote, na kila mtu ana haki ya kumiliki ardhi, badala ya kuangalia namna ya kuwagawia wafugaji maeneo ya kufugia, wanatumia helikopta kuwapiga bunduki, huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu na usalama wa raia na mali zao,” alisema Cheyo na kuongeza:

“Nasema hivyo kwa sababu Tanzania ni nchi moja na kila mtu anao uhuru na haki ya kuishi mahali anapotaka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa ibara ya 17,  aya ya kwanza ya katiba ya Tanzania.

Kwa upande wake, Mbatia alisema, kauli ya kwamba wafugaji warudi walikotoka na wengine kulazimika kuhanishwa katika makazi yao waliodumu kwa zaidi ya miaka thelathini, ni uzalilishaji wa utu na heshma ya watu wa jamii hiyo.

“Mbali na kufukuzwa, lakini pia wanatozwa fedha nyingi na kunyang`anywa mifugo yao,  wakati hakuna sheria yeyote inayowaruhusu kufanya hivyo, hakika tunasikitishwa na  kulaani sana vitendo hivi,” alisema Mbatia.

Aliongeza: “Hatuna budi kukemea vitendo hivyo vinavyoelekeza na kudhibitisha kauli na vitendo vya kibaguzi na unyanyasaji kwa binadamu wenzetu, na tunatoa wito kwa Rais kuhakikisha wale wote walioshiriki vitendo hivyo vya wizi na unyang`anyi wachukuliwe hatua kali na haraka kabla taifa halijaingia katika machafuko, ikiwa ni pamoja na kuwarudishia fedha wafugaji.”

Aidha, Mbatia alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel  Bendera, kuomba radhi na kufuta kauli yake ya kuwataka wafugaji  kurudi walikotoka.

“Kauli ya Bendera ya kuwaambia wafugaji warudi walikotoka haifai, na inaashiria ubaguzi, endapo leo hii ikaamuliwa kwamba kila mtu arudi alikotoka, si itakuwa vurugu, tunaomba  aombe radhi na Rais aliangalie hili haraka,” alisema Mbatia.

Kiongozi huyo wa NCCR-Mageuzi aliongeza kuwa ikiwa  suala hili halitashughulikiwa, watawasaidia wafugaji hao kwenda mahakamani.

Zoezi la kuondoa mifugo katika Hifadhi ya bonde la Kilombero lilianza Octoba 31, mwaka huu katika Wilaya za Ulanga na Kilombero kwa lengo la kuzuia uharibifu unaofanywa na mifugo katika bonde hilo, ambapo zaidi ya Mifugo 50, 000 inatarajiwa kuondolewa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment