Tuesday, 9 October 2012

SIO KUPATA KATIBA MPYA TU, SHERIA MBAYA LAZIMA ZIONDOLEWE

Chanzo: Imeandikwa na Lucy Ngowi wa gazeti la Tanzania Daima


KITUO cha Demokrasia Tanzania (TCD), kimemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kuanza mchakato mapema wa kubadili sheria kandamizi ambazo zinafanya uchaguzi usiwe huru na wa haki.
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari siku moja baada ya kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa taifa hivi sasa.
Mbatia alisema ipo haja ya kuangalia sheria namba 5 ya vyama vya siasa ili ifanyiwe marekebisho.
“Ili tuweze kupata tume huru ya uchaguzi na uchaguzi tunaoutaka, ni vema Mwanasheria Mkuu akaanza mchakato,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema suala la kubadili sheria hizo zilizopitwa na wakati, lilitakiwa liende sambamba na mchakato wa Katiba mpya ili uchaguzi mkuu ujao utakapofanyika usimamiwe na Katiba hiyo mpya.
Akizungumzia tume huru ya uchaguzi alisema inapaswa kuwa huru inayojitegemea, yenye bajeti yake hivyo isisubiriwe mpaka uchaguzi mkuu ufike ndipo misuguano ianze.
“Katiba mpya tunatarajia kuipata 2014 lakini inabidi kujipanga kama hili lisipofanikiwa tunaangalia njia nyingine mbadala. Maandalizi ya sheria mpya ni vizuri yakafanyika sasa yaendane na mchakato wa Katiba mpya,” alisema.
Katika kikao hicho walichokutana na Waziri Mkuu Pinda, Mbatia alielezea mambo waliyokubaliana ni Jeshi la Polisi kuangalia upya utendaji kazi wao, kwa kuwa yeyote anayetaka kufanya mkutano anapaswa kutoa taarifa na wala sio kuomba.
Pia walizungumzia upungufu katika sheria za vyama vya siasa kwa kumpa Msajili wa Vyama madaraka makubwa.
“Tuangalie sheria hii kwa sasa iendane na mazingira ya sasa.”
Vilevile kukomesha matukio yote ya mauaji yanayoendelea nchini katika mikutano ya kisiasa au kwa wanasiasa na umwagaji wa damu pamoja na matusi.
Awali mwenyekiti huyo wa TCD alisema kuwa baada ya uchaguzi mkuu uliopita, hali ya sintofahamu ilitokea ambapo wananchi katika maeneo mbalimbali nchini waliuawa katika matukio tofauti.
Kutokana na hali hiyo, walikubaliana wakutane na Pinda ili kukomesha mauaji hayo, kwa kuwa jambo hilo ni zito sio la kufumbia macho.
Alisema kuwa mauaji hayo yalianza kuripotiwa mkoani Arusha, Igunga, Arumeru, Morogoro na Iringa.
Katika mkutano huyo, Mbatia alisema kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hakikushiriki kwa maelezo kuwa kilishaandika barua ya malalamiko kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, hivyo kinasubiri kukutaa naye.

No comments:

Post a Comment