Saturday, 28 July 2012

TAARIFA YA NDG.F.SUNGURA KUHUSU KESI YA UCHAGUZI - MOSHI MJINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH: KESI YA UCHAGUZI JIMBO LA MOSHI MJINI
Ndugu waandishi wa habari, mwaka 2010 niliteuliwa na chama changu (NCCR – Mageuzi) na baadae Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea ubunge katika jimbo la Moshi Mjini
Pamoja na mimi, Tume pia iliwateua wagombea wa vyama vingine kugombea ubunge wa jimbo la Moshi Mjini.
Mimi sikuridhika na uteuzi wao, niliwawekea pingamizi baada ya kubaini kuwa uteuzi wao ulikiuka sheria za uchaguzi, pingamizi zangu zilitupiliwa mbali,  na kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi nilifungua shauri  No 1/2010 la kesi ya uchaguzi, katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi kati ya FAUSTIN SUNGURA dhidi ya MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI na NDESAMBURO PHILEMONI.

Mara baada ya kufungua shauri hilo kwa mujibu wa kifungu cha 115 (1) cha sheria ya uchaguzi,  nilitakiwa pia kufungua shauri la maombi N0 39/2010 juu ya dhamana ya mahakama kama ilivyo matakwa chini ya kifungu cha 111 (3) cha sheria hiyo.(CAP 343 RE 2010).

Hata hivyo, kesi yangu imekuwa inaendeshwa kwa upendeleo, kinyongo, lakini pia kinyume cha sheria.  Mahakama Kuu kanda ya Moshi  chini ya Jaji Moses Mzuna, imekuwa inanikandamiza na kuhakikisha ninakata tamaa ya kudai haki yangu, ili kumpa nafasi Mhe, Ndesamburo Philemoni amalize muda wake bila kesi yangu ya msingi kusikilizwa.


UKIUKWAJI WA SHERIA,VINYONGO NA UPENDELEO
(1)  Mnamo tarehe 7/12 /2010 nilifungua maombi N0 39/2010 juu ya kiasi cha dhamana ya kulipa mahakama au kusamehewa kulipa dhamana yoyote, maombi haya yalitakiwa kutolewa uamauzi kabla ya  au tarehe 21/12/2010. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 111 (3) cha sheria ya uchaguzi.

Hata hivyo, Jaji Moses Mzuna aliamua kutoa uamuzi baada ya miezi sita (Tarehe 24/6/2011) kinyume cha sheria, lakini pia kuhakikisha kesi inachukua muda mrefu ili kunikatisha tamaa.

(2)  Mara baada ya mahakama kuridhika kuwa sina hela, alitoa uamuzi akinieleza kuchangisha Tshs: 8,000,000/= ndani ya siku 14 kutoka kwa marafiki zangu, maamuzi haya ni kinyume cha kifungu cha 111(5) (a) na (b) cha sheria ya uchaguzi (CAP 343 RE 2010), lakini pia yalilenga kuhakikisha ninakata tama ya kuendelea na kesi yangu.

(3)  Baada ya kutoridhishwa na uamuzi huo, sheria inanipa haki ya kuomba marejeo ya uamuzi wa Jaji, hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 78 (b) au Order XLII (1) (b) vya sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai (CAP 33 RE 2002), niliwasilisha  maombi hayo na yalisajiliwa na kupewa namba 11/2012.

Pasipo halali na wala sheria yoyote, Jaji alitolea uamuzi maombi hayo bila kunisikiliza, aliamua kuyafukuza mahakamani, hii ni kinyume cha Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya nchi (Sheria kuu/mama ya nchi)
Jaji alilenga kunikatisha tama na kuhakikisha Mhe Ndesamburo Pholemoni anaendelea kuwa mbunge bila kesi ya msingi kusikilizwa.

(4)  Mnamo tarehe 6/1/2012, wadaiwa wangu walipokea  hati /wito kuwasilisha nyaraka mahakamani (Summons), walitakiwa na sheria, Amri ya VIII, kanuni ya 1 (2) na kifungu cha 5 vya sheria ya mwenendo wa kesi za madai  kusajili nyaraka zao kabla au tarehe 28/1/2012, au kuwasilisha maombi ya kusajili nyaraka nje ya muda kabla au tarehe 17/2/2012.

