Friday, 16 November 2012

ZIARA YA CHAMA KATIKA JIMBO LA BUSANDA

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Danda Juju, amewasha moto wa kisiasa katika Jimbo la Busanda, Wilaya ya Geita Mkoa wa Geita, baada ya kuhutubia mikutano ya hadhara na kupata wanachama wengi.

Juju alihutubia mikutano mitatu ya hadhara jimboni humo juzi, wakati wa ziara yake ya kichama kwa ajili ya kukiimarisha chama hicho na katika mkutano wake wa kwanza Mjini Katoro, alifanikiwa kuwashawishi wanachama 36 wa vyama vingine na kujiunga na NCCR-Mageuzi.

Mbali na kupata idadi hiyo ya wanachama, Juju ambaye pia ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alifungua ofisi ya NCCR-Mageuzi katika Jimbo la Busanda na kufanikiwa kusajili wanachama wapya 88.

Pia, alihutubia mkutano mwingine mkubwa katika Kijiji cha Rwamgasa, ambapo pia alipata wanachama wapya wanane, sita wakitokea CHADEMA na wawili wakitokea CCM.

Katika ziara hiyo, waliohama na kujiunga na NCCR-Mageuzi ni Mwenyekiti mstaafu wa Chadema katika Jimbo la Busanda, Elikana Sono, Mwenyekiti wa Wanawake wa Chadema jimboni humo, Evodiah Silvat, Katibu wa Chadema wa jimbo hilo, Frola Raphael na Katibu wa Kata ya Nyamigota kupitia Chadema, Rugambwa Faustine.

Wengine ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Kata ya Katoro, Hanifa Gelvas pamoja na Shimba Kunini, ambaye aligombea udiwani kupitia Chadema wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano hiyo, Juju aliwataka wananchi kufanya mabadiliko ya kweli kwa kuikataa CCM kwa vitendo kwa kuwa imeshindwa kuboresha maisha yao.

Kwa mujibu wa Juju, kitendo cha wananchi kutoonyesha chuki ya wazi wazi dhidi ya CCM, kutakifanya chama hicho tawala kuendelea kutawala japokuwa kimeonyesha kila dalili ya kushindwa kuiongoza nchi.

Pamoja na hayo, alisema kuna haja wananchi kuviunga mkono vyama vingine vya upinzani ili viwe na nguvu kubwa ya kupambana na CCM, ambayo imeshindwa kuiongoza nchi.

Kwa mujibu wa Juju, kitendo cha kuwepo chama kimoja cha upinzani ambacho kina nguvu ya kupambana na CCM, hakileti picha nzuri kisiasa kwa kuwa hata chama hicho kikipewa ridhaa ya kuongoza nchi, kitakuwa kama CCM ambayo inaongoza nchi kwa mazoea.

Kutokana na hali hiyo, alisema vyama vya upinzani vyenye nguvu, vinatakiwa kuwa zaidi ya kimoja, kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuimarisha demokrasia nchini

No comments:

Post a Comment