Monday, 26 November 2012

NCCR-Mageuzi Wachangishana Kuweka Umeme

 Chanzo cha habari: Gazeti la Tanzania Daima

VIONGOZI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, wamechangishana fedha kwa ajili ya kuweka umeme katika Kituo cha Afya Bonga kilichoko, wilaya ya Babati, mkoa wa Manyara.
Viongozi hao walifikia hatua hiyo wakati wa mkutano wa hadhara kijijini hapo katika ziara yao ya kukijenga chama na kuwepo taarifa kwamba licha ya umuhimu wa kituo hicho, serikali imeshindwa kuweka umeme na hivyo kusababisha baadhi ya huduma zisitolewe.
Baada ya taarifa hizo, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Danda Juju na Hemed Msabaha, waliwahamasisha wananchi juu ya kuchangia fedha za kuweka umeme kituoni hapo, ili huduma ambazo hazitolewi ziweze kuanza kutolewa.
Kutokana na hamasa hizo, Mwenyekiti wa Jimbo la Babati Mjini, Mwalimu Augustino Gwandu, aliahidi kuchangia sh 50,000 huku Katibu wake, Yusuf Khatibu, akiahidi kuchangia sh 20,000, ili zisaidie kupatikana umeme katika kituo hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juu ya tukio hilo, viongozi hao walionekana kutoridhishwa na kukosekana kwa umeme huo na kuahidi kuendelea kusaidia maendeleo kila itakapowezekana.
Kwa upande wake, Juju alisema pamoja na kwamba wananchi wanalalamikia ukosefu wa maendeleo, kimsingi hawapaswi kumlaumu mtu kwa kuwa wao ndiyo wanaoichagua CCM.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi wasiendelee kuwachagua wagombea wa CCM kwa kuwa kitendo cha kuwachagua kinakifanya chama hicho kiendelee kuwa na nguvu za kutawala.

No comments:

Post a Comment