Monday, 2 July 2012

SERIKALI IONDOE KESI DHIDI YA MADAKTARI

Mbatia/NCCR-Mageuzi waitaka Serikali kuondoa kesi dhidi ya Madaktari

Picture
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho
SERIKALI imetakiwa kuifuta kesi iliyofungua Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga Mgomo wa Madaktari na kurudi katika meza ya mazungumzo na wanataaluma hao ili kuyanusuru maisha ya Watanzania.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya chama hicho uliofanyika katika hoteli ya Mbezi Garden, Dar es Salaam leo.

Alisema ni muda muafaka kwa serikali kwenda mahakani kufuta kesi hiyo na kurejea kwa mara nyingine katika meza ya mazungumzo na madaktari hao badala ya kukaa kimya huku watanzania wakendelea kukosa huduma za matibabu na wengine wakipoteza maisha.

"Serikali ilikimbilia Mahakamani kuzuia jambo hilo lisizungumziwe lakini, kipi bora kati ya uhai wa binadamu kupoteana na suala hilo kuendelea kuwa Mahakamani huku Watanzania wakiendelea kufa?" alihoji Mbatia.

Alisema Serikali inatakiwa isiweke kiburi kwa jambo hilo na Madaktari nao walegezeze uzi wao na kukaa na Serikali katika meza ya majadiliano.

Alisema hali hii ni changamoto kwa Serikali kwani itapitiwa na Watanzania na kuwa itabaki katika kumbukumbu zao hivyo ni wajibu kwa Serikali kulimaliza jambo hilo.

Alisema wakati Serikali ikidai haiwezi kuzungumzia masuala ambayo yapo Mahakamani  hasa hilo la mgomo wa Madaktari juzi bungeni limeongolewa sakata la fedha za DECI baada ya mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuibana Serikali na kutaka kufahamu imeokoa kiasi gani cha fedha katika mchezo wa upatu uliokuwa ukiendeshwa na taasisi hiyo.

"Unaona jinsi Serikali inavyojichanganya? Wakati inadai inasimamia Utawala wa Sheria kwa kutoingilia mahakama katika masuala makubwa na muhimu kwa Taifa hawataki kuzungumzia kwa kivuli cha mahakama lakini haya yasiyohusu uhai  wa binadamu wanayapa kipaumbele; si ni hatari hii ?" alihoji Mbatia.

Akizungumzia misamaha ya kodi, Mbatia amesema ni eneo ambalo linadidima mno maisha ya Mtanzania kwani katika kipindi cha miaka mitano ilisamehe kodi ya trioni 5 jambo ambalo linaturudisha nyuma kimaendeleo.

Akitolea mfano taasisi ya Aga Khan Foundation alisema, tangu wa Serikali ya awamu ya  kwanza ilitiliana mkataba wa kusamehewa kulipa kodi kwa vile inatoa huduma kwa jamii.

Alisema taasisi hiyo licha ya kusamehewa kulipa kodi, bado wananchi hawanufaiki nayo kutokana na huduma za matibabu wazitoazo kuwa ni kubwa ukilinganisha na Hospitali nyingine kubwa ambazo zinatoa huduma za matibabu.

Alisema baadhi ya makampuni ya ujenzi yamekuwa yakipunguziwa gharama za ununuzi wa saruji kwa mgongo wa  taasisi hiyo ambapo nao uenda kuiuza kwa bei ya soko lililopo hali ambayo ni ya kulididima Taifa.

Alisema msamaha huo wa kodi upo hadi katika Shule mbalimbali za taasisi hiyo ambazo huduma wazitoazo kwa jamii zinaweza zisiwe sahihi kwa kumsaidia mwananchi na hali hiyo ni mwanya mwingine wa kuwaibia watanzania hivyo kuwa ni pango la kifisadi.

No comments:

Post a Comment