Tuesday, 16 October 2012

SERIKALI IFANYE MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA DINI

Imeandikwa na Christina Gauluhanga wa gazeti la Mtanzania
 
CHAMA cha Mageuzi na Ujenzi wa Taifa (NCCR-Mageuzi ) kimemuomba Rais Jakaya Mrisho Kikwete kufanya mazungumzo na viongozi wa dini pamoja na wanasiasa, ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, likiwemo suala la uchochezi wa kidini.
Akizungumza jana na Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa chama, James Francis Mbatia alisema, nchi inakoelekea si kuzuri na endapo hali hiyo isipodhibitiwa, kunaweza kutokea machafuko ikiwemo umwagaji damu.
Alisema kuna hali ya uchochezi imejengeka miongoni mwa jamii, huku baadhi ya vyombo vinavyohusika, vimekaa kimya na kusisitiza kuwa endapo juhudi za makusudi hazitafanywa hali itazidi kuwa tete kila kukicha. 

Kwa mfano;
“Suala lililotokea kule Mbagala la kumwagia haja ndogo kitabu cha dini, halipaswi kusikilizwa na kuachiwa hewani, kwani kuna kitu kimejificha ndani yake, hivyo ni muhimu likakemewa na  vitendo vya namna hiyo kukomeshwa,” alisema Mbatia.
Aliongeza kwa kuangalia umri wa watoto waliokuwa kwenye mabishano pale Mbagala, haiingii akilini kwamba ni akili zao binafsi tu zilizowaingiza katika ubishani, bali huenda wanapandikizwa chuki au kujifunza mambo ambayo siyo kwenye mikutano mbalimbali ya dini inayofanyika maeneo mbalimbali nchini ya kukashfiana kidini.
“Katika historia ya nchi yetu hatuna ugomvi wa kidini na ndio maana tunafanya kazi au kuoleana sote kwa kuweka itikadi zetu pembeni, hivyo ni muhimu mahusiano hayo  mazuri yakajengewa heshima kwa ajili ya kulinda amani ya nchi,” alisema Mbatia.
Alisema masuala hayo yanatakiwa yajadiliwe kwa busara na amani, vinginevyo jamii itazidi kupandikizwa chuki . Tayari kuna matukio mengi ya kujifunza, ikiwemo lile lililohusishwa na Uamsho Zanzibar ambapo zaidi ya makanisa 20 yalichomwa moto.
“Kama hata Kamanda wa Polisi anaweza akauawa kwa kupigwa risasi, nani yupo salama katika nchi hii, ni vyema kukabuniwa mbinu mpya,” alisema Mbatia.
Pia Mbatia alilalamikia mfumo wa elimu uliopo hivi sasa nchini, ambapo alisema unachangia kumomonyoka kwa maadili ya watoto wengi na kuahidi kuipeleka hoja hiyo bungeni, ili mfumo huo ujadiliwe upya.

No comments:

Post a Comment