Hata hivyo, katika kesi yangu, wagomvi wangu waliamua kusajili nyaraka zao, hati za viapo kinzani (Counter affidavits) takribani miezi mine (4) baadae na nje kabisa ya muda, lakini Jaji Moses Mzuna akawaonea haya wagomvi wangu na kuifumbia macho sheria na akazikubali nyaraka zilizoingizwa mahakamani kupitia dirishani badala ya mlangoni. Yote hii ni kunifanya nikate tamaa ya kuendelea  kudai haki yangu mahakamani.

(5)  Mnamo tarehe 9/5/2012,  Mhe Ndesamburo Philemoni alisajili mahakamani hati ya kiapo kinzani (counter affidavit)., nami nilipewa nakala ya hati hiyo kutoka mahakamani hapo. Baada ya kuipitia niligundua ina makosa makubwa ya kisheria.

Mnamo tarehe 18/5/2012 nililipia ada ya ukaguzi wa jalada (perusal fee)na kupewa stakabadhi No 41539584

Katika ukaguzi wa jalada la mahakama linalohusiana na kesi yangu, nilikuta hati ya kiapo kinzani (counter affidavit) ya Mhe: Ndesamburo Philemoni inafanana na ile nakala niliyopewa mimi, na kwamba hati hiyo ilisajiliwa mahakamani hapo tarehe 9/5/2012 kwa stakabadhi No 41539390 iliyolipiwa Tshs: 3000/= pamoja na ada ya pingamizi
Baada ya ukaguzi huo, nilisajili pingamizi la kupinga hati ya Mhe: Ndesamburo kuendelea kubaki kwenye kumbukumbu za mahakama kwa sababu;

(a) Mnamo tarehe 9/5/2012 Mhe Ndesamburo alisajili hati kinzani ya kiapo (counter affidavit).  Pasipo kufuata sheria na kwa nia ya kumlinda na au kumsaidia Mh Ndesamburo, Jaji/ Mahakama baada ya kuona hati hiyo ina makosa ya kisheria, alimuita kinyemela, akamrudishia hati hizo ili akazikamilishe na kuzirudisha mahakamani siku hiyo hiyo na njia za kinyemela.

(b)Mhe: Ndesamburo alizipokea, lakini kutokana na majukumu mengine, au kwa uzembe alisahau kukamilisha ufisadi huo kwa siku hiyo na badala yake akaenda kula kiapo kesho yake (10/5/2012) na kukamilisha mapungufu yote, na bila halali na wala kufuata utaratibu wa kisheria, akairudisha hati mahakama tarehe 10/5/2010 kinyemela.

Mnamo tarehe 14/6/2012, mahakama ilikaa kwa ajili ya;  pamoja na mambo mengine, kusikiliza ufafanuzi wa pingamizi langu juu ya hati ya kiapo kinzani ya Mhe: Ndesamburo. Baada ya mahakama kusikiliza pingamizi hilo, ilipanga tarehe 22/6/2012 kuwa siku ya kutoa uamuzi wa pamoja na mambo mengine, juu ya pingamizi hilo

Kabla ya kutoa uamuzi, Mahakama au Jaji Moses Mzuna,  Mhe Ndesamburo  na wakili Patrick Paul, pasipo halali na kinyume cha kifungu cha 8 cha sheria  ya Mdhibiti wa vipo (Section 8 of the Notary Public and Commissioner for Oaths )walizinyofoa  hati za kiapo kinzani zilizokuwa zimekosewa, na kinyume cha mila za mahakama na taaluma ya sheria, wakaandaa hati zingine zinazoonyesha kwamba Mhe: Ndesamburo alikula kiapo tarehe 9/5/2012 badala ya tarehe 10/5/2012 na baadae kumpa nafasi Jaji Moses Mzuna kuikubali hati hiyo kuwa ni halali

Jaji Moses Mzuna, aliamua kuwalinda au kuwasaidia mawakili wa Mhe: Ndesamburo na wale wa Serikali ili kesi ya msingi isisikilizwe na kumpa nafasi Mhe Ndesamburo kumaliza muda wa ubunge alioupata kwa njia za kienyeji na zisizo rasmi.

