Monday 5 December 2011

TAMKO LA CHAMA CHA NCCR MAGEUZI KUHUSU MWENENDO WA MCHAKATO WA KATIBA MPYA NCHINI.

TAMKO  LA CHAMA CHA NCCR MAGEUZI KUHUSU  MWENENDO WA MCHAKATO WA KATIBA MPYA NCHINI.
NOVEMBA 27, 2011.
DAR ES SALAAM.
1.   UTANGULIZI
Sisi wana NCCR-Mageuzi tungependa ifahamike kuwa msingi mkubwa wa umasikini unaolikabili Taifa letu ni mfumo mbovu wa utawala. Katiba ya nchi ndio silaha ya kuhakikisha mapinduzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kuweza kujenga Taifa lenye maendeleo endelevu ambalo ndio makusudio na ndoto ya wazee wetu walio asisi na kupigania uhuru wa Taifa hili.
Ni katika msingi huo, NCCR- Mageuzi  kama chama cha siasa ambacho asili yake ni madai ya katiba mpya kuanzia uasisi wake kwa maana ya Kamati ya Taifa ya  Madai ya Mabadiliko ya Katiba (National Committee For Constitution Reform (NCCR) iliyoketi tarehe 11 na 12 Juni 1991 na baadaye kujibadili kuwa chama cha siasa mwaka 1992). Mchakato huu kuwa ni muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa letu.
Hata hivyo, pamoja na mchakato huu kuwa muhimu sana kama mapigo ya  moyo wa Taifa letu, Kama Chama tunasikitishwa sana kwa namna ambavyo mchakato huu unachezewa kwa dharau na jeuri ya watawala na Chama Cha Mapinduzi.

2.   UPUNGUFU KATIKA MCHAKATO
NCCR - Mageuzi tungependa ikumbukwe kuwa kabla na hata baada ya Ndugu Rais Jakaya Mrisho Kikwete  kutangaza kukubali haja ya kuwa na mchakato wa kuandika Katiba mpya  vimekuwepo viashiria  vibaya vinavyo onesha kutokuwepo kwa utayari na dhamira ya kweli ya chama tawala na serikali yake kuhusu dhana nzima ya Katiba mpya.
(i) Chama Cha Mapinduzi hakikuona umuhimu wa kuandika Katiba mpya ndio sababu hawakukubali kubainisha kwenye ilani yao ya uchaguzi ya  mwaka 2010
 (ii) Kutokana na kutokuwepo kwa utayari huo wa chama tawala na Serikali yake kama ilivyobainishwa hapo juu, ndio maana hata baada ya Rais Kukubali shinikizo la Katiba mpya, bado inaonekana CCM na Serikali yake wamedhamiria kuhakikisha mchakato mzima unakuwa mikononi mwa dola na chama tawala kwa kuwa haikuwa dhamira yao.
(iv) Katika kutekeleza azma hiyo ya kuhakikisha mchakato wa katiba mpya unatekwa nyara na serikali ili Umma usishiriki ipasavyo, imetungwa sheria mbovu ya mchakato wa katiba. Sheria hiyo iliwanyima wananchi haki ya kujadili mchakato wa kutunga katiba kwa kuruka hatua ya kuisoma mara ya kwanza bungeni. Sheria hiyo ilipelekwa na kusomwa kwa mara ya pili na tatu bila wananchi kupewa fursa ya kuujadili kwani wananchi waliomba uandikwe kwa Kiswahili ili umma upate fursa ya kutoa maoni yao kwa lugha inayoeleweka na Watanzania walio wengi, kinyume chake Serikali imeliburuza Bunge kwa kwenda kuusoma Muswada kwa mara ya pili na ya Tatu na kuunyima Umma wa Watanzania kutoa maoni yao.
 (v) Katika hotuba yake kwa wazee CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameonekana kuwa amepata ushauri hasi kuhusu mchakato wa kutunga katiba. Sasa Watanzania tunabishania nani ana mamlaka ya kuteua chombo hiki au kile badala ya kuzungumzia jinsi ya kuwashirikisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika mchakato huo.

