Wednesday, 21 November 2012

ZIARA YA CHAMA MKOANI MANYARA

Habari hii imeandikwa na Mwandishi wa gazeti la Mtanzania.

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimewataka wananchi wasivae sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa kitendo cha kuzivaa kinaonyesha ni kwa jinsi gani wanavyokiunga mkono.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, Danda Juju, alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Madunga, Kata ya Madunga, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara.

“Sisi NCCR-Mageuzi hatuna ugomvi kabisa na vyama vingine vya siasa, sisi hatuna siasa za vurugu kama vilivyo vyama vingine.

“Sisi siasa zetu ni za kistaarabu, hatutaki siasa za kugombana na watu na hatutaki kuendesha siasa za maji taka kwa sababu tunajua madhara yake.

“Hizi siasa za maji taka zinasababishwa na tabia ya baadhi ya wananchi kupenda kuishabikia CCM wakati wakijua haina uwezo tena wa kuitawala nchi hii.

“Kwa hiyo, jamani nawaomba muonyeshe chuki za wazi wazi kwa kukataa fulana, kofia, vitambaa na kanga za CCM kwa sababu mnapokuwa mnazivaa mnakitangaza chama hicho bure wakati mnastahili kulipwa fedha,” alisema Juju.

Akizungumzia uchaguzi mbalimbali, alisema lawama ambazo zimekuwa zikitolewa na wananchi dhidi ya CCM, kwamba chama hicho tawala kimekuwa kikiwaibia wapinzani kura wakati wa uchaguzi hazitakuwapo tena kama wananchi wataamua kulinda kura zao.

“Nataka niwaambie kitu kimoja, kwamba kila mtu ni sehemu ya siasa, kwa sababu nchi nyingi zinaongozwa na wanasiasa ambao huchaguliwa kwa kupigiwa kura.

“Kwa maana hiyo ni vigumu mtu kusema hataki siasa wakati wanasiasa ndio wanaotuongoza, jamani changamkeni wakati wote, ikiwa ni pamoja na kulinda kura zenu wakati wa uchaguzi,” alisema Juju.

No comments:

Post a Comment