Monday 17 September 2012

KIFO CHA NDG.SAMSON SABUNI: RAMBIRAMBI

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, Ndg. James Francis Mbatia, amemtumia salamu za rambirambi Kamishina wa chama wa Mkoa wa Kigoma, kufuatia kifo cha Mwanachama maarufu mkoani na kiongozi shupavu Ndugu Samson Sabuni aliyefariki jana tarehe 16/09/2012.

Kamishna wa Chama wa Mkoa,
NCCR-Mageuzi,
Mkoa wa Kigoma,
S.L.P 93,
Kasulu,
KIGOMA.
YAH: SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA NDG. SAMSON SABUNI SAMA
Uongozi wa kitaifa  wa chama cha NCCR – Mageuzi tumepokea kwa mshtuko, majonzi na simanzi kubwa, taarifa za kifo cha katibu wetu wa jimbo la Manyovu na diwani wa kata ya Mgera,  MAREHEMU SAMSON SABUNI SAMA.

Hatuna maneno ya kuweza kueleza vizuri namna kifo hiki kilivyotugusa; ila pokea salamu hizi kama ishara ya uwepo wetu viongozi wa kitaifa pamoja nanyi katika msiba huu.

Hakika Sote tunafahamu fika umahiri wake katika utendaji kazi na uaminifu mkubwa aliokuwa nao kwa chama. Hivyo kifo chake ni pigo lisilomithirika.

Kwa kuwa kifo ni amri ya Mungu; yatubidi kuupokea msiba huu kwa imani ili tujaliwe nguvu ya kusonga mbele.

Chama cha NCCR – Mageuzi kitaifa kinatuma salamu za rambirambi kwa wanafamilia, ukoo na marafiki  wote, wapiga kura wote wa kata ya Mgera na jimbo la Manyovu kwa ujumla.

Katika kuheshimu mchango wake na kwa faida yetu sote tunalo jukumu la kumuenzi marehemu kwa njia ya kuendeleza kazi na matendo yake mema aliyotutendea sisi mmoja mmoja na chama kwa ujumla.
Mwisho, tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu ampe pumziko la amani katika umilele. Nasi tuliosalia, atujaze moyo wa uvumilivu na subira ili tupate kuendelea na mapambano yetu ya kuifanya dunia mahali pazuri panapofaa kuishi kwa kila chenye uhai, kama alivyotamani marehemu Samson Sabuni Sama.
“Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina la Bwana lihimidiwe”
Ndimi katika utumishi wa umma,


James Francis Mbatia (Mb)
MWENYEKITI WA TAIFA

No comments:

Post a Comment