Monday, 03 September 2012 08:28 |
Kutoka gazeti la Mwananchi MBUNGE wa Kuteuliwa, James Mbatia amewalipua vigogo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa ufisadi wa fedha za mradi wa vitabu na kwamba atawasilisha hoja binafsi bungeni kufichua uozo huo. Alisema vigogo hao ambao ni watendaji wa wizara hiyo, wametumia Sh20.4 bilioni zilizotolewa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (Usaid), kuandika vitabu vilivyo chini ya viwango. Mbatia alisema hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Mwananchi ikiwa ni siku moja tangu atoe tuhuma hizo katika Kituo cha ITV. Alisema baada ya Usaid, kuipatia wizara hiyo fedha, vigogo hao na jamaa zao walijipa kazi za kuandika vitabu wao wenyewe. “ Unakuta mtendaji wa wizara anaandika kitabu, anakihariri na kukichapisha, pia yuko kwenye kamati ya kukipitisha kitumike katika shule za msingi na sekondari,” alisema Mbatia. Alisema watendaji hao wanachotaka ni kupata fedha bila kujali ubora wa vitabu wanavyoviandika. “Wanachotaka ni pesa tu vitabu vina makosa mengi kwa sababu hawafuati kanuni za kiuandishi, hili ni janga kubwa katika elimu ya watoto wa Tanzania,” alisema. Akitoa mfano wa makosa hayo kwenye vitabu, Mbatia alisema kwenye vitabu hivyo hata jina la wizara linatofautiana wakati vimetungwa mwaka mmoja. “Unakuta kitabu kimeandikwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwenye kava, lakini ndani wameandika Wizara ya Elimu na Utamaduni,” alisema Mbatia na kuongeza kwamba ofisi ya Spika imeshakubali kuwasilishwa kwa hoja hiyo binafsi. Alisema hoja hiyo, binafsi ataiwasilisha kwenye kikao kijacho cha Bunge kinachotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Alisema katika hoja hiyo anataka kufumuliwa kwa mfumo mzima wa elimu ambao hata mitalaa haieleweki vizuri. “ Hivi sasa hata ukitaka kumnunulia kitabu mtoto wako utapata shida kufahamu ni kitabu gani kinachotumika katika darasa lake,” alisema Mbatia. |
Wednesday, 5 September 2012
Mbatia aibua uozo Wizara ya Elimu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment