Thursday 31 January 2013

UDHAIFU KATIKA ELIMU TANZANIA: BUNGE LARINDIMA


 
Ndugu James Mbatia (Mb) mwenye tai nyekundu wakipeana mkono na Mhe. Job Ndungai (Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano), Mjini Dodoma


Hoja binafsi ya Ndugu James F. Mbatia (Mb), aliyoiwasilisha  jana ya tarehe 31.1.2013  juu ya Udhaifu katika elimu ya Tanzania, ililifanya Bunge kurindima.

Baada ya kuiwasilisha hoja hiyo, Bunge lilirindima kwa mabishano kati ya Wabunge wa Chama tawala na Wabunge wa upande wa pili (wapinzani).
Wabunge wote wa upinzani waliweka kando tofauti zao na kuwa kitu kimoja. Wapinzani waliungana pamoja kuhakikisha hoja ya Ndugu Mbatia (Mb), inapita.

Mjadala huo, unaendelea kesho tarehe 1/2/2013 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Katika hoja yake, Mhe. Mbatia alisema yafuatayo:

Bunge jana lilijigawa vipande viwili kati ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao waliunga mkono mapendekezo ya serikali kwa upande mmoja dhidi ya wabunge wa vyama vya upinzani waliokuwa wakiunga mkono hoja ya mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, kwa upande mwingine.

Tofauti hizo za kiitikadi na kivyama zilijidhihirisha baada ya Mbatia kuwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu katika sekta ya elimu nchini. Tofauti hizo za wabunge zilijitokeza mapema baada ya Mbatia kutoa hoja yake na kuungwa mkono na wabunge wa upinzani pekee.

Hoja ya Mbatia ilileta tofauti zaidi pale alipohitimisha kwa kuliomba Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza kwa kina udhaifu wa kimfumo katika sekta ya elimu nchini ambayo pia itapendekeza hatua za kuchukua ili kuinusuru sekta ya elimu.

Alisema utafiti alioufanya kwa miaka 17 sasa umebaini kwamba sekta ya elimu ina udhaifu mkubwa kuanzia kwenye sera, mfumo rasmi wa elimu, mitaala, mihtasari na udhaifu katika vitabu vya kiada na ziada.

Alisema matatizo hayo yana harufu ya
ufisadi kwa kuwa vitabu vinavyotumika nchini ambavyo vimethibitishwa na kupewa ithibati vina makosa mengi ambayo kimsingi, yanadidimiza elimu.

Alisema hata nyaraka za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zilizoandikwa kwa Kiswahili zinaonyesha kwamba malengo ya elimu ni 10 wakati malengo yaliyoandikwa kwa Kiingereza tisa na malengo ya elimu ya msingi kwa lugha hiyo yameainishwa kuwa ni 18, lakini kwa Kiswahili ni 10 pekee.

Mbatia alisema tangu Tanzania ipate uhuru, haijawahi kuwa na mitaala ya elimu na kuitaka serikali iwasilishe bungeni kama ipo.

Alisema inasikitisha kwamba baadhi ya vitabu vilivyopewa ithibati mwandishi mkuu, mhariri mkuu na msomaji mkuu ni mtu mmoja, jambo ambalo halikubaliki kitaaluma.

Alisema tatizo hilo la kitaaluma linachangiwa na mgongano wa kimaslahi kati ya watendaji wa kamati inayotoa ithibati ambao nao ni waandishi wa vitabu ya kiada na ziada.

Alisema elimu inayotolewa kwa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hailengi kulikomboa Taifa na kuwajengea walengwa uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya kuhitimu.

Alisema Sera ya Elimu ya Taifa inayotumika kwa sasa imekuwapo kwa muda mrefu na kwamba kuna haja ya kuifanyia tathmini ili kuangalia nini kimetekelezwa na nini hakijatekelezwa na kujirekebisha kulingana na mahitaji ya sasa.

 Alisema masuala mengi ya kisera katika elimu yanayotekelezwa nchini, yametokana na masharti yanayotolewa na vyombo vya kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Alitoa mfano kwamba miaka ya 1980 vyombo hivyo viliitaka serikali ipunguze matumizi ya rasilimali za umma katika kugharamia huduma za jamii ikiwamo elimu, jambo ambalo limechangia uduni wa shule za umma nchini.

Alisema vyombo hivyo pia viliwahi kuielekeza serikali ielekeze zaidi rasilimali katika elimu ya msingi tu kwa maelezo kwamba elimu ya juu ni anasa na katika miaka ya hivi karibuni vimebadili ushauri huo na kudai rasilimali zaidi zielekezwe katika elimu ya juu.

Alisema serikali imekuwa ikikubali maelekezo yote hayo jambo lililopelekea nchi kuwa jalala la sampuli bila kuangalia ubora wa sera hizo na matunda yake kwa taifa.

Alisema rasimu mpya ya sera ya elimu ambayo inaandaliwa inaeleza kwa ujumla maana ya mtaala kwamba ‘Ni jumla ya mambo ambayo mlengwa anatakiwa kuyapata katika mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa lengo la kufikia matarajio ya jamii na taifa’.

Alisema nchi zote duniani wazazi au walezi wa kila mtoto wana haki ya kujua mitaala ya masomo husika ya shule na kwamba vyombo vya elimu huwajibika kumpatia kila mzazi au mlezi nakala ya mtaala, jambo ambalo nchini halipo.

“Mihutasari yote iliyopo inaonyesha kwamba, kama taifa tumeshindwa kutofautisha madhumuni na malengo ya elimu ya Mtanzania,’’ alisema Mbatia.

 Alisema kamati ya wizara inayotoa ithibati kwa vitabu vya kiada na ziada (EMAC), imeshindwa kutekeleza wajibu wake kama ipasavyo na kusababisha mafuriko ya vitabu vinayopotosha dhana ya elimu kwa kuthibitisha vitabu vingi vya  kiada vikiwa na makosa mengi ya kitaaluma.

Alisema mwaka 2009 kupitia mpango uitwao ‘Teaching and Learning Materials Programme (TLMP)’ Tanzania ilipata msaada wa dola za Marekani milioni 13 (Sh. 20,400,000,000) kutoka Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), kwa ajili ya kuandika na kuchapisha vitabu na kugharamia vifaa vya kufundishia masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia na Biolojia kwa idadi ya vitabu 2,250,000.

Alisema inatisha na kusikitisha kutokana na vitabu vilivyochapishwa kwa kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilipata uwezeshwaji wa jopo la wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha South Carolina cha Marekani.

“Mathalani, katika vitabu vya ‘Mathematics for Secondary Schools, Volume I, II, III and IV’ vilivyoratibiwa na EMAC; kama inavyoonekana kwenye utangulizi wake, mwandishi mkuu ndiye huyo huyo mhariri mkuu na mhakiki mkuu. Taaluma na maadili ya uandishi wa vitabu, inazuia mtu kuandaa, kuhariri na kuhakiki andiko lake mwenyewe. Wataalamu walioshiriki kuandaa vitabu hivyo walikuwa na majukumu mengi ikiwamo kuandika, kuhariri na kuhakiki vitabu walivyoandaa wenyewe chini ya uratibu wa EMAC,’’ alisema Mbatia.

Alisema utaratibu huo ulitumika pia kwa wataalamu wa masomo mengine yote yaliyoandaliwa wakati huo chini ya uratibu wa EMAC na tayari vimepewa ithibati.

“Elimu iliyopangwa kwa sera bora na mitaala bora pekee yenye mihitasari na vitabu vilivyotayarishwa kwa umakini mkubwa na uadilifu ndiyo yenye uwezo wa kujenga Taifa la watu waadilifu, wazalendo, wachapakazi, watambuzi wa haki na wajibu wao,” alisema.

Alisema mfumo wa elimu uliopo unatia wasiwasi ikiwa Tanzania itaweza kufikia Dira ya Taifa (2025) ya kuhakikisha mwaka huo, Taifa linakuwa na watu walioelimika kwa upeo wa juu.
Alitahadharisha pia kwamba udhaifu katika sekta ya elimu utaisababisha nchi kushindwa kufikia lengo la pili la Milenia la elimu bora kwa wote.

WAZIRI KAWAMBWA
Baada ya Mbatia kuwasilisha hoja yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliwasilisha maelezo ambayo pamoja na mambo mengine, alilitaka Bunge kutounda kamati teule kwa kuwa serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa sera ya elimu ambayo itaainisha mitaala na mihutasari.

Alisema mfumo wa elimu wa Tanzania una mitaala na mihutasari na kwamba siyo kweli kuwa hakuna mitaala. Alisema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi lakini serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuiboresha kama kununua vifaa vya kufundishia, kujifunzia, kuandaa walimu na kujenga madarasa ya kutosha.

Alisema sekta ya elimu inaongozwa na sera kubwa tatu ambazo ni sera ya elimu na mafunzo (1995), sera ya elimu ya ufundi na mafunzo (1996) na ile ya elimu ya juu (1999).

Alisema mwaka 1997 serikali ilianzisha programu ya maendeleo ya sekta ya elimu iliyowezesha kuongeza fursa za utoaji wa elimu, ubora, usawa wa kutoa elimu na kuimarisha mbinu za uongozi, utawala na ugharimiaji wa elimu.

Alisema sera hizo pamoja na programu hiyo zimesaidia ongezeko la shule za msingi, sekondari, vyuo vya elimu ya ufundi, vya ualimu na vyuo vikuu.

Alipinga hoja ya Mbatia kwamba sekta ya elimu inaongozwa bila mitaala rasmi na kusema kwamba ipo na pia mihtasari.

Alisema serikali imeanza kufanya mapitio na marekebisho makubwa ya sera ya elimu na mafunzo ya ufundi.

