Tuesday, 25 September 2012

RUFAA YA KESI YA UCHAGUZI JIMBO LA BABATI VIJIJINI YASIKILIZWA

RUFAA YA KESI YA UCHAGUZI JIMBO LA BABATI VIJIJINI YASIKILIZWA
Na Mwandishi wetu
Babati Arusha,
Jana tarehe 24-09-2012, mahakama ya rufani ya Tanzania katika kikao chake kilichofanyika Arusha, ilisikiliza rufaa ya kesi ya uchaguzi wa jimbo la Babati vijijini ambapo Ndg. Laurent Shumbu Tara (NCCR-Mageuzi), alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu ya Tanzania, kanda ya Arusha – Babati, uliohalalisha ushindi wa Mhe. Jittu Soni, mbunge wa jimbo hilo. Uamuzi huo ulitolewa tarehe 28-03-2012.
Rufaa imesikilizwa na majaji watatu; Jaji Mkuu Othman Chande, Jaji Salum Masati na Jaji Natalia Kimaro. Majaji hawa wamesema watatangaza katika siku za karibuni ni lina watatoa hukumu yao.
Katika rufaa hii, Ndg. Tara anatetewa na mawakili Severin John Lawena, na Haruna Msangi. Hoja zake za rufaa ni pamoja na kwamba; msimamizi wa uchaguzi wa jimbo anatuhumiwa kughushi matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010, na jaji aliyeamua kesi ya awali hakuchambua vizuri ushahidi wa madai hayo. Vile vile, inadaiwa kwamba, msimamizi alipata fursa ya kughushi matokeo kupitia utaratibu wa kutumia fomu tatu za matokeo endapo wagombea wanafika kumi na wawili au zaidi, lakini endapo ni pungufu ya idadi hiyo basi hujazwa fomu mbili tu. Msimamizi alijaza mbili na zikasainiwa na mawakala wa vyama, kisha akajaza fomu ya tatu peke yake.  Katika fomu hiyo ya tatu inadaiwa kwamba baadhi ya nakala rudufu zake hazina saini kabisa, na baadhi zina saini zilizoghushiwa. Katika uchaguzi wa jimbo hilo wagombea walikuwa wanne tu, hivyo kiutaratibu zilipaswa kujazwa fomu mbili tu zenye nakala rudufu (carbonated) sita kila moja.

No comments:

Post a Comment