3.   UPUNGUFU WA MUSWADA
Vifungu vya 28 na 29 cha sheria mpya vinaonesha kuwa Tume ya Taifa ya uchaguzi ndio chombo kitakachosimamia kura ya maoni. Wengi hatuna imani na tume ya sasa ya Uchaguzi. Tume hii si tume huru.
Kifungu cha 26 kinaonesha kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya kuhakikisha Bunge la Katiba  linakuwa chini yake. Sisi tunapendekeza kuwa Bunge la katiba liwe huru ili liweze kufanya kazi yake bila shinikizo la mtu au kikundi chochote. Pia Bunge la Katiba ambalo linaundwa na Wanasiasa walio wengi tena wengi watatoka katika Chama tawala litakidhi matakwa ya Kisiasa hasa kutoka katika Chama kinachounda Serikali na kupuuza maoni na Matakwa ya Umma wa Watanzania. NCCR-MAGEUZI bado tunapendekeza Bunge la katiba litokane na Wananchi.
Kifungu cha 20 cha sheria mpya kinabainisha kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya kuteua wajumbe 116 kutoka asasi zisizokuwa za kiserikali; asasi za kidini; vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu; taasisi za elimu ya juu; na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii. Sisi tunapendekeza kuwa wawakilishi hawa wateuliwe na taasisi husika badala ya kuteuliwa na Rais. 
Kifungu cha 5 kibadilishwe ili Tume ya katiba iwe chombo cha Bunge la katiba na tume hii pamoja na tume na vyombo vingine vya kutunga katiba viundwe na Bunge la katiba.
Kifungu cha 13 kinaonesha kuwa Katibu wa Sekretarieti ya Tume atateuliwa na Rais huku wajumbe wakiteuliwa na Waziri wa Sheria na Katiba. NCCR-Mageuzi tunapendekeza kuwa Katibu na wajumbe wa sekretarieti  ya Tume wateuliwe na Bunge la Katiba na kuwajibika kwa Bunge hilo.

Inaonesha kuwa baada ya kupokea muswada wa Katiba Rais atamkabidhi Waziri wa sheria na Katiba kuwasilisha muswada wa Katiba kwenye Bunge la Katiba. Hapa ikumbukwe kuwa ni Tume iliyofanya kazi na hivyo ni Tume iliyopaswa kuwasilisha muswada huu badala ya Waziri. Kitendo cha kumtaka waziri kuwasilisha muswada ambao hakuufanyia kazi ni sawa na kuteka mchakato kutoka kwa  Tume kuwa wa serikali.
Pia kifungu cha 18 kinaonesha kuwa baada ya Tume kukamilisha kazi yake itawasilisha muswada wa katiba kwa Rais. Hii si sawa. Tume ya kutunga katiba inawajibika kwa Bunge la katiba  na hivyo itawasilisha mswada kwa Bunge la katiba.
Sheria hii inapendelea upande mmoja wa Muungano, yaani Zanzibar. Nafasi ya Tanganyika na Watanganyika haionekani katika sheria hii. Ni dhana potofu kudhania kuwa Jamhuri ya Muungano ni sawa na Tanganyika. Mara hii lazima Watanganyika wapate nafasi ya kutambuliwa Utanganyika wao sawa na Wanzanzibari kwenye kutunga katiba. Kama ni kweli kuwa Zanzibar ni nchi, basi Tanganyika pia ni nchi. Tukubaliane kuwa nchi hizi mbili zinaunda nchi moja iitwayo Tanzania.

4.   MSIMAMO WA CHAMA
Baada ya kuzingatia mwenendo wote huo na viashiria vyote tunatambua sasa kuwa mchakato wa katiba utakuwa shughuli ngumu kama tusipokubaliana kusikilizana na kila kundi kuchangia bila kuweka masharti yanayokwamisha maridhiano. Katiba ni mchakato wa Taifa na si wa kikundi kimoja. Lazima tujue kuwa katiba ni matokeo ya maridhiano ya kitaifa.
Chama Cha NCCR - Mageuzi kinapenda kuweka msimamo wake wazi. Tutapiga vita kwa nguvu zetu zote hatua ya kikundi au chama chochote kubinafsisha hoja ya katiba. Hii ni hoja ya Taifa na kila mwananchi ana haki sawa kushiriki na kuchangia.
Pia ieleweke kuwa zoezi tunalofanya sasa siyo mwisho wa hoja ya katiba. Katiba ni uhai wa Taifa. Taifa hai huongozwa na katiba hai, inayokua na kuboreshwa siku hadi siku na vizazi vyote. Hakuna kitu kinachoitwa ‘katiba ya kudumu’.
Chama Kitahakikisha kwa kushirikiana na wadau wengine wa Demokrasia  nchini na  kwa namna mbalimbali kitatoa elimu ya katiba kwa watanzania ili kujenga hoja na kauli ya pamoja ya wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kikatiba. Lengo la NCCR-Mageuzi ni kuhakikisha kuwa wananchi wanachangia hoja za kikatiba kutokana na uelewa mpana. 

5.   USHAURI  KWA RAIS
 Sisi NCCR-Mageuzi tunamshauri Ndugu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete asiweke saini sheria hiyo mpaka ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa sehemu tata zitakazokwamisha mchakato hata kabla haujaanza. Hii ni kwa nia njema tu ya kutuunganisha Watanzania wote ili tuzungumze lugha moja na kwamba tusiliingize Taifa kwenye malumbano hasi kwenye jambo nyeti kama hili la  katiba ya nchi.
Chama chetu kinapendekeza kuwa mchakato wa kutunga katiba utawaliwe na kuongozwa na Baraza la Taifa la kutunga katiba na tume ya katiba iwe chombo tu cha Baraza hilo. Hii inaondoa mgongano wa maslahi kwa mchakato huu kuonekana umetawaliwa na chama kimoja cha siasa. Ikumbukwe kuwa Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa CCM na kofia hizi mbili si rahisi kuonekana kuwa hazihusiani. Hivyo maagizo na maelekezo ya Vikao vya CCM ambavyo Mwenyekiti wa vikao hivyo ni Ndugu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ndio yatapewa umuhimu Mkubwa kwani atakuja kuyatekeleza kwa kofia ya Urais.
Sisi tunaona giza likilikumba taifa letu. Ukweli ni kuwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania haipo kisheria wala kihalisia. Tangu Zanzibar wabadili katiba yao na kusema kuwa Zanzibar ni nchi, Muungano kama unavyotangazwa na ibara ya kwanza ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977 haupo.

Kwa mfano tumeona kuwa masharti yaliyowekwa na Kifungu cha 9(2) kuwa inaruhusiwa tu kuhifadhi na siyo kukataa uwepo kwa Jamuhuri ya Muungano yanazaa utata na malumbano yatakayoleta ghasia na machafuko. Tunajua kuwa Zanzibar wanadai kuwa wao ni nchi na wakiambiwa kuwa wabadili katiba yao ya sasa ili tuwe nchi moja kwa hakika patachimbika!
Wanzanzibari hawatatawaliwa na kura ya maoni ya sheria ya Muungano kwa kuwa wanayo sheria yao ya kura ya maoni. Katiba ya Zanzibar haibadilishwi bila kura ya maoni iliyopigwa kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar kuridhia.
Haya ni machache tu ambayo kama Serikali itayasikiliza, basi Rais hatasaini sheria hiyo mpya kwa sasa kwa kuwa haina maslahi kwa Taifa.

HITIMISHO
Mwisho tunapenda kusisitiza kuwa NCCR - Mageuzi ambao ndio waasisi wa hoja hii ya katiba tunayo imani kubwa na watanzania na uwezo wao kujipatia katiba wanayoitaka. Bado tunasimamia tamko letu tulilolitoa mwezi  April 2011 kama ndiyo Msingi bora wa kuelekea kuandikwa kwa katiba mpya.
Sisi tunasema: PAMOJA TUTASHINDA!
Aksanteni sana kwa kunisikiliza.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ndimi Mtumishi wenu mtiifu,


James Francis Mbatia
MWENYEKITI WA TAIFA.

No comments:

Post a Comment