Saturday, 4 August 2012

'MOTO' WA MBATIA NA MACHALI BUNGENI

Mbatia, Machali ‘wanavyo washa moto’ bungeni


 
AHADI aliyotoa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi kitaifa, James Francis Mbatia, baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mbunge, kwamba atakapoingia bungeni “atawasha moto” kutetea maslahi ya umma hususan wananchi fukara, inatimia.
Kwa sura hiyo, NCCR –Mageuzi kinazidi kupata umaarufu kutokana pia na utendaji na hoja za Mbunge wake wa Jimbo la Kasulu Mjini, Moses Joseph Machali ambaye amekuwa akisema kwa dhati kuwa, furaha yake kama kiongozi, ni kuwatumikia watu wa jimbo na taifa lake kwa uaminifu na kiuadilifu; iwe ni katika wakati unaofaa, au usiofaa.
Katika safu hii ya Karai Mseto wiki hii, wanasiasa hao machachari wa NCCR-Mageuzi, ndio nitakaojadili.
Kwa kuteuliwa kwake na Rais Kikwete kwa mujibu wa Katiba ya nchi inayompa Rais mamlaka ya kuteua wabunge 10, Mbatia ameweka historia Tanzania kwa kuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama cha upinzani aliyeteuliwa na Rais wa Serikali ya Chama Tawala (CCM) tangu kuanza kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Wengi waliamini kuwa, James Mbatia anakwenda bungeni kuwa “bubu” na kwamba, itakapotokea kuzungumza, eti atazungumza kama “wakili wa kuitetea” Serikali.
Kimsingi, waliodhani hivyo sasa wanatambua kuwa walikosea kwani sasa Mbatia anathibitisha kwa vitendo kuwa, hakuteuliwa kwenda bungeni kuwa mbunge wa “ndiyo mzee”, bali kujenga hoja kwa kielelezo.
Wanaomfahamu vyema walijua, Mbatia hataacha kuikosoa Serikali kwani ni mtu anayejenga hoja zenye nguvu kwa manufaa ya wengi, na mwanasiasa asiyeyumbishwa.
Ushahidi unaothibitisha kuwa, ahadi ya Mbatia kwamba hataenda kuwa mtetezi wa Serikali bungeni, bali kuwasha moto kwa kutumia nguvu ya hoja na kuzisimamia akitumia hoja kwa kielelezo kulishawishi Bunge.

Julai 21, 2012, Mbatia aliweka historia nyingine baada ya kutoa hoja ya msingi, iliyokwamisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika akitumia Kanuni ya Bunge ya 112 (1) inayoelekeza kuwapo kwa nusu au zaidi ya wabunge ili kupitisha bajeti.
Hii ilikuwa kwa mara ya kwanza, kwa bajeti kushindwa kupitishwa bungeni kutokana na uchache wa wabunge waliohudhuria kikao cha bajeti. Haya yakajiri baada ya Waziri wa Wizara hiyo, Christopher Chiza kujibu hoja na michango ya wabunge katika makadirio ya Bajeti ya Wizara yake.
Mbatia alisisitiza kuwa, Katiba ya Nchi, Ibara ya 94 inasema, lazima nusu ya wabunge wawepo bungeni ili maamuzi yawe halali.
Baadaye alipoulizwa kufafanua suala hili, Mbatia alisisitiza kuwa, Kanuni ya 77 ya Bunge, imeweka utaratibu wa kujenga hoja. Akasema, wabunge wote kwa sasa ni 352.
“Waliopaswa kuwapo ni 176 ambao ni nusu au zaidi, lakini waliokuwapo ni takriban 110…. Haiwezekani Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa taifa; maana asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima, halafu tupitishe bajeti yao bila wawakilishi wao, hapana…” akasisitiza.
Kwa upande wake, Machali anakiri kuwa baadhi ya wabunge ni watoro sugu, ingawa si wote kwani wengine huwa na udhuru wa kweli. Anasema uamuzi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda kuweka utaratibu wa kusaini mara mbili unaweza kupunguza tatizo hilo kidogo, lakini si suluhisho la kudumu.
Anapendekeza wabunge warudi katika maadili, wasemane na Spika awe mkali kwa kuongoza kulisimamia hilo ikibidi kuweka hadharani hata majina ya wanaokosekana bila udhuru katika wiki mbili zilizopita.
Taarifa zinasema kutokana na kutoa hoja ya msingi na yenye nguvu kiasi cha kukwamisha bajeti, wabunge wengi sasa wanamwita Mbatia kwa jina la utani “Kiranja wa Bunge.”

