Friday 16 November 2012

ZIARA YA CHAMA MAJIMBO YA MSALALA NA KAHAMA

Habari imeandikwa na mwandishi wa TanzaniaDaima
Ijumaa 16 Novemba 2012

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimevuna zaidi ya wanachama 128 walionunua kadi katika majimbo mawili ya Msalala na Kahama yaliyoko wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga.
Wanachama hao walipatikana wakati wa mikutano ya hadhara iliyohutubiwa na viongozi wa chama hicho waliokuwa katika ziara ya kichama wiki hii.
Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Danda Juju.
Katika kijiji cha Kagongwa jimboni Msalala, linaloongozwa na Ezekiel Maige (CCM), Machali alitikisa kijiji hicho kwa kuhutubia mkutano wa hadhara na kisha akahutubia mkutano mwingine mkubwa katika viwanja vya CDT mjini Kahama juzi.
Katika mkutano huo, alifanikiwa kuzoa wanachama 50 waliohama kutoka vyama vingine vya upinzani na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Pia mbunge huyo alifungua matawi katika maeneo ya Nyanjende na Mseki alikozaliwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), ambako watu 30 walinunua kadi za chama hicho.
Jana jioni, Machali alitarajia kufungua tawi mjini Kahama kama sehemu ya kukiimarisha chama kisiasa.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Danda Juju, aliwasha moto katika kata za Ulowa na Ushetu ambako alifanikiwa kupata wanachama zaidi ya 30.
Juju aliwaambia wananchi kuwa umefika wakati wa kuvichagua vyama kwa kuwapima viongozi wake badala ya kutumia ushabiki usiokuwa na maana.
Alisema Watanzania wana kila sababu ya kuiunga mkono NCCR-Mageuzi kwa kuwa ndicho chama kilichoasisi mageuzi kuliko vyama vingine vyote nchini.

No comments:

Post a Comment