Ndugu waandishi wa habari,  maamuzi ambayo yamekuwa yanatolewa katika Mahakama Kuu kanda ya Moshi , na ambayo hayaendani na mila za sheria, hayawezi kukatiwa rufaa katika mahakama ya rufaa. Bali yanatakiwa kuombewa marejeo katika mahakama kuu na  iliyotoa maamuzi hayo.

Kutokana na hali ya upendeleo na ukiukwaji wa wazi  wa sheria kunakofanywa na Jaji Moses Mzuna na hata kung’ang’ania kusikiliza mashauri yangu, nimejiridhisha kwamba, siwezi kupata haki kama nitaendelea kung’ang’ania kudai haki yangu katika Mahakama Kuu kanda ya Moshi na mbele ya Jaji Moses Mzuna.

Kwa sababu hiyo, nimeamua kulalamika kwa kutumia njia za kiutawala kwenye ngazi zingine zikiwemo kwa;

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheri mkuu wa Serikali, Jaji Mkuu,  Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,  Inspekta Jenerari wa Polisi, Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu, Jukwaa la wahariri, Ngd Philemon Ndesamburo, Kiongozi wa balozi za nje waliopo nchini na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa (Barua zote nimezifikisha ofisi husika kati ya tarehe 9 na 17 Julai 2012).

(i)             Mkuu wa nchi  - ili ajue nchi yake inavyoendeshwa

(ii)        Jaji Mkuu – ili aitishe jalada langu na akiridhika na malalamiko yangu, anipangie majaji watatu hadi watano wa kusikiliza kesi yangu, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17(1) iliyoundwa chini ya kifungu cha 11 7(1) cha Sheria ya uchaguzi.

(iii)            Mkurugezi Mkuu wa Tasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa - ili afanye uchunguzi wa kuona kama rushwa ndiyo inamfanya Jaji msomi  kuacha kufuata sheria na kutoa maamuzi kwa kadiri invyowapendeza wagomvi wangu.

(iv)           Insekta Generali wa Polisi - ili kitengo cha polisi kizifanyie uchuguzi hati za kiapo za Mhe: Philiemon Ndesamburo (ile iliyo ndani ya jalada la mahakama na ile niliyonayo mkononi) kama zote zilisainiwa na Mhe Ndesamburo pamoja na wakili Patrick Paul wa Moshi au kama mimi nimegushi saini ya Mh, Ndesamburo na ile ya wakili Patrick Paul pamoja na mhuri wa pfisi ya wakili huyo, vilevile kama nimegushi mhuri wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi pamoja na saini ya karani wa Mahakama hiyo,  baada ya uchunguzi achukue hatua zinazofaa na bila kujali nani ni nani.

(v)             Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  kwa sababu Tanzania ni mwanachama wa umoja huo.

(vi)           Jukwa la wahariri – ili kutoa nafasi kwa watanzania wenzangu na hasa maskini,  kujua kinachoendelea na hata ikiwezekana tuunganishe nguvu zetu pamoja kutetea ustawi wa utawala wa sheria.

Nimeandika pia katika kuenzi maneno ya busara na ustawi wa haki ya baba wa taifa, Marehemu Julius Kambarage Nyerere kwamba, “kuna kazi katika jamii zinawezwa kufanywa na watu wasio na nidhamu, na wanaoweza kutiliwa mashaka, Jaji au Hakimu siyo kazi inayoweza kufanywa na watu kama hao”.

Ndugu waandishi wa habari, hatua hii niliyofikia ya kuwahabarisha jambo hili watu muhimu na akiwemo mkuu wa nchi, ni hatua mbayo na ya mwisho wa matumaini ya kutendewa haki na hasa kama niliowaandikia nao wataamua kuwalinda watuhumiwa wangu.

NB, kesi yangu kwa sasa haipo mahakamani, inaweza kujadiliwa kwa uhuru.


Ninawashukuru kwa kunisikiliza


………………     24/7/2012
Faustin Sungura

No comments:

Post a Comment