Monday 2 July 2012

MISAMAHA YA KODI

Mbatia: Sera ya Misamaha ya Kodi Itizamwe Upya
Monday, 02 July 2012 08:39
Imeandikwa na Fidelis Butahe wa Gazeti la Mwananchi
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema misamaha ya kodi isiyo na tija inaikosesha nchi mapato.
Mbatia ambaye pia ni mbunge mteule alisema kuwa tangu Julai mwaka jana mpaka Februari mwaka huu Serikali imepoteza zaidi ya Sh1.04 trilioni za misamaha ya kodi, fedha ambazo zingeweza kuongezwa katika fungu la fedha za maendeleo ambazo ni kidogo katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Mbatia lisema kuwa msamaha huo wa kodi ni sawa na asilimia 30 ya fedha zote za maendeleo katika bajeti ya mwaka huu. Fedha ya maendeleo katika bajeti ya mwaka huu ni Sh5 trilioni.
Bila kutaja mashirika wala taasisi hizo, Mbatia alisema zipo ambazo tangu nchi inapata uhuru hazijawahi kukatwa kodi, lakini hivi sasa zimegeuka mwiba mchungu kwa wananchi kwa kuwa zinatoa huduma ambazo haziwanufaishi watanzania, zina gharama kubwa.
“Sera ya taifa ya misamaha ya kodi inatakiwa kutizamwa upya, je, kuna uaminifu katika hili, kuna umuhimu gani wa kuwa na misamaha ya namna hii” alihoji Mbatia.
Alisema kuwa tangu mwaka 2006 mpaka sasa zaidi ya Sh5.05 trilioni zimesamehewa na kuongeza, “Fedha hizi ni sawa na zile la maendeleo ambazo zimetengwa na serikali katika bajeti ya mwaka huu, hapa kuna tofauti kubwa, jambo hili litizamwe upya.”
Alisema kuwa Serikali inatakiwa kuangalia maeneo mengine ya kukusanya kodi kubwa kuliko kupandisha kodi katika sigara, vinywaji na kuendelea kutoa misamaha kwa taasisi na mashirika mbalimbali.
“Katika sekta ya madini Serikali inaweza kukusanya kodi kubwa, hata haya mashirika na taasisi ambazo hayakatwi kodi, Serikali inatakiwa kuyaangalia upya kwa sababu yapo mashirika mengine hayakatwi kodi lakini huduma yanazotoa zina gharama kubwa hivyo kugeuka mwimba kwa wananchi,” alisema

No comments:

Post a Comment