“Naomba Bunge lako Tukufu liitake serikali kuzingatia hoja zilizotolewa kwenye hoja hii (ya Mbatia) na kuzifanyiakazi kwa kina wakati ikikamilisha mapitio ya sera ya elimu na mafunzo,” alisema.

Pendekezo hilo la Dk. Kawambwa liliungwa mkono na mawaziri pamoja na wabunge wa CCM, jambo ambalo liliibua mvutano.

Mbatia alipoulizwa kama anakubaliana na pendekezo la Waziri, alikataa akieleza kwamba ni kamati teule ya Bunge ndiyo itaweza kubaini kiini cha udhaifu katika sekta ya elimu.

KITI  CHA SPIKA CHAYUMBA
Hata hivyo, kiti cha Spika kilionekana kuyumba baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliyeanza kupinga uundwaji wa kamati teule akieleza kwamba Mbatia hajataja jambo mahsusi ambalo litachunguzwa na kamati hiyo.

TUNDU LISSU
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliomba mwongozo kupitia kanuni ya 57 (7), na kukumbusha kwamba kanuni za Bunge zinaeleza kwamba badiliko lolote halipaswi kupingana na hoja ya msingi, lakini pendekezo la waziri linataka kuondoa hoja ya kulitaka Bunge lisiunde kamati teule.

Hata hivyo, hoja ya Lissu ilipingwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margaret Sitta, ambaye aliomba wabunge wakubali hoja ya serikali ili ikamilishe kazi ambayo ilikuwa imeanza.

WAZIRI LUKUVI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alilitaka Bunge kukubali mapendekezo ya serikali na kuahidi kwamba hoja za Mbatia zitazingatiwa katika mchakato huo. Alisema serikali haijadharau hoja ya mbatia na kwamba mapendekezo yake ni mazuri na ya msingi.

Hata hivyo, alipinga uundaji wa kamati teule kwa maelezo kwamba haitaweza kukamilisha kazi hiyo kwa kuwa Mbatia amezungumzia mambo mengi.

Maelezo ya Mbatia yaliwainua wabunge wengi wa upinzani ambao walikuwa wakipinga pendekezo la serikali.

OLE SENDEKA
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema hoja za Mbatia ni za msingi, lakini Bunge haliwezi kuunda kamati teule kwa kuwa hoja imetaja mambo mengi ambayo hayawezi kuchunguzwa na wanasiasa hasa suala la mitaala ambalo ni la kitaalamu.

MCHUNGAJI MSIGWA
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alitaka Bunge lifanye kazi yake ya kuisimamia Serikali badala ya kuondoa hoja ya Mbatia; akitahadharisha kwamba elimu ni gharama na hivyo ni lazima nchi igharamie sekta hiyo.

FELIX MKOSAMALI
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema ibara ya 117 ya kanuni za Bunge inaeleza kwamba Bunge linaweza kuunda kamati teule kuchunguza jambo mahsusi na kwamba hoja ya Mbatia ndilo jambo mahsusi la kuundiwa kamati.

NAIBU SPIKA
Naibu Spika, Job Ndugai, alisema kamati teule ingeweza kuundwa kama Mbatia angekuja na hoja mahsusi moja.

JOSHUA NASSARI
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alisema kupinga hoja ya Mbatia kunadhihirisha kwamba wabunge wanakimbia kazi yao ya kibunge ya kuisimamia serikali.
Alisema mfumo wa elimu ni mbovu ndiyo maana vyuo vinazalisha watafuta ajira badala ya wazalisha ajira.

Baada ya mvutano wa muda mrefu, Spika Makinda aliamuru hoja hiyo iamuliwe kwa kura za ndiyo na hapana na wabunge wengi wakaunga mkono pendekezo la serikali.

MOSES MACHALI
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alipinga pendekezo la serikali na kusema kwamba serikali inahofu ya kuundiwa kamati teule kwa sababu ina mambo inayaficha.

SUZAN LYIMO
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo aliitaka serikali kueleza bayana ni lini itarekebisha hali hiyo kwa kuwa sekta ya elimu ni kama ipo chumba cha wagonjwa mahtuti (ICU).

Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema, alisema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba hoja ya Mbatia ya kutaka iundwe kamati teule ni ya msingi kwa sababu kuna upotevu mkubwa wa fedha zikiwamo Sh. bilioni 20 za wafadhili zilizotolewa kwa ajili kuchapisha vitabu.

JABIR MAROMBWA
Mbunge wa Kibiti (CCM), Jabir Marombwa, aliunga mkono mapendekezo ya serikali na pia hoja ya Mbatia na kuitaka serikali kuzingatia mambo yote ya msingi yaliyoainishwa kwenye hoja hiyo.

MARGARET SITTA
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margaret Sitta, alipendekeza kuwa tume ya utumishi wa walimu irudishwe wizarani kwa kuwa ilipoondolewa imeathiri sana kada ya ualimu. Hoja hiyo itahitimishwa leo kwa Waziri Kawambwa na Mbatia kutoa maelezo ya kuhitimishwa.
SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment