Sunday 22 July 2012

Bajeti ya Wizara ya Kilimo yakwama Bungeni

JUMAPILI, JULAI 22, 2012 09:32 MAREGESI PAUL NA DEBORA SANJA, DODOMA
*Kisa utoro wa wabunge ukumbini
*Mbatia ataka marekebisho ya kanuni

BUNGE, jana lilishindwa kupitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 kutokana na utoro wa wabunge.
Tukio hilo lilitokea jana mchana, baada ya Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kuomba utaratibu na kutumia Kanuni ya 112 inayoeleza jinsi Spika anavyoweza kuahirisha mjadala wa Bunge wa kufanya maamuzi yoyote kutokana na idadi ndogo ya wabunge walioko bungeni.
Kutokana na hoja hiyo ya Mbatia ambayo iliungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani, Naibu Spika, Job Ndugai, alilazimika kuahirisha Bunge baada ya wabunge kukaa kama Kamati ya Bunge zima na kupitisha bajeti hiyo kifungu kwa kifungu.

Kabla ya Naibu Spika kuahirisha Bunge, Mbatia alisimama na kusema kuna haja Bunge likaahirishwa kwa kuwa wabunge waliomo ndani walikuwa chini ya nusu ya wanaotakiwa kufanya maamuzi kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.
“Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 112 inataka Bajeti ipitishwe ikiwa tu ididi ya wabunge waliohudhuria watafikia nusu ya wabunge wote.
“Hapa tulipo, mimi nimehesabu wabunge wote hatuzidi 110, na tunajua idadi ya wabunge wote tunaotakiwa kuwamo humu ni 352 na nusu yake ni wabunge 176.
“Kwa hiyo, ili tutende haki, nakuomba mheshiwa Naibu Spika, uhesabu idadi ya wabunge waliopo kabla ya kupitisha bajeti hii ili tuwatendee haki Watanzania,” alisema Mbatia.

Mbatia alipokaa, alisimama Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) na kutumia Kanuni ya 77 (1) na (2).
“Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 77 (1) inasema hivi, akidi kwa kila kikao cha Bunge wakati wa kufanya maamuzi itakuwa ni nusu ya wabunge wote, kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 94 ya Katiba isipokuwa kwamba, idadi hiyo haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa kubadilisha masharti yoyote ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.
“Mbunge yeyote aliyehududhuria anaweza kumjulisha Spika kwamba, wabunge waliopo ni pungufu ya akidi inayohitajika kwa ajili ya shughuli inayoendelea.
“Kwa maana hiyo, mheshimiwa Naibu Spika, nasisitiza kuwa, hatufiki nusu humu ndani, naomba Bunge liahirishwe tusipitishe bajeti hii” alisema Mkosamali.

Mkosamali alipomaliza kujenga hoja yake, ilifuatia zamu ya Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) ambaye naye alizungumzia kanuni hiyo hiyo, kipengele cha tatu kinachosomeka hivi.
“Endapo Spika ataridhika, kwamba idadi ya wabunge walio ndani ya ukumbi wa Bunge ni pungufu ya idadi inayohitajika, basi atasimamisha shughuli za Bunge kwa muda atakaoutaja na atamwagiza Katibu kupiga kengele,” kinasomeka kipengele hicho.
Wabunge hao, walipomaliza kuzungumza, Bunge lilikaa kama Kamati ya Bunge zima ili kupitisha bajeti hiyo kifungu kwa kifungu, lakini Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), alisimama na kusema Bunge halifai kuendelea kwa kuwa wabunge waliopo ni chini ya nusu na hawapaswi kupitisha bajeti. Hoja hiyo ilipingwa na Naibu Spika na Kamati ya Bunge zima kuendelea.

Hatua hiyo ilipokamilika, Bunge lilirejea tena na Naibu Spika aliagiza kengele ipigwe ili kuwaita wabunge waliokuwa nje ya ukumbi wa Bunge.
“Naomba kengele ipigwe, lakini waheshimiwa wabunge kama nilivyowaambia mwanzoni, Mbatia, Machali na Mkosamali, wamezungumzia Kanuni ya 77 (3) inayoeleza jinsi Bunge linavyoweza kuahirishwa kutokana na upungufu wa wabunge.
“Lakini, kumbukeni kwamba, wabunge wengine wako Zanzibar kweye ile ajali ya meli tena kwa idhini ya Spika na wengine wamekwenda Longido kwenye msiba wa mama yake mzazi, Lekule Leizer (Mbunge wa Longido- CCM) kwa idhini yangu.
“Lakini pia, nilikuwa najaribu kuangalia kama kuna wabunge wamesaini leo asubuhi lakini sasa wako kwenye kamati mbalimbali.

“Kwa kuwa zoezi hili la kupitisha bajeti kama Kamati ya Bunge zima imekamilika, sasa naahirisha Bunge hadi Jumatatu wiki ijayo na itapitishwa kwa muda mfupi sana,” alisema Naibu Spika.
Awali, baada ya Mbatia kuwasilisha hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alikuwa akihangaika kuwashawishi wabunge waliokuwa nje ya ukumbi wa Bunge ili waingie ndani.
Wakati Lukuvi akifanya hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, naye alikuwa akiteta jambo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ingawa haikujulikana walikuwa wakizungumzia jambo gani.

Wakati huo huo, wabunge wa NCCR- Mageuzi, walikutana na waandishi wa habari mjini hapa na kueleza jinsi Kanuni za Bunge zinavyokiukwa na viongozi wa Bunge.
Waliokuwa katika mkutano huo ni pamoja na Mbatia, Machali, Mkosamali, Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaituni Buyogela na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

Katika mkutano huo, Kafulila alisema wataangalia uwezekano wa kuwasilisha hoja bungeni ili kutengua maamuzi yaliyowahi kufanywa na Bunge chini ya nusu ya wabunge.
Alisema tabia ya wabunge kuwa watoro bungeni, imekuwa ikiwasumbua na wamewahi kuijadili katika vikao vyao.
Kutokana na hali hiyo, alisema NCCR-Mageuzi imetimiza wajibu wake wa kuwatumikia Watanzania kwa kutaka haki itendeke wakati wa kupitisha bajeti.

No comments:

Post a Comment