Mbatia ameibua masuala ya tahadhari ya miradi na majanga mbalimbali (Risk Management) wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambapo Waziri wa Wizara hiyo, John Magufuli alikubali kulifanyia kazi suala hilo kwa kuliundia kitengo maalumu.
Mbatia alisisitiza kuwa, hata kushindwa kudumu kwa barabara nyingi na madaraja kubomoka ovyo, ni matokeo ya kukosekana kwa kitengo hicho maalumu.

Amefichua pia mpango uliodaiwa kuratibiwa na baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM na wa upinzani, wanaotaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi wawajibishwe.
Wabunge hao wanataka Muhongo na Maswi wawajibishwe wakiwatuhumu kuwa, waliingilia Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na kuipa zabuni ya kununua mafuta Kampuni ya PUMA ENERGY kinyume cha sheria ya ununuzi.
Alhamisi iliyopita, Mbatia amelipua mpango huo akisema wamezibaini njama za kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara hiyo na kutetea mafisadi ndani ya TANESCO na Wizara ambao wamekuwa wakivuruga mfumo wa uzalishaji na usambazaji umeme nchini.
Kadhalika, Mbatia alisema mjini Dodoma kwamba, taarifa za uhakika zinaonesha kuwa mgawo wa umeme unaoonekana ukiendelea kulitesa taifa, ni mpango wa makusudi wa baadhi ya wabunge na watendaji wa TANESCO aliougeuza kuwa mradi wa kujinufaisha wao binafsi.
Anaonesha kukerwa na mpango wa baadhi ya wabunge kutaka kuwasafisha baadhi ya watu wanaoendelea kuihujumu TANESCO huku wananchi wakibebeshwa mzigo wa gharama.
Akasema baadhi ya wabunge wanashirikiana na baadhi ya watendaji katika Wizara ya Nishati na Madini kulihujumu Taifa na wao kutumia nafasi walizo nazo kuwatetea watendaji hao, kitu ambacho si jukumu la wawakilishi hao wa wananchi.
Akiifafanulia safu ya Karai Mseto, Mbatia anabaisha kuwa, kupitia mpango huo, hao wanaolindana, kila baada ya wiki mbili za katizo la umeme (mgawo), wanafaidi kibinafsi takriban shilingi bilioni 3.
“Serikali imenunua mafuta katika kampuni ya PUMA ENERGY kwa bei ya shilingi 1460, wao wanaenda kununua kwa takriban shilingi 1800; utaona kwamba kwa wiki mbili za mgawo wa makusudi, wanagawana zaidi ya shilingi bilioni tatu,” amesema.
Amewashangaa wanaobeza hatua iliyochukuliwa Katibu Mkuu (Maswi) kuipa zabuni PUMA ENERGY ya kusambaza mafuta ya uzalishaji umeme kwa TANESCO na IPTL na kuziacha kampuni nyingine zenye bei kubwa, akisema, hawana uzalendo.
“Hawa ndio majambazi na wahujumu uchumi tunaowasema. Kwanini upinge uamuzi unaolifanya taifa liokoe shilingi mabilioni ambayo siku zote yalikuwa yanaingia kwenye mikono ya wajanja?" alihoji na kuongeza, “Tunatoa wito kwa vyombo vya dola, vichunguze kuna nini hapa na wote watakaopatikana wanalihujumu taifa wachukuliwe hatua bila kujali nyadhifa zao.”
Mbatia anasema, “Tanzania haipaswi kabisa kuwa na mgawo wa umeme kwa kuwa unaozalishwa ni mwingi (Megawati 720), lakini matumizi yote yakiwamo ya viwanda, ni megawati 650… Hivyo, utaona kwamba, tunao umeme wa ziada usiopaswa kuzimwa, lakini unashangaa unazimwa; hii ni kwa sababu ni mradi wa wakubwa wanaofanya biashara ya mafuta kupitia kuzima umeme.”
Mwenendo wa TANESCO, anasema Mbatia, umekuwa ukishangaza kwani Januari mwaka huu, shirika hilo lilitaka kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 145, ikabidi Serikali iipe ruzuku ya shilingi bilioni 136.
“NCCR tulitaka kuandamana, lakini baada ya kuzungumza na Rais, badala ya kupandisha kwa asilimia 145, wakashusha ongezeko la bei hadi asilimia 40.29 iliyopo sasa.
Anasema, kigogo mmoja wa TANESCO kwa kushirikiana na mkewe (kigogo huyo) wakimiliki kampuni moja (jina tunalo), Desemba 20, 2011 waliingia mkataba wa shilingi 884,550,000 kwa ajili ya usambazaji wa vya vifaa mbalimbali vya ofisi katika shirika hilo.
“Yeye (anamtaja) alisaini mkataba kama shirika, na upande mwingine wa mkataba ukiwa ni mkewe… Ndivyo watu wanavyojinufaisha na rasilimali za nchi, lakini eti baadhi ya wabunge wanawatetea," alisema.

Machali kwa upande wake, amewasha moto bungeni huku “akionja joto ya jiwe” kutokana na juhudi zake za kutetea na kutaka Kanuni za Bunge ziheshimiwe na kulindwa.
Julai 2, mwaka huu, wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba, alimtoa nje ya Bunge wakati akitetea kanuni hizo.
Mabumba alimtoa nje Machali akidai kuingilia mjadala na mvutano iliokuwa umeibuka baina ya wabunge kadhaa wa CHADEMA (Tundu Lissu na John Mnyika) na wale wa CCM (Stella Manyanya na Mwigulu Nchemba) kiasi cha kukifanya Kiti cha Spika kuyumba huku kikionesha upendeleo wa waziwazi kwa wabunge wa CCM.
Mwenyekiti huyo (Mabumba) alimkejeli Machali kuwa, ana “kiherehere” cha kudandia mambo yasiyomhusu ingawa Machali hakuwa amekwishasema neno lolote mbali na kuomba “kuhusu utaratibu”.
Baadaye alipoulizwa, Machali alisema, “Niliona Kanuni za Bunge zinakiukwa kwa malumbano huku muda wa kuwawakilisha wananchi ukipotea bure.
Nikatumia Kanuni ya 68 (1) kusimama kuomba Kuhusu Utaratibu… Nikashangaa Mwenyekiti (Mabumba ) ananitukana kwamba nina kiherehere na ninadandia hoja kutafuta umaarufu.”
Akaongeza, “Lengo lilikuwa kukemea lugha chafu zisitumike bungeni maana kulikuwa na masuala mengi ya kujadili… hilo lilinifedhehesha sana. Wakati huo alikuwa ameniambia ‘kaa chini’ na mimi nikakaa, lakini nikalazimika sasa kusimama kumwambia hana mamlaka ya kumtukana mbunge; anapaswa kuwa mfano bora ndipo akanizimia mic (kinasa sauti) na kuamuru askari wanitoe nje...”
Machali anasema, “Kiti cha Spika kiliyumba maana wabunge wa CCM wakiomba Mwongozo wanaruhusiwa, Kuhusu Utaratibu, wanaruhusiwa, Taarifa wanaruhusiwa, lakini wabunge wa upinzani, wanafokewa tu. Hili sio jambo jema kabisa na linatushangaza wengi na kukidhalilisha kiti chenyewe.”
Mbunge huyo wa Kasulu Mjini anasema, Kiti cha Spika kinaonekana kufanya kazi ya kuilinda Serikali na kinatumia vibaya Kanuni za Bunge. “Tunaona Kanuni za Bunge zinakiukwa, tunaambiwa ‘kaa chini’; wengine tunafuatilia vizuri na tunataka kuona kanuni zinalindwa na kuheshimiwa…”
Machali anasema, Kiti kimekuwa kikipotosha umma kuwa, mbunge anapotaka kuomba Mwongozo, Taarifa au Kuhusu Utaratibu, anapaswa kusimama na kutulia. “Jiulize, kama mbunge anazungumza, akakosea na mbunge mwingine anataka kumpa Taarifa, huyo mbunge akisimama kimya na yule anaye endelea kuzungumza na ikumbukwe kuwa, Spika naye ni binadamu labda ameinama anaandika, atamuona saa ngapi aliyesimama? Matokeo yake, yule atamaliza na kukaa.”
Anasema kwa mujibu wa kanuni za Mwongozo wa Spika (68) (vii), Taarifa (68) (8) na Kuhusu Utaratibu (68) (i), mbunge anayeomba nafasi hiyo anapaswa kusimama na kusema hicho anachoomba ili Spika asikie na kumuona aliposimama amruhusu na kanuni hii ni nzuri.”
Aidha, Machali amewasha moto bungeni baada ya kuanika uozo uliopo katika Idara ya Ardhi wilayani Kasulu na karibu nchi nzima ambapo maofisa ardhi wanagawa ardhi kwa watu zaidi ya mmoja na wengine kugawa viwanja katika maeneo ya wazi na hata maeneo ya barabara ili wajipatie fedha.
Hoja ya Machali kuhusu ufisadi huu, ikazua mjadala mkali bungeni kiasi cha kumfanya Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuahidi kwenda Kasulu kujionea mambo hayo.
Kadhalika, wabunge walipotaka ajali ya mv. Skagit ijadiliwe bungeni, Machali aliomba mwongozo na kuishutumu Serikali waziwazi kuwa imezoea “kuwaziba watu midomo” wakiwamo wabunge kwa kutoa hoja kuwa jambo fulani lipo mahakamani au linashughulikiwa lakini majibu hayatolewi na akasisitiza umuhimu wa ajali hiyo kujadiliwa bungeni hapo kama dharura.

No comments:

Post a Comment