Sunday, 20 May 2012

IJUE NCCR MAGEUZI

Chama hiki kiliundwa kama kamati ya taifa ya mabadiliko ya Katiba, (National Committee for Constitutional Reform) kwa kifupi NCCR.
Kamati hiyo iliundwa Juni 12, 1991 na hadi kufikia Februari 15, 1992 ikageuzwa chama rasmi cha siasa kilichosajiliwa Januari 21, 1993 kwa jina la NCCR-Mageuzi. Tafsiri ya jina la chama hicho kwa Kiswahili ni Chama cha Mageuzi na ujenzi wa taifa, kinachotumia bendera yenye rangi kuu mbili za bluu na nyeupe.
Mashuke mawili yaliyoko kila upande wa nembo ya chama hicho, yanawakilisha amani na rangi ya bluu ni utajiri wa mito, maziwa, bahari na rasilimali nyingine tulizonazo hapa nchini.
Nembo ya chama yenye picha ya mwanamama anayesoma kitabu, inamaanisha umuhimu wa elimu na maarifa. Pia mwanaume anayelima kwa trekta inamaanisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuzalisha mali na kutoa huduma, nembo inakamilishwa na utepe wenye maneno ‘Demokrasia na maendeleo’.
Chama hiki chenye makao yake makuu hapa jijini kinazingatia misingi ya uhuru, usawa, ustawi wa jamii, haki za binadamu na mshikamano wa kindugu miongoni mwa umma. (Itikadi ya UTU inaongeza misingi ya Imani/trust, wajibu, kazi, maendeleo endelevu/sustainability, na mabadiliko ya mifumo)  
Kisiasa misingi ya chama hicho ni kama ifuatavyo; kukubali itikadi ya demokrasia ya jamii (sasa itikadi ya UTU) kwa lengo la ujenzi wa jamii huru inayozingatia haki za binadamu, kwa msingi wa mmoja kwa wote na wote kwa mmoja. Kukubali na kuheshimu demokrasia ya vyama vingi vya siasa, pia kuheshimu mchango wa vyama na vikundi vingine vya kijamii katika kukuza
na kudumisha demokrasia ya kweli. Kukubali na kuheshimu usawa na haki ya kila mtu kisiasa, kiuchumi, kisheria na kijamii. Kuwapa wanyonge upendeleo maalum, ili waweze kujiendesha kwa kasi zaidi.
Misingi mingine ya kisiasa ni pamoja na kuheshimu kazi na shughuli halali za watu binafsi, katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi. Kupenda ushirikiano na watu, vyama na jamii zinazoamini na kutetea itikadi inayoshabihiana na ya chama hiki.
NCCR inatoa kipaumbele na upendeleo wa makusudi kwa wananchi walio nyuma kimaendeleo, kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa wananchi hao ili kuinua maisha yao.
Kuna msingi ambao moja kwa mja unatugusa, naunukuu: “Kuwa na sekta huru ya habari yenye vyombo huru vya habari vyenye haki ya kupata na kusambaza habari bila woga.” Mwisho wa kunukuu. Misingi mingine ni pamoja na haki ya mtu binafsi kumiliki mali, ambayo imepatikana kwa njia halali.
Mazingira safi na salama kwa uhai wa binadamu na viumbe, ni msingi unaohusu mazingira na kuhusu usawa kuna msingi unaobainisha kuwepo kwa jamii isiyo na ubaguzi wa rangi, kabila, dini au jinsia. Msingi huo unakwenda mbali zaidi kwa kubainisha hakikisho la usawa na haki kijinsia, baina ya wanawake na wanaume katika nyanja zote kimaisha.
Kwa ujumla wake misingi mingine minne iliyosalia inahusu mipango ya maendeleo ya jamii inayozingatia mahitaji ya walemavu, kuzingatia na kulinda haki na maslahi ya watoto katika jamii, kuendeleza na kulinda haki na maslahi ya wazee katika jamii, kujenga jamii inayozingatia kuwapa fursa vijana kama taifa la leo (sio la kesho) na kuwepo mfumo bora wa uchumi duniani uliojengeka katika misingi ya usawa unaolinda haki za nchi changa kujiendeleza.
Huu msingi wa mwisho kati ya misingi ya kisiasa ya chama hiki, unahusu siasa za kimataifa na mahusiano ya nje. Tugeukie sifa za kuwa mwanachama wa chama hiki, kwanza ni lazima uwe Mtanzania mwenye umri usio chini ya miaka 18.
