NCCR-MAGEUZI
National Convention For
Construction And Reform – Mageuzi
Taarifa kwa wanachama
kupitia vyombo vya habaria
YAH: KUANGUKA KWA NDG. EMMANUEL PETRO OLE – SIRIKWA
Ndugu wanahabari,
Asubuhi ya kuamkia tarehe 28 Septemba, 2012 aliyekuwa kamishna
wa Chama chetu mkoa wa Arusha, mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama, mmoja wa wajumbe wa Baraza la
Wadhamini, mmoja wa waasisi wa Chama na aliyekuwa na kadi Na.3 ya NCCR-Mageuzi,
Mzee Emmanuel Petro Ole- Sirikwa alifariki dunia katika hospitali ya AICC Mkoani Arusha alikokuwa amelazwa kwa takribani
majuma mawili.
Chama kimempoteza mtu muhimu, alikuwa ndiye kinara miongoni mwa wanachama waliopewa kadi za mwanzo. Waasisi wenzake waliokuwa na kadi Na.1 na Na. 2, misukosuko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi
iliwafanya wamsaliti mtoto waliyemzaa (NCCR-Mageuzi) na kukimbilia vyama
vingine.
Emmanuel Petro Ole- Sirikwa, hakuyumba na aliendelea kubaki
ndani ya chama chake,hali iliyotufanya baadhi ya yetu kumuona kama mzee wa boma
la chama.
Mzee Sirikwa alibaki ndani ya chama kwa sababu ya:
- Kuheshimu na kuthamini kile alichokianzisha
- Lengo na madhumuni ya kuanzisha chama hayajafikiwa
- Uwepo wa demokrasia chanya hapa nchini bado ni kitendawili
Pamoja na haya yaliyomkuta (Mauti) sisi tuliobaki tutaendeleza na kuyasimamia mazuri yote
aliyosimamia hadi hapo malengo ya kuanzisha chama hiki yatakapotimia.
Kutokana na heshima na historia yake ndani ya chama, na
vilevile ikizingatiwa kuwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu hayana makosa na wala
hayawezi kukatiwa rufaa. Chama kimeamua kuenzi uvumilivu na misimamo yake kwa
kuuita ukumbi wa mikutano ulioko makao makuu ya chama kwa jina la “ UKUMBI
WA SIRIKWA”.
Maziko yake yanatarajiwa kufanyika Kijijini kwake Olijilah-
Arumeru Mkoani Arusha tarehe 3-10-2012.
Katika maziko hayo, chama kitawakilishwa na viongozi wakuu
wa chama wakiongozwa na Ndugu James Francis Mbatia (Mb), Mwenyekiti
wa Chama Taifa.
NCCR-Mageuzi inawaomba wanachama wetu, wapenzi na mashabiki
kuupokea msiba huu kwa jicho chanya,na kuendeleza mazuri yote aliyoyaishi wakati
wa uhai wake.
……………………………
Mussa Kombo Mussa
NAIBU KATIBU MKUU (Zanzibar)
No comments:
Post a Comment