Sunday 27 May 2012

NCCR yaendelea kuishambulia CCM


na Mwandishi wa Tanzania Daima, Mtwara
VIONGOZI wa kitaifa wa Chama cha NCCR –Mageuzi, walioko mjini hapa, wameendelea kukishambulia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwataka wananchi wasikichague katika uchaguzi wowote.
Wamesema kama wananchi wanataka maendeleo ya kweli, na njia pekee ya kuwafikisha mahali hapo ni kukihama chama hicho tawala kwa kuwa ndicho kimesababisha maisha magumu yanayowakabili.
Mashambulizi hayo yalitolewa jana na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Danda Juju na Salum Msabaha walipokuwa wakihutubia mikutano ya hadhara katika Majimbo ya Mtwara Mjini na Nanyumbu.
Akihutubia katika Jimbo la Nanyumbu, Juju alisema umefika wakati sasa wananchi wa Mtwara kuonyesha kwa vitendo jinsi wanavyochukia maisha magumu yanayosababishwa na CCM kwa vile bila kufanya hivyo maisha bora kwa kila Mtanzania hayatapatikana.
“Ndugu zangu, wakoloni tuliwakataa na kuwataka watuachie nchi yetu kwa sababu walishindwa kutufikisha mahali tulipokuwa tukitakiwa kufika ikiwamo kutotoa demokrasia ya kweli.
“Wakoloni tuliwakataa kwa sababu hatukuona sababu ya kuendelea nao, lakini kwa bahati mbaya baada ya watu hao kutuachia nchi yetu, wamekuja wakoloni wengine ambao ni CCM, hawa nao sasa wanatakiwa kutupisha.
“CCM hawana tena chao, waambieni tumechoka, waambieni hatuwataki tena kwa sababu hao CCM ndio wanaosababisha zao la korosho linakosa bei na hao hao ndio wanaosababisha maisha magumu kwa kila Mtanzania.
“Maisha kila siku yanakuwa magumu, yaani nawahakikishia kama mtaendelea kuichagua CCM ipo siku mtaanza kula mlo mmoja kwa siku ingawa sasa wengi wetu tunaishi maisha ya kubahatisha,” alisema Juju.
Naye Msabaha alisema kama viongozi wa serikali wataendelea kutumia vibaya rasilimali za taifa, chama hicho kitaitisha maandamano ya aina yake kwa wananchi kuzingira nyumba za viongozi hao, ili kuwashinikiza wajiuzulu.
“Korosho mnakopwa kila siku halafu mnapolipwa mnakatwa makato yasiyokuwa na maana, nawaambia kama viongzi wataendelea kuwanyanyasa wananchi, sisi NCCR tutakuja na maandamano mapya na ya aina yake.

No comments:

Post a Comment