Uwe na akili timamu na ukubaliane na itikadi, misingi ya kisiasa, madhumuni, sera, kanuni na taratibu za chama. Ukishakubaliana na hayo unatakiwa kunua kadi na kulipia ada za chama, kisha utaorodheshwa katika orodha ya wanachama wa tawi husika ulilopitia kujiunga na chama.
Ukiwa mwanachama una haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika ngazi yoyote ya uongozi wa chama, hili tutalifafanua zaidi tutakapoanza kudadavua masuala yanayohusu uongozi wa chama hiki.
Haki nyingine ambazo mwanachama anapaswa kuzipata ni pamoja na kupata taarifa zote za yaliyojadiliwa na kutolewa uamuzi na wanachama, katika kumbukumbu ya vikao vinavyomhusu mwanachama.
Pia mwanachama ana haki pia ya kutoa hoja za kusahihisha na kuweka sawa miongozo ya chama bila hofu wala upendeleo, lakini hoja hizo zinapaswa kuwasilishwa kwa maandishi kwa katibu wa chama wa ngazi inayomhusu mtoa hoja husika.
Mwanachama pia ana haki ya kujitetea mbele ya kikao cha chama kinachohusika, kwa tuhuma zozote dhidi yake na ana haki ya kukata rufaa ngazi za juu endapo hakuridhika na uamuzi wa vikao vya chini. Lakini licha ya haki zake mwanachama naye pia ana wajibu wa kutimiza, ili kukiimarisha na kukiendeleza chama.
Wajibu muhimu wa kwanza kwa mwanachama ni kulipa ada kila mwezi, ili kufanikisha shughuli za chama. Anapaswa kujitoa mhanga kufanya shughuli za chama, bila kutegemea malipo na kuchanga fedha na mali kukijenga na kukiimarisha chama.
Mwanachama anapaswa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za chama, pamoja na kueneza sera na programu ya chama. Wajibu mwingine wa mwanachama ni kutoa ushirikiano kwa kuheshimu uamuzi wa pamoja, kuwa mwaminifu na mwadilifu kwa kusema na kutenda mambo ya kujenga na kukitukuza chama. Ni muhimu mwanachama akawa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu, kupinga uonevu, udhalimu, rushwa na ubaguzi wa kila aina na matendo yanayoharibu maadili ya jamii.
Mwanachama anapaswa kujenga weledi kwa kujielimisha juu ya masuala ya jamii, kuelewa matatizo ya watu na kiini cha matatizo hayo kwa kujitahidi kutafuta majibu ya matatizo hayo kwa ushirikiano na wanaohusika. Majungu na vitendo vya kukidhoofisha chama, vinapaswa kuepukwa ili kukilinda chama dhidi ya mitafaruku.
Kuhusiana na kutoka uanachama yafuatayo yakitokea, mwanachama atakoma kuwa mwanachama husika wa chama. Akijiuzulu kwa hiyari yake mwenyewe, akifukuzwa baada ya kukiuka Katiba, kanuni, taratibu na maadili ya chama. Pia mwanachama akijiunga na chama kingine cha siasa au kufariki dunia, uanachama wake hukoma mara moja.
Lakini angalizo ni kuwa yule anayejiuzulu na kufukuzwa uanachama, hatarejeshewa ada au mchango wowote aliotoa kwa chama. Aliyejiuzulu uanachama anaweza kuomba upya kujiunga, kupita tawi lake. Kamati tendaji ya jimbo itaridhia, baada ya kamati tendaji ya tawi kuridhika naye.
Aliyejiuzulu au kufukuzwa ana nafuu zaidi kurudia uanachama wake, kwa maelekezo yaliyotajwa katika ibara ndogo za (6) na (7) za ibara ya sura ta tatu inayohusiana na uanachama. Lakini angalizo pia ni kwamba aliyejiuzulu au kufukuzwa uanachama, atawajibika kurejesha mali na amana za chama zilizo katika hodhi yake.
Anayefukuzwa uanachama akikubali kurejea katika chama, anawajibika kununua kadi mpya.

Makala hii iliandikwa katika gazeti la Tanzania Daima, 21 April 2010

No comments:

Post a Comment