Friday, 8 February 2013

SUALA LA MITAALA YA ELIMU BADO UTATA

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dr. Shukuru Kawambwa (kulia), akizungumza na Mheshimiwa James Mbatia (kushoto), katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.

Kutoka gazeti la Mtanzania, Arodia Peter anaandika;

SAKATA la mitaala ya Elimu nchini sasa linaonekana kuwa kama mchezo wa kuigiza, baada ya Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kupinga mitaala iliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Utata huo umejitokeza baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kulitangazia Bunge jana kwamba, timu ya wabunge iliyoundwa juzi kuchunguza uhalali wa mitaala iliyokuwa ikipingwa na Mbatia, imeridhika kwamba mitaala hiyo ni halali.
Timu hiyo ya wabunge ilimhusisha     Mbunge wa Viti Maalum, Magreth Sitta (CCM), Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa (CUF), Mbunge wa Viti Maalum, Bernadeta Mshashu (CCM), Mbunge wa Kibiti, Abdul Malombwa (CCM), Mbunge wa Karatu, Israel Natse (Chadema) na Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF).
Pia timu hiyo ilimhusisha Mbatia mwenyewe ambaye aliingia kama mjumbe maalum.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya timu hiyo, Spika Makinda alisema; “Kamati iliyoundwa kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge namba 5 sehemu ya kwanza, ilipewa hadidu za rejea.
“Kamati imejiridhisha kwa nyaraka halisi kutoka serikalini ambazo ni Sheria Namba Sita ya Elimu ya Mwaka 1975, Waraka wa Elimu Namba moja wa mwaka 2006 na nyaraka nyingine zilifafanuliwa na wataalam kuhusiana na hoja zilizoletwa mezani.
“Nachukua nafasi hii kutangaza kwamba, nakala zilizotangazwa ni sahihi na ni mitaala rasmi ya Elimu,” alisema Spika Makinda.
Hata hivyo, Spika hakueleza kwa kina kuhusu suala hilo badala yake alisema aliagiza mitaala hiyo igawiwe kwa wabunge wote.
Baada ya kutoa tangazo hilo, alimwachia kiti, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kuendelea na kikao.
Kabla ya Zungu kukaa katika kiti chake, wabunge wengi walionekana kusimama hususani wa upinzani kuomba mwongozo wa Spika.
Kwa upande wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliosimama ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy Mohamed na Mbunge wa Singida Magharibi, Mwigulu Nchemba. Upande wa upinzani waliosimama walikuwa ni Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR Mageuzi), Mbatia, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) na Mbunge wa Biharamlo Magharibi, Dk. Anthon Mbassa (Chadema).
Pamoja na wote hao kusimama, Zungu alitoa nafasi kwa Mbatia kutoa taarifa yake kwa kutumia Kanuni ya 37 sehemu ya nne.
Mbunge huyo alipopewa nafasi hiyo, alisema, “Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala niliyoomba Oktoba 30 mwaka jana ni ya mwaka 1997 hadi 2005, lakini ule ulioletwa na Serikali ni wa mwaka 1998 hadi 2008.
“Kwa maana hiyo, mtaala ule wa 1997 niliouomba hapa, haujaletwa mezani. Lakini pia Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala ulioletwa na Serikali umeandikwa ni wa Tanzania Bara, wakati suala la elimu ya sekondari ni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Utata mwingine ambao umegubika mtaala huo wa Serikali, ni kukosekana kwa namba rasmi inayotambulisha vitabu vyote nchini, yaani International Standard Book (ISB).
“Mtaala huo haujaonyeshwa nani muidhinishaji wa mitaala hiyo ambaye anapaswa kuwa ni Ofisa Elimu Kiongozi. Kwa taarifa hiyo, naomba suala la mitaala lijadiliwe kwa sababu iliyowasilishwa siyo niliyoomba,” alisema Mbatia.
Hata hivyo, Zungu hakuwa tayari kuruhusu suala hilo lijadiliwe badala yake akaamua kuendelea na ratiba na shughuli nyingine za Bunge.

Nje ya Ukumbi wa Bunge
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge, Mbatia alisema bado anasimamia hoja yake kama alivyoliambia Bunge, kwamba Serikali haina mitaala ya elimu.
Alisema kwamba, Serikali imejikanganya katika mambo kadhaa ambayo yanazidisha utata wa uhalali wa mtaala huo.
Alisema suala la mitaala kukosekana kitu muhimu kama namba ya ISB, ambayo inatolewa na Maktaba Kuu ya Taifa katika mitaala yote mitatu ya shule za awali, shule za msingi na sekondari si suala la bahati mbaya.
“Hawa watu ni wababaishaji kwa sababu mitaala hiyo imeandikwa kwamba ni ya Tanzania Bara, wakati suala la elimu ya sekondari ni la muungano na ndiyo maana mtihani wa sekondari ni mmoja kwa Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema.
Alipoulizwa timu ya wabunge iliyoundwa kuchunguza mitaala hiyo ilichukuliaje upungufu huo, Mbatia alisema.
“Wao walijitetea kuwa hilo ni kosa la kawaida na haliwezi kuathiri uhalali wa mitaala hiyo.
“Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuutangazia umma wa Watanzania kwamba, mtaala rasmi haupo, wizara badala ya kuendeleza vuta nikuvute hii, ikubali kwamba kuna tatizo na tukae chini tulisahihishe,” alisema Mbatia.

Dk. Kawambwa anena
Naye, Waziri Dk. Kawambwa katika ufafanuzi wake kwa waandishi wa habari, alikiri mitaala hiyo kutokuwa na ISB na kusema kwamba hilo ni kosa la kawaida ambalo haliwezi kuathiri uhalali wa mitaala.
Pia kuhusu mtaala kuandikwa Tanzania Bara badala ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema hayo ni makubaliano ya pande hizo mbili ambayo si rasmi kwa sababu Zanzibar wanaye waziri wao wa elimu kama ilivyo Tanzania Bara.
Hata hivyo, alikiri wazi kwamba mtihani wa kidato cha nne unaofanywa na pande hizo mbili za muungano ni mmoja.
“Tulikubaliana na wenzetu wa Zanzibar, kwamba mtihani wa elimu ya sekondari uwe mmoja ingawa wao wanaweza kutumia vitabu tofauti na vinavyotumika Tanzania Bara.
“Suala la ISB si jambo muhimu sana kwa vitabu vyote vinavyochapishwa nchini, mitaala si lazima iwe na hiyo namba ya ISB, kimsingi siyo issue.
“Mbatia alinitaka niwasilishe nyaraka mezani na mimi sasa namtaka awasilishe nyaraka zake kwa Spika, akiweza kufanya hivyo, hata mimi nitajiuzulu.

Mchungaji Natse
Mmoja wa wajumbe wa kamati iliyochunguza uhalali wa mitaala hiyo, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse, alisema makosa aliyoainisha Mbatia ni ya msingi na wataalam wa Serikali walikiri mbele ya timu ya wabunge kwamba ni makosa ya kiuchapaji.
Alisema wizara imekiri kuna upungufu katika suala zima la mitaala, kwa sababu maelekezo yote kuhusu mtaala yalikuwa yanatolewa kwa waraka na kusainiwa na Kamishna wa Elimu.
“Kwa kweli katika hili, tumekubaliana na hoja zote za Mbatia na zitachukuliwa na kufanyiwa kazi,” alisema Natse.

No comments:

Post a Comment