Friday, 23 November 2012

ZIARA YA CHAMA INAENDELEA MKOANI MANYARA

Habari hii ni kwa hisani ya gazeti la Tanzania Daima

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimesema ili wananchi wapate maendeleo, wanapaswa kutochagua viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wowote kama walivyoanza kufanya wananchi wa Mkoa wa Kigoma.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, Danda Juju, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Guse kilichoko Kata ya Bashnet, Jimbo la Babati Vijijini, Mkoa wa Manyara.
“CCM ni wajanja, wao siku zote wanapeleka maendeleo kwa wananchi waliowakataa na wanafanya hivyo ili wawashawishi kwa kuwapelekea maendeleo.
“Kwa mfano, Kigoma katika nchi hii ndiyo mkoa ambao umewakataa CCM kwa vitendo kwa sababu katika majimbo manane ya uchaguzi yaliyoko huko, CCM inaongoza majimbo matatu, CHADEMA wanaongoza Jimbo moja la Kigoma Kaskazini na sisi NCCR-Mageuzi tunayo majimbo manne.
“Kwa kuwa CCM ni chama cha upinzani Kigoma, sasa maendeleo yanapelekwa kwa kasi kweli na wanafanya hivyo ili wananchi waanze kuwaamini na kuwachagua.
“Sasa na nyinyi ili mpate maendeleo kama ilivyo Kigoma, msiwachague wagombea wa CCM, wakataeni kila wakati na mtakapofanya hivyo, mtaletewa kila huduma muhimu zikiwamo barabara za lami, hospitali, majisafi na huduma nyinginezo.
Katika hatua nyingine, alimshangaa Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Son (CCM), kwa kushindwa kubadilisha maisha ya wananchi wakati uwezo wa kufanya hivyo anao.
Kwa mujibu wa Juju, kitendo cha mbunge huyo kutowatembelea wananchi wake, ni kielelezo cha kujali zaidi maslahi yake badala ya kuwajali waliomweka madarakani.

No comments:

